Monday, January 14, 2013

SUALA LA GESI MTWARA LISIFANYWE KAMA AJENDA YA KISIASANa Baraka Mfunguo,

Kilichotokea tarehe 13/1/2013 uwanja wa mashujaa ni funzo kwa wanasiasa wote wanaochukulia suala la gesi kama ajenda yao ya kisiasa. Majira ya saa 9:00 alasiri, nikiwa sina hili wala lile nashtuliwa na jirani yangu kwamba kuna mkutano wa hadhara juu ya suala lile lile la gesi. Maana kwa siku za hivi karibuni suala la gesi limekuwa gumzo huwezi kuwapita watu watano bila kusikia suala la gesi, naam mgeni rasmi ni James Mbatia mwenyekiti wa chama cha NCCR -Mageuzi.

Kabla ya Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi kuzungumza, ulifuata utangulizi wa baadhi ya wanasiasa kuzungumza akiwamo Mh Moses Machali Mbunge pamoja na viongozi wengine waandamizi walioambatana na mwenyekiti huyo. Kisha ukafuatia wakati wa Ndugu Mbatia kuzungumza, kimsingi Mbatia alikuwa na hoja ya msingi isipokuwa hakuweza kung'amua kwamba wananchi hawakutaka kusikiliza historia ama maneno ya siasa isipokuwa wao wanataka azimio moja gesi isitoke Mtwara.

Kilichofuata hapo sidhani kama atakuja kusahau katika maisha yake, blogu hii inampa pole kwani hii ndio changamoto ya kisiasa. Suala lingine wananchi walimchukulia Ndg Mbatia kama kibaraka wa CCM haswa baada ya kupata ubunge wa kuteuliwa na Rais, na hapo wananchi wakawa wanahoji uhalali wa yeye kuweza kuwa mtetezi wao.

Fundisho ni moja tu kwa wanasiasa, wawaeleze wananchi ukweli kama sepetu iite sepetu na sio kijiko kikubwa kama wanavyotaka kuwahadaa wananchi. Suala lingine ni suala la elimu lakini nadhani pia hilo ni "too late" wamechelewa mno. Kinachotaka kufanyika ni kama kutumia neno elimu kisiasa kama mbinu ya kuwalainisha wananchi ili waweze kuruhusu gesi yao itolewe Mtwara.

Taarifa zisizokuwa rasmi zinaeleza kwamba tayari makachero wa vikosi mbali mbali wapo mkoani Mtwara kwa ajili ya kufanya tathmini na namna ya kuweza kukabiliana na machafuko yoyote ambayo yanajitokeza. Ikiwamo uvunjifu wa amani unaohatarisha usalama wa taifa.

Suala hapa ni moja tu wanansiasa waelewe wananchi wanataka nini, wawatimizie wananchi, waelewe changamoto za wananchi wao na pia washirikiane na wananchi wao kuzitatua changamoto zao. Wanasiasa wakishapata madaraka yao inakuwa kana kwamba wameshajipandisha daraja na kujiweka juu ya wananchi na wao kuwa kila kitu kwa kupata stahiki za maisha bora huku wananchi wakiteseka na wao kutia pamba masikioni. Sasa suala ni moja "GESI HAITOKI MTWARA" iwe funzo kwao na wanasiasa wote ambao wanatumika kama vibaraka na wapokea rushwa kupitia wawekezaji wakubwa ambao wanawatumia kwa ajili ya kuweza kupata influence ya uwekezaji huku wao wakiwa wanafaidika kwa muda mfupi na wananchi wakichafuliwa mazingira na athari za muda mrefu pamoja na umaskini. Hao ndio akina chifu Mangungo tulionao leo hii.

No comments: