Tuesday, February 5, 2013

KAMATA KAMATA YA POLISI MASASI YAENDELEAHuko Masasi kumeendelea kuwa na matukio ya kamata kamata ya Polisi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni matokeo ya vurugu za tarehe 26 mwezi wa kwanza mwaka huu. Kwa mujibu wa mashuhuda sambamba na vitendo vya kamata kamata ya raia wasio kuwa na hatia, na wanao hisiwa kuwa na hatia vitendo vya udokozi kutoka kwa mapolisi hao vimeweza kushuhudiwa. Hivi sasa ni nadra sana kwa mtu kukaa barazani ama kuongozana na rafikize kwenda pahala.

Kasi hii ya kamata kamata imekuwa kama vile nguruwe anaye tapa tapa akikaribia umauti asijue pa kukimbilia. Imekuwa kana kwamba vile haina macho ni kama njia ya kujenga woga miongoni mwa raia ili kuweza kufanikisha upelelezi. Lakini matokeo yake badala ya kuwajenga woga raia imekuwa ni kinyume chake sasa hivi ni chuki na visasi miongoni mwa raia na Polisi.

Polisi wamekuwa chombo cha kufanikisha malengo na ajenda za watawala na wanasiasa ilihali wao wakiwa hawana mamlaka ya kuhoji uhalali wake ikiwa uhalisia unajulikana. Polisi wamegeuzwa kuwa Punda ambaye bosi anasema bora Punda afe mzigo ufike.

Taarifa zinaeleza watu wanaokamatwa wakipelekwa Polisi dhamana ya kuwatoa ni shilingi za kitanzania Laki tano, haijalishi mtu kama ametenda kosa ama laa. Haijulikani kama ni mradi wa kurudisha gharama za hasara za uharibifu wa mali za wanasiasa ama la. Na haijulikani kama ni njia ya kulipizana visasi ama la. Na hivi leo watu kadhaa wamekamatwa na wamewekwa rumande kwa siku 14 bila dhamana kwa wao Polisi wanachosema ni amri ya mkuu wa nchi.

Swala ni kwamba je , aliyeanzisha na kusababisha kadhia hii ambaye ni serikali haijawajibishwa leo hii mwananchi asiyekuwa na hatia anawajibishwa, inajenga nini kwake na inatarajia nini kutoka kwake? Jibu wanalo na watalipata siku zote mtu huvuna anachopanda ukipanda mbigili usitarajie mahindi. Huu uonevu wa Polisi una mwisho wake. Haitakuwa swala la bomba la gesi tena isipokuwa watu watawachoka watawala wetu na huo ndio utakuwa mwisho wao.

No comments: