Thursday, February 14, 2013

WANATAKA KUTUROGA BUNGENI?


Na. M. M. Mwanakijiji,


Vikao vya wachawi hufanyika kwa siri. Sasa sijui kama uchawi upo na una nguvu au ni imani tu lakini ukweli ni kuwa wapo watu wanaamini katika nguvu za uchawi. Vikao vya wachawi hawaalikwi waandishi wa habari. Sababu kubwa ni kuwa vikao hivyo vinahusiana na mambo ya kudhuru zaidi kuliko kitu kingine chochote. Wachawi basi hupenda mambo yao yawe ya siri sana.


Mtu anapoamua kwenda kutafuta msaada wa wachawi (ni wale waganga wa kienyeji wenye uwezo wa kudhuru) ni kwa sababu ameshindwa kukabiliana na kile alichokiona kuwa ni tishio. Mara zote watu wanapoamua kutafuta msaada huo ni kwa sababu wanaamini mbinu za kawaida za kukabiliana na mtu zimeshindikana. HIli ni kweli siyo katika Afrika tu bali hata katika mataifa mengine ambayo imani hizi za kishirikina zipo.

Kwa vile vikao vya wachawi ni vya siri basi ndio maana havirushwi 'live' ila nina uhakika kama tukiwapa nafasi warekodi vikao vyao makaburini watatupatia 'edited versions' ya vikao hivyo. Unafikiria watakapoleta hayo matoleo yaliyohaririwa wataonesha nani wanapanga kumla nyama? Wachawi hawaachi hadi wakamatwe! Sasa kama ni kweli upo uchawi mimi sijui; ila kwamba wapo watu wanaoamini nguvu zake hilo halina shaka. Na kwa wale wenye kuamini nguvu zake, uchawi ni tishio kubwa sana kwani mambo yanayofanywa na wachawi yanavunja kanuni zote zinazojulikana za Fizikia.

Uamuzi wa Bunge kuamua kuleta pendekezo kwenye kikao kijacho kuwa Bunge lisioneshwe moja kwa moja kwa mamilioni ya wananchi wa Tanzania ndani na nje ni uamuzi unaofanana na kikao cha wachawi. Sijui ni nani aliyekuja na wazo hili sasa hivi baada ya wazo hilo kutupwa miezi michache huko nyuma. Lakini kwamba sasa umekuwa ni uamuzi rasmi na kwamba wapo watu wenye akili timamu bungeni wamefikia uamuzi huu ni lazima niulize kama hawa ndugu zetu si vigagula!

Wanachoogopa hawa watu wa Bunge kwa wananchi kuona moja kwa moja vikao vya Bunge ni nini? Kwamba wananchi watawaona wabunge wenye kutoa hoja zisizo na mashiko na hivyo wabunge hao wataanza kupunguza ujiko waliodhania kuwa wanao? Ama wanaogopa kuwa kwa kadiri wananchi wanavyozidi kuwaona wabunge wao wanavyobishana na kulumbana basi kule kulegalega kwa Bunge kutazidi kuwa dhahiri? Au wanaogopa kuona kuwa wananchi watazidi kuona kupwaya kwa serikali yao? Au wanaogopa zaidi kibinafsi kuwa waliodhaniwa kuwa ni viongozi kumbe si lolote na si chochote? Au wanaogopa watu kuona jinsi sera za CCM zisivyoweza kutetewa na jinsi ambavyo kwenye kila kikao sera hizo zikioneshwa kuwa hazitekelezeki huku majibu ya "serikali ina nia" na "serikali iko njiani" yakiendelea kutolewa kwa miaka hamsini sasa?

Lakini mimi nafikiria kuna sababu nyingine ya kutisha zaidi - wanataka kuturoga. Nadhani jaribio lao lile la "unga unga Bungeni" lilikuwa ni jaribio la kwanza kutaka kuliroga taifa zima tuwe mazezeta tusiofikiri, tusiouliza maswali na wenye kuamini kila tunaloambiwa na watawala. Kwa vile ndumba zile nusura zinaswe kwenye luninga jaribio lao la kuturoga lilishindikana. Matokeo yake ni kuwa wananchi wamefunguka zaidi na kuwaelewa wabunge wao; wameilewa serikali yao na kwa kweli wananchi hawakumwogopa kabisa mchawi wao. Aliyedhaniwa ni mchawi mkuu wa taifa aligundulika kuwa ni kilaza tu tena tapeli.

Sasa inaonekana wanataka kujaribu tena. Lakini katika kujaribu huku wameficha nyuma yake dharau. Wametudharau Watanzania na dharau ambayo kwa kweli inapita kwa mbali matusi ambayo Spika na Naibu wake wanadaiwa kutumiwa kwa sms. Maana kudharau taifa zima kwa kweli inataka moyo! Wanaweza vipi kuamua tu kuwa "hatutaki Watanzania watuone tunavyozungumzia mambo yao hadi tuamue tuwaoneshe nini". Sasa kama hii siyo dharau ya taifa (contempt of the nation) tuiite nini? Kwanini wasiamue tu kuvunja Bunge au wafanyie vikao kwenye jumba la spika lile jipya? Au waende kwenye nyumba ya Waziri Mkuu? au wakitaka wakafanyie vichakani baada ya kulishana yamini kwanza!?

Binafsi napinga, nalaani, na ninakataa kudharauliwa hivi. NInakataa kuonekana mjinga na kuwa sisathili kujua wale ambao wamechaguliwa na wananch na waliopita kuomba kura wengine kwa kupiga magoti na kulamba watu miguu leo wana ujasiri wa kusema 'tuwafiche wananchi waliotuchagua". Mtanisamehe - huu ni miongoni mwa maamuzi ya kipumbavu. Mtu mwenye akili akikushauri jambo la kijing akijua wewe nawe una akili halafu ukakubali atakudharau - alisema Baba wa Taifa. Wametuambia jambo la kijinga swali ni je tunajitambua na sisi tuna akili?

Nina pendekezo - kama kweli uamuzi huu utachukuliwa naomba uchukuliwe hadharani angalau mara hiyo moja kabla hawajaacha kurusha matangazo wapigiwe kura ya kuitwa majina (roll call) ili tujue wabunge wetu ambao wanataka kutuficha wanachofanya Bungeni ni kina nani? Na kama kuna wabunge wa upinzani wanaofikiri hili ni jambo jema wasimame na waseme sasa; kama wapo wabunge wa CCM wanaamini kuwa hili ni jambo jema wasimame na wajitaje kwa majina yao Bungeni kuwa wanaunga mkono kuwaficha wananchi waliowaajiri kujua nini wanafanya.

Angalau tutawajua wachawi wetu kwa majina yao!No comments: