Sunday, February 3, 2013

IMETOSHA, TUACHE UPOTOSHAJI
Hakuna ufisadi bomba la gesiNa George Simbachawene,

MRADI wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam, umegawanyika katika makundi mawili. Kwanza ni ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi katika maeneo ya Songo Songo-Kilwa na Madimba-Mtwara Vijijini.

Pili, ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi hiyo lenye vipengele vitatu. Kwanza ni kutoka Madimba-Mtwara Vijijini hadi Kinyerezi- Dar es Salaam lenye ukubwa wa kipenyo cha inchi 36 na urefu wa kilomita 487.

Kipengele cha pili ni kutoka kisiwani Songo Songo kupitia chini ya Bahari na kuungana na bomba linaloka Mtwara katika eneo la Somanga Fungu, lenye ukubwa wa kipenyo cha inchi 24 na urefu wa kilomita 25; kipengele cha tatu ni kutoka Kinyerezi hadi Tegeta, lenye ukubwa wa kipenyo cha inchi 16 na urefu wa kilomita 30. Jumla ya urefu wa bomba litakalojengwa ni kilomita 542.

Mitambo ya kusafishia gesi asilia

Gharama za mradi huu zinajumuisha, kwanza mabomba ya kusafirisha gesi kutoka kwenye visima hadi kwenye mitambo ya kusafishia pamoja na vituo vya kukusanya gesi hiyo (flowlines and gathering station). Hii ni tofauti na ujenzi wa bomba kuu la kupeleka gesi Dar es Salaam.

Pili gharama za mradi zinahusisha ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi na tatu ni kuhusu ujenzi wa kambi za kuishi wafanyakazi wa mitambo ya kusafishia gesi na ofisi za kuendeshea mitambo hiyo.

Katika ujenzi wa mabomba ya kusafirisha gesi kutoka kwenye visima hadi kwenye mitambo ya kusafishia pamoja na vituo vya kukusanyia gesi hiyo (flowlines and gathering station), gharama yake ni dola za Marekani 18,211,000.

Lakini kwenye ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi (Songo Songo-140 mmscfd- dola za Marekani 121,366,800 na Mnazi Bay-210 mmscfd- dola za Marekani 182,050,200, jumla ya gharama yake ni dola za Marekani 303,417,000, wakati ujenzi wa kambi mbili za kuishi wafanyakazi wa mitambo ya kusafishia gesi na ofisi za kuendeshea mitambo hiyo, gharama yake ni dola za Marekani 27,984,000.

Kwa hiyo, utabaini kwamba gharama ya jumla katika ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi ni dola za Marekani 349,612,000.

Bomba la kusafirisha gesi

Hapa kuna ujenzi katika maeneo manne. Kwanza ni ujenzi wa bomba kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Somanga Fungu. Pili, ujenzi wa bomba kuu kusafirisha gesi kutoka Somanga Fungu hadi Kinyerezi- Dare s Salaam.

Tatu ni ujenzi wa bomba kutoka Songo Songo kupitia baharini na kuungana na lile linalotoka Mtwara katika eneo la Somanga Fungu na nne; ni ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Kinyerezi kupitia Ubungo hadi Tegeta.

Tuanze na gharama za ujenzi bomba kuu kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Somanga Fungu (inchi 36, kilomita 290). Katika ujenzi huu, gharama ni dola za Marekani 379,794,598.

Lakini kwa upande wa ujenzi wa bomba kutoka Songo Songo kupitia baharini na kuungana na lile linalotoka Mtwara katika eneo la Somanga fungu (inchi 24, kilomita 25), gharama ujenzi ni dola za Marekani 174,542,400.

Katika eneo la tatu la ujenzi, yaani ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha gesi kutoka Somanga Fungu hadi Kinyerezi jijini Dar es Salaam (inchi 36, kilomita 197) gharama yake ni dola za Marekani 257,998,399. Pia ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Kinyerezi kupitia Ubungo hadi Tegeta (inchi 16, kilomita 30), hili gharama za ujenzi wake ni dola za Marekani 15,025,209.

Lakini kuna gharama nyingine zinazoambatana na ujenzi huu ambazo ni pamoja na ujenzi wa karakana ya matengenezo ya bomba Somanga Fungu, gharama za dharura, gharama za vituo vya kupokelea gesi Somanga Fungu, Kinyerezi na Tegeta, pamoja na gharama za mitambo miwili ya kupunguzia mgandamizo wa gesi na gharama za kujenga ofisi. Hizi zote zimetengewa dola za Marekani 48,354,394 na kwa hiyo, gharama za jumla za ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi ni dola za Marekani 875,715,000.

Gharama ujenzi bomba la kitaifa

Kitaalamu, gharama za ujenzi wa boma hukokotolewa kwa kuzingatia urefu na ukubwa wa bomba, yaani kipenyo. Gharama hizi huwakilishwa kwa kiasi cha fedha kwa kilomita moja kwa milimita za kipenyo (USD/km.mm).

Hivyo basi, bomba la nchi kavu, kutoka Mtwara hadi Kinyerezi Dar es Salaam, likiwa na kipenyo cha inchi 36 na urefu wa kilomita 487, gharama yake ni dola za Marekani 1,309,637 kwa kilomita (US$/km) au dola za Marekani 1,426 kwa kilomita kwa milimita (US$/km.mm).

Bomba la nchi kavu, kutoka Kinyerezi hadi Tegeta lenye kipenyo cha inchi 16 na urefu wa kilomita 30, gharama yake (US$/km) ni dola za Marekani 500,840.3 au kwa dola 1,228 kwa kilomita na milimita (US$/km.mm) wakati bomba la baharini kutoka Songo Songo hadi Somanga Fungu, kwa kipenyo cha inchi 24 na urefu wa kilomita 25 ni dola za Marekani 6,981,696 (US$/km) au dola 11,408 (US$/km.mm).

Hoja za kuzingatia dhidi ya upotoshaji unaofanywa ni kwamba, hakuna ufisadi wowote. Na kwa kujua au kutokujua wanaozusha hoja hiyo wameshindwa kuwa makini na kutafiti ili kubaini ujenzi wa miundombinu kama hiyo huhusisha ujenzi wa ofisi na kambi kudumu za watumishi. Hii ni nchi yetu, tuipende na kuilinda kwa kusema ukweli.


RAIA MWEMA

No comments: