Friday, March 1, 2013

FALSAFA YA MWALIMU KATIKA ELIMU NA DHANA YA AZIMIO LA ARUSHA
Makala hii ni moja ya makala niliyowahi kuandika Tarehe 14/10/2010 ikiwa ni kumbu kumbu ya miaka 11 baada ya Mwalimu kututoka. Nimeona leo niirudie kuitundika upya japo katika baadhi ya vipengele ili wale ambao wanadhani kwamba Mwalimu alizembea katika suala la elimu wajizodoe wenyewe. Miaka ya hivi karibuni kumetokea na wimbi kubwa la kumkashifu Mwalimu kwamba alikuwa mdini, mbaguzi kwa kigezo cha wao kama wanasiasa wa sasa kuonekana kwamba wako sahihi (Kwa kweli sio rahisi kuelezea mazuri aliyoyafanya Mwalimu Nyerere katika nchi hii ya Tanzania ni ngumu kudhani kama hawa watawala wetu wangekuja kuyageuza kiasi hiki). Kuna msemo watu huwa wanasema "KAMA SIO JUHUDI ZAKO NYERERE .........NA FULANI ANGETOKA WAPI.....? " Nyerere alitumia nguvu nyingi kuwasomesha tena bure. Leo hii wanatugawa kwa misingi ya ukabila,jinsia,dini,kipato na vyeo. Ni kiongozi gani wa serikali anayeweza kumsomesha mtoto wake shule ya kata? Hao wanaotunga hizo sera vichwa vyao ni mstatili,pembe tatu, duara ama  trapeza?  Malengo yao ni kuwafanya watoto wa makabwela mambumbumbu wa kwao wawasomeshe shule za gharama tena nje kwa masurufu ya serikali ambayo ni kodi ya huyo huyo kabwela ili watoto hao waje kututawala na umbumbumbu wetu. HAIWEZEKANI Makala imeanzia kwenye paragrafu ya Azimio la Arusha. Endelea kusoma.......


AZIMIO LA ARUSHA

Mwaka 1967 tarehe 5 mwezi wa pili, Mwalimu alitangaza Azimio la Arusha. Sababu kuu ya kutangaza Azimio la Arusha ilikuwa ni kutekeleza ahadi kwa wananchi wakati wa kudai uhuru yaani kutaifisha rasilimali mbalimbali kuwa mikononi mwa wananchi, kuwa na uchumi imara unaorandana na utamaduni wa mtanzania, kupiga vita unyonyaji na ubaguzi. Zipo sababu zilizojikita kitaalam ambapo wachambuzi na wataalam wa masuala ya Siasa wanasema zinaweza kuwa chachu ya AZIMIO LA ARUSHA. Nitazitaja kwa ufupi

 • Tukio la uhaini wa Jeshi la K A R tulilolirithi kutok kwa mkoloni. Ambapo baadhi ya makamanda wake bado walikuwa ni wakoloni na hivyo kuleta mtafaruku miongoni mwa wazawa/wananchi kuhusu jeshi hilo. Wakati huo huo wazungu wale tayari walikuwa ni raia wa Tanganyika. Tukio hilo lilifanikiwa kuzimwa na jeshi kuvunjwa na kuundwa upya.

 • Sera ya Uhuru na maendeleo kwa wananchi. Mwalimu aliwaahidi wananchi wakati wa uhuru kwamba chama cha TANU kikifanikiwa kukamata dola jambo la kwanza ni kuwawezesha wananchi nafasi mbalimbali serikalini pamoja na fursa mbalimbali. Jambo hilo halikuweza kutendeka kutokana na mizizi ya mkoloni na hivyo wananchi waliona kana kwamba wamesalitiwa.

 • Muungano wa Tanzania na Zanzibar mwaka 1964.

 • Vita baridi baina ya Jamhuri ya Kisovieti na mataifa ya magharibi yaliyofuata sera za kibepari. Ambapo yapo mataifa mengine madogo madogo yaliyoingia katika mkumbo huo.

 • Mgogoro wa kidiplomasia baina ya Ujerumani magharibi na Mashariki. Tanganyika ilikuwa na mahusiano ya kidiplomasia na Ujerumani Magharibi wakati Zanzibar ilikuwa na mahusiano na Ujerumani Mashariki. Ulipoanzishwa Muungano jitihada za makusudi zilifanyika ili kusawazisha hiyo hali na Tanzania ikafuta rasmi uhusiano wa Kidiplomasia baina yake na Ujerumani Magharibi. Ujerumani Magharibi ilikuwa na miradi mingi Tanganyika wakati huo na ndio inayosemekana kuwa ilijenga jengo lile la kubwa Mwavuli(Nkurumah Hall) lililopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambalo nalo halikumalizika kutokana na kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia baina yake na Tanganyika.

Tukiachana na chambuzi za watafiti, wanazuoni ama wasomi, Nyerere alikuwa na wazo ambalo baadhi ya watu waliliona kama ni ndoto za Alinacha ama wazungu huita " Utopian" lakini ukweli ni kwamba Mwalimu aliona mbali. Msingi mkubwa wa Azimio la Arusha ulijikita katika Ujamaa na Kijitegemea. Ujamaa kama imani, Ujamaa kama maisha ya kila siku ya Mtanzania, Ujamaa kama utamaduni halisi wazungu huita " Ujamaa as an attitude of mind".

Kilimo ndio kilikuwa nguzo muhimu kwa kuzingatia usawa wa wakulima na wafanyakazi. Nyerere alitilia mkazo zaidi maendeleo vijijini na hapa alisadifu mataifa mbalimbali ambayo leo hii hatuyashiki kwa maendeleo kwa mfano mkazo wa muasisi wa Taifa la Uchina Komredi Mao Ze Dong ulianzia vijijini na walioleta Mapinduzi ya China walikuwa ni wanakijiji/wakulima.

Mao Ze Dong hakukata tamaa japokuwa alisalitiwa na mwenzake waliyetofautiana naye kiitikadi Chang Kai Shek ambaye baadae alikimbia na kwenda kuanzisha Taifa la Taiwan lakini kimsingi Taiwan ni mali ya Uchina. Ninataka nikupe picha kamili ndugu msomaji uone jinsi gani Mwalimu alivyojaliwa karama ya kuona mbali wakati ule. Leo hii China ni moja ya mataifa tajiri kabisa Ulimwenguni lakini ni kwa misingi ile ile aliyoianzisha Mwalimu kupitia Azimio la Arusha.

Kupitia mpango wa Ujamaa Vijijini Nyerere aliona ili wananchi wapate huduma mbalimbali za kijamii ni vizuri wakikaa pamoja na kushirikiana katika mikakati mbalimbali ya maendeleo. Kuwa na mashamba ya pamoja na kuwa na maisha bora. Kule Israel wana vijiji wanavyoviita "Kibutz" vijiji hivi ni mfano halisi wa vijiji vya Ujamaa ambavyo alivitaka Nyerere. Israel ni taifa dogo sana kijiografia lakini ni taifa lenye nguvu za kutisha sana katika ulimwengu huu tukiachilia mbali masuala yake ya ndani ya migogoro katika mashariki ya kati.

Kama nilivyosema Azimio la Arusha lilijikita katika siasa ya Ujamaa na kujitegemea lakini siasa hiyo ililenga Usawa yaani kutokuwa na matabaka, unyonyaji, kipato cha haki, Watu kutoishi kwa jasho la wenzao na pia haki za watoto, Wazee na wasiojiweza. Hata hivyo katika kipengele fulani Azimio hilo linahadharisha na ninanukuu

" Nchi yetu ni nchi ya wakulima na wafanyakazi, lakini si nchi ya Ujamaa kamili. Ina misingi ya ubepari na ukabaila na vishawishi vyake. Misingi hii ya ubepari na ukabaila yaweza kupanuka na kuenea" (Uk.5 AZIMIO LA ARUSHA)

Katika Ujamaa Mwalimu alisisitiza pia kuhusu njia kuu za uchumi kumilikiwa na wananchi(Wakulima na Wafanyakazi). Ninasema Mwalimu kwa sababu historia inanieleza kwamba falsafa hii aliyeiasisi na kuanzisha ni yeye. Mwalimu aliainisha njia hizo katika Azimio la Arusha kama vile Ardhi, Misitu, madini, maji, mafuta na nguvu za umeme (nishati), njia za habari, njia za usafirishaji, mabenki, bima, biashara na nchi za kigeni na biashara za jumla, viwanda vya chuma, mashine, silaha, magari, simenti, mbolea, nguo pamoja na mashamba makubwa hasa yale yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda vikubwa (uk. 6 AZIMIO LA ARUSHA)

Katika Demokrasia, Azimio la Arusha lilitilia mkazo katika serikali inayochaguliwa na kuongozwa na Wananchi wenyewe. Hakuna Ujamaa wa kweli pasipo demokrasia ya kweli.

Lakini Ujamaa ni imani yaani kuyaishi na kuyafuasa yote yale ambayo ni sahihi kwa taifa lako na pia kutenda yale ambayo unayahutubia jukwaani. Mwalimu mpaka anafikwa na umauti wake alikuwa na hulka hiyo ya uongozi.

Fedha haikuwa msingi wa Maendeleo katika Azimio la Arusha kama inavyoonekana leo na kuhubiriwa majukwaani. Yeye alisisitiza kutotegemea fedha kama msingi wa maendeleo na alisema katika Azimio la Arusha na ninanukuu
" Ni jambo la kijinga kuchagua fedha kuwa ndio chombo chetu kikubwa cha maendeleo na hali tunajua kuwa nchi yetu ni maskini. Ni ujinga vile vile, kwa kweli ni ujinga zaidi tukidhani kuwa tunaweza kuondoa hali hii ya unyonge wetu kwa kutegemea fedha za kutoka nje badala ya fedha zetu wenyewe. Kwa sababu fedha hizo haziwezi kutosha kutimiza mipango yetu ya maendeleo lakini taifa la kweli haliwezi kujitawala kwa kutegemea misaada ya nchi za nje " (Uk. 15 AZIMIO LA ARUSHA). Leo hii nusu karibia nusu ya bajeti ya nchi inategemea misaada ya wahisani huku Tanzania ikiwa na rasilimali lukuki ambazo kwazo zinatafunwa na hao hao wahisani kupitia viongozi wetu kwa kusaini mikataba mibovu inayolifilisi taifa letu. Kwa sababu wamegeuzwa watumwa tayari kwa fedha.

Azimio la Arusha lililenga kumsaidia mkulima kijijini na Nyerere aliona unyonywaji ulio dhahiri kutoka kwa watu wa mijini kwenda kwa watu wa vijijini na ninanukuu kipande
" Tusisahau hata kidogo kwamba wakaaji wa mijini wanaweza wakawa wanyonyaji wa jasho la wakulima vijijini. Hospitali zetu kubwa zote ziko katika miji zinafaidia sehemu ndogo sana ya wananchi wa Tanzania. Lakini kama tumezijenga kwa fedha za mkopo walipaji wa mkopo huo ni wakulima, yaani wale ambao hawafaidiwi sana na hospitali hizo(" Uk 21 AZIMIO LA ARUSHA)

Azimio la Arusha linaelezea ili kupata maendeleo kwa mwananchi, juhudi na maarifa inabidi vitumike na hivyo mkazo umewekwa katika Ardhi na Kilimo, Wananchi, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Uongozi bora.

Kabla ya kumalizia katika kipengele cha Azimio la Arusha ningependa nizungumzie katika uongozi na tuone tofauti kubwa kati ya viongozi tulio nao leo. Sifa za kiongozi mjamaa zilikuwa

 • Awe mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au kikabaila.
 • Asiwe na hisa katika makampuni yoyote.
 • Asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.
 • Asiwe na mishahara miwili au zaidi
 • Viongozi walioainishwa ni wajumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa, Mawaziri, Wabunge na wakuu wa mashirika ya serikali.

Leo hii tuna mabepari wakubwa wakubwa ambao wengi wao walikuwa ama ni wakuu wa mashirika ya umma waliokabidhiwa dhamana na jukumu la kusimamia mashirika hayo lakini matokeo yake wameyafilisi na kufa katika kifo cha mende. Baada ya kuachana na Utumishi wa Umma wanakuwa wanasiasa huku katika dhamira zao wanajua mabaya waliyoyafanya. Unategemea watafanya maamuzi yepi wakiwa katika baraza la kutunga sheria? Huu ndio mfumo tulio nao leo hii Tanzania wengi wa hao wanaojiita wanasiasa ni zao la ufisadi katika utumishi wao wa umma na katika dhamira zao wanalitambua kabisa hilo na hakuna ubishi. Kwa kuona hivyo pia wanaamua kuwarithisha watoto wao, wake zao na vizazi vyao kana kwamba nchi hii ni ya kwao. Kumbe matokeo yake ni kuzalisha mfumo taahira katika nchi.


FALSAFA YA MWALIMU NYERERE KATIKA ELIMU

Kwa mujibu wa Yusuf Kassam katika "Prospects: The quarterly review of comparative Education " (Vol XXIV, no 1/2, 1994, page. 247-259. UNESCO). Falsafa ya mwalimu katika elimu imenyumbulishwa katika makundi mawili nayo ni elimu ya kujitegemea na Elimu ya watu wazima .Elimu ya watu wazima ilijumuisha kusoma kwa kujiendeleza na elimu kwa ajili ya kujikwamua na ujinga.Elimu ya kujitegemea imeelezwa zaidi katika kitabu cha sera ya elimu ya kujitegemea ya mwaka 1967.

Falsafa ya Elimu kwa Watu wazima iliyoasisiwa na Mwalimu ilionekana ni dhana chanya na endelevu miongoni mwa taasisi za kimataifa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yaliyojihusisha na shughuli za maendeleo. Falsafa hii ya Elimu kwa watu wazima ilirandana na dhana nzima ya ufahamu, uwezeshwaji na Ukombozi. Dhana hii imeelezwa kiundani na Paulo Freire katika kitabu chake cha "Pedagogy of the Oppressed".

Mawazo ya Mwalimu kuhusu Msingi wa Elimu kwa watu wazima yaliendana kabisa na wataalam kama Malcom Knowles na J. Roby Kidd wa Kanada. Ni kutokana na dira na mwongozo wa Mwalimu katika jitihada zake za kuinua kiwango cha elimu kwa watu wazima iliyopelekea kuombwa kuwa mwasisi/mwanzilishi na Rais wa heshima wa Baraza la kimataifa la Elimu kwa watu wazima mwaka 1973.

Elimu ya kujitegemea ililenga zaidi vijana kujifunza kazi za uzalishaji mashuleni kujitegemea kutokana na uzalishaji ule na shule kuweza kujiendesha. Mbali na shule kujitegemea mwanafunzi aliweza kujengwa kifikra na kisaikolojia kuhusiana na falsafa ya kujitegemea kwa faida yake na pia kuleta mabadiliko katika jamii kufuatana na ujuzi alioupata. Mwanafunzi alipata elimu ya darasani na elimu ya stadi za maisha kwa vitendo.

Kimsingi elimu ya kujitegemea ilitizama udhaifu na mapungufu ya elimu ya kikoloni pia iliainisha aina ya jamii ya Jamhuri ya Muungano inayoijenga, kutathmini baadhi ya maeneo ya mfumo wa elimu katika kipindi cha mwaka 1967 katika mwangaza wa malengo mapya na mipango endelevu ya Ujamaa na kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu ambao utajikita zaidi katika ukuaji wa uchumi vijijini.

Kwa mujibu wa mwalimu, mfumo wa elimu ya kikoloni uliegemea zaidi katika jamii ya kibepari na uliwaandaa watu kutawaliwa na sio kujitawala lakini sio kutawaliwa tu bali mfumo wa elimu ya kikoloni ulijenga matabaka na kasumba ya kuuabudu utamaduni wa kigeni , kutokuwa na usawa, ubinafsi, urasimu na kutegemea kuajiriwa kuliko kujiajiri.

Kwa ufupi mfumo wa elimu ya kujitegemea aliouanzisha Mwalimu ulilenga yafuatayo:-

 • Elimu ililenga kuwapa watu mbinu na mikakati ya kuweza kuukabili umaskini pamoja na maisha ya kijijini kwa kutegemea kilimo.

 • Walimu na wanafunzi kushiriki pamoja katika shughuli za uzalishaji mali huku wanafunzi nao wakishiriki katika mipango ya kufanya shughuli hizo.

  • Elimu ya kujitegemea pamoja na uzalishaji viliendana na vilikuwa ni sehemu ya mtaala wa elimu uliotoa maana chanya ya uzoefu wa kujifunza elimu ya kujitegemea kwa nadharia na vitendo.

   • Mitihani ilitolewa lakini haikuwa kigezo cha kutathmini utendaji, uwajibikaji wa mwanafunzi

    • Wanafunzi walitakiwa kuanza shule wakiwa na miaka 7

    • Elimu ya masingi ilikuwa ni lazima ijitosheleze na sio njia kuu au nyenzo kuelekea elimu ya juu

    • Wanafunzi walitakiwa kujiamini, kushirikiana na kuanzisha changamoto mbalimbali kupitia nguvu ya hoja jadidi yenye kuleta mtazamo chanya kwenye maendeleo ya nchi yao

    ELIMU YA JUU

    Mwalimu pia alichangia ukuaji wa elimu ya juu kwa misingi ya kuwa chachu ya maendeleo na fikra. Wakati anakifungua chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka 1970. Mwalimu alinukuliwa akisema "Chuo Kikuu ni taasisi ya elimu ya juu ambayo kwayo watu wanapata mafunzo ya kupanua wigo wa uelewa wao, fikra huru na sahihi, uchambuzi wa matatizo na kuyatatua kwa kiwango cha juu."

    Mwalimu kwa namna fulani aliona kwamba vyuo vikuu vya ndani vilikuwa muhimu kuanzishwa kwani vina jukumu kubwa la kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazoikabili nchi yetu kama vile ujinga, maradhi na kujikwamua na umaskini ambayo yeye aliyapa kipaumbele.

    Mwalimu alijenga mfumo wa elimu ya juu ambao unamwezesha Mtanzania kupata uwezo na ujuzi wa kutoa huduma kwa jamii, usawa katika kupata elimu ya juu bila kujali tabaka, Elimu ya juu kama nyenzo ya kujiajiri na elimu ya juu kwa ajili ya kukuza demokrasia. Kabla ya vijana kwenda vyuo vikuu walipitia katika operesheni maalum katika jeshi la kujenga Taifa ikiwa ni njia mojawapo ya kuwajenga vijana kinidhamu na kuzingatia maslahi ya taifa. Operesheni za Jeshi la kujenga taifa ziliondolewa kama masharti ya benki ya dunia na taasisi zake ili Tanzania iweze kupata mkopo wa kujikwamua kiuchumi.

    Mwalimu alipata shahada ya udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu Huria tarehe 05/03/1999 ambapo alitoa hotuba iliyojaa hamasa kuhusu mahusiano ya elimu na changamoto zake nchini. Miezi saba baadae akafariki dunia.

    Kikubwa, pamoja na changamoto za kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na nchi za kibepari, elimu ambayo aliitoa Mwalimu ilikuwa bure kwa sababu ya kuinua na kuleta maendeleo katika nchi yetu ambayo ilikuwa ya makabwela. Leo hii waliofaidi matunda ya elimu wamegeuka mabwanyenye wanaojaribu kuifanya elimu iwe chombo cha anasa na cha gharama na iwe ya kwao na vizazi vyao huku mtoto wa kabwela akiumia na kuisotea kwa jasho jingi. Na mwisho wa siku kupigwa kikumbo na kurudi nyuma kutokana na ushindani. Viongozi wetu wamegeuza elimu kuwa biashara na hivyo ubora wa elimu umeshuka kwa kiasi kikubwa hivi sasa ni kazi kubwa kufikia ushindani katika soko la ajira hususan katika changamoto ya Afrika Mashariki. Watanzania tumerudi nyuma sana kielimu. Kingine ni serikali kutokuwa na mfumo imara wa kuwatunza wataalamu wetu waliosomeshwa kwa gharama kubwa na hivyo wengi wao kukimbilia katika nchi za nje kwa ajili ya maslahi zaidi. Hii sio haki na huku ni kumsaliti mwalimu.

    Kama sio juhudi za Mwalimu Nyerere, nina hakika leo hii tusingekuwa na mawaziri, wakurugenzi, makatibu wakuu au hata Marais tulio nao leo. Yeye ndiye aliyewawezesha mpaka wakafika hapo walipo leo hii. Adha ya mikopo, Rushwa ya ngono katika elimu na rushwa kwa ujumla, Ukabila na matabaka ni vitu vinavyotawala katika elimu ya sasa. Na kwa misingi hiyo, hali hii imeingia hata katika utaratibu wa soko la ajira. Aibu Tanzania ... Aibu watawala wetu.

    Suala la bodi ya mikopo katika elimu bado ni changamoto kubwa kwa mtoto wa kabwela. Mikopo inayotolewa haitoshelezi mahitaji , wakati mwingine kutokwenda kwa wakati na kumsababishia usumbufu mkubwa mwanafunzi awapo chuoni. Kwa ujumla elimu imegeuzwa kuwa biashara na matokeo yake ni kuzaa uozo wa ufisadi unaojitokeza katika nchi yetu.

    Pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwepo kiuchumi wakati wa utawala wa Mwalimu, bado aliweza kuwapatia watanzania wengi elimu ya bure na yenye ubora wa hali ya juu. Sasa hivi tuna utitiri wa vyuo ambavyo vimeweka shabaha na msingi mkubwa katika biashara na sio kukuza kiwango cha elimu.

    Endapo Serikali ingekuwa imedhamiria maendeleo ya kweli katika nchi yetu, ingeacha kukazania kununua magari ya kifahari ambayo yanapita kwa fasheni na kuwekeza katika elimu angalau katika kila mkoa wa nchi hii ya Tanzania kuwe na Chuo Kikuu na hilo naamini linawezekana kwani wataalam tunao.

    3 comments:

    Mbele said...

    Shukrani kwa mchango huo murua. Kuna wajinga wengi siku hizi, wengine wenye wadhifa katika jamii, ambao wanaeneza umbea na majungu kumhusu Nyerere, wakati ushahidi wa yale aliyosema na aliyofanya upo tele kwa yeyote mwenye macho, masikio, na dhamiri njema.

    Nami niliwahi kuandika kijimakala kuhusu suala hilo hilo la Mwalimu Nyerere na elimu. Soma hapa.

    Baraka Mfunguo said...

    Shukran Prof. Nimetembelea na kujionea mwenyewe.

    Ezekiel Kwilla said...

    Kwa wale wenye ufahamu na walio na jicho la tatu katika kuona ndio wanaoweza kuyaona mapenzi mema ya mwalimu katika taifa letu.Mara nyingi huwa napata uchungu kuona taifa lililoongozwa na mwalimu linaangamia....