Thursday, November 22, 2012

WAHAFIDHINA CCM WANAPOIKANA MISINGI YA TANU NA ASP
Na Joseph Zablon,


KATIKA kitabu 'Tujisahihishe' kilichoandikwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962 ukurasa wa pili, anaeleza dhana nzima kuhusu ukweli.

Anasema, “Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo, haujali adui au rafiki wote kwake ni sawa. Pia ukweli una tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa.

“Ukiona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya.

“Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole, japo ningekuwa nani.

“Ukweli haupendi kupuuzwa puuzwa! Wakati mwingine mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.

“Nikisema mbili na tatu ni sita nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha.

“Ni kweli mbili mara tatu ni sita, lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita.

“Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema meno yangu ni machafu, au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana.

“Huu ni mfano wa upuuzi, lakini mara nyingi hoja tunazotumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda, au kukubali mawazo yetu, huwa hazihusiana kabisa na mambo tunayojadili,” anasema Mwalimu katika kitabu chake hicho.

Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume katika Mkutano Mkuu wa nane wa CCM Mjini Dodoma uliomalizika hivi karibuni analia na mtindo wa baadhi ya watu ndani ya chama kupuuzwa hata kama wanasema ukweli.

Anasema kumezuka mtindo ambao sio uliojenga misingi ya TANU na ASP wa baadhi ya watu kupuuzwa wakati wa kutoa maoni au kuchangia hoja mbalimbali, na wakati mwingine kupachikwa majina ya ajabu ambayo hayahusiani kabisa na hoja inayojadiliwa.

Karume anahimiza kuvumiliana katika utoaji wa maoni kuhusu Katiba kwani watu wamegawanyika kuhusiana na kile ambacho wanataka kiwemo katika Katiba mpya hususani suala la Muungano.

Anasema kuna watu ambao wanapendekeza Muungano uliopo udumu na wapo ambao wanataka uwe wa Serikali mbili pia kuna ambao wanapendekeza ziwe mbili lakini za mkataba.

"Wote hao ni haki yao muwastamilie, muwavumilie na wengine bungeni nimesikia wanataka Serikali tatu, si hiyari yao?" anasema Karume katika mkutano huo huku miguno na sauti za kuzomea zikianikiza katika ukumbi wa mkutano huo.

Rais huyo mstaafu wa Zanzibar hafichi hisia zake na badala yake anaeleza kuhusiana na vitendo vya wanaCCM kukosa uvumilivu wa kisiasa "uvumilivu unakushindeni hapa...! na hapa tupo wapi? Katika Mkutano Mkuu wa CCM, si mnaona?" anasema.

Anawataka wanaCCM hao wajifunze uvumilivu akiamini kuwa wanaweza, tena wanaweza vizuri sana na anawahoji iwapo maoni hayo wanakusanya wao CCM, na vipi wasiwaache waliopewa jukumu kutekeleza wajibu wao na wao kusubiri matokeo.

"Watu waachwe watu wafanya kazi yao kisha tutajua, lakini jambo la kushangaza wakitokea watu wakatoa maoni tofauti hao wanaitwa majina ya ajabu," anasema.

Anauliza vipi iwe nongwa na mtu aitwe majina ya ajabu jambo ambalo anasema sio haki wala utu na mambo kama hayo hayapo katika msingi ya TANU na ASP, vyama ambavyo vimezaa CCM.

Karume anadai kuwa Zanzibar kuna watu ambao wanawatisha wenzao kuwa mawazo yao yana lengo la kurejesha utawala wa kisultan Zanzibar.

Anasema kuwa chama hicho hivi sasa kina vijana wadogo wengi ambao hawajui kitu kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa na wanatakiwa kujifunza kwa watangulizi wao, jambo ambalo wengi hawalifanyi.

"Vijana wapya mlioingia jifunzeni kutokana na viongozi wenu waliowatangulia ili muimarishe chama chenu na matumaini ya chama chenu yapo mikononi mwenu," anasema.

Karume anasema ukweli kuwa kuna maelfu ya wanaCCM ambao ni majeruhi wa kisiasa ambao kutokana na maoni au michango yao wakati wa kujadili hoja mbalimbali likiwemo suala la Katiba.

Mifano ipo ya wahanga wa mfumo huo mbovu ndani ya chama lakini la msingi ni kuwa huyo anayesakamwa kutokana na kutoa maoni yake katika Katiba anafanyiwa hivyo kwa faida ya nani na ili iweje?

Karume ana hoja na hata wanaopingana na maoni yake wanajua hilo na hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachagizwa na ukweli kuwa kuna wajasiriamali ambao wameijingiza katika siasa, wakiwamo vijana na hata watu wazima ambao hawajui dhana nzima ya siasa.

Pia watu hao ndio ambao hawajui chimbuko la chama wanachodai kuwa wao ni wanachama, kilipo na wapi wanaweza wakakipeleka kwani misingi ya TANU na ASP.

Misingi ya vyama hivyo inatajwa kuwa ni pamoja na pamoja na kupigania na kudumisha uhuru na raia wake.

Kulinda heshima ya kila binadamu kwa kufuata ipasavyo kanuni za tangazo la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 na kupinga ubaguzi wa namna yoyote na kuiwezesha nchi kuondoa ujinga, umaskini na magonjwa kwa njia ya kushirikiana.

Karume anaposema vijana wa sasa hawajui lolote anajua anachokisema kwani wanachama wanapovunja kanuni na Katiba ya chama chao kwa sababu yoyote ile ni wazi kuwa wanaofanya hivyo kwa maslahi binafsi na wala si ya umma.

Chuo cha Siasa Kivukoni au taasisi nyingine ya namna ile iwapo ingekuwepo na kutumika kama ilivyokusudiwa awali ni wazi kuwa hali ya wengine kunyooshewa vidole kutokana na kutoa maoni yao katika hoja mbalimbali ikiwemo ya Katiba isingekuwepo.

Pamoja na yote, wanaCCM na hata wanasiasa wengine lazima wakubali kuwa kila mmoja ana haki ya kuwa na maoni yake katika masuala mbalimbali, hivyo sio busara kuminywa uhuru na haki za watu ambazo zimeainishwa katika Katiba na matamko ya umoja wa mataifa.No comments: