Tuesday, January 22, 2013

BANDARI WAANZA KUTIMUANA.
WIZARA YA UCHUKUZI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe 27 Agosti, mwaka jana, Waziri wa Uchukuzi aliunda Kamati ndogo ya Uchunguzi ya watu saba kubaini chanzo cha matatizo yanayozorotesha ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kukimbiwa na wateja wa ndani na nje ya nchi. Imekuwa kawaida kuona wakazi wa Dar es Salaam au kampuni zenye makao yake Dar es Salaam zikipokelea mizigo yao Mombasa, kilometa 555 kutoka Dar. Ukiuliza jibu ni moja kwamba wanakwepa usumbufu au adha kubwa wanayopata kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam: ucheleweshaji mizigo usio wa lazima, urasimu uliotegewa rushwa ndogondogo na kubwa, udokozi uliokithiri na wizi mkubwa wa mtandao nk.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Benki ya Dunia na DANIDA waliielezea Bandari ya Dar es Salaam kuwa ni moja ya Bandari za mwisho kwa ufanisi duniani. Ni matokeo ya utafiti mkubwa uliofanyika mwaka jana kuhusu ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam na njia za kusaidia kuboresha ufanisi wa Bandari.

Mwaka jana hiyo hiyo, taasisi ya utafiti ya kimataifa ya AFRITRAMP ilifikia tamati hiyo hiyo kuwa Bandari yetu ni ya mwisho kwa ufanisi kati ya bandari 36 wakizozitafiti barani Afrika.

Kutokana na picha hiyo na hali halisi bandarini ya wizi mdogo na mkubwa, ubadhirifu, ugoigoi, ajira za upendeleo n.k. Waziri Uchukuzi aliunda kamati hiyo ya uchunguzi ikiongozwa na wakili mzoefu wa Mahakama Kuu, Benard Mbakileki, na kusaidiwa na Mhandisi mwenye uzoefu mkubwa Mhe. Eng. Ramo Makani (Mb), Wakili Paul Wanga, Mhe. Halima Mamuya, Mkaguzi wa Mahesabu Said Sauko, Mtaalam wa Vipimo Bernadino Mwijarubi na Mchumi Richard Kasesera. Kamati hii ilifanyakazi nzuri sana, iliyosheheni weledi, uzalendo na ujasiri wa hali ya juu. Kamati ilimaliza kazi yake mwezi Oktoba mwaka jana na kumkabidhi Waziri.

Baada ya kuipitia taarifa hiyo, Waziri aliwaondoa wajumbe wote wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na kuteua wapya ili kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa taarifa hiyo. Mchakato wa kuipitia kwa kina taarifa ya uchunguzi ulianza mara tu baada ya kuteua wajumbe wapya wa Bodi.

Bodi imefanyakazi nzuri na kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia misingi ya haki kwa kuteua Kamati ndogo ya Bodi ya Staff and Establishment kwa lengo la kupitia kwa kina taarifa ya uchunguzi, taarifa ya CAG kuhusu Bandari na taarifa ya PPRA. Kamati hiyo ndogo ya Bodi ikafanya kazi ya kupitia taarifa hizo na kutoa mapendekezo kuhusu hatua za kuchukuliwa kwa kila mtuhumiwa. Kwa mfano, Kamati ilipendekeza kuwa menejimenti ya Mamlaka iagizwe kuandaa mashtaka (ku-draft charges) kwa kila mfanyakazi au kingozi aliyetuhumiwa, pendekezo ambalo lilitekelezwa.

Baadaye Bodi nzima ikakaa kama Mamlaka ya Nidhamu kusikiliza TUHUMA na UTETEZI. Matokeo yake kwa ujumla ni kwamba Bodi imewatia hatiani watumishi au viongozi wa Mamlaka ya Bandari watano. Aidha, Bodi haikuridhishwa na tuhuma zilivyoandaliwa kuhusu mtumishi au kiongozi mmoja hivyo imeamliwa tuhuma zake ziainishwe upya; na Bodi haikumkuta na hatia mtumishi au kiongozi mmoja hivyo ikaamuriwa arejeshwe kazini.

2. UFAFANUZI:

(i) Bw. Ephraim Mgawe, Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

Bodi ililidhirika kuwa alikuwa na makosa yafuatayo:-

a) UZEMBE ULIOKITHIRI - (kuruhusu kuwepo kwa muda mrefu utaratibu usiofaa wa upokeaji na uondoshwaji bandarini wa mafuta machafu (slops), hivyo kuachia kiasi kikubwa cha mafuta safi kuibiwa; na kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji bandarini wa mafuta machafu kinyume na mikataba iliyowekwa).

b) UFANISI DUNI ( gross inefficiency) - (kushindwa kudhibiti wizi uliokithiri bandarini wa mizigo na mali ya Mamlaka; kushindwa kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya TICTS na TPA ambapo TICTS kwa muda mrefu wamekuwa wakikiuka mkataba huo; kuipotosha Bodi mpaka ikaridhia uanzishwaji wa chombo cha pili cha manunuzi ndani ya Mamlaka kinyume ya Sheria).

c) KUKOSA UAMINIFU KULIKOPINDUKIA - (kutumia chombo cha pili cha manunuzi kilichoanzishwa kinyume ya sheria na kuingia zabuni mbalimbali bila kufuata taratibu na kanuni za zabuni kama zilivyoainishwa na sheria ya manunuzi. Miradi mingi iliyongiwa kwa njia hiyo haikuwa na tija kwa Mamlaka zaidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma).

d) KUKIUKA SHERIA NA TARATIBU - (kuingia mkataba na kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC) bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka; kutekeleza Nyongeza za mishahara kwa asilimia 15 tarehe 1 Julai, 2012 bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi, hivyo kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria.

KWA KUZINGATIA MAKOSA HAYO KWA UJUMLA NA UTETEZI WAKE, BODI ILIMPELEKEA WAZIRI WA UCHUKUZI MAPENDEKEZO YA KUMWACHISHA KAZI, MAPENDEKEZO AMBAYO WAZIRI ALIYAAFIKI. HIVYO MTENDAJI MUU WA MAMLAKA YA BANDARI, BW. EPHRAIM MGAWE, AMEACHISHWA KAZI KUANZIA IJUMAA YA TAREHE 18/01/2013.

(ii) Bw. Hamadi Koshuma, Naibu Mkurugenzi Mkuu (Huduma)

Bodi iliridhika kuwa alikuwa na makosa yafuatayo:

a) MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA - (kuruhusu michakato mbalimbali ya zabuni bila kufuata utaratibu kwa kisingizio cha kwamba ni miradi mikubwa).

b) UFANISI DUNI ( gross inefficiency) - (akiwa yeye kama Mjumbe wa Bodi ya Zabuni, alishindwa kuijulisha Bodi ya PPRA kuhusu ukiukwaji wa sheria ya manunuzi kwa mujibu wa kifungu cha 31(4) k.m. mamlaka kuingia mkataba wa kibiashara na CCCC bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni; kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji wa Mamlaka.

c) KUKOSA UAMINIFU KULIKOPINDUKIA - (kushiriki katika kuipotosha Bodi mpaka kuanzishwa cha chombo cha pili cha manunuzi kinyume ya sheria na baadaye kutumia chombo hicho batili bila kufuata utaratibu kwa kisingizio kuwa ni miradi mikubwa. Miradi mingi iliyongiwa kwa njia hiyo haikuwa na tija kwa Mamlaka zaidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma).

d) KUKIUKA SHERIA NA TARATIBU - (kushiriki katika kuingia mkataba na kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC) bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka; kushiriki kwenye maamuzi ya kutekeleza Nyongeza za mishahara kwa asilimia 15 tarehe 1 Julai, 2012 bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi, hivyo kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria.


KWA KUZINGATIA MAKOSA HAYO KWA UJUMLA NA UTETEZI WAKE, BODI IMEAMUA KUMWACHISHA KAZI KUANZIA TAREHE 09/01/2013.

(iii) Bw. Julius Mfuko, Naibu Mkurugenzi Mkuu (Miundombuni)

Bodi iliridhika kuwa alikuwa na makosa yafuatayo:

a) KUSHINDWA KUSIMAMIA MAANDALIZI YA MIRADI MBALIMBALI YA MIUNDOMBINU YA MAMLAKA: mfano miradi ya ex-AMi yard, Port Community System, CCTV ambayo kwa muda mrefu iko kwenye utekelezaji bila kukamilika kutokana na misingi mibovu ya maandalizi. Fedha nyingi ya Mamlaka imetumika kwenye miradi hiyo bila matokeo tarajiwa.


b) KUSHINDWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MIKATABA MBALIMBALI, hivyo kutokamilika kwa wakati na kuisababishia mamlaka hasara kubwa.

c) KUSHINDWA KUISIMAMIA KWA UFANISI DIVISHENI YA MAENDELEO YA MIUNDOMBINU, hivyo kuathiri maendeleo ya Mamlaka kwa ujumla.

d) Kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji wa Mamlaka.

KWA KUZINGATIA MAKOSA HAYO KWA UJUMLA NA UTETEZI WAKE, BODI IMEAMUA KUMWACHISHA KAZI KUANZIA TAREHE 09/01/2013.


(iv) Bw. Cassian Ngamilo, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam.

Bodi iliridhika kuwa alikuwa na makosa yafuatayo:

a) MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA.

Amekuwa akitoa nyongeza za mikataba kwa makampuni yanayohudumia bandarini bila kupitia Bodi ya Zabuni kinyume na taratibu zilizowekwa na sheria. Mfano wa kampuni hizo ambazo zimepewa nyongeza mara kadhaa na Port Manager ni: Nagla General Shipping Services; HAI Sub Supplier, TRICON Investment, Evans Manyasi Co. nk.; kuachia uondoshaji bandarini kwa mafuta machafu bila kufuata mikataba husika).

b) Uzembe uliokithiri:

i. Kushindwa kusimamia Mktaba wa ukusanyaji na uondoshaji wa mafuta machafu (slops) katika bandari ya Dar es Salaam kati ya TPA na Ms Singilimo Enterprises na hivyo kutioa mwanya kwa Kmapuni hiyo kuchukua mafuta masafi wakati wa ukusanyaji na uondoshaji wa mafuta machafu. Kwa mfano tukio la mwezi Agosti, 2012 ambapo gari 2 mali ya mzabuni huyo zilikutwa na zilikuwa na lita ishirini na sita elfu kila moja badala ya lita elfu tisa tu zinazoruhusiwa kwa mujibu wa mkataba.

ii. Kushindwa kudhibiti mchezo wa kuiba mafuta kwa kutumia zabuni ya uchukuaji mafuta hivyo kuisababishia Mamlaka hasara.

c) Ufanisi duni

i. Kushindwa kusimamia ipasavyo watendaji wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama na hivyo kusababisha wizi na ubadhirifu wa mali za Mamlaka na wateja kwa mdfano wizi wa makontena manne ya shaba.


d) Kukiuka sheria na taratibu mbalimbali

i. Kutoa misamaha ya tozo la hifadhi (storage charges) kinyume na taratibu zilizoanishwa kwenye Kanuni za fedha za Mamlaka ya Usimamizi wa bandari.

ii. Kutoa nyongeza za mikataba ya Zabuni kwa M/S NAGLA General Shipping Serbices; M/S HAI Sub Supplier; M/S Tricon Investment; M/S Evans Manyasi Co bila ya kushirikisha Bodi ya Zabuni na Sheria ya Manunuzi ya Umma.


KWA KUZINGATIA MAKOSA ALIYOTIWA NAYO HATIANI, UTETEZI WAKE, NA KUZINGATIA MAJUKUMU YA NAFASI YAKE, BODI ILISHINDWA KUMWONDOA HATIANI NA HIVYO KWA KULINGANA NA MAKOSA ALIYOTIWA NAYO HATIANI AMEACHISHWA KAZI KUANZIA TAREHE 9 JANUARI, 2013.


(v) Capt. Tumaini Massaro, Oil Terminal Manager.

Bodi ilimkuta na makosa yafuatayo:

a) Uzembe iuliokithiri

i. Kushindwa kusimamia udhibiti wa kiwango cha uchukuaji mafuta machafu kilicho kwenye mkataba hivyo kusababisha Mzabuni (M/S Singilimo Enterprises) kupata mwanya wa kuchukua kiwango cha mafuta machafu (slops) zaidi ya kile kilichopo kwenye Mkataba na kuingiza Mamlaka hasara.


b) Ufanisi duni

i. Kushauri Menejimenti kuomba idhini ya kutotumia mita (by-pass of flow meters) huku akijua kwamba utaratibu huo si sahihi na umeisababishia hasara Serikali. Kuendelea kuomba kutumia “by-pass” kwa muda mrefu, bila kuchukua hatua za kurekebisha mfumo wa upimaji wa mafuta.

ii. Kutotoa kwa muda mrefu ushauri wa kitaalamu wa udhibiti na utumiaji bora wa utaratibu wa kutoa mafuta machafu.

iii. Kushindwa kusimamia ipasavyo utaratibu wa kuhakikisha kiwango cha mafuta machafu (slops) yanayochukuliwa na mzabuni (M/S Singilimo Enterprises) yanaendana na nyaraka zinazoidhinisha utoaji wa mafuta machafu. Mwanya huu umesababisha uchukuaji wa mafuta machafu (slops) zaidi ya kiwango kilicho kwenye mkataba na hivyo kuisababishia Mamlaka hasara.

KWA KUZINGATIA MAKOSA ALIYOTIWA NAYO HATIANI, UTETEZI WAKE, NA KUZINGATIA MAJUKUMU YA NAFASI YAKE, BODI ILISHINDWA KUMWONDOA HATIANI NA HIVYO ALIACHISHWA KAZI KUANZIA TAREHE 9 JANUARI, 2013.

vi) Eng. Emmanuel Mataro, Oil Terminal Engineer (Meneja wa Kituo cha Mafuta)

Bodi haikuona makosa yake waziwazi, hivyo ikaamua arejeshwe kazini.

vii) Capt. Joseph Gwakabale, Jetty Master (Mkuu wa Kitengo cha Mafuta cha Kurasini)

Bodi haikuridhishwa na uainishaji wa tuhuma dhidi yake, hivyo ikaamuru tuhuma zake ziandaliwe upya na kwa ufasaha.


MSEMAJI WA WIZARA

WIZARA YA UCHUKUZI

21 JANUARI, 2013

No comments: