Monday, January 21, 2013

SIMBACHAWENE WANAOTAKA GESI IBAKI SI WAPINZANI, NI WANANCHI WAZAWA
Na Mwana Mapinduzi,

Umetokea mkanganyiko wa kauli kutoka kwa watendaji wa serikali, hususani wananchi kuhusiana na kunufaika na gesi ya Mtwara. Mfano mdogo tu ni wa Naibu Waziri Simbachewene ambaye anawashutumi wapinzani kuhusu kauli zao kwa wana-Mtwara. Sasa naamini kuwa hata James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi si Mpinzani bali ni Mtu wa Serikali; kufuatia kupingwa na Wananchi wa Mtwara na hata kutishiwa uhai wake, kutokana na kauli aliyoitoa kwa wananchi.


Simbacheweni amesahau kabisa hali ilivyo kwa sasa Tanzania, hususani katika maeneo mengi yenye raslimali ambapo wananchi wameishia kuwa maskini na kujeruhiwa na pengine kuuawa kabisa. Mfano mdogo juu ni juzi pale wananchi walipopigwa risasi na polisi miguuni wakichukua mchanga wenye dhahabu kwenye mkoa mmoja wa kaskazini hapa Tanzania. Wananachi wa Mtwara wamejifunza kutokana na dhuluma ya maendeleo ambayo wameipata. Adha na mahangaiko ya kutokuwa na barabara ya lami mpaka leo hii ambapo bado wanapita kwenye vumbi ukiacha Lami ya vipande vipande. Pia wananchi hawa wanaona dhuluma ya maendeleo kutokana na kutonufaika kabisa na Korosho yao, ambapo serikali ilihodhi soko kupitia Mamlaka ya Korosho na hivyo kuwasababishia umaskini.

Wapinzani ambao wanawadanganya wananchi ni akina nani? Nadhani wapinzani wa dhuluma ya haki na maendeleo yao ni wao wenyewe. Kama Simbachewene anabisha, aende mwenyewe na kutoa tamko hilo kwa wana Mtwara kuwa gesi inakuja DAR es Salaam.

Lakini tujiulize, kwani mitambo ya umeme haiwezi kujengwa Mtwara ambako kuna gesi na umeme wake kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa? Mpaka ije DAR. Hapa pana ufisadi. Dar es Salaam kuna Gesi tayari. Bomba limejengwa kutoka Mkuranga na inatumika. Bado hatujaona unafuu wowote wa gesi hii kuwepo hapa DAR. Sasa ya Mtwara itakuja na miujiza gani.

Gesi ya Majumbani bado inaagizwa toka nje na gharama yake kwa mtungi mmoja ni kubwa mno, utadhani hatuna gesi. Gasi maarufu kwa jina na Songas ipo hapa kwenye mitambo ya Ubungo. Lakini bado bei ya umeme kila siku wanaomba ipande.

Simbacheweni huna jipya. Simamia ipasavyo gesi iliyopo Dar kwa sasa, ifanye kazi vizuri na tuone mafanikio na si kupapalikia gesi ya Mtwara. Acha gesi ya Mtwara kwanza iibadili Mtwara na mabadiliko yakionekana ndipo muisogeze mikoa mingine. Hiyo tabia ya dhuluma ya mali ya wana Mtwara siyo nzuri. Tumeona dhuluma ya aina hiyo kwenye ziwa Victoria na kuacha wakazi wa kanda ya ziwa wakila mapanki badala ya minofu ambayo mnaipeleka Ulaya.

Wananchi wa North Mara wameambulia kuchafuliwa maji yao ya kunywa kwa kemikali za sumu na kuwasababishia madhara ya ngozi na hata vifo. Mifugo na mazingira ya eneo hilo imeathirika. Sumu pia inaendelea kutishia uhai wa vizazi vya maeneo hayo. Mashimo ndiyo wanayoachiwa wakazi wa Mkoa wa Mara. Acha Vifo vya kupigwa risasi, kuhamishwa na dhuluma lukuki.

Acha wale wakazi wa Geita Mwanza, Bulyahulu na Mwadui Shinyanya na Mererani Arusha, nao wanasota kwa umaskini uliokithiri. Licha ya kuwa na neema ya madini wameishia kuishi katika migogoro, kuhamishwa, vifo na umaskini uliokithiri.

Wana-Mtwara, msimamie msimamo wetu, tunawaunga mkono.


JAMII FORUMS

No comments: