Monday, January 28, 2013

KUSHINDWA KWA SERA ZA CCM, CHANZO CHA MIGOGORO YA KITAIFA

Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,
SERA za Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeshindwa na zimeshindwa si kwa kukosa watekelezaji wazuri bali zimeshindwa kwa sababu ni sera mbaya ambazo zimegeuka kuwa janga la kudumu la Taifa.

Sera hizi katika ujumla wake ndizo chanzo, kiini, na sababu ya kudumaa kwa maendeleo nchini na ndizo chanzo kikuu cha umasikini Tanzania. Sera hizi ambazo zimejaribiwa kwa miaka 50 na zaidi sasa zimethibitisha kitu kimoja tu – kushindwa kwake.

Sera ya CCM kuhusu maji imeshindwa; sera ya CCM kuhusu elimu imeshindwa ; sera ya CCM kuhusu nishati imeshindwa; sera ya CCM kuhusu madini imeshindwa; sera ya CCM kuhusu gesi imeshindwa; sera ya CCM kuhusu ulinzi wa rasilimali za asili imeshindwa; sera ya CCM kuhusu ulinzi na usalama imeshindwa; Sera ya CCM kuhusu Usalama wa Taifa imeshindwa. Kwa kila kipimo sera zote za CCM zimeshindwa na hakuna iliyofanikiwa.

Heri ya mwaka mpya mpendwa msomaji

Watanzania inawapasa kuanza kutambua na kukubali ukweli ulio dhahiri mbele yao kuwa matatizo yao mengi na yale ambayo wanayaona sehemu nyingine nchini yanatokana na ubovu wa sera za CCM.

Ni sera hizi ndizo ambazo matokeo yake tunayaona katika jamii yetu. Matokeo hayo yameonekana na yanaendelea kuonekana kwa uzito zaidi huko Mtwara ambako wananchi wa Mtwara wakiwa wamefunguliwa kifikra wameamua kusimama dhidi ya chama chao ambacho kwa miaka karibu 50 wamekuwa wakikichagua, kukitetea na kukipigia sifa. Sasa hivi wametambua kuwa wasipoangaliia sera za CCM zitaendelea kuwadumaza na sasa wameamua kukataa.

Tunachoshuhudia Mtwara ni uthibitisho wa kile ambacho wengine tumekisema kwa miaka sasa – sera za CCM ni tatizo la msingi kwa mustakabali wa Taifa. Mtwara, Lindi, Kigoma, Manyara, Katavi, Rukwa, Singida na kwa kweli jumla ya mikoa yote mingine sera za CCM zimekuwa ni kiini cha matatizo ya maendeleo.
Tatizo hili la sera za CCM ni kuwa msingi wake ni mbaya, mapendekezo yake ni mabaya na zimetengenezwa zikiacha misingi ya Taifa. CCM imetengeneza utegemezi mbaya kabisa katika sera zake.

Kutegemea uwekezaji kutoka nje kama msingi wa maendeleo

Tatizo kubwa la sera za CCM ni kuwa zimetengenezwa kutokana na kutegemea misaada ya nje na uwekezaji wa nje. Zimeacha tunu ya msingi ya Taifa – yaani kujitegemea. Leo neno “kujitegemea” halisikiki tena katika kauli za viongozi wetu kwa sababu hawawezi tena kuzungumzia kujitegemea kwani wameacha jambo hili.

Leo hii sera za CCM zinategemea ‘wafadhili’ na wale ambao wanawaita “washirika wa maendeleo”.

Utegemezi huu umerasmishwa kiasi kwamba viongozi wa CCM hawawezi kufikiria maendeleo bila kufikiria wawekezaji kutoa nje. Hii ndiyo maana Rais Kikwete mwenyewe aliwahi kunukuliwa huko nyuma akisema kuwa bila wawekezaji hatuwezi kuendelea. Huu siyo utegemezi wa fedha tu bali ni utegemezi wa kifikra.

Matokeo ya utegemezi huu ni kuwa wageni wanapewa kipaumbele, wanatengenezewa mazingira ya kunufaika na rasilimali zetu na wanafanya hivyo wakati mwingine na kiburi juu.

Wawekezaji hawa wa kigeni wamefika mahali wanaweza kuweka ngumu na kupiga mkwara serikali kuwa ikibadilisha sera zake basi watakimbia na serikali inawapigia magoti! Leo hii miaka karibu saba baadaye ahadi za kupitia mikataba na kuiboresha zimebakia kuwa ahadi zisizotekelezeka na badala yake serikali ya CCM imeacha makampuni ya madini kukubali mapendekezo mapya kwa hiari yao na pale inapokuja sheria uhuru mkubwa bado umewekwa kwa makampuni kukwepa.

Kutegemea fedha kama msingi wa maendeleo

Mojawapo ya mambo mabaya kabisa ambayo ni matokeo ya sera hizi mbovu za CCM ni kutegemea fedha kama msingi wa maendeleo. Kosa hili lilifanywa mara baada ya uhuru lakini Nyerere – Baba wa Taifa – alilitambua hilo mara moja na katika kutangaza Azimio la Arusha alitangaza ukweli ambao ulikuwa yakini wakati ule kama ulivyo leo hii.

Azimio la Arusha lilisema hivi kuhusu kutegemea fedha kama msingi wa maendeleo: “Lakini ni dhahiri kwamba tumefanya makosa katika kuchagua silaha; kwani silaha tuliyochagua ni fedha. Tunataka kuondoa unyonge wetu kwa kutumia silaha ya wenye nguvu, silaha ambayo sisi wenyewe hatuna. Katika mazungumzo yetu, mawazo yetu, na vitendo vyetu ni kama tumekata shauri kwamba bila fedha mapinduzi yetu hayawezekani. Ni kama tumesema, “Fedha ndiyo msingi wa maendeleo. Bila fedha hakuna maendeleo”

Na Azimio la Arusha kama likitoa mashtaka miaka karibu hamsini iliiyopita likasema hivi “Viongozi wa TANU mawazo yao ni kwenye fedha. Viongozi wa Serikali, wanasiasa na watumishi, mawazo yao na matumaini yao ni kwenye fedha. Viongozi wa wananchi na wananchi wenyewe katika TANU, NUTA (ilikuwa chama cha wafanyakazi), Bunge, UWT., Vyama vya Ushirika, TAPA (kilikuwa chama cha wazazi) na makundi mengine ya wananchi, mawazo yao na maombi yao na matumaini yao ni FEDHA. Ni kama wote tumekubaliana na tunasema kwa sauti moja, “Tukipata fedha tutaendelea, bila fedha hatutaendea.”

Hivi ndivyo yalivyouwa mawazo ya viongozi wakati huo; je sivyo ilivyo sasa kweli? Si leo hii tunawasikia wakiulizia pesa zaidi huko Bungeni; leo wametengeneza kitu kinaitwa “mfuko wa maendeleo wa Jimbo”; na zipo akaunti za Halmashauri kwenye majimbo hayo na kila siku kuna fedha zaidi inatolewa. Kwanini hatujaona mabadiliko makubwa basi ya maendeleo?

Leo viongozi wa CCM wanaangalia fedha kama msingi wa maendeleo na bila haya wala soni utawasikia wanasema “tunatafuta wafadhili” au “serikali haina fedha”! Mwanzo na ukomo wa upeo wa mawazo yao kuhusu maendeleo ni fedha.

Lakini kushindwa kwa sera za CCM ni zaidi ya kutokana na kutegemea fedha; kushindwa kwa sera zake kunatokana na ubovu wa ndani wa sera hizo (intrinsic deficiencies).

Yaani, hata ukiwapa mabilioni ya fedha kila siku matokeo ya sera hizo bado yatakuwa mabaya. Ikumbukwe kuwa tatizo la maendeleo Tanzania si ukosefu wa fedha bali ni upotofu wa sera. Ukizisoma kwa juu juu sera za CCM unaweza kufikiria ni sera nzuri na kweli inasikitisha wapo watu – wengine wana dalili ya usomi – ambao wanaaini sera za CCM ni nzuri “ila zimekosa watekelezaji”.

Wanafikiria kuwa kama akija mtekelezaji mzuri wa sera za CCM basi ubora wa elimu utapanda, umeme utakuwa mwingi na wa ziada, miji yetu itakuwa ya kisasa n.k. Ukweli hata wajipange wana CCM elfu wenye kusifiwa kwa uwezo na hata wakipata watu kutoka nje hawataweza kuharakisha mabadiliko kwa sababu moja – sera zao ni mbaya.Jukumu la Upinzani ni kuonyesha ubovu wa sera za CCM

Kati ya vitu vinavyoniudhi na kunikera sana na nimeshaandika hapa mara nyingi ni hii tabia ya viongozi (baadhi yao angalau) wa chama kikuu cha upinzani nchini Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujaribu kutoa mawazo ya kuishauri serikali iwasikilize.

Mara nyingi nakwazika na kukata tamaa ninaposikia viongozi wa CHADEMA wanaililia serikali eti ‘ifanye hivi au vile vinginevyo”. Hata kwenye suala la Mtwara nasikitika kuwasikia viongozi wa upinzani wakiibembeleza serikali ya CCM “iwasikilize wananchi wa Mtwara”.

HIvi, kama serikali ya CCM ikitaka kusikia mnafikiri haiwezi kusikia? Ina wakuu wa wilaya, ina wakuu wa mikoa, ina mameya, ina madiwani maelfu n.k na ina vyombo vyote vya dola; inaendesha kila idara ya serikali kuu, na kwa kweli kabisa ndio wanamtandao mkubwa zaidi ya kujua nini kinaendelea nchini. Hivi kama wangetaka kusikia ya Mtwara si wangesikia?

Wapinzani wanapojitahidi kuibembeleza CCM isikilize ni kana kwamba wao wapinzani wanaamini kuwa sera za CCM ni nzuri na kuwa CCM ianze kuzitekeleza. Kama kuna mpinzani anaamini kuwa anaweza kuzitekeleza sera za CCM vizuri zaidi kuliko wana CCM wenyewe kwanini asiende kujiunga nao huko ndani ili wampe nafasi ya kuzitekeleza. Si kina Wassira walikuwa upinzani na wakarudi CCM na wakapewa nafasi ya kuzitekeleza sera za CCM? Leo anaweza kutamba kuwa kazitekeleza?

CHADEMA iachane na kubembeleza serikali. Ianze mara moja na daima kuonyesha kwa wananchi ubovu wa sera za CCM, ioneshe kuwa matatizo yanayotokea nchini kiutawala na kiutendaji yanatokana na ubovu wa sera hizo na licha ya kuonyesha ubovu wa sera hizo ifike mahali ionyeshe sera zake na tofauti kati yake na zile za CCM na kwanini wananchi waamue kuiunga mkono zaidi si kwa sababu wanaichukua CCM bali kwa sababu wameamini kuwa sera za CCM mbaya na za CHADEMA ni nzuri na bora zaidi.

Kwa bahati mbaya katika zoezi hili CHADEMA imeshindwa na kuna dalili kuwa itaendelea kushindwa na wananchi wataendelea kuamua kuwa ni bora sera mbovu wanazozijua na walizozizoea kuliko sera nzuri wasizozijua.

Hatuwezi kuwalaumu wakiendelea kuichagua CCM hadi wapewe sababu ya kutosha ya kwanini waachane na CCM, na sera zake, na ahadi zake, na mipango yake na mambo yake yote.

RAIA MWEMA

No comments: