Monday, January 21, 2013

GASI ASILIA: HIVI NI NINI HASWA?Na Hassan Samli,
Giza linaendelea kutanda mingoni mwa Wananchi wa Mikoa ya Kusini hasa Lindi na Mtwara kuhusu mgogoro wa gesi kwenda Kinyerezi. Wengi, wakiwemo Wanasiasa wandani ya Mikoa hii na hata nje wamekuwa wakijiuliza nini hasa kiini cha mgogoro huu; Je! Ni ubinafsi wa Wananchi wa Mikoa hii kutaka kujilimbikizia rasilimali zao peke yao? Ni shinikizo la wanasiasa kujitafutia umaarufu? Maslahi ya nchi kama inavyodaiwa na viongozi wa Serikali? Au ni Ubinafsi wa wachache, hasa Raisi Kikwete kama inavyodhaniwa na wengi wa Wananchi?


Inaaminika kwamba, Wananchi wa Mikoa hii wanachokidai si rasilimali gesi kutotumika kwa maslahi ya Kitaifa la! Bali wanasema kutolewa gesi ambayo ni ghafi (ambayo haijachakachuliwa) ni sawa na kuondoa fursa za Viwanda ambavyo ni nyenzo kubwa na muhimu katika upatikanaji wa ajira ambayo nayo ni kilio chao cha muda mrefu. Wanasema, Nchi hii hujiendesha kwa kodi na makato mbalimbali kutoka katika rasilimali na vyanzo vingine. Na hivyo, gesi hiyo hata ikichakachuliwa Mtwara au popote pale nchini bado Serikali itajivunia jambo hilohilo (kodi na makato) na si kingine zaidi jambo ambalo pia linawezekana na linafanyika hata leo kwa rasilimali ambazo ziko Mikoa hiyo na mingine.

Baadhi ya watu wamekuwa wakisema ya kwamba, Wananchi hawa wamelazimika kupingana na jambo hiyo kutokana na kushindwa kwa Serikali inayotawala kuwaletea wananchi maendeleo na wakadiriki hata kutolea mfano wa baadhi ya maeneo ambayo rasilimali zao zimetumika hovyo bila watu hao kuendelezwa chochote; hasa wanataja maeneo yenye migodi ya madini na mbuga za wanyama. Wengine wanasema eti ni kutokakana na hali mbaya ya umasikini wa wananchi ambao umewafanya wakate tamaa ya mstakabali wa maisha yao na kujiona eti kwamba mikoa hii imetengwa katika mipango ya maana ya maendeleo ya nchi hii. Mh! Sinahakika!


Lakini nilichoka zaidi nilipoambiwa haya maneno, eti kwamba; “Raisi kikwete ameonesha kuwa MBINAFSI, kwani kila kitu analazimisha kiende kunufaisha kwao…”. Hapa walitolea mfano namna yeye anavyojenga viwanda hasa maeneo ya KIBAHA na BAGAMOYO, eti kusema kuanzia mwaka 2010 amejenga viwanda zaidi ya vinne katika mji wa Kibaha. Hivi ni kweli haya? Mlioko huko Kibaha mtatujuza. Mwingine akasema, “We Bro. hebu fikiria, bandari ya Bagamoyo iliwashinda Wakoloni na ndio maana ule mji ukahamishiwa Dar es Salaam maana ile sehemu huwa inajaa mchanga kila kukicha, lakini leo hii Mheshimiwa kwa kuwa ni kwake anataka iwe na isiwe, IJENGWE TU. Kwanini asiendeleze Bandari zilizopo kuliko hiyo ambayo hata hivi VIDAU VYETU huwa inakuwa shida kutia nanga?” Mifano ikawa ni miingi hapa, lakini huyu akasema; “Kaka, umesikia kujengwa kwa Barabara ya Msata Bagamoyo na kuhamishwa kwa Kituo cha Mabasi cha Ubungo, lakini pia kubadilishwa kwa ruti za magari yaendayo Mikoa ya Kaskazini, Kati na Nyanda za Juu Kusini? Kwamba, magari yooote sasa ni lazima yapitie Bagamoyo hadi Msata ndipo yatafute wapi yanapaswa kuelekea. Je huu nao si ufisadi?” Mh! Hapo napo nikakosa majibu.

Swali la mwisho nililoulizwa ni kuhusu kutokamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kusini, kipande cha Kilomita 60 maeneo ya Nyamwage. Mmoja aliniuliza; “Hivi wewe na akili zako, kilomita 60 na kutandika bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar, kipi chenye kuhitaji muda mwingi? Iweje huyo unayemuita raisi wako ashindwe kukamilisha kipande hicho zaidi ya miaka 8 sasa na atake bomba la gesi litandazwe kwa miezi 18? Aache uhuni, nyie wasomi kama hamtaki kuungana na sisi basi tuacheni na umasikini wetu tutafia hapahapa na umasikini wetu na GESI HAITOKI NG’O!”.

Mundu wangu, hapa nilikosa majibu lakini pia nilishituka kidogo. Kwanini ameniita msomi, inamaana wasomi ndo miongoni mwa wale wanaoshinikiza gesi iende Dar au?! Pengine ni kutokana na kauli za viongozi wetu kuwa wanaodai gesi ibaki ni MAMBUMBUMBU WASIOSOMA, ambapo napo hapo sina hakika saaana, maana naona hata wenye SHAHADA; kama Mheshimiwa wetu Mkuu wan chi nao wamo mule.


Ila iwe isiwe, bado Serikali inawajibu wa kujitafakari upya kuangalia nini hasa na wapi nchi yetu inaelekea. Mgogoro huu uko mwanzoni kabisa lakini hali inaonekana kuwa ni tete sana, sijuwi itakapofikia ikalazimishwa kweli mtaro ukaanza kuchimbwa, ni nini kitatokea? Sijuwi!

Serikali ijitafakari upya kwani nimesikia miongoni mwa Wabunge wa Kusini wakilaumiana kwamba; mara tu baada ya Baraza la Mawaziri kuridhia mkataba huu, wao (Wabunge) walipaswa kuja kuwaelimisha Wananchi juu ya mradi huu, kitu ambacho hawakufanya. Kwa mantiki hiyo, inaonesha wazi kwamba Wananchi hawakushirikishwa katika mchakato huo mbali ya baadhi ya WATAWALA kudai kuwa tayari Wananchi wameridhia.

Tujitafakari upya, kwani kama umeme umeweza kutolewa KIDATU, NYUMBA YA MUNGU, MTERA na kwingineko hadi Dar es Salaam, iweje leo ishindikane kutolewa Mtwara hadi huko? Labda kuwe na hoja nyingine.

Lakini pia tutafakari juu ya kauli zetu viongozi za hapo awali, namna tulivyokuwa tunawaahidi wananchi hawa kuhusu gesi, lakini pia mikakati na mikataba ya mwanzo kabisa ya uendelezwaji wa nishati hii hasa wakati wa ARTUMAS, ambapo katika nyaraka zake waliita “Commercialization Opportunities” Fursa za Kibiashara). Ambapo katika kutaja fursa hizo, fursa namba mbili ilikuwa; “Construction of a large-scale power generation facility in Mtwara and a high-voltage transmission line linking the power plant to the Tanzania integrated power grid” (Yaani, ujenzi wa MTAMBO MKUBWA wa uzalishaji wa umeme Mtwara na KUTANDAZA NYAYA ZENYE KUSAFIRISHA UMEME MWINGI ili kuunganisha kwenye chanzo cha umeme wa gridi ya Taifa -- na hapa walimaanisha KIDATU).

Lakini pia katika mipango yao ilionesha kile walichokiita; “A proposed 300 MW generation plant would be fuelled by natural gas from Mnazi Bay, and would link Mnazi Bay/Mtwara to the East Africa Integrated power grid, encompassing Tanzania, Kenya and Uganda” (kwamba, Kunategemewa kujengwa mtambo wa kuzalisha umeme wa Megawati 300 ambao utatokana na gesi ya asili ya MNAZI BAY ambapo itaunganishwa kutoka Mnazi Bay/Mtwara hadi kwenye gridi yenye kuunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda).

Je! Haya mazuri yote mbona yalifikiliwa na ARTUMAS kwa kutokea Mtwara na hata kufikia kunufaisha nchi zingine za Kenya, Uganda na Kwingineko? Iweje leo jambo hilohilo lishindwe kulinufaisha Taifa hili?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki WATANZANIA.

Hassani Samli,
+255717340671


CHANZO: WAVUTI

No comments: