Monday, May 20, 2013

CUF YAKANA KUHUSIKA NA VURUGU ZA MTWARA


Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF), kimekana kuhusika na vurugu zinazotokea katika Mikoa ya Lindi na Mtwara na kwamba zinatokana na sera mbaya za Serikali za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro ambaye alisema wamepata taarifa kuwa katika vikao vya viongozi wa mikoa hiyo, wamekuwa wakiishutumu CUF kuwa ndiyo inayosababisha vurugu hizo.

“CUF haiungi mkono vurugu, tunataka wananchi wadai haki zao kwa njia ya amani lakini inapotokea wananchi wakafanya vurugu Serikali iwajibike kwani yenyewe ndiyo imezuia haki za wananchi,” alisema Mtatiro.

Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani katika ununuzi wa korosho na gesi ni mambo yanayowafanya wananchi wa mikoa hiyo kusababisha vurugu.
Mtatiro alisema kwa mfano zao la korosho, wakulima wamekuwa wakidhulumiwa kwa kutokulipwa fedha za awamu ya pili kwa kisingizio cha kushuka kwa bei ya zao hilo katika soko la dunia.

“ Kilo moja ya korosho inauzwa kwa Sh1,200 kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, awamu ya kwanza hulipwa Sh600 lakini awamu ya pili wamekuwa hawalipwi ama wakati mwingine wanalipwa Sh200, zinazobaki Sh400 zinakwenda wapi, ndiyo maana wananchi hawa wanafanya vurugu,” alisema.
Alisema wananchi wa Lindi na Mtwara wanafahamu haki zao na kuzidai.
“CUF inaionya Serikali ya CCM isitafute mahali pa kubambikizia makosa, viongozi wa CUF wasiendelee kugeuzwa kuwa ndiyo wa kuhojiwa kuhusu makosa ya Serikali na CCM,” alisema Mtatiro katika taarifa yake.

Alisema Serikali inapaswa kuwahoji watendaji wake na sera zake mbovu, ilizoshindwa kuongoza nchi.
Kwa mujibu wa CUF, wabunge kadhaa wa Mikoa ya Lindi na Mtwara walihojiwa katika vikao hivyo wakidaiwa kuwa ni miongoni mwa watu wanaopandikiza chuki kwa wananchi.

MWANANCHI    

No comments: