Tuesday, December 4, 2012

SUALA LA UCHIMBAJI URANI LAVAA SURA MPYA


TANZANIA imeshauriwa kutochimba madini ya urani badala yake yaachwe kama yalivyo aridhini kwa sababau athari zake ni tishio katika mazingira na afya ya binadamu ukilinganisha na aina nyingine za madini yanayopatikana hapa nchini.


Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaamu na Mwenyekiti wa Uranium Network Organization kutoka nchini Ujerumani, Gunter Wippel, wakati akielezea uzoefu wa nchi nyingine katika uchimbaji wa madni hayo pamoja na athari zake huku akishauri Tanzania iachane na zoezi hilo.

Kwa mujibu wa watalaamu madhara ya urani ni kansa ya ini, kuzaliwa watoto wenye viungo pungufu au zaidi na kubadilika kwa DNA. Mara kadhaa watalaamu wa madini hayo wamekuwa wakitoaangalizo juu ya suala la kufanya maandalizi mazuri kabla ya kuanza kuchimba madini hayo.

Mjerumani huyo alisema lazima mikataba hiyo ionyeshe ni kwa vipi Tanzania itazuia athari hizi baada ya uchimbaji kwani madini hayo yanapatikana kwa uchache ardhini lakini eneo ambalo linachimbwa ni kubwa, na kwamba kwenye mwamba mmoja kuna asilimia 0.01 ya madini.

Alieleza kuwa nchi mbalimbali zilizoendelea ikiwamo Ujerumani hazijaweza kuzuia madhara hayo ingawa wana teknolojia na fedha za kutosha kwa ajili ya kutatua madhara mbalimbali.

Alifafanua kuwa Ujerumani imetumia zaidi ya Dola 7 bilioni za Marekani kwa ajili ya kuhakikisha madhara hayo yanakwisha kabisa lakini tatizo bado lipo.

“Naishauri Tanzania iachane na uchimbaji wa madini haya kwa sababu hakuna njia sahihi ya kuchimba madini haya hivyo ni bora Tanzania isitishe zoezi hili,” alisema Wippel.

Wippel alisema kuwa uchimbaji wa madini ya urani una athari nyingi na pia unahijitaji gharama nyingi ikiwamo maji na umeme wa kutosha kwa ajili ya kuchimba na kuosha madini hayo. Alieleza kuwa nchi kama Namibia ilivuna maji kutoka baharini ili kuweza kuchimba madini hayo na akahoji kwamba kama maji ya Mto Ruvuma yatatosha kwa uchimbaji wa madini hayo?

Pia anasema kuwa Tanzania kuna tatizo la kutokuwapo kwa umeme wa kutosha kwa ajili ya kuendeshea mitambo mbalimbali, hivyo itakuwa vigumu kupata umeme imara kwa ajili ya kutumika migodini.

“Tujifunze kwa wenzetu ambao tayari wameshachimba madini haya kama Namibia ambao walitumia maji kutoka baharini ndipo wakafanikiwa kuchimba, Mto Ruvuma pekee hautatosha na hata umeme tulio nao siyo umeme imara, anasema Wippel.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Imelda Urio, alisema kuwa zoezi la hilo lisitishwe kwani taifa halijajipanga namna ya kudhibiti madhara yuatakayotokana nauchimbaji wa madini hayo.

Alisema kuwa Tanzania ina vyazo vingi vya mapato na mipango madhubuti ambayo inaweza kutumika vizuri na ikaleta mafanikio kwa taifa ukiwamo mpango wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wa Kilimo Kwanza, hivyo siyo lazima viongozi waangalie madini ya urani tu.
  “Tanzania ina mipango mingi ukiwamo mpango wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wa Kilimo Kwanza pamoja na vyanzo vingi vya mapato ambapo kama vikitumika vizuri vitaleta maendeleo kwa taifa kwa hiyo siyo lazima Serikali waangalie madini ya Urani pekee kwani yana madhara makubwa kwa wananchi, alisema Urio.

Alisema kuwa Serikali ifikirie wananchi wataishi vipi na athari hizo hasa wananchi wa wilaya za Namtumbo mkoani Ruvuma.MWANANCHI

No comments: