Monday, December 3, 2012

MTU HULA ILI ASHIMBE, AKIENDELEA HUVIMBIWA MWISHO NI MPASUKO
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.


Mpenzi Frank,

VIPI hali yako mpenzi? Nimeamua kuacha kukuita TANESCO maana naona hitilafu za miundombinu kwa maana ya mgao usio mgao zinazidi kuongezeka na nina wasiwasi kwamba ukiamua kufuata jina lako la TANESCO sitakuona tena.

Sasa nashindwa kuelewa kwa nini watu hawawezi kufanya kaziara kadogo kuona kama yaliyosemwa kuhusu kina cha maji ni kweli au la. Hata hivyo natafuta njia ya kubembeleza Mama Bosi na mimi nije nyumbani mara moja maana naona mama yangu ameanza kuniita TANESCO na mimi tehe tehe tehe.

Lakini pia nadhani sababu nyingine ya kutaka kuja nyumbani ni kwamba nimechoka kabisa kuishi ndani ya uozo, kukanyaga uozo, kula na kunywa na kujisaidia uozo kila siku. Sote tunajua kwamba hali hii ipo serikalini hadi hata wanene wa nchi wanaiongelea, ingawa sioni kwamba wanachukua hatua. Nadhani kama alivyosema yule fyatu wako, Makengeza, sasa imekuwa ushuru badala ya hongo maana inaonekana kuwa sehemu ya maisha kabisa. Hata kama ni michuzi ya ushuuzi unaonuka hasa.

Lakini juzi nilishangaa sana kusikia kinyesi cha ushuuzi huu kilivyotapakaa kila mahali. Unajua juzi alikuja kaka yake Bosi (au tumwite KB). Ni mtu mcheshi sana na anapocheka chumba kizima kinatetemeka kutokana na kutetemeka kwa tumbo lake. Basi KB naye ana kaAZAKI kake. Nilipomwuliza Binti Bosi, kwa nini ahangaike na kaAZAKI badala ya kushirikiana na mdogo wake apate neema zaidi, BB alicheka sana.

‘Kumbe wewe Hidaya bado huelewi mambo. Huko nyuma, baba yangu na kaka yake walikubaliana kimsingi kwamba aanzishe hii ili kuhakikisha kwamba wafadhili na mafedhuli wakitoa upande wa kushoto, yaani serikali, wamo, na wakiamua kutoa upande wa kulia, yaani kupitia hizi AZAKI, wamo pia. Na wakitoa kotekote, ndiyo poa zaidi. Watafaidika katika kuwafaidisha wengine.’

Nilimwangalia BB kuona kama kuna kejeli ndani yake lakini hakutabasamu wala kununa. Lakini baada ya hapo kidogo nimwangalie KB kwa jicho tofauti kidogo. Sijui watu kama hawa watavimbiwa lini maana hawawezi kuacha tonge hata siku moja, hata kama wameshiba namna gani, meno yanaanza kuwasha na watadaka tonge au mnofu harakaharaka ili mradi iingie tumboni mwao.

Kumbe wadakavitonge wako wengi zaidi kuliko nilivyofikiria. Juzi KB alikuja kumtembelea mdogo wake kidogo. Sasa wakati wanabugia wiski zao raha mstarehe, KB alianza.

‘Unajua mdogo wangu, nafikiria kuachana na hii kazi ya AZAKI.’

Bosi alishtuka.

‘Unasemaje? Kwa nini?’

‘Haina tija Bwana maana hata watoaji siku hizi wanataka kuwa wapokeaji. Wanatoa pesa kwa ajili ya mradi fulani wa maendeleo lakini lazima uwarudishie asilimia kumi kama si zaidi. ‘

‘Unasemaje? Wao wanapaswa kutupatia hii asilimia kumi si sisi kuwapatia wao.’ Bosi akacheka kwa nguvu sana lakini kaka yake alikaa kimya.

‘Siyo kichekesho. Hebu fikiria, juzi walitaka kutupatia milioni mia mbili kwa misingi kwamba tungemrudishia mwenye mkataba kiasi cha shilingi milioni ishirini. Sasa kwa hesabu hizo tungewezaje kufanya kazi. Mwisho watatulaumu kwamba tumeshindwa kufanya kazi iliyotakiwa.’

‘Kaka, mbona hivyo. Najua wewe ni mtaalamu sana wa kuchezacheza na pesa za miwarsha na kadhalika.’

‘Ndiyo lakini kwa kweli naanza kuchoka mambo hayo. Unaenda kwa wananchi na ahadi kibao kutokana na pesa ambazo unapaswa kupewa. Tena kwa misingi ya maendeleo siku hizi, unapanga nao kabisa na kufanya maamuzi pamoja. Sasa utarudije kwa watu walewale na stori kwamba pesa zilipwaya. Watajua umekula mwenyewe kumbe umeliwa.’

‘Lakini ndiyo mtindo wa kisasa. Ukiona tonge … daka. Ukiona mnofu … daka.’

KB alimwangalia mdogo wake.

‘Unajua mdogo wangu mara nyingine naona siasa imekuharibu kweli. Unaweza kusema hivi mbele ya kadamnasi?’

‘Kadamnasi itaninasa wapi? Mbona na wewe ulijua AZAKI ni sehemu ya kula pia. Biashara ya familia ha ha ha.’

‘Si hivyo. Kweli mtu anatafuta kula ili ashibe, lakini akiendelea kula baada ya kushiba, anavimbiwa. Na mwisho wa kuvimbiwa ni mpasuko. Sasa hawa wafanyakazi wa mashirika haya makubwa ya ufadhili au ufedhuli hawana mshahara mzuri? Wanao.

Lakini bado wanaona ni haki yao kutumia nafasi yao kula vya wengine na wanaoteseka ni sisi.’

Bosi bado hakutaka kutilia maanani.

‘Kwani na serikali inafanya nini kwa sasa. Kila mtu anatafuta kula vya wengine.’

‘Kwa sababu ya mfano mbovu, na wengine kwa sababu ya mshahara mbovu pia. Lakini hawa tayari ni wafalme na malkia, ya nini kuvimbiwa?’

‘Ndiyo dunia ilivyo.’
‘Sawa mdogo wangu. Lakini nakuambia nimeapa. Nimeapa kwamba wakati umefika kuwafichua hawa mafedhuli na ufedhuli wao. Lazima tuwafichue na kuwakamata hawa mawakala wa kutudhalilisha. Wanadai rushwa kubwakubwa kisha wanasimama hadharani na kulaani sisi Wabongo kwa kuwa wapenda rushwa. Huu unafiki hauvumiliki.’

Kwa mara ya kwanza Bosi alionekana kushtuka.

‘Hapana kaka. Usifanye hivyo. Hujui methali ya usimwamshe aliyelala …’

‘Najua na najua aliyetengeneza hiyo ni yule anayekula chakula cha aliyelala hadi jamaa haamki tena maana ameshaenda kuzimu kutokana na utapiamlo mkali. Watu wanapiga kelele juu ya akina nyinyi ingawa bado haijaleta mabadiliko ya kutosha. Sasa tuwafichue na hawa?’

‘Lakini ukifanya hivyo wanaweza kukasirika na kutuacha.’

‘Potelea mbali. Nakuambia mambo yamezidi na tungesimama imara tungeweza kukomesha hayo. Nilikuja kwako si tu kama mdogo wangu bali kama Waziri lakini naona nimepoteza muda. Kweli anayebugia ndani ya nyumba hawezi hata kuwaona wenye njaa nje ya nyumba maana ameweka pazia nzito kuficha hali halisi.’

Yaani mpenzi, nilikuwa sijawahi kuona KB akikasirika namna hiyo. Aliamka na kutoka bila hata kuaga. Lakini naona Bosi bado hakushtuka. Na labda si jambo la ajabu maana hawa mafedhuli ndani ya mashirika ya mafedhuli wana tofauti gani na yeye. Ndiyo maana hashangai vitendo vyao. Mmm! Sijui tuanze wapi?

Akupendaye sana mia kwa mia bila kupunguza hata asilimia moja

Hidaya.

RAIA MWEMA

No comments: