Tuesday, February 5, 2013

HUDUMA ZA AFYA TANZANIA NA MATARAJIO YA BAADAE

Na Rutashubanyuma,

Katika utafiti wangu wa muda mrefu kwenye hospitali za umma umebaini yafuatayo:-


1) Huduma ni mbaya sana na pia wagonjwa wengi hawapewi matibabu yanayokidhi khali zao.

2) Pamoja na baadhi ya madawa kutolewa kwa bei poa lakini hayawafikii wagonjwa bali kwa kutakiwa kuyalipia au kuelekezwa kwenye maduka ya madawa yanayomilikiwa na wahudumu wa hospitali za umma.

3) Wahudumu wengi wa hospitali za umma wanafanya biashara ambazo zinashindana na huduma za mwajiri wao na hivyo kuleta mgongano mkubwa wa kimasilahi na hivyo kuzorotesha huduma za mwajiri wao.

4) Madai ya khali bora yaliyosababisha mgomo wa madaktari yana msingi isipokuwa viwango vya malipo wakiyokuwa wakidai yako juu ya uwezo wa serikali.

5) Kutokana na mazingira mabaya ya kufanyakazi, tabia za wahudumu (Yaani madaktari na wauguzi na wasaidizi wao wote kwa ujumla) ni mbaya na wamekuwa wakitumia matusi, vipigo na hata kuwahujumu wagonjwa kinyume na maadili ya kazi zao.

6) Majengo mengi yamechoka na hata ukarabati hayafai ila kubomolewa na kujenga mapya na yenye ghorofa nyingi angalau zisipungue 8 ili kumudu mahitaji yaliyopo ya wagonjwa na uhaba wa ardhi.

7) Dawa nyingi ambazo zimepitwa na wakati kwenye famasia za wahudumu tajwa baadhi yao hurudishwa na kubadilishwa na zile ambazo ni nzima na zile dawa zisizofaa kupewa wagonjwa ambao wengi wao ni masikini na wala hawajui hata kusoma au kuandika. Na hata yule anayejua kusoma huwa hana mazoea ya ukaguzi tajwa.

8) Wahudumu wengi bila ya hata haya hudai rushwa kutoka kwa wagonjwa ili kufanyakazi ambayo wanalipwa mishahara kama mikataba yao ya ajira inavyosema.

9) Tatizo la maji ni kubwa kwenye hospitali hizo.

10) Mrundikano wa wagonjwa wanaolazwa kwenye chumba kimoja na wengine hata kulala kitanda kimoja unatishia usalama wa afya za wagonjwa wenyewe na hata watoa huduma.

11) Maabara hazifanyi kazi masaa 24 na wikiendi na sikukuu eti zimefungwa. Mgonjwa akilazwa siku hizo inamaanisha matibabu yake ni ya kubahatisha tu kwa gharama kubwa kwa mgonjwa na serikali kwa sababu ni tiba pata potea tu..........MATARAJIO YA BAADAE(The way forward):-

1) Serikali lazima itenge angalau bilioni mia tatu kwa mwaka katika mradi maalumu wa kuimarisha hospitali zetu za Umma. Visingizio kuwa hakuna pesa sasa vifikie ukomo tumechoka kuona wagonjwa masikini wanavyotaabika!

2) Waziri wa afya na Katibu Mkuu wake lazima wawe walikwisha kuwahi kuwa madaktari/wauguzi ambaye wanayoyafahamu matatizo ya hospitali za mikoani na wawe wametoa huduma kwenye hizi hospitali kwa miaka isiyopungua 15 hivi.

3) Kwenye katiba ya nchi iwekwe wazi kuwa hakuna hata sumni ambayo itagharimia watumishi wa umma katika hospitali ambazo siyo za umma. Mwanya wa viongozi kutibiwa nje ya nchi na hata kwenye hospitali za binafsi hapa nchini kunachangia sana katika kuzorota kwa huduma za umma. Viongozi ni wabunifu wa kuja na misamiati mingi ya kuonyesha wanajali huduma kwenye hizi hospitali lakini matunda yao kwenye hospitali husika ni ushahidi kuwa wafungwe kifungo cha milele kutumia fedha za umma kwenda ng'ambo au hata hospitali za hapa nchini. Haya yakifanyika utashangaa kuona huduma tajwa zitakavyopendeza.

4) Majengo yote ya hospitali zilizopo yafanyiwe tathmini na mengi yao ni ya kuyabomoa na kujenga majengo ya kisasa yenye huduma zinazokwenda na wakati. Lisiwepo jengo jipya ambalo ni chini ya ghorofa nane kukidhi mahitaji ya kihuduma na hadhi ya ardhi kesho na kesho kutwa. Mfano tu wagonjwa kwenye chumba kimoja wasizidi wawili na wawe na choo na bafu lao. Kila hospitali iwe na kisima na jenereta lao mbali ya kutegemea huduma za taasisi nyingine.

5) Zipitishwe sheria za kuwakataza watumishi wa umma kuanzisha na kumiliki au hata kuajiriwa na makampuni ambayo yanafanyakazi ambazo zinashindana na kazi za mwajiri wao ili kuondoa migongano mikubwa ya kimasilahi.

6) Vifaa vya uchunguzi wa kiawali vinunuliwe na kuwekwa kwenye hospitali zote za mikoa. Baadhi ya huduma hizi ni pamoja na T-scan/ C-Scan n.k. Taarifa nyingi za madaktari ambazo huzifanyia kazi ni za kukisia tu na hivyo hazina msingi wa kitaalamu na hivyo huongeza gharama kubwa kwa wagonjwa na mzigo kwa serikali kwa kutibu vitu ambavyo havipo!

7) Masilahi ya watumishi wote wa umma kuanzia Raisi hadi mfagiaji iwe na uwiano ambao umepitishwa na sheria ya bunge yakiwemo mafao ya kustaafu na kuondoa matabaka makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yameleta msononeko uliopo kwenye sekta zote za huduma kama ya afya, elimu, polisi n.k na kuchangia huduma kuwa mbaya sana na hivyo kuhatarisha utaifa wetu ambao wanasiasa ni magwiji kuukemea bila ya kubainisha vyanzo vya mmommonyoko wa utaifa ambao unachangiwa sana na tofauti za kimapato kwa kazi ambazo zinafanana.

8) Baadhi ya hospitali tajwa zinatoza gharama ya tshs 10,000/= kwa kitanda ambao ni wizi wa macho macho mbali ya ukweli huduma ya umma ni lazima iwe bure. Inawezekanaje kitanda ambacho watu wamerundikwa kama ghala la kutunzia nafaka mgonjwa alipie chochote? Gharama tajwa zifutwe mara moja na tuachane na huu wizi wa kimachomacho kabisa.....

9) Maabara zifanye kazi masaa 24 kama ni wafanyakazi waongezwe wafanye kazi kwa shift na vipimo vya kisasa viwekwe. Ni upumbavu kutumia pesa nyingi kununua madawa ya tiba huku hatuna vifaa vya kung'amua magonjwa ya wateja wa hospitali zetu.............


JAMII FORUMS

No comments: