Monday, November 26, 2012

MAKAZI YA MACHEL, MUGABE YALIVYOTELEKEZWA NACHINGWEA
Jengo ambalo alikuwa anaishi Samora Machel. 

KILOMETA zipatazo 34 kutoka makao makuu ya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, lipo eneo maarufu linalojulika kama Farm 17.


Katika eneo hili hivi sasa kuna shule ya Sekondari iliyoazishwa na wananchi kama hatua ya kuyaokoa majengo ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu, hivyo kugeuka kuwa makazi ya wanyama wadogowadogo na kuzongwa na vichaka.

Ni makazi ya waliokuwa wapigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika, zikiwamo Msumbiji, Angola na Afrika ya Kusini ambazo kwa miaka kadhaa zilihenyeshwa na Makaburu waliokuwa wakiendesha siasa za ubaguzi wa rangi, pia Zimbabwe ambayo olikuwa chini ya utawala wa Waingereza hadi 1980 ilipopata uhuru wake.

Hapa ni mahali walipowahi kuishi wapiganaji wa vita ya ukombozi wakiwamo Rais wa sasa wa Zimbabwe, Robert Mugabe na viongozi wawili wa Msumbiji ambao wote ni marehemu kwa sasa, Edward Modline na mrithi wake, Samora Machel.

Kwa maana hiyo, unapozungumzia harakati za uhuru au ukombozi Kusini mwa Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa ziliongozwa na Tanzania chini ya Hayati Mwalimu Nyerere, huwezi kukosa kutaja wilaya ya Nachingwea, hususan eneo la Farm 17.

Hali ilivyo

Hata hivyo eneo hili licha ya kuwa sehemu ya historia hii muhimu ya Bara la Afrika, ni kama limetelekezwa na laity kama siyo busara ya wakazi wa Nachingwea kuligeuza kuwa kitovu cha elimu kwa kuanzisha shule ya Sekondari, basi lingeweza kufutika.

“Naamini kama Samora na Nyerere wangekuwa hai eneo hili lisingeachwa hivi kwani wangelithamini na kulienzi,” anasema mmoja wa wananchi wanaoioshi pembezoni mwa Farm 17.

Kauli hiyo ni kati ya kauli nyingi zinazotolewa na watu ambao wanaonekana kukatishwa tama na hali ilivyo katika eneo la Farm 17, kutokana na kutoeziwa ipasavyo.

Wakazi hawa wa Lindi na hasa wale wa wilayani Nachingwea baadhi yao wanakumbuka walivyoishi kwa wasiwasi wa kushambuliwa na Makaburu, ambao wakati wote walikuwa wakiwasaka wapiganaji wa vita ya ukombozi.

Hivyo kutelelezwa kwa majengo yaliyokuwa makazi ya viongozi wakuu wa nchi, kuliwafanya wapate mawazo ya kuyatumia kwa ajili ya kuanzisha shule ya Sekondari kupitia uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea.Viogozi wanena

Mkuu wa shule ya Sekondari hiyo ya ya Farm 17, Longinus Nambole anasema eneo hilo kwa sasa linapata uhai kwa kuwa kuna shule.

Hata anasema baadhi ya viongozi wa nchi ambazo wakuu wake waliwahi kuishi hapo, wamekuwa wakifika na kutoa ahadi mbalimbali za kulifanyia marekebisho lakini ahadi hizo hazijatekelezwa hadi sasa.

“Hata Serikali yetu ya Tanzania haionyeshi kama hili ni eneo muhimu maana hakuna jitihada zozote zinazofanyika kutunza majengo haya,”alisema Nambole.

Nambole anasema Wizara ya Maliasili na Utalii, pia iliwahi kuaihidi kwamba ingeliendeleza eno hilo ili kulinda historia yake lakini ahadi hiyo haijatekelezwa hadi sasa.

Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Regina Chonjo yeye anasema hali ya majengo hasa lile alimokuwa akiishi Marehemu Machel ni mbaya kwani yemeanza kubomoka hasa barabara ya chini ya ardhi ambayo inahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Chonjo anasema katika njia hiyo ya chini kwa chini, ukarabati unaopaswa kufanyika ni kuweka umeme na taa kuanzia kwenye nyumba hadi lilipo handaki ambako alikuwa akijificha Machel.

“Tunakiomba kitengo cha mambo ya kale kukarabati lile jengo na kusafisha pango na kuweka taa ili kuvuta watalii, kama tukipaendeleza tunaweza kupata watalii wengi ambao naamini wanapenda kuona sehemu hii,”anasema Chonjo.

Aidha mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kupitia halmashauri ameigiza kutenga kiasi cha fedha kwenye bajeti yake ili kutengeneza eneo hilo wakati wakisubiri wizara husika kuliendeleza.

Mkazi wa kijiji cha Farm 17 Judith Bathromeo alisema kuwa iwapo eneo hilo litaboreshwa, litazalisha ajira kwa wananchi wa kijiji hicho kwani lingevuta watalii kutoka maeneo mbalimbali Duniani na pia kuchangia pato la taifa.

“Tunashangaa watu kila siku tunalia ajira hakuna, ajira hakuna, maisha magumu kama hapa wangepatengeneza ingekuwa nafasi ya wengi wetu kujipatia ajira, lakini ndiyo hivyo kama unavyoona hakuna jitihada yeyote ya kulienzi eneo hili,”alisema Balthoromoe.

Alidai kuwa mabalozi na viongozi ambao waliwahi kutembelea eneo hilo na kuahidi kusaidia ukarabati wake ni Balozi wa Msumbiji nchini, Jose Rui Amaral wa Msumbiji, aliyekuwa Balozi wa Zimbabwe nchini, Chipo Zindoga, Waziri Mkuu wa Msumbiji Carlos Cassa na Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Josenio Henriques.

Hata hivyo Balthoromeo anasema ahadi hizo hazijawahi kutekelezwa.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Farm 17 Juma Alli alisema kuwa serikali ya kijiji hicho imejiwekea mikakati ya kulinda na kuheshimu mipaka ya maeneo kwa kutofanya shughuli za zozote za kibinadamu.

Historia ya Farm 17

Eneo la Farm 17 lipo umbali kilometa zipatazo 34 nje kidogo ya makao makuu ya wilaya ya Nachingwea, barabara inayoelekea Kilimarondo, ikipakana na wilaya ya Masasi.

Wapigania uhuru wa nchi za Msumbiji, Zimbabwe, Angola na Afrika ya Kusini walipata mafunzo na mbinu za kupambana na wakoloni na makaburu hadi nchi zao zilipofanikiwa kupata uhuru.

Waliacha majengo mbalimbali ya kihistoria likiwemo jengo alilokuwa anaishi Rais wa Msumbiji Marehemu Machael ambalo lilikuwa na njia ya chini ya ardhi yenye urefu wa kilometa zipatazo kumi.Njia hii inaazia kwenye jengo hilo hadi kwenye handaki ambalo linasemekana ndipo alipokuwa anaishi, kisha kuendelea hadi kwenye uwanja mdogo wa ndege ambao alikuwa anautumia pale alipokuwa akisafiri.

Historia ya Farm 17 inaanzia miaka ya 1947 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wakati Serikali ya wakoloni wa Uingereza iliamua kufuta baadhi ya ajira kwa waliokuwa askari wa vita hyo na kuamua kuwatafutia ajira mbadala.

Serikali hiyo ya wakoloni iliamua kuwatafutia ajira kwa kuwakopesha wapiganaji hao fedha na kuanzisha mashamba ya karanga katika maeneo ya Nachingwea kupitia kampuni ya John Molem.

Kupitia mpango huo mashamba 18 yalianzishwa yakipewa majina kuanzia mashamba kuanzia Farm one hadi Farm 18. Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali mashamba hayo hayakuendelea na Waingereza hao kuamua kuondoka na kwenda kuishi Afrika ya Kusini.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru Desemba 9, 1961 Serikali iliamua kutumia eneo la Farm 17 kuwa kituo cha kufundishia wapigania uhuru wa nchi zilizo Kusini mwa Afrika.

Viongozi mbalimbali wapigania uhuru katika nchi hizo wakiwamo Komredi Mondlane, Komredi Machel na Komred Mugabe waliishi kwa kujificha na kupewa mbinu mbalimbali, hivyo walichana kumbukumbu ambazo ni muhimu kwa historia ya ukombozi wa Afrika.

Baada ya nchi hizo kufanikiwa kujipatia uhuru eneo hilo lilikabidhiwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 41, baadaye wanajeshi hao waliondoka.

Hatua ya JWTZ kuondoka ilitoa mwanya wa majengo hayo kuhujumiwa kwani watu wasiofahamika walianza kuiba baadhi ya vifaa ikiwa ni pamoja na kung’oa mabati, huku eneo hilo likizungukwa na msitu mnene.

MWANANCHI

No comments: