Friday, January 4, 2013

DENI LA TANZANIA LAFIKIA 22 TRILIONITAASISI isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya Madeni ya Taifa na Maendeleo (TCDD), imesema kitendo cha Serikali kukopa fedha kwa ajili ya matumizi yasiyo na umuhimu pamoja na kuwalipa watumishi wake mishahara, kimesababisha taifa kuwa na deni la Sh22 trilioni.


Imesema hali hiyo ni hatari hasa ikizingatiwa kuwa miaka kadhaa iliyopita, Tanzania kupitia Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC), ilifutiwa kiasi kikubwa cha madeni , lakini sasa imeanza kukopa tena.

Taasisi hiyo pia imesema kitendo hicho kimechangia kuporomoka kwa uchumi wa taifa kwa sababu mikopo hiyo ina riba kubwa.

Imeeleza kuwa Serikali inakopa fedha hizo Benki Kuu (BoT), Benki za Biashara, Kampuni za Bima na Mashirika ya Hifadhi za Jamii, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ambayo kazi yake kubwa ni kuishauri Serikali katika suala zima la deni la taifa na maendeleo, Hebron Mwakagenda, alisema hadi kufikia Oktoba mwaka jana, deni la nje lilikuwa Sh15.9 trilioni.

“Hiki ni kiwango cha juu kabisa kwa nchi kuweza kukopa kutoka kwenye masoko ya kimataifa, deni limeongezeka kwa dola 456.1 milioni katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu Oktoba 2011,” alisema Mwakagenda.

Alisema taarifa za Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha kuwa deni la ndani limefikia Sh5.1 trilioni hadi kufikia Oktoba mwaka jana na kwamba kiasi hicho ni sawa na ongezeko la Sh513 bilioni tangu mwaka 2011.

“Deni la ndani linakua kwa kasi kubwa inayotokana na Serikali kuanza kukopa kwenye benki za biashara ambazo zinatoza riba kubwa. Hii ni hatari kwa uchumi wa nchi,” alisema Mwakagenda.

Alisema zipo fedha zinazotumika kujenga barabara, madaraja, majengo mbalimbali ya shule na vyuo, lakini kinachotakiwa ni Serikali kufikiri mara mbili kabla ya kuamua kukopa na kuzitumia fedha hizo za mkopo.Katika mapendekezo yao, Mwakagenda alisema wameitaka Serikali kuwa na nidhamu katika kukopa kwa kuwa deni hilo limevuka kiwango cha kimataifa.

“Pia umefikia wakati kwa Serikali kutokopa mpaka ipate ridhaa ya Bunge kwa kuwa mikopo mingine haina faida kwa taifa zaidi ya kuwaumiza wananchi,” alisema.

Alisema kuwa hadi sasa hakuna juhudi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha kuwa inapata mikopo yenye riba nafuu.

Alisema kitendo cha Serikali kuendelea kukopa kutaifanya nchi kutoaminika tena na hivyo kutokopesheka iwapo kutaibuka mahitaji ya lazima.

“Pia wawekezaji wanaweza kupunguza imani na mazingira ya kiuchumi ya Tanzania na hivyo kutokuja kuwekeza, nchi itashindwa kulipa madeni, thamani ya shilingi itashuka,” alisema Mwakagenda.

Alisema Serikali inatakiwa kujifunza kwa nchi za Hispania, Ugiriki na Ireland ambazo zimekubwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na kuwa na madeni makubwa.
“Tunaelezwa kwamba deni la taifa ni endelevu na bado nchi inakopesheka, sijui wanatumia takwimu za wapi,” alisema.

Alisema deni la nje si tatizo kubwa sana kwa kuwa fedha hizo hutoka katika mataifa makubwa na mashirika tajiri na  kwamba deni la ndani ndiyo kikwazo kwa maelezo kwamba riba yake ni kubwa zaidi.


MWANANCHI

No comments: