Friday, May 10, 2013

HATA MIMI NINGEMPA IGP MWEMA NISHANI YA UTUMISHI ULIOTUKUKA

 Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,
KUNA una wakati unaweza ukasema umeishi na kuona kila kitu; halafu mengine yanatokea. Katika mambo ya ajabu ambayo yametokea wiki iliyopita kwenye sherehe za Muungano ni kuwa Rais Kikwete amewatunuku maafisa mbalimbali wa jeshi (na watumishi wengine) nishani na tuzo mbalimbali. Kwa kweli sijali sana baadhi ya wengine lakini ni tuzo ya Inspekta Generali wa Polisi (IGP) Said Mwema imenifanya nikune kichwa changu kwa kujiuliza maswali mbalimbali. 

Inawezekana Mwema alikuwa anastahili nishani ya aina fulani lakini kupewa nishani ya “Utumishi Uliotukuka” ni lazima nijiulize kama Rais Kikwete na tume yake ya Nishani walikuwa wanaangalia vigezo gani hadi kufikia kumpa mtu kama Mwema tuzo ya Utumishi Uliotukuka. Unapompa mtu tuzo ya aina hii kwa kweli unapaswa kuangalia uongozi na utumishi wake kwa upana wake kiasi kwamba jambo hata moja ambalo linaonesha ukosefu wa weledi, hekima, au maono ya uongozi kunatosha kabisa kumnyima mtu tuzo hiyo.
Binafsi naamini kuwa  Mwema hakustahili nishani hiyo. Mlolongo wa matukio kadhaa chini ya uongozi wake kwenye jeshi la polisi kunamuondolewa sifa ya kuwa amelipa taifa utumishi uliotukuka! Naomba mniruhusu nitolee mifano michache.

Mauaji ya Albino
Kama kuna kashfa za utendaji mbovu wa jeshi la polisi ni kuibuka kwa wimbi la mauaji ya albino katika baadhi ya mikoa ambapo watu wenye matatizo ya chembe za kutengeneza rangi ya ngozi (albinism) walianza kuwindwa na kukatwa mikono yao au miguu kutokana na imani za kishirikina. Ilichukua watu karibu 50 kuuawa kabla ya hali kuletwa katika udhibiti. Na mapema mwaka huu matukio hayo  yameanza tena. Kwamba kulikuwa na watu wanapanga na kutekeleza mauaji ya albino bila kujali matokeo (with impunity) inashangaza. Hadi pale watu wa Usalama wa Taifa walipoingilia ndani na kutokana na mashinikizo ya jamii ya kimataifa tukaona jeshi la polisi likijaribu kufanya kamatakamata. Unaweza vipi kumpa mtu tuzo ya utumishi ulioutuka katika mazingira kama haya?
 
Vitendo vya Polisi kutumia nguvu kuliko kawaida
Kama kuna kashfa nyingine ni jinsi gani jeshi la polisi chini ya Said Mwema bado halijaelewa nafasi yake katika utawala wa demokrasia na hasa katika kulinda haki za kiraia na haki za binadamu. Tumeshuhudia watu kadhaa wakiuawa na kunyanyaswa haki zao chini ya mikono ya jeshi la polisi. Hakuna mfano mkubwa wa kuonesha hili kama tukio la mauaji ya Mwandishi Daud Mwangosi. Kama kulikuwa na wakati ambapo Jeshi la Polisi lingepewa uongozi uliotukuka basi ni wakati ule lakini tuliona mojawapo ya udhaifu mkubwa wa IGP Mwema kutoa uongozi na kusimamia watu wa chini yake. Leo Kamanda Kamuhanda bado yupo.
Na mfano mwingine ni huu wa juzi ambapo naamini kabisa kilichotokea Arusha katika kumkamata Mbunge wa Arusha Godbless Lema ni matumizi mabaya madaraka (abuse of power). 

Kweli jeshi la polisi linaweza kwenda kutumika kwa sababu kuna kiongozi kazomewa na polisi wanaenda kumkamata Mbunge? Kwamba kuna mtu kasema maneno ya kebehi yamekuwa ni uchochezi kwa vile hisia za kiongozi mmoja zimeumizwa? Na jeshi la polisi kweli linaingilia kati na kuwa watumishi. Na hawa ndio watu ambao Mwema anawasimamia? Turudi na kutoa mifano ya jeshi hili kutumiwa kisiasa kama tulivyoona Tukuyu, tulivyoona Songea, tulivyoona Mtwara? Kweli huyu bwana kuna mtu anasema anastahili kupata nishani iliyotukuka?
 
Jeshi la Polisi na kuminya vyama vya upinzani
Kama kuna namna ambayo tumeona jeshi hili la Polisi chini ya “utumishi uliotukuka” wa Said Mwema limetumika na zaidi ya kutumika kukandamiza upinzani na hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Tumeona watu wakipigwa na polisi kule Kiteto kwa sababu za kisiasa; tumeona jeshi likishindwa kutoa ulinzi unaostahili kwa wapiga kura kama ilivyotokea Igunga, tumeshuhudia jeshi la polisi likiingilia kati mikutano ya kisiasa na kusababisha mauaji (imetokea Arusha, imetokea Morogoro na imetokea Songea na Iringa).

Pia tumeona jeshi hilo likitumika kuwanyanyasa viongozi wa CHADEMA kila wakipata nafasi; ni nani hakumbuki jinsi Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alivyobebwa juu juu kwenye ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha eti kutimisha amri ya mahakama? Hatujaona jinsi wabunge wa upinzani wakinyanyaswa mbele ya hawa ‘wenye nyota’? Yote haya yamefanyika chini ya Said Mwema kweli kuna ma-genius wamesema anastahili nishani ya utumishi uliotukuka?

Ipo sababu moja tu ya kumpa nishani hiyo
Sasa baada ya kutafakari sana nimeona jambo lililo wazi. Hakukuwa na jinsi isipokuwa kumshukuru kwa kuibeba CCM na serikali. Rais Kikwete alikiri katika mojawapo ya hotuba zake huko nyuma kuwa jeshi la polisi limekuwa likiibeba CCM.  Sasa ni namna gani ya kulishukuru zaidi ya kumpa tuzo ya aina hiyo mkuu wake? Sitoshangaa huko mbeleni kina Kamuhanda nao watapewa nishani kama hizi.

Ukifikiria sana utaona kuwa hata kama ningekuwa mimi kwa kweli kwa kazi ambayo Mwema ameifanya kukilinda chama cha Mapinduzi na kuhakikisha kuwa serikali haisumbuliwi na wananchi ni haki lazima apewe nishani. Mwema na viongozi wenzake wamekuwa ndio maadui wa demokrasia na haki za raia labda kuliko polisi ya wakati wa ukoloni. Nikisikiliza baadhi ya kauli za hawa makamanda na viongozi wa mikoa mbalimbali nimefikia hitimisho kuwa baadhi ya hawa kwa kweli wangekuwa ni wazuri sana kumtumikia Mkoloni!

Mtu anaweza  vipi kujiinua juu ya wananchi kiasi hicho na wala haoni tatizo. Eti kwa vile anapigiwa saluti na ana ngao na mwenge mabegani basi dunia yote ikimbie mbele zake! Baadhi ya makamanda hawa ambao wengi wao wamepandishwa vyeo na Mwema kwa kweli kabisa ni ishara tu ya jinsi gani fikra za Said Mwema hazijaingia katika ulimwengu wa demokrasia. 

Lakini kama utumishi wake wote alioufanya Mwema umeisaidia CCM kushinda chaguzi na kuendelea kutawala si ni wazi kuwa hakuna jinsi isipokuwa kwa Kikwete kumshukuru. Kumshukuru kabla ya muda wake wa kustaafu na kwa hakika akitoka huku kama ilivyokuwa kwa Adadi Rajabu lazima Kikwete ampatie ka-ubalozi ka mahali fulani.  Kwani pamoja na mengine ni mwanafamilia.RAIA MWEMA

No comments: