Tuesday, January 22, 2013

MTWARA ILIPOTOKA, IPO WAPI NA INAELEKEA WAPI.Na EMT,
Nilikuwa nasoma kitabu kilichoandikwa na Michael Longfold kiitwacho “The Flag Changed at Midnight: Tanganyika’s Progress towards Independence.” Katika kitabu hiki, Michael Longfold anaelezea ushuhuda wake wa macho kama mfanyakazi (District Officer) wa utawala wa kikoloni katika miaka 10 ya mwisho kabla ya Tanganyika kupata uhuru.


Michael Longfold alifanya kazi sehemu mbalimbali Tanganyika zikiwemo Iringa na Rungwe kabla ya kuhamimishiwa Mtwara kuwa Staff Officer wa Kamishna wa muda wa Southern Province (Jimbo la kusini lililojumuisha Lindi na Mtwara). Kitabu kina jumla ya kurasa 572. Hata hivyo, ningependa, ku-share Sura ya Nne yenye kichwa “Southern Province” hasa kutokana na yanayoendelea Mtwara hivi sasa.

Wapo ambao hawapendi kujua yaliyopita, lakini kwa hili suala la gesi nadhani siyo vibaya kutakafari Mtwara ilitoka na kujiuliza ilipo sasa na inaelekea wapi. Hii itasaidia kujua kama Mtwara iko kwenye mkondo mzuri. Kitabu kimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza; nitajitahidi kuelezea hiyo ibara ya nne kwa Kiswahili kadri ya uwezo wangu kwa faida ya wengi.

Waliosoma historia watakumbuka kuwa hadi mwaka 1953, makao makuu ya Southern Province (kwa sasa Kanda ya Kusini) yalikuwa Lindi. Makao makuu ya mji wa Mtwara yalikuwa Mikindani. Bandari mpya na yenye kina kirefu ilikuwa imeshajengwa Mtwara na mji mpya ulikuwa unaandaliwa chini ya ramani nzuri kabisa ambayo iliruhusu mji kupanuka siku za usoni.

Mpango wa kujenga mji wa Mtwara kama bandari kubwa kusini mwa Tanganyika ulikuwa sehemu ya mpango mzima wa kilimo cha karanga. Mpango huu ulianzishwa na serikali ya Labour ya Uingereza iliyoingia madarakani mwaka 1945 chini wa Waziri Mkuu, Clement Attlee.

Baada ya kuingia madarakani, serikali ya Clement Attlee ilipitisha sheria mbalimbali (ambazo ni maarufu sana nchini Uingereza hadi leo) ili kukabiliana na matokeo ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mojawapo ni ile sheria (National Health Service Act) iliyoanzisha huduma ya afya kwa taifa (National Health Service, kwa kifupi, NHS). Sheria hii iliwawezesha Waingereza kupata huduma ya afya bure mpaka leo.

Tatizo lingine ambalo serikali ya Clement Attlee ilitaka kulitatua ni utapiamlo uliosababishwa na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Baada ya vita kulikuwa na ukosefu wa vitu kama mafuta ya kupikia. Mwaka 1946 serikali yake iliamua kupitisha mpango ambao ulihusisha hekari milioni tatu za ardhi ya Tanganyika ambayo ingetumiwa kwa ajili ya kilimo cha karanga ili kupunguza tatizo la ukosefu wa margarine fats, moja ya mafuta ambayo yangesaidia kutatua tatizo la utapia mlo Uningereza.

Mwaka 1948 serikali ya Clement Attlee ilipitisha sheria ambayo siku hizi imesahaulika kabisa kwenye vitabu vya sheria. Sheria hii iliitwa Overseas Resources Development Act 1948. Sheria hii ilianzisha Shirika la Chakula la Nje (Overseas Food Cooperation), kwa kifupi OFD.

OFD ilipewa mtaji wa kuanzia wa Pounds milioni 50 na kuanza rasmi mpango wa kilimo cha karanga mwaka 1948. Kutokana na umuhimu wa mpango huu, haukusimamiwa na ofisi ya makoloni bali wizara ya chakula. Aliyeusimamia mpango huu alikuwa generali wa jeshi.

Baada ya kufanya majaribio ya kilimo cha karanga sehemu mbalimabli Tanganyika kama Kongwa na Urambo, OFD iliona kuwa zao la karanga lingeweza pia kustawi Nachingwea. Pia reli ilijengwa kwa ajili ya kusafirisha karanga kwenda bandarini Mtwara. Uingereza ilitarajia kuvuna tani 400,000 za karanga kwa mwaka na kuzisafirisha nje kwa ajili ya kushughulikia tatizo la utapiamlo.

Lakini mpango mzima wa kilimo cha karanga Nachingwea ulikumbwa na matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na taratibu mbaya za mipango, ukaguzi wa hesabu na marejesho. Kwa mfano, walijenga bandari yenye kina kirefu lakini baadae wakaja kugundua kuwa maji yalikuwa na kemikali zenye madhara kwa boilers za meli.

Muhimu zaidi, wakati mpango wa kilimo cha karanga ulipokufa mwanzoni mwa miaka ya 1950, iligundulika kuwa kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha na zana za kilimo yaliyosababishwa na usembe na rushwa. Kwa mfano, matrekta yalikuwa yanapotea ovyo Nachingwea, sehemu ambayo haikuwa na watu wengi wala barabara nzuri.

Kwa hiyo, kilimo cha karanga kikafa rasmi mwaka 1950-1951 baada ya wizara ya chakula kuachana na huo mpango na nafasi yake kuchukuliwa na ofisi ya makoloni. OFC nayo ilikufa rasmi mwaka 1954 baada ya kubadilishwa na kuwa Shirika la Kilimo Tanganyika (Tanganyika Agricultural Corporation aka TAC).

Waliopanga mpango mzima ya kilimo cha karanga ni kama vile walikuwa wanaishi maisha ya ndotoni. Of course, wapo wachache ambao walikuwa na matumaini kuwa mpango huo ungefanikiwa. Hata hivyo, mpango wa kilimo cha karanga uliajiri wataalamu wengi kutoka Uingereza ambao walikuwa na nia tuu ya kunyonya mali za wenyeji tena bila ridhaa yao.

Hawakuonyesha kabisa moyo wa kutaka kuiendeleza South Province na watu wake. Wananchi wa maeneo husika hawakushirikiswa kabisa wakati kilimo cha karanga kilipoanzisha kilimo. Hii ilisababisha kuvunjika kwa uhusiano uliokuwepo kati ya watawala wa Kiingereza na Waafrika na Waasia. Mtwara ni mfano wa jinsi kilimo cha karanga kilivyokufa. Zipo pia historia mabaya ya kilimo cha karanga Kongwa na Urambo.

Mwanzoni, mji wa Mtwara ulikuwa umepangwa kusaidia maelfu ya wakazi wake hapo baadae na pia kuvutia wakazi wapya. Waingereza walikuwa na mpango wa kujenga mji maarufu wenye vitu kama maktaba, sehemu za kuombea, shule, hospitali, kumbi za sinema, n.k. Lakini mipango yote hii iliwekwa kapuni baada ya kuanguka kwa kilimo cha karanga.

Inakaridiwa kuwa mwaka 1954 Mtwara mjini ilikuwa na wazungu 100, Waasia 50 na Waafrika 700. Wazungu wengi walikuwa wameajiriwa serikalini na hawakuwa na mpango wa kuishi Mtwara baada ya kustaafu. Walikuwepo pia Waafrika wachache waliokuwa wameajiriwa serikalini lakini wengi wao walikuwa wametokea nje ya Mtwara na walikuwa hawana mpango wa kuishi Mtwara.

Waasia walikuwa wamejikita zaidi kwenye biashara ya maduka baada ya kushawishiwa kuwa wangekuwa matajiri haraka kama wangeanzisha biashara Mtwara. Hata hivyo, wafanyabiashara wengine walikuwa makini zaidi na kuogopa kuomba vibali vya kumiliki ardhi.

Kimsingi, kuanguka kwa mpango mzima wa kilimo cha karanga Mtwara, ambao uligharibu fedha nyingi, kuliharibu sana heshima ya Uingereza kimataifa kama nchi iliyopewa mamlaka na Umoja wa Mataifa kuindaa Tanganyika kupata uhuru.

Pia utawala ya kikoloni ulikuja na mpango wa kuhamisha makao makuu ya Mtwara kutoka Mikindani kwenda Mtwara mjini ya sasa bila ridhaa ya wananchi. Wananchi wa Mtwara waliupinga sana mpango huo kwa madai kuwa hawakushirikishwa kabisa. Maamuzi ya kulifunga boma la Mikindani yalitoka Dar Es Salaam, na siyo Mtwara.

Mwandishi anasema alibahatika kulipitia faili ambalo lilikuwa na nakala ya barua ya uamusi wa kuhamisha makao makuu ya mji na kukuta malalamiko mengi ya kimaandishi kutoka kwa wakazi wa Mikindani lakini hakuna aliyehangaika kuwasikiliza.


JAMII FORUMS

No comments: