Tuesday, November 27, 2012

MUUNGANO WATAWALA MAONI YA KATIBA

WANANCHI na wakazi wa Zanzibar wameligeuza maoni ya mabadiliko ya Katiba kuwa jukwaa la kujadili mambo ya Muungano na kero zake.


Maoni mengi yanayotolewa yanahusu muundo wa Muungano kuliko masuala mengine yaliyomo katika Katiba, kama haki na wajibu wa raia, haki na wajibu wa serikali, ulinzi na usalama, madaraka ya umma, madaraka ya Rais, madaraka ya Bunge na Mahakama.

Kinachozungumzwa na walio wengi ni muundo wa Muungano, kwamba wanataka Serikali ya Tanganyika ijipambanue na iwe na mamlaka yake kamili, kisha Zanzibar nayo iwe na mamlaka kamili na baadaye ndiyo nchi mbili ziketi kuamua kuunda muungano kwa baadhi ya mambo.

Suleiman Juma Suleiman, mkazi wa Kianga alihoji ilipo Tanganyika na kwanini Watanganyika wenyewe hawaidai nchi yao.

“Tanganyika haionekani, iko wapi? Itoeni kwanza Tanganyika ndipo tuzungumze masuala ya Katiba na masuala ya Muungano,” alisema Suleiman.

Ramadhan Faki mkazi wa Kianga, alisema hivi sasa Wazanzibari wengi wanataka serikali yao iliyo huru na yenye uamuzi wa mambo yote ya ndani na ya nje, hasa kwa sababu wanaona kama viongozi wao hawawezi kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano.

Hassan Mohamed Abdallah mkazi wa Kianga alisema yeye anataka Serikali ya Tanganyika irudi, ndipo wazungumzie masuala ya kuimarisha muungano.

Kwa wale waliozungumzia haki za binadamu wengi wao wanaelezea unyanyasaji unaofanywa na polisi.

“Tumechoka vipigo, jambo si jambo bakora zinatembea, sasa kwani hawa askari kutoka Bara wameletwa Zanzibar kulinda wananchi au kutukomesha?” alihoji Haji Ali Haji.

Haji alisema yeye anaamini wananchi wanayo haki ya kutoa mawazo yao kuhusu serikali yao au jambo lolote linalohusu maslahi yao.

“Sisi (wananchi) tunao uhuru wa kutoa mawazo, sasa kwanini tunaposema kile tunachokitaka, tunapigwa na kunyanyaswa?” alihoji Haji.


MWANANCHI

No comments: