Sunday, February 10, 2013

HAYA NDIYO MADUDU YENU MLIOCHAGUA CHAMA TAWALA

Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

NIMEWAHI kusema huko nyuma kuwa kila kura ina matokeo; kila uchaguzi una matokeo.
Unapochagua mgombea fulani dhidi ya mgombea mwingine – iwe ndani ya chama au kwenye uchaguzi mkuu – unakuwa umechagua aina ya matokeo ambayo uko tayari kuyapokea.

Uchaguzi basi una maana hiyo hasa kwamba unachagua nini unataka wale uliowapa kura wakufanyie. Sasa uchaguzi wa 2010 ulikuwa ni uchaguzi ambao umehusisha matokeo. Tatizo ni kuwa wapo ambao walipiga kura lakini sasa wanashangaa matokeo ya uchaguzi huo.

Kwenye wabunge ni kweli zaidi. Wabunge wote wa kuchaguliwa au wakujipachika wameingia ama kwa kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja au kuteuliwa na Rais.

Waliochaguliwa moja kwa moja wametoka kwenye majimbo na wengine wa viti vya upendeleo wote wanaingia katika nafasi zao wakiashiria matokeo yake.

Ulienda kuchagua nini mwaka 2010?

Kwa wale waliopiga kura Oktoba 2010 leo tunaweza kuwauliza vizuri na wao wafikirie; walipoingia kwenye chumba cha kupigia kura walikuwa wanaenda kupigia nini? Je, walikuwa wanapigia sura ya mgombea, chama chake, sera zake au rekodi yake?

Je, walikuwa wanapiga kura wakifikiria taifa zaidi au walikuwa wanafikiria mtaa wao na jimbo lao tu na hivyo walikuwa wanachagua mtu wa kuwapigania wao tu hata kama hapiganii taifa? Walipopiga kura walikuwa wanachagua mabadiliko gani au mwendelezo wa sera zile zile?

Jibu ni rahisi; tukiamini kuwa matokeo ya uchaguzi yalikuwa ndivyo yalivyokuwa basi tunaweza kusema kuwa wapiga kura wengi zaidi waliichagua CCM na wagombea wake.

Wapiga kura hawa walichagua kuendelea na utawala ule ule, wenye uongozi ule ule, sera zile zile na mtazamo ule ule wa kiutawala. Watanzania hawa walikuwa wanaujua utawala wa CCM na kwa kiasi kikubwa walikuwa wanawajua wagombea wao.

Ukiangalia katika wagombea wa CCM ni wachache sana walikuwa hawajulikani kwani wengi tayari walikuwa wanajulikana ama ndani ya Bunge tayari au wakiwa nje kwenye shughuli mbalimbali.

Hivyo, wale waliokwenda kuwapigia kura wabunge walikuwa wanachagua kile wanachokijua na matokeo yake walikuwa wanatakiwa kuyajua. Vinginevyo ni lazima tuhoji hawa wenzetu walipokwenda kupiga kura walifikiria wanafanya nini?

Walienda kuchagua maisha yao kwa miaka mitano; walikuwa wanachagua nchi iongozwe vipi kwa miaka mitano ijayo.

Hivyo, tunapoona wabunge wanafanya mambo wanayofanya ndani ya Bunge, na tunaposhuhudia Bunge likiburuzwa kama ng’ombe asiye na pembe huku wabunge wa CCM wakijipanga kutoa adhabu kwa vile wanatetea “heshima ya Bunge” ni lazima tuhoji kuwa hawa wabunge wengi wa CCM waliwekwa na nani?

Tunapoona mtu kama Job Ndugai – Naibu Spika – anashindwa kuongozakikao cha Bunge na bado anaendelea na nafasi yake ni lazima tuhoji wapiga kura wake walikuwa wanafikiria nini? Alikuwa na uwezo hata wa kuongoza mkutano wa kijiji?

Tunachoshuhdia sasa hivi kuanzia Mtwara hadi Tabora, Mwanza hadi Dodoma, Arusha hadi Mbeya na kila sehemu katikati yake ni kuwa matokeo ya uchaguzi yameanza kujionesha.

Watu wa Mtwara ambao kwa miaka 50 wamekuwa wakitoa sadaka kwenye madhabahu ya CCM sasa hivi wanaamua kurudi na sadaka zao; wanakataa kuendelea kufukiza uvumba kwenye madhabahu hayo. Na baada ya miaka mingi ya kuendelea kuwaridhisha mahoka kwa pombe, ugali na kindi sasa wamekataa na kusema inatosha. Na wanafanya hivyo kwa sababu wamegundua kuwa matokeo ya kuchagua CCM ni haya ambayo wameyaona na wanaendelea kuyaona.

Lakini tumeona mengine. Unaweza vipi kuelezea tukio ambapo mbunge wa CCM anashirikiana na wengine kumpiga mwanaCHADEMA bila kujali utawala wa sheria. Inawezekana mtu huyo huyo ambaye alivunja sheria ya uchaguzi na akaendelea kuwa mbunge leo anashiriki kumpiga raia na chama chake kiko kimya?

Je, wananchi waliomchagua wanaona fahari kuwa naye au wakati umefika Tabora napo pafunguliwe waanze kumtimua kama alivyowatimua wengine? Hivi leo watu wa CHADEMA wakiamua kulipiza kisasi na kumpopoa kwa mawe kuna watu watatuambia ‘utawala wa sheria’ na togwa ya “amani, umoja na utulivu”?

Hadi hivi sasa – na nimeshasema jambo hili katika makala za nyuma – ni hawahawa waliothibishwa kuwa wanaleta vurugu za kisiasa nchini. Mahali pote ambapo damu imemwagika ni kutokana na vitendo vya hawahawa. Na hadi hivi sasa ni wabunge wa CHADEMA na viongozi wake ambao wanalipia vitendo hivi; kuanzia Mwanza, Arusha, Mbeya na kwingine wameendelea kunyanyaswa na kubanwa.

Lakini tumeyaona zaidi ndani ya Bunge juzi Jumatatu na wabunge wa upinzani wamesema sasa inatosha kama ni undava basi na wao wanauweza. Tulichoshuhudia siku hiyo ya Jumatatu ni kile ambacho Nyerere aliikita “tumepuuzwa kiasi cha kutosha”.

Mwanadamu hapendi kupuuzwa, kudharauliwa au kuonewa. Unaweza kumpuuza, kumdharau au kumuonea mwanadamu kwa muda lakini kuna kipindi kinafika anasema imetosha. CHADEMA wametuma ujumbe kwa Kiti cha Spika kuwa undava, ugangwe na ubabe wa kulazimisha hoja kwa vile CCM ni wengi ndani ya Bunge umepita. Mambo ya kutumia “kanuni” kwa ajili ya kuzima hoja kwa vile zinaweza kuitikisa serikali hayana nafasi tena.

Tunapoelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na ule uchaguzi mkuu wa 2015 kila mpiga kura anapaswa kuanza kujiuliza na kufanya uamuzi sasa. Uamuzi huu unahusiana na hatima yake mpiga kura. Kama anafurahia maisha chini ya utawala wa CCM basi anapaswa aichague CCM. Lakini akichagua CCM awe tayari kuishi na matokeo yake.

Siyo leo uchague CCM wakati umeshaambiwa wanatawalaje halafu wakitawala kama ilivyo kawaida yao uwe wa kwanza kung’aka.

CCM wataendelea kutawala kama walivyotawala huko nyuma; hawawezi kubadilika kwani wakibadilika hiyo haitakuwa CCM tena.

Ni kulijua hili ndiko kunakopaswa kuwa msingi wa uchaguzi wa viongozi tunaowataka. Lakini, kama mtu anakwenda kupiga kura kwa ajili ya kuukomoa upinzani au kupiga kura kwa sababu hataki wapinzani washinde au anapiga kura kwa sababu kwake CCM ni kama mama yake basi mtu huyo hatuwezi kumsaidia. Ila tunamuasa tu kuwa ukishachagua uwe tayari kuishi na matokeo yake.

Si tayari tunayaona matokeo ya uchaguzi wa wale walioirudisha CCM madarakani. Si taifa linaendelea kulipa. Sasa watu wanaiona ngondo wanaanza kufunga milango?


RAIA MWEMA

No comments: