Thursday, March 28, 2013

NATANGAZA KUJITOA CHAMA CHA WALIMU

 Na Mwl. Salim Mpanda,
 
Walimu tunadhani Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kipo kwa ajili yetu na maslahi ya kazi yetu. Lakini ukweli ni kwamba Chama hiki kinatamka tu kwamba kipo pamoja na sisi lakini hakipo nasi hata kidogo. Ikiwa ni takribani miezi 7 iliyopita yangu mgomo wa walimu Nami nikiwa mmoja wa wapiga kura kuunga mkono mgomo huo halali wa walimu uliokuwa na lengo la kuishinikiza Serikali itutekelezee mahitaji ya msingi ya Kielimu kama vile Madai ya malipo ya walimu, Mazingira bora ya utumishi pamoja na vitendea kazi, leo nadiriki kusema kwamba ule haukuwa Mgomo bali ni uigizaji tu wenye lengo la kupumbaza akili za walimu ambao kwa mujibu wa Katiba ya CWT, Walimu ndio tunaoandaa Viongozi Bora wa Leo na Kesho wa Nchi yetu.

 Kifungu hicho kinasema “ KWA KUWA sisi Walimu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunalo jukumu kubwa la kuelimisha Umma na kutayarisha Viongozi wazuri wa leo na kesho kwa nchi hii….”

Zipo hoja za msingi ambazo nataka leo Watanzania wote waelewe kwamba CWT ni aidha ni Kitega Uchumi tu cha Serikali au ni Kitengo ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa sababu kuna kila namna ya kufanana nacho. Hja hizo ni kama ifuatavyo:

 
1. Upigaji kura ambao uliungwa mkono na walimu kwa asilimia 95% ulikuwa na lengo la kukusanya takwimu za idadi ya walimu waliopo kazini. Kwa sababu kuna maelfu ya majina ya walimu hewa yameondolewa kwenye “Pay roll”, ambao mishahara yao ilikuwa bado inapelekwa kwenye Halmashauri ingawa walimu hao hawapo aidha kwa vifo au kuacha kazi. Hii ni kutokana na zoezi la upigaji kura lilitaka Kila mwalimu katika shule husika kuandikwa Jina na Check Number (namba ya malipo ya hazina).
 
2. Upigaji kura ulilenga kutambua idadi ya walimu wote wapya ambao walikuwa bado taarifa zao hazijapelekwa CWT kwa ajili ya kuanza kukatwa ada za kila mwezi toka katika mishahara yao. Hii inajithibitisha kwa kuwa miezi miwili baada ya mgomo, walimu wapya wote wameanza kukatwa ada ya CWT (CWT Contribution) kila mwezi jambo ambalo halikuwa lengo la mgomo

3.
CWT imetumia zaidi ya Tsh 780,000,000 kwa ajili ya Posho za vikao vya maandalizi ya mgomo, kuandaa nyaraka za kisheria, matangazo na machapisho mbalimbali juu ya mgomo. Lakini viongozi hao walifanya makusudi kufanya hivyo wakijua kabisa kwamba wanafanya mgomo huo kwa kuzuga na utaangukia wakati wa likizo ya sensa ya watu na makazi na hivyo hautakuwa na madhara yoyote bali utaibua mijadala tu.

4.
CWT ilifanya makusudi kuanzisha mgomo, wakati ambao walijua kwamba ni dili kati ya viongozi na Serikali ya CCM kwa lengo la kutuondolea jazba. Halafu kwa ulaini Mahakama ikaweka zuio la mgomo. Jiulize hiyo kesi ni namba ngapi, ipo mahakama gani? Na huwa inasomwa lini na lini?

5.
Upigaji kura na katazo (zuio) la mahakama vilitengenezwa mahsusi na maalumu ili kuwaaminisha Watanzania kwamba CWT imetumia njia sahihi kuwaunganisha walimu na wakati huohuo kuzugia kwamba Serikali kupitia Mahakama imetumia suluhisho sahihi kutatua madai ya walimu ingawa hadi sasa madai ya msingi ya walimu juu ya sekta ya elimu hayajatekelezwa hata moja.

Walimu wenzangu, tusujidharau, tusijidharaulishe na wala tusikubali kudharaulika! Sisi tunaweza kujenga au kubomoa nchi, hivyo basi huu ni wakati wetu wa kuamka na kudai haki za Sekta hii muhimu hadharani. Tuache kujidanganya na kujifariji kwamba tunacho Chama kinachotutetea maana si kwamba tu hakina uwezo huo, bali pia kimekuwa kitengo cha Propaganda cha Chama tawala.  

Natambua kwamba hadi sasa walimu bado tupo kwenye mgomo. Lakini mbaya zaidi ni kwamba tunagomea vichwani mwa watoto (wanafunzi) madarasani na hivyo tunajikuta tunaandaa tabaka bovu zaidi katika Nyanja zote. Kwani matokeo ya darasa la saba na Kidato cha nne ya 2012/13 ni uthibitisho tosha kwamba mgomo ni mkali zaidi. 

Lakini ni wazi kwamba mgomo huu hauna manufaa yoyote zaidi ya hasara kubwa kwa vizazi vyetu huku matatizo yetu ya msingi yakiendelea kutusulubu, kwani hao wanaotusulubu na Serikali yao, watoto wao hawasomi hapa nchini au katika shule zenye hali mbaya, bali wanasoma shule za hadhi za kimataifa na hivyo tunajikuta sisi tunaandaa TABAKA LA KUTAWALIWA DAIMA na wao wakiandaa TABAKA LA WATAWALA DAIMA maana hadi sasa mifano ya wazi tunayo juu ya hili.
 

Pia ipo dhana potofu ambayo chanzo chake ni Serikali inayotafsiri kwamba “Ualimu” ni sekta ya watu waliofeli na hivyo kila mtu kwenye nchi yetu anapokusikia unajitambulisha kwamba wewe ni mwalimu, basi haraka sana mawazo yake yatagonga kwamba wewe ni mtu uliyefeli. 

Dhana hii imebebwa na Serikali ya Chama tawala kwa lengo la kudumaza ufahamu wetu kisaikolojia ili tujidhani kwamba sisi ni watu tusio na mchango wowote hapa nchini na ni watu tuliosaidiwa tu kwa kupewa ajira za ualimu na hivyo kuutuia uhuru wetu dhidi ya Serikali ni kuhatarisha ajira za misaada. 

Pamoja na hivyo bado CWT hakioneshi kukerwa na hili wala kuchukua hatua yoyote kukabiliana nalo. Kwa mantiki hii naweza kusema yafuatayo juu ya Chama cha Walimu Tanzania kama msimamo wangu, na nitaomba walimu wengine waniunge mkono ili iwe mwanzo wa kutoka hapa tulipokwama:i. CWT hakina uhalali wa kuendelea kuhodhi michango yetu ambayo haitunufaishi kwa lolote zaidi ya wachache wanaoitafuna, bila mantiki yoyote ya sisi kuendelea kuwapa fedha zetu.

ii.
CWT sio baba wala mama na hivyo tusikubali kuendelea kuwa wanachama wake hata kidogo kwa kuwa hata kama leo tutaiondoa CWT hakuna mtu atakayelaaniwa hata na Mungu kwa kuwa ni chama cha kilaghai tu kwa Walimu.

iii. CWT kimeendelea kujilimbikizia utajiri mkubwa unaofaidiwa na wachache wenye maslahi na Serikali na ndio maana nadiriki kusema yamkini CWT ni Idara ndani ya CCM kama vile UWT na UVCCM na JUWATA kwa sababu matendo yao ya kifisadi wote yanafanana.
iv. CWT imetufanya sisi walimu ni shamba la bibi kwa kutuvuna lakini hawana wanalorudisha kwetu zaidi ya kututia aibu kwa wanafunzi wetu na kutufanya sisi walimu tuonekane ni watu dhaifu, tusiojitambua na ndio maana tunatandikwa bakora hadi na wanafunzi wetu.

Mwisho kabisa naomba tukumbuke namna Mwalimu mmoja aliyeyaona mateso ya walimu wenzake na sekta nyingine, akakumbuka wajibu wae kwamba ni kutoa elimu kwa jamii yake na hivyo hakuogopa, hakusita wala hakurudi nyuma, bali aliwaunganisha kwanza wanafunzi wake (Enzi hizo Pugu Sekondari na nyingine alizofundisha). 


Akatumia muda wake wa mapumziko kutembea huku na kule kupeleka ujumbe wa mabadiliko, akasikilizwa kwa sababu dhana ya walimu ni watu waliofieli haikuwepo siku hizo na leo tunamwita Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tuige njia zake kuelekea ukombozi wa Taifa letu kwani kwa sasa DENI LA TAIFA ni Tsh Trilioni 21, Ufisadi katika mashirika ya Umma, Ufisadi wizarani, Mikataba ya Kilaghai kama ule wa Chifu Mangungo inaendelea kusainiwa kimya kimya kuiuza Nchi yetu, na hapa ndipo ninapojiuliza sasa nini fahari ya kazi yetu ikiwa sisis ndio tuliowaandaa Viongozi wa namna hii?

Nawaomba walimu Tukumbuke wakati wa TANU, namna watumishi wa sekta mbalimbali walivyofanikisha kuliondoa Taifa letu mikononi mwa wanyonyaji. Na leo hii hatuna TANU, lakini vipo vyama vya Siasa kama TANU, vyenye mtazamo uleule wa TANU. Tuviunge mkono kwa NGUVU zote ili tubadili sura ya Taifa letu lakini sio kuendelea kuburutwa na Mfumo huu wa CHAMA CHA MAPINDUZI ambao ulianza mwaka 1977 baada ya kufanikiwa kuharibu Mtazamo thabiti wa TANU, na hivyo tuwaelimishe wenzetu kwamba UHURU haukuletwa na CCM bali TANU tena ni kwa kuungwa mkono na wananchi. Na sisi leo tunalo jukumu la kurejeshea nchi yetu UHURU WA KIUCHUMI. 


  Sababu kubwa ya kunena hayo ni kutokana na ukweli kwamba msingi wa matatizo ya Taifa letu yapo ndani ya Serikali na sisi walimu ndio watu tuliopewa dhamana ya kuandaa viongozi BORA. Lakini kikwazo kikubwa ni hiki Chama ambacho kimeshindwa kabisa kuwa Trade Union kati wa Walimu na Serikali na badala yake kimekuwa kitengo ndani ya serikali. Ni bora tupate mwakilishi mwingine na sio CWT tena BINAFSI NATANGAZA KUJITOA CWT.

Nawashukuru kwa kunielewa
.

Mwl Salim Mpanda – Dodoma 


 KWA HISANI YA JAMII FORUMS

No comments: