Wednesday, December 12, 2012

HOJA YA MUUNGANO


Na M.M Mwanakijiji,

Mtu akikuambia jambo la kijinga na anajua na wewe una akili nawe ukalikubali atakutumikisha. Nimebadili kidogo tu kauli ile ya Nyerere kuwa "Mtu mwenye akili akikushauri jambo la kipumbavu akijua nawewe una akili ukalikubali atakudharau". Kuna hoja inatolewa na baadhi ya watu Zanzibar ambao wanaamini wanatoa hoja ya kiakili pale wanapopendekeza kuwa wanataka Zanzibar itoke kwenye Muungano wa sasa ili iwe "dola kamili" na baadaye ufatiwe "muungano wa mkataba" na Tanganyika.


Katika hili kama maji machafu ya maporomoko wengi wamekumbwa. Wamekumbwa vijana, wamekumbwa wazee na wamekumbwa wasomi na wasio wasomi. Wengi wanaimba wimbo wa "Muungano wa mkataba" ambao kibwagizo chake hakipo zaidi ya 'Zanzibar kwanza'. Hoja hii imeanza siyo tu kukubaliwa na watu wengine wenye akili lakini inaonekana ndio hoja pekee inayoweza kutolewa na kuridhisha watu. Naomba kupendekeza kwa heshima na taadhima kuwa hoja hii ni ya kipuuzi, haina mantiki na inapaswa kukataliwa na watu wote wenye akili.

Hoja Mbili tofauti

HOJA YA KWANZA - 'DOLA KAMILI KWANZA'

Bahati mbaya sana watoa hoja hawa wamejaribu kwa kutumia akili kuchanganya hoja mbili zisizohusiana kabisa. Hoja ya kwanza ambao wanaitoa na labda ina nguvu zaidi kuliko ile ya pili ni kuwa "tunataka Zanzibar yetu kwanza, dola kamili, ikiwa na mamlaka yake yote". Hoja hiikwa Kiingereza inaweza kufupishwa kwa maneno mawili tu "FULL SOVEREIGNTY" yaani "HAKIMIYA KAMILI".

Katika historia ya dunia jamii za watu zinapodai 'DOLA KAMILI' wakimaanisha dola yenye hakimiya kamili manake ni kuwa jamii hizo zinatawaliwa na wengine, au hakimiya yake haipo ndani yake. Kwa mfano, baadhi ya mataifa yana uhuru wote wa ndani lakini hakimiya iko kwa Malkia wa Uingereza ambaye huitwa 'SOVEREIGN' manake ni mkuu wa dola hiyo. Nchi kama Canada, Australia na nyingine 13 ziko namna hii. Ziko huru kwa kila kitu lakini zinamtambua Malkia wa Uingereza kama Malkia wake. Baadhi ya hizi sasa zinataka kwenda kwenye mfumo wa Kijamhuri na kutoka kuwa chini ya Malkia.

Marekani ni mfano mzuri wa nchi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa chini ya Mfalme wa Uingereza; walitawaliwa na watu walioko London. Harakati za Mapinduzi ya Marekani zilitokana kwa kiasi kikubwa na mengi ya malalamiko ya koloni la Marekani kupuuzwa na Mfalme George III na hivyo kusababisha vita vya mapinduzi. Wamarekani katika Azimio lao la Uhuru walieleza kabisa kwanini wanaamua kuachana na utawala wa mfalme na hivyo kujitangazia uhuru wao milele daima. Licha ya Uingereza kujaribu kuzima mapinduzi Marekani ilijitangaza huru July 4, 1776. Ilipata kuwa dola kamili.

Historia hata hivyo inaonesha kuwa ukaribu wa Uingereza na Marekani haukuvunjwa na vita hivyo kwani hadi leo hii udugu wao, ujamaa na ushirikiano wao unadumu kupitia makubaliano mbalimbali ya kimataifa. Makubaliano hayo hata hivyo siyo muungano wa "mkataba"; bali ni makubaliano (treaties) kama yalivyo makubaliano mbalimbali kati ya nchi mbili. Leo hii hakuna nchi rafiki kwa Mwingereza kama Marekani na hakuna nchi rafiki kwa Mmarekani kama Uingereza. Hakuna Muungano wa Mkataba baina yao isipokuwa ushirikiano wa karibu unaotokana na historia yao moja.

Wazanzibari hivyo wanaweza kabisa kudai na kutoka kwenye Muungano huu na kuwa dola kamili. Hili wanaweza kulifanya bila kudai "muungano wa mkataba". Hawana haki nyingine ya kudai "muungano wa mkataba" haki yao ni kudai "dola kamili tu". Watoke kwanza na wakishatoka na kuunda utawala wao na serikali ya yatafuata mambo ya makubaliano mbalimbali na Tanganyika au na nchi nyingine yeyote ile ambayo viongozi hao watataka.

Kudai kutoka nje ya Muungano ni haki kama ilivyokuwa kwa baadhi ya nchi tena kwa utaratibu mzuri tu; Wazanzibari walete mswada kwenye Bunge lao (Baraza la Wawakilishi) wa kusimamia kura ya maoni na waulizwe tu swali moja jepesi "JE UNATAKA ZANZIBAR IJITOE KWENYE MUUNGANO NA TANGANYIKA IFIKAPO JANUARI 1, 2014?" Na kama asilimia kubwa ya watu (zaidi ya 2/3) wakisema "Ndiyo" basi vipengele vingine vya sheria hiyo vitaanza kutekelezwa ikiwemo kuweka utaratibu wa kuachana na Tanganyika, kugawana mali (haiwezi kuwa nusu kwa nusu isipokuwa kama katika kila gharama kila upande ulichangia nusu kwa nusu) na kupeana majukumu mbalimbali ili kuhakikisha kujiondoa kwa Zanzibar kunakuwa katika hali nzuri (smooth) na isiyoleta matatizo yoyote visiwani humo.

Hata hivyo sheria hiyo iweke wazi pia maana ya kukataa kujitoa ni nini? Kwamba mfumo wa Muungano utaendelea kuwa ulivyo sasa ambao ni 'nchi moja serikali mbili' ama "nchi moja serikali moja'. Wazanzibari wajue katika kura hiyo kusema ndio ni kutoka kwenye Muungano BILA kufuatiwa na "mkataba" wowote mwingine.

Watanganyika hawatakiwi kuamua hatima ya Zanzibar

Mojawapo ya maswali ambayo yanaulizwa na ndugu zetu ni kuwa "kwanini nyinyi Tanganyika mmetung'ang'ania hamtaki kutuachia?" au "Kwanini Tanganyika inaogopa Zanzibar kuondoka". Kwa upande wangu - na labda nawakilisha mawazo ya wengine - Watanganyika (Watanzania Bara) hawajali kabisa kama Zanzibar itatoka kwenye Muungano kwani hawajali upande mwingine kama Zanzibar ipo. Kwao uwepo wa Zanzibar ndani ya Muungano haubadilisha maisha yao kwa namna yoyote ile. Mtu wa Mara, Singida, Mbeya, au Kagera hatosikia chochote kama Zanzibar itajitoa kwenye Muungano na hivyo hawafikirii sana. Kitu pekee ambacho Watu wa bara watakisikia na Mwalimu alikisema vizuri kwenye ile hotuba yake ya "Nyufa" pale Kilimanjaro Hotel mwaka 1995 ni kuwa watanganyika watajikuta wamepigwa na butwaa "yaani Wazanzibari kweli wamejitoa?" Watakuwa wapweke kwa muda kwa sababu Tanzania kama Muungano wa nchi mbili haitokuwepo tena.

Lakini kama Nyerere alivyosema hata hivyo Watanzania bara "watabaki salama". Mshtuko wa Zanzibar kutoka utapita kama ukungu wa asubuhi. Na kuna uwezekano mkubwa watu wa bara wakaamua kuendelea kujiita Watanzania kwani hawana tatizo na utambulisho wao; kwani kwao Tanzania ni njozi ya umoja iliyounda taifa letu.

Ni kwa sababu hiyo Tanzania bara haipaswi kabisa kuamua Zanzibar inabakia au haibakii. Mwezi Novemba wananchi wa visiwa vya Puerto Rico walipiga kura kama wanataka kuwa dola kamili au wawe jimbo la 51 la Marekani. Kwa wingi wao waliamua badala ya kuwa nchi huru kamili wawe jimbo hilo. Wamarekani wote hawakuulizwa Puerto Rico iingie kama jimbo au ibakie. Ni suala la Puerto Rico siyo suala la Marekani nzima.

Mwezi Oktoba Waziri Mkuu wa Uingereza na Waziri Kiongozi wa Scotland waliingia makubaliano ili Scotland ipige kura ya kuamua kuendelea kubakia ndani ya United Kingdom au itoke na kuwa nchi kamili. Miaka 700 kabla George Wallace aliongoza vita vya kudai uhuru (filamu ya Mel Gibson 'Braveheart' iliigiza tukio hilo) na miaka 300 nyuma Uingereza na Scotland ziliingia kwenye Muungano. Makubaliano ya Cameron na Alex Salmond yametengeneza njia kuwa mwaka 2014 Scotland watapiga kura ya "ndio" au "Hapana" kuhusu nafasi ya Scotland kwenye Muungano. Kura hiyo haitopigwa na Waingereza wote. Kura za maoni sasa hizi zinaonesha ni asilimia kama 30 ya Wascot wanataka kutoka kwenye UK.

Mwaka 2005 serikali ya Sudan na uongozi wa Sudan ya Kusini waliingia makubaliano ya kuitisha kura ya maoni ili kuamua hatima ya eneo la Sudan ya Kusini ndani ya Sudan. Kura ile ilikuwa inataka kujua kama watu wa Sudan ya Kusini wanataka kubakia sehemu ya Sudan au watoke nje ya Muungano. Kura ile ilipopigwa January 2011 na asilimia zaidi ya 99 ya wananchi wa Sudan ya Kusini waliamua kujitenga na Sudan na kuunda taifa lao. Kabla na Baada ya kujitenga na kuwa nchi huru serikali hizo mbili zimekuwa zikifanya mazungumzo ya makubaliano mbalimbali ya ushirikiano baina yao. Hakuna Muungano wa Mkataba kati yao yapo makubaliano ya kimataifa baina ya nchi mbili. Hata hivyo, siyo Sudan nzima iliyopiga kura ya kuamua hatima ya Sudan ya Kusini ni watu wa Sudan ya Kusini tu waliokuwa na uhuru wote wa kuamua.

Zanzibar na wale wanaotaka kuwa nje ya Muungano hawahitaji kibali cha Watanzania bara wao kujitoa; wanaweza kabisa kuanzisha mchakato wao na watu wa bara hawapaswi hata kidogo kutoa maoni ya upande wowote ule. Watu wa bara watapaswa kubakia ABSOLUTELY NEUTRAL bila kutoa ahadi wala vitisho ili wananchi wa Zanzibar waamue hatima yao kwa uhuru wote. Ni kwa sababu hiyo baadhi yetu tunataka Wazanzibari kama kweli wanataka watoke kwenye Muungano waanze mchakato wa kuandika sheria ya kura ya maoni mapema ili kura ya maoni iitishwe Julai mwakani na Zanzibar iwe taifa huru ifikapo January 1, 2014.

HOJA YA PILI - UFUATIE MUUNGANO WA MKATABA

Hakuna Muungano wa Mkataba

Sasa kama nilivyosema hoja hizi mbili hazihusiani. Hakuna nchi yenye muungano wa mkataba duniani. Kuna nchi zenye Muungano wa kikatiba (ambao ni Mkataba Mkubwa zaidi kama ulivyo sasa) na kuna makubaliano ya mahusiano ya kimataifa (treaties on international cooperation). Hili ni muhimu kulielewa. Hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kuja kuingizwa kwenye hicho kinachoitwa "MUUNGANO WA MKATABA" ambacho hakiwezi kujadiliwa na kuingizwa katika Muungano wa sasa.

Tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari wamekuwa na mikataba mingi baina yao. Hii ni kweli ukiondoa kwanza makubaliano ya Muungano (Articles of the Union) ambao ni Mkataba mkubwa zaidi. Tayari kuna vitu ambavyo vinafanywa kwa mujibu wa mkataba wa Muungano na kuna vitu vingine ambavyo japo vipo nje ya Makubaliano ya Muungano lakini vimekubaliwa baina ya serikali mbili kwa mikataba mbalimbali.

Kumbe basi Muungano wa Mkataba upo tayari. Ni muungano huu wa mkataba umewezesha ushirikiano wa sehemu hizi mbili. Lakini, endapo Zanzibar itaamua kutoka kwenye Muungano huu makubaliano yote ambayo yamekuwepo hadi hivi sasa yatafutwa na itabidi waanze moja. Na hapo ndipo watakapokutana na wanasiasa wa Tanganyika ambao nao watahitaji kulinda maslahi ya Tanganyika katika makubaliano yoyote na Nchi ya Zanzibar. Wasije kufikiria kuwa Zanzibar ikijitoa kwenye Muungano basi itagawiwa kila "nusu kwa nusu"; kwa ujiko gani wapewe kila nusu kwa nusu?

Makubaliano yoyote baada ya Muungano wa sasa kuvunjwa yataangaliwa kwa kupima mchango wa kila sehemu, gharama mbalimbali na kiasi cha fedha ambacho kimetoka bara kwenda Zanzibar nje ya makato yanayotakiwa kisheria. Vitaangaliwa madeni mbalimbali ambayo Zanzibar inadaiwa bara na yale ambayo bara inadaiwa Zanzibar. Baada ya mahesabu yote kupigwa ndipo nini Zanzibar itastahili kitaamuliwa na bila ya shaka kutokana na uchumi wake mdogo serikali ya Tanganyika itajitolea mambo kadhaa ili kuipa nguvu serikali ya Zanzibar kama vile Sudan ilivyofanya kwa Sudan ya Kusini. Mojawapo ya vitu ambavyo naamini Tanganyika itaweza kufanya ni kulipa madeni ya kimataifa ya Zanzibar na kuendelea kulipa pensheni za wale waliowahi kuwa watumishi wa jamhuri ya Muungano.

Nje ya hapo mambo mengine yote yatazungumzika katika majadiliano kama yanavyofanyika baina ya nchi mbili.

HITIMISHO

Hivyo basi, kwa vile hakuna kitu kama Muungano wa Mkataba nje ya Muungano wa sasa ambao ni wa mkataba, hoja pekee ambayo nawahimiza Wazanzibari wote duniani kushikana pamoja na kuidai ni kuwang'ang'ania wawakilishi wao ili walete mswada wa kupiga kura ya maoni ili Zanzibar iamue hatima yake kwenye Muungano wa sasa wa Mkataba. Kama wabaki au watoke. Haitoshi watu kudai kuwa ni "waumini wa muungano wa mkataba"; wangejitangaza ni waumini wa Zanzibar nje ya Muungano huu wa Mkataba". Hapa wangepigiwa makofi.

No comments: