Monday, February 4, 2013

UJINGA WA MWAFRIKA: MABABU ZETU WALIKUWA NA UDHURU SISI JE?Na M .M Mwanakijiji,

Kwa wale wenzangu na miye watavikumbuka vizuri "Mfululizo" wa vitabu vya "Ujinga wa Mwafrika". Vitabu hivi vilikuwa kwa muda mrefu sehemu ya simulizi la "Mazungumzo Baada ya Habari" na vilisimulia hadithi fulani ya maisha wakati wa ukoloni au baada ya ukoloni na jinsi gani Waafrika tulikuwa hatujui vitu vya wageni na hivyo tulijikuta tunafanya vitu ambavyo baadaye tukivifikiria tunacheka.


Lakini mojawapo ya vitu ambavyo vinatokana na somo hilo ni habari ya jinsi gani mababu zetu walivyoweza kuuza utajiri wa ardhi yao kwa wafanyabishara ya ukoloni ambao kinara wao alikuwa Carl Peters (Mkono wa Damu)- Mjerumani. Sasa Carl Peters ndiye kwa kiasi kikubwa alisababisha Ujerumani itafute makoloni Afrika na alifanya hivyo baada ya kuona Waingereza na Wabelgiji (Chini ya Mfalme Leopold II) wakitanua maeneo ya mamlaka yao.

Carl Peters alipokuja maeneo haya ya Tanganyika enzi hizo alijileta kama Mwakilishi wa Ujerumani na akabuni mikataba mbalimbali ambayo aliingia na machifu na watawala mbaalimbali (akiwemo Sultani wa Zanzibar na Kabaka Mwanga wa Uganda) na alifanya mikataba hiyo kwa niaba ya kampuni aliyoiunda ya German East African Company (mliosoma historia mtaikumbuka).

Mojawapo ya mikataba hiyo ule maarufu wa Chifu Mangungo wa Usagara na mingine mingi. Katika mikataba yote hiyo machifu walikuwa wanakubali kuyaachilia maeneo ya ardhi yao kuwa chini ya ulinzi wa Mjerumani na kutumiwa kwa faida ya Mjerumani kwa milele yote. Wengi tunafahamu kuwa wazee hawa walikubali kwa sababu moja kubwa walikuwa hawajui kilichomo kwenye mikataba hiyo na hivyo hata walipokuja kugundua kuwa wameuza ardi yao "mikataba" ile ilikuwa halali na Ujerumani ilikuwa tayari kuhakikisha inasimama hata kwa vita (Kilimanjaro ni mfano mmoja wapo).

Mikataba hii ilifichwa kwa wenyewe na ilifanywa na watawala wao; wakulima na wanakijiji wengine hawakujua kuwa machifu wao wameuza ardhi yao. Na hata kama wangetaka kujua wasingeweza kujua kwani mikataba ilikuwa ni siri kati ya watawala na kampuni hiyo ya kigeni. Na hivyo ndivyo kihistoria eneo ambalo baadaye lilikuja kujulikana kama Tanganyika lilivyoangukia mikononi mwa Ujerumani - hii ilijumuisha Rwanda na Burundi. Hii ilibadilika baada ya vita ya kwanza ya dunia ambapo Tanganyika ikawekwa chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa kupitia Uingereza.

Mjerumani kwa kutumia kampuni ya GEAC kujenga reli, kuanzisha mashamba ya katani, pamba n.k na vyote hivi vilifanywa si kwa ajili ya kuwanufaisha wazawa au wananchi bali hatima yake mazao yanayopatikana yapelekwe Ujerumani kuwa malighafi katika viwanda vyao na zile nyingine za kuuzwa sehemu nyingine kuwa chanzo cha mapato kwa Ujerumani. Wananchi hawakuwa na uchaguzi wowote wa nini kinapandwa, nani anasimamia na hata hawakuwa na uamuzi juu ya matumizi ya faida ambayo Mjerumani alikuwa anapata. Hapa ndipo ulipokuwa Ujinga wa Mwafrika.

Sasa ujinga si ugonjwa au tusi; ujinga ni hali ya kutokujua (ignorance). Mtu aliye mjinga akijuzwa anaerevuka na ujinga humtoka katika lile jambo ambalo alikuwa halijui. Na kila mwanadamu ana ujinga wa aina fulani na hivyo katika maisha yote anatakiwa awe tayari kujifunza. Lakini kwenye eneo ambalo ufahamu upo tayari na unapatikana mtu hatakiwi kuendelea kuwa mjinga. Ujinga wa aina hiyo ambao mtu anauchagua ndio huitwa upumbavu au wengine wanaitwa ujuha kwani ni mtu ambaye hata akijuzwa hajui na hawezi kujua kwa sababu hayuko tayari kujua!

Leo hii watawala wetu wametuambia mikataba ni siri na kuwa mikataba hiyo ikiwekwa wazi basi wawekezaji wanaweza kukimbia na kuwa mikataba hiyo ni siri kati ya 'serikali na wawekezaji' hata kama inahusu ardhi ya umma na mali umma. Ujinga ni kuwa tumekubali kuwa hilo ni kweli! Na ujinga zaidi ni kuwa watawala wetu wanaingia mikataba na wanaamini ni vizuri kuifanya siri na hivyo hatujui nini kilichomo. Mkataba ule wa Carl Peters na Chief Mangungo ulikuwa na kipengele kinachosema kuwa ardhi hiyo ingeweza kutumiwa "exclusively" kwa matumizi ya Mjerumani.

Kwanini nimesema hili....

Well, mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi kati ya Kampuni ya Kichina na serikali (Chief Mangugu wa leo) una kipengele kinachosema kuwa sehemu ya gesi ambayo itakuwa inachimbwa huko itauzwa kwa China. Hivyo Wachina wamehakikishiwa gesi ya Mtwara na kutokana na ujuzi wa mtu aliyenisimulia hili na ameona mkatbaa huo anasema Wachina wamehakikishiwa kwa asilimia...

Na sisi tumekubali, Wabunge wamekubali

Mikataba siri....

No comments: