Friday, November 23, 2012

SERIKALI IMEWATOSA WAKULIMA WA KOROSHO

ZIARA ya siku moja mkoani Mtwara aliyofanya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana juzi imedhihirisha pasipo shaka kwamba Serikali ya chama hicho ndiyo kikwazo kwa maendeleo ya wakulima wa zao la korosho hapa nchini. Kiongozi huyo alipigwa butwaa baada ya kubaini kwamba viwanda 12 vya Serikali vilivyonunuliwa na vigogo, wakiwamo wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi serikalini vimefungwa na kugeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia mazao.


Moja ya mambo yaliyomchefua kiongozi huyo ni wananchi mkoani humo kuendelea kukabiliwa na umaskini wa kutisha kutokana na ukosefu wa ajira baada ya viwanda hivyo kufungwa, huku maghala ya viwanda hivyo yakiwa yanahifadhi korosho ambazo hazijabanguliwa zikisubiri kupelekwa katika viwanda vya nchi za Asia ambavyo vinatoa ajira kwa maelfu na maelfu ya wananchi wa nchi hizo.

Sisi tunampongeza kiongozi huyo wa CCM kwa kufanya ziara hiyo na kujionea mwenyewe jinsi wananchi mkoani humo wanavyoendelea kuteseka na kuishi maisha ya udhalilishaji katika nchi yao. Kinana amejionea mwenyewe jinsi Serikali ya chama chake ilivyovuruga uchumi wa mkoa huo kwa kula njama na baadhi ya wafanyabiashara na wanasiasa kuuziana viwanda vya korosho kwa bei ya kutupa. Viwanda hivyo vilitelekezwa na wamiliki hao baada ya kugundua wangepata faida kubwa kwa kuuza korosho nje ya nchi kabla hazijabanguliwa.

Hicho ndio chanzo kikubwa cha umaskini unaoendelea kuwatesa wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani, kwani kuua viwanda vya korosho kulisababisha pia kuzorotesha kilimo cha zao hilo lenye thamani kubwa katika masoko ya dunia. Matokeo yake ni kwamba wamiliki wa viwanda hivyo walibadilisha mbinu na kuwa walanguzi wakubwa wa zao hilo, tena kwa kuwalipa wakulima hao fedha kiduchu.

Kwa kuua viwanda vya korosho, wakulima wengi wa zao hilo waliachwa njia panda, kwani walanguzi walihifadhi korosho hizo maghalani bila kuwalipa fedha na kwa wakati. Hali hiyo ndiyo iliyozaa utapeli ambao sasa umepewa jina la ‘stakabadhi ghalani’, kwamba wakulima wanauza korosho lakini wanapewa ahadi tu badala ya fedha, huku wakiamrishwa kusubiri malipo wakati wa kile wanachokiita ‘msimu wa ununuzi wa korosho’.

Wananchi hao wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, lakini watendaji wa Serikali na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Korosho na vyama vya ushirika wamekuwa wakiweka pamba masikioni kwa sababu wengi wao wana masilahi binafsi katika biashara hiyo. Siyo siri kuwa, wao na wafanyabiashara ambao wengi ni wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho ni pete na kidole.

Ndiyo maana wananchi waliohudhuria mkutano uliohutubiwa na Katibu Mkuu huyo wa CCM juzi mkoani Mtwara walipaza sauti zao kwa hasira na kuwazomea mawaziri wa Serikali walioandamana na kiongozi huyo. Hasira za wananchi hao ambao maisha yao yamekuwa duni kwa miongo mingi sasa zilisababisha waziri anayehusika na kilimo, Christopher Chiza aamriwe kubaki Mtwara kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya wakulima hao wa korosho.

Yafaa ifahamike bayana hapa kwamba Serikali isifanye makosa ya kuyaona matatizo hayo sugu ya wakulima wa korosho kwa kutumia mboni za kisiasa. Na kama tulivyoeleza hapo juu, matatizo hayo pia yanawakabili wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi na Pwani, hivyo Serikali lazima iweke mikakati endelevu itakayowakwamua wakulima wa zao hilo kwa kuhakikisha viwanda hivyo vinafufuliwa au vinarudishwa serikalini. Wananchi katika mikoa hiyo wanataka ajira na bei nzuri ya zao hilo la korosho ili nao waishi maisha ya heshima na neema, badala ya kuishi kama wakimbizi katika nchi yao.

Katibu Mkuu huyo wa CCM asiishie kutoa ahadi za kupata suluhisho la matatizo hayo. Kwa kuwa imedhihirika kwamba Serikali ya chama chake nayo ni sehemu ya tatizo, chama chake kitekeleze nadharia ya kuisimamia Serikali hiyo kwa vitendo. Tunategemea kwamba vigogo walioua viwanda hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za uhujumu uchumiMWANANCHI

No comments: