Wednesday, January 23, 2013

KELELE ZA GESI NA HADITHI YA DOWANS


Na Mayage S Mayage,
MAKALA yangu ya wiki iliyopita iliyobeba kichwa cha habari; Gesi Mtwara sawa, maji ya Morogoro? imeniwezesha kupata hasia halisi za Watanzania wenzangu, na hasa wana wa mikoa ya kusini mwa nchi yetu, kwa maana ya Mtwara na Lindi. Wasomaji wangu walionipigia simu moja kwa moja, kutuma ujumbe mfupi (sms) na wengine kuniandika kupitia mtandao wa e-mail, kwa hakika kabisa, wengi wao wameonyesha kuwa na uchungu mkubwa na rasilimali za nchi yao.

Kama ilivyo ada, wapo waliokubaliana na mawazo yangu na kunipongeza; wapo pia waliopingana na mawazo yangu na kisha kunimiminia matusi. Wote hao nawashukuru kwa kutenga muda wao na kupitia makala yangu hayo, na kisha kunipa mrejesho wao uwe chanya au hasi. Imani za dini yangu ya kimapokeo, inanifundisha kwamba mawazo na matendo ya malaika, muda wote ni sahihi. Lakini mawazo na matendo ya mwanadamu yanaweza kuwa sahihi au yakawa na kasoro, na huo ndio ubinadamu wenyewe. Hakuna mwanadamu aliye mkamilifu kwa kila jambo.

Binadamu yeyote makini, anayesimama katika msingi wa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu, unapoibuka mjadala wa kitaifa na unaogusa hisia za watu walio wengi kama huu wa sasa wa ‘gesi ya Mtwara,’ inampasa kuweka jazba pembeni na kuongozwa na busara zaidi, hata kama kiwango chake cha busara hakitoshelezi hata kwa pishi la mchele. Mjadala wa ‘gesi ya Mtwara’ hata ukiendelezwa kwa miaka 100, hautapata mshindi. Kitakachopatikana ni muafaka wa maridhiano. Kupata na kukosa!

Ni kutokana na msingi huo, Wachina walikuja na msemo wao wa kwamba ‘wacha mamia ya maua yachanue, na lile litakaloweza kustahimili misimu yote ya mabadiliko ya hali ya hewa, ndilo litakalokuwa ua bora miongoni mwa mamia ya maua hayo! Mijadala inayogusa hisia za kijamii, haizimwi kwa nguvu. Busara ni kuacha mijadala hiyo ishamiri, na mwisho wa siku mwafaka wenye maridhiano ya kupata na kukosa, utapatikana tu!

Makala haya ya leo yanaendelea na mjadala wa gesi. Nafanya hivyo kwa sababu zile zile. Ni mjadala unaogusa hisia za wengi. Tatizo la Tanzania, limekuwa ni taifa la wajuaji. Wapo baadhi yetu, wanadhani viongozi wetu ni wajinga kiasi kwamba hawayajui madhara au athari zitokanazo na kugundulika kwa hazina kubwa ya gesi ndani ya nchi yetu, kama ilivyo kwa baadhi ya watawala wetu kudhani kwamba wananchi hawajui madhara au athari zitokanazo na kugundulika kwa maliasili hiyo ya gesi.

Ni katika ujuaji huo, mmoja wa wasomaji wangu aliniandikia sms akisema wao, wananchi wa Mtwara, hawataki gesi ipelekwe Dar es Salaam kwa kuwa nchi hii inaongozwa na majizi. Ujuaji wa mtu huyu, haumtumi kwamba hata kama mtambo wa kusafisha gesi na mitambo ya kufua umeme itajengwa Mtwara, mjengaji na msimamizi mkuu wa miradi hiyo ni Serikali hii hii ya mijizi. Kujengwa Mtwara, hakutampa fursa mjuaji huyo kusimamia mapato yatokayo na gesi hiyo ili yasiporwe na hao anaowaita majizi!

Baadhi ya wasomaji wangu na baadhi ya wanaoshiriki mjadala huu wa gesi, kutokana na dhana hiyo ya ujuaji, wamekuwa wakitolea mifano ya migogoro ya mafuta katika maeneo ya Niger Delta na Sudan kusini kana kwamba wao pekee ndio wanaojua jinsi migogoro hiyo ilivyoathiri jamii za maeneo hayo kuliko Profesa Sospeter Muhongo, Eliackim Maswi na viongozi wetu wengine serikalini.

Ndugu zangu, tunapojadili masuala muhimu yanayohusu uchumi wa nchi yetu, ni muhimu kufahamu ukubwa wa vita ya kiuchumi ilivyo leo duniani. Kampuni iliyopewa kazi ya kutandaza mabomba ya gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni ya Kichina. Fedha za mradi huo, zimetoka China. Lakini tunajua vita ya kiuchumi inayoendelea kati ya mataifa makubwa ya magharibi na mashariki. Tunajua kasi ya kukua kwa uchumi wa China inavyoyatikisa mataifa ya Magharibi. Kwa hiyo, taarifa za mradi mkubwa kama huo wa gesi kukabidhiwa kwa taifa la China, haziwezi kuyafurahisha mataifa ya magharibi.

Hiyo ni vita ya nje. Tunayo vita ya ndani pia. Kuna kampuni hapa nchini ambazo tayari zimewekeza mamilioni yao ya fedha katika miradi ya umeme wa dharura. Mitambo yao inatumia mafuta mazito. Habari za kugundulika kwa gesi itakayotumika kuzalisha umeme, kamwe haziwezi kuwafurahisha. Watafanya kila wawezalo kukwamisha mradi huo.

Kuna kampuni za kufua umeme uwe kwa kutumia mafuta au gesi, ambazo mikataba yao ni ya kuiuzia TANESCO umeme. Habari kwamba Serikali sasa, kupitia TANESCO imeamua kujenga mitambo yake pale Kinyerezi yenye uwezo wa kuzalisha megawati 690 na mtambo mwingine kule Somanga Fungu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 320 za umeme, haziwezi kuzifurahisha kampuni ambazo zilikuwa zinachuma fedha TANESCO kupitia ‘dili’ za kuuza umeme, ziwe zimezalisha au la!

Kwa hiyo, katika mazingira yote hayo, upo umuhimu mkubwa wa kuchukua tahadhari kubwa, kwa sababu, pengine kelele hizi za gesi, gesi, gesi, gesi kila kona zinaweza kuwa zinachochewa na vita hiyo ya kiuchumi ya ndani na nje kwa kuwatumia Watanzania wenzetu ambao wanatumika, pengine bila kujijua. Huko nyuma tuliwahi kuambiwa kwamba Serikali isiponunua mtambo wa Dowans, basi nchi itaingia gizani. Baadhi yetu, tulisema wakati ule kwamba kauli ile haikuwa kauli ya waliyoitoa. Ilitokana na nguvu fulani ya wakubwa. Wakubwa hao wangalipo bado hadi leo!

Tukubaliane sote, hata kama ni kwa shingo upande, gesi ya Mtwara isafirishwe kwa bomba hadi Dar es Salaam kwa ajili ya soko kubwa la gesi na kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika. TANESCO izalishe umeme kiasi cha megawati 690 katika mitambo yake ya Kinyerezi na pia megawati 320 katika mitambo yake ya Somanga Fungu, sawa na megawati 1,100.

Kiasi hicho cha umeme, kikijumuishwa na kingine kutoka vyanzo vingine, adhima ya Serikali ya kuwa na megawati 2,780 kufikia mwaka 2015 na hivyo mgawo wa umeme kubakia historia katika nchi hii, itakuwa pigo kwa mafisadi! Huko nyuma mafisadi waliratibu mgawo wa umeme, wakaifikisha Serikali kwenye kona ya kufikiria umeme wa dharura tu. Hilo halipo tena, Serikali walau imezinduka, imewasitukia mafisadi! Imesema hakuna mgawo, na kweli hakuna.

Kwa hiyo, tuishauri Serikali namna bora ya rasilimali gesi asili inavyoweza kuwasaidia kiuchumi wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla wao. Tuishauri bila jazba, tuishauri iachane na lugha za jumla jumla. Kwa mfano, Serikali inasema imepunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wakazi wa Mtwara. Sawa, lakini huyu mwananchi anayepunguziwa gharama ana kiwango gani cha umasikini?

Tunao Watanzania wenzetu wanaoishi kwenye nyumba za mbavu za mbwa. Ni nyumba za udongo na nyasi. Sheria na masharti ya umeme, yanawabagua watu hawa. TANESCO inasema haiwezi kupeleka umeme kwenye nyumba za nyasi kuanzia chini hadi juu! Masikini huyu Serikali inamsaidiaje kuondokana na nyumba zao hizo ili nao wafaidike na umeme wa gesi yao? Mfuko Maalumu wa gesi uwatafute hawa, uwasaidie kuondokana na nyumba zao hizo ili nao wafaidi rasilimali ya nchi yao.

Kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Gaddafi, pamoja na vikwazo vyote vya kiuchumi vya karibu miongo miwili alivyowekewa na jumuiya za kimataifa, aliweza kutumia rasilimali ya mafuta ya nchi hiyo kuwapa makazi bora, huduma bora za afya na elimu wananchi wake. Sisi hatuna vikwazo vya kiuchumi, tunakopesheka bado. Hawa masikini kabisa kabisa hawa, wasaidiwe kutoka hapo walipo.

RAIA MWEMA

No comments: