Thursday, November 22, 2012

KUELEKEA 2015 -1

Makala hii niliwahi kuandika wakati wa maadhimisho ya miaka 12 baada ya Mwalimu. Nimeihariri kidogo sijabadili maudhui yake. Nieamua kuirudia tena katika mtiririko wa ghilba na hila za CCM za kuwahadaa watanzania kuelekea 2015. Huu ni mtazamo chanya wenye kujenga na kamwe isisomeke kwamba mwandishi anaeneza propaganda za chuki dhidi ya Chama Tawala. Makala za kuelekea 2015 zimeanza rasmi.

Na Baraka Mfunguo,

Ni miaka kadhaa baada ya  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aghalabu wapo wale ambao roho zao zinawauma wanapoona taifa linapozizima kwa kumkumbuka Mwalimu na wapo wale ambao ndio sisi wengi wetu tunaoamini kwamba Mwalimu alikuwa hazina kubwa katika taifa hili na historia inavyoelekea inaniashiria kwamba hatutaweza kumpata kiongozi aliyekuwa na haiba ya kipekee kama yeye. Labda Mwenyezi MUNGU ashushe rehema yake atuletee mkombozi mwingine na tuombe Mungu atupe hekima tusimsulubishe kama wanavyosulubishwa wengine kwa shinikizo la mabeberu kwa kigezo cha kutetea demokrasia ili hali wakihalalisha uharamia wao.

Hivi sasa Chama cha Mapinduzi kimeanza kukumbuka blanketi wakati jogoo wa alfajiri keshawika mara kadhaa, adhana imeshapigwa watu wameshaswali, jua la alfajri lishaanza kukolea wao wamekumbatia blanketi. Kimsingi CCM ilitakiwa kuyatekeleza haya yote kuanzia mwanzo kilipopewa dola. Kinachojitokeza sasa hivi ni hila zao na baadhi ya watu wenye nia na malengo ya kupata vyeo mwaka 2015. Kinachofanyika hivi sasa ni kama kuwahadaa watanzania. Swali la kuwauliza hawa . KWA NINI SASA? ama kwa kimombo WHY NOW?

Serikali ya CCM baada ya Mwalimu imeonyesha udhaifu mkubwa katika Uongozi, Maadili na Utaifa katika nyanja mbali mbali hata wale ambao tulikuwa tunawategemea wangeyaendeleza yale mazuri ya Baba wa Taifa wamekuwa wa kwanza kuyapiga vita kwa kigezo cha ubinafsi na uchu wa madaraka. Serikali yetu leo ina vyanzo vingi vya mapato kulinganisha miaka ya Utawala wa Julius Kambarage Nyerere . Lakini cha kushangaza serikali hii imekuwa omba omba ya kutupwa. Pamoja na misaada ya wahisani, kodi mbalimbali, machimbo mbalimbali ya rasilimali za nchi bado kipato cha mwananchi kipo duni, mfumuko mkubwa wa bei, elimu ya kununua tena isiyokuwa na ubora pamoja na huduma mbovu za afya kote nchini. Tujiulize fedha zote wamepeleka wapi?

Baada ya Uchaguzi wa mwaka 1995 ndipo tulipoanza kushuhudia utitiri mkubwa wa mashirika ya umma kufilisika. Wapo wale ambao walisema kwamba mashirika hayo yalikuwa yakitegemea ruzuku za serikali na yalikuwa hayajiendeshi kwa faida na kuwaaminisha Watanzania hivyo. Tumeshuhudia mashirika mengi mfano Simu yakiwa hoi taaban na mengine mengi, lakini utaaban huo ukiyaneemesha mashirika binafsi ambayo yako katika sekta moja.

Ukweli ni kwamba mwaka wa uchaguzi wa 1995, serikali ya  CCM ya awamu ya pili haikuwa na fedha yoyote kutokana na serikali kutokuwa na mipango madhubuti ya ukusanyaji wa kodi kutokana na kukithiri kwa rushwa. Kutokana na hilo, pesa nyingi ya kampeni zao za uchaguzi zilitokana na mafungu  ya mitaji kutoka mashirika ya umma pamoja na vyanzo vingine. Kwa kigezo cha kisiasa, mashirika mengi ya umma yakafa ndugu zetu wakakosa kazi na mafao yao kwa kigezo cha CCM kukaa madarakani.

Ninakumbusha tena na tena juu ya misingi bora aliyoiweka baba wa taifa ili mwenye macho aone na mwenye masikio na asikie. Na mwenye kufahamu kama ameikosea nchi hii katika dhamira yake awaombe radhi watanzania kwa usaliti waliotufanyia. Kwa ufupi CCM iwaombe radhi watanzania kwa usaliti wao. Ni wakati wa utawala wao tumeona na kushuhudia vurugu za kidini, ni wakati wa utawala wao tumeona na kushuhudia chuki za kikabila na ubaguzi wa wazi wazi, ni wakati wa utawala wao tumeshuhudia nyumba za ibada zikichomwa moto na ni wakati wa utawala wao tumeshuhudia matatizo ya mipaka na yale ya Muungano.

Tumekuwa "Banana Republic" serikali isiyoheshimiwa ndani na nje ya mipaka kwa sababu hata maadui zetu wameshaujua undani na udhaifu wetu. Haya ndio matunda ya Azimio la Zanzibar lililofanywa na wachache wenye uchu na haraka na tamaa ya mbio za panya na sasa tuko ukingoni.

Ndio ni wasaliti hawa kwa kupitia wabunge wao na wawakilishi wao wameshindwa kusimamia ukweli na kubakia kama "Rubber Stamp" kuyafanya hata yale ambayo wao binafsi wasingependa kufanyiwa ali mradi wao wapate mkate wa kila siku na maisha mazuri kwa familia zao. Tuwaulize je siku moja hawatakufa?, Wataishi milele? , Watatuhadaa milele? Mikataba mingi ya nchi hii yenye kuleta tija na neema kwa wananchi imegeuka shubiri kwa Watanzania chini ya Utawala wa CCM.

Leo wanawahadaa wana Mtwara juu ya gesi yao asilia na mafuta kupitia watendaji wenye asili ya Mtwara kwamba watapata neema ilihali watendaji hao wamejilimbikizia ardhi, mali za kutisha za maeneo ya Mtwara wao na vibaraka wao na ushahidi uko wazi. Leo wanawahadaa wana Mtwara pamoja na vibaraka wao walionunuliwa RAV 4 na SANLG kupiga porojo mtaani badala ya kuwapa elimu. Leo wanawahadaa wana wa Mtwara na kuibua hoja ya ukabila dhidi ya wengine wanaogundua hila zao pale wanapoibua masuala ya msingi. Tusubiri 2015  umma wa Watanzania uamue


Nitajikita zaidi katika misingi mikuu ya Azimio la Arusha nayo ni falsafa nzima ya Ujamaa na Kujitegemea pamoja na matokeo yake nayo ni Utaifishwaji wa njia kuu za uchumi , Vijiji vya Ujamaa changamoto zake nikihusisha na muelekeo wa Tanganyika katika miaka 50 ya uhuru

Kama inavoelezwa na wachambuzi wengi, misingi ya Azimio la Arusha ilijikita zaidi katika umiliki wa njia kuu za Uchumi pamoja na Uchumi wenyewe mikononi mwa wananchi ili kujenge jamii yenye usawa, jamii yenye kuheshimiana pamoja na kuthamini utu wa mtu. Azimio la Arusha la mwaka 1967 lilikuja kama mbadala wa kuwawezesha wananchi wengi kupata fursa mbalimbali katika ujenzi wan chi yao na ninaweza kusema katika nyakati zile watu walikuwa wana uzalendo na utaifa wa kweli. Yote hii ilitokana na miongozo na misimamo madhubuti aliyokuwa nayo mwalimu.

Katika hayo kuna falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo ilijikita katika misingi ya utu pamoja na utamaduni wa Mwafrika hususan Mtanzania iliyojikita katika familia na maisha ya kidugu kwa ujumla. Watanzania wote tuliitana ndugu mchaga kwa mzaramo….Mhaya kwa Mjita……Mngoni kwa mhehe…..Mmakonde kwa Mmwera na hata endapo kutatokea mtu yeyote ambaye hana asili ya kitanzania ama kwa rangi yake au vinginevyo, madhali ni Mtanzania, alikuwa ndugu na alipata fursa ambayo waliipata watanzania wengine. Hivyo basi twaweza kusema kwamba sera ya Ujamaa ilikuwa ni moja ya mwongozo mkubwa ambao ulilenga katika kutuletea maendeleo katika misingi ya Uhuru, Umoja na Usawa. Kwa mujibu wa Mwalimu, alisema ni muhimu kuwapo na usawa kwani hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuwawezesha watu kushirikiana na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Ni vyema kukawa na uhuru kwa sababu mtu hawezi kuhudumiwa na jamii . Kila mtu ilimlazimu afanye kazi ili kupata ujira halali. Na ni lazima jamiii iwe na umoja utakao wawezesha wananchi kuishi kwa amani kufanya kazi kwa pamoja na pia usalama wa uhakika wa watu pamoja na mali zao.SERA YA UTAIFISHWAJI WA NJIA KUU ZA UCHUMI NA CHANGAMOTO ZAKE

Sera ya utaifishaji wa mali ililenga katika kukuza uchumi wan chi. Ikumbukwe kwamba moja ya sababu iliyochochea vuguvugu la kudai uhuru lilikuwa ni kutokuwa na usawa katika umilikaji wa njia kuu za uchumi baina wa Waafrika na Wakoloni. Kwa kiasi kikubwa Wakoloni walitugawa kwa madaraja kutokana na rangi ya ngozi zetu na hata katika fursa mbalimbali ilikuwa hivyo hivyo. Kutokana na sera ya utaifishwaji wa mali masuala yote ya kiuchumi yalikuwa yamegawanywa katika makundi matatu mosi yale ambayo yalisimamiwa moja kwa moja na serikali ama nchi, pili yale ambayo serikali ilikuwa na umiliki mkubwa wa mtaji wa uwekezaji na tatu asasi binafsi ambazo zingweza kuwekeza kwa kuishirikisha ama pasipo kuishirikisha nchi katika umiliki wa mtaji wa uwekezaji Baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha Mwalimu Nyerere alitangaza moja kwa moja kutaifishwa kwa mali ikijumuisha mabenki yote, viwanda vikubwa, viwanda vya usindikaji vilivyotokana na Kilimo. Sehemu ya sekta ya Biashara ilitaifishwa pamoja na umiliki wa asilimia sitini wa uzalishaji wa kilimo cha mkonge (Arkaide 1973:37). Mpaka mwisho wa mwaka 1967 Serikali ilikuwa imeshamiliki njia zote kuu za uchumi.

Changamoto iliyojitokeza ilikuwa ni kukubalika kwa sera ya utaifishaji wa njia kuu za uchumi kwenda mikononi mwa serikali kimataifa. Kulikuwa na mkanganyiko mkubwa wa baadhi ya nchi katika kuukubali ama kuukataa mkakati huu. Kwa mfano nchi zote za Kiskandinavia ziliufurahiaa mkakati huu na kuuona kuwa wa manufaa kwa nchi wakati mataifa mengine ya magharibi hayakuufurahia mpango huu na mataifa hayo ndiyo viranja wakuu wa uchumi huria. Kwa mfano banki kubwa maarufu za Uingereza kama vile Barclays, Standard, National na Grindleys hazikutoa ushirikiano na lengo lao kuu ilikuwa ni kuhakikisha mashirika ya umma pamoja na mabenki yanakufa. Hili liliendana sanjari na kuwaondoa wafanyakazi wao pamoja na kuwapa masharti na maelekezo ambayo yalilenga kabisa kushusha ari na kiu ya watanzania katika kuumiliki uchumi wao ikiambatana na kauli za kejeli kuhusiana na mauzo ya nje ya mazao ya chakula na biashara yananyozlishwa nchini. Lengo lao kuu lilikuwa ni kuhakikisha sera hii haifanikiwi kwani kufanikiwa kwake kungeweza kuzishawishi nchi nyingine za kiafrika kuiga hususan Kenya na Uganda ambazo zilikuwa zinafuata mfumo wa kibepari. (Coulson, 1985:41)

Pamoja na kwamba katika Azimio la Arusha kulikuwa na sera ya kutaifisha njia kuu za uchumi na kumilikiwa na wananchi, Asilimia kubwa ya Asasi zilizotaifishwa na kuwa za serikali ziliingia ubia na kampuni za nje ambazo zilikuwa wamiliki wa awali kabla ya kutaifishwa kwa mfano Kampuni kubwa ya kimataifa ya ushauri kwenye masuala ya Uongozi na uendeshaji ya Mckinsey ilipatiwa mkataba wa kusimamia na kuratibu usimamizi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Mkonge, Shirika la Bandari la Afrika Mashariki (Loxley na Saul, 1975:72). Ni kutokana na sababu hizi wachambuzi wengi wanasema kwamba, pamoja na kuwa na sera ya kutaifisha njia kuu za uchumi kwenda mikononi mwa wananchi kufanyika, maamuzi bado yalibaki mikononi mwa wageni . Shivji anatanabaisha kwamba , mchakato wa kutaifisha njia kuu za uchumi haukuipatia serikali/wananchi fursa ya kumiliki njia kuu za uchumi na wala kufanikiwa kuzuia muingiliano wa mtaji wa makampuni makubwa ya nje katika sera ya uchumi na siasa ya Tanzania (Shivji 1973)

Viashiria vya awali kuhusu maendeleo baada ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi kwenda mikononi mwa wananchi ulikuwa chanya . Moja ya Malengo ya kutaifisha njia kuu za uchumi yalikuwa kuhakikisha mtaji unaozalishwa ndani ya nchi ni wa kutosha kwa matumizi ya wananchi kwa kupunguza kiwango cha mtaji kinachosafirishwa nje ya nchi. Na hii ilisaidia kupunguza mfumo tegemezi wa kifedha wan chi dhidi ya asasi kubwa za mikopo za kidunia mathalan IMF. Benki ya Tanzania ilifanikiwa kudhibiti na kusimamia hifadhi ya hazina ya Taifa dhidi ya pesa ya Mwingereza ya Sterling pound na kujihakikishia kutoshuka thamani ya shilingi ya Tanzania jambo ambalo lisingewezekana kabla ya Azimio la Arusha la mwaka 1967 (Nnoli 1978 :213).

Kiashiria kingine kikubwa cha mafanikio cha sera hii ya Utaifishwaji wa njia kuu za uchumi kilikuwa ni kuongezeka kwa ukusanyaji na udhibiti wa rasilimali za ndani ambapo mwaka 1964 kiwango cha mtaji kilikuwa ni Asilimia 15% ya GDP mwaka 1969 iliongezeka kwenda asilimia 20% na kupaa mpaka asilimia 26% mwaka 1970. Mafanikio mengine yalikuwa ni kuongezeka kwa mapato ya nchi yaliyotokana kwa sekta ya viwanda pekee kutoka shilingi milioni 81.9 mwaka 1968 mpaka shilingi milioni 134.5 mwaka 1969 (The United Republic of Tanzania, 1970:16)

Hata hivyo kulikuwa na changamoto za msingi na za wazi kabisa ambazo zilibainika wazi wakati sera hii ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi ikiwa inatumika Serikali haikuweza kusimamia na kuimarisha umiliki wake wa njia kuu za uchumi kwa kujenga uchumi imara wa kujitegemea hususan katika sekta ya viwanda kama inavyobainishwa na mtafiti Dianne Bolton (1985:154) katika utafiti wake uliohusiana na utaifishwaji wa sekta ya viwanda uliotokana na zao la mkonge Tanzania. Bolton anahitimisha kwa kusema “dhana ya utaifishwaji kama inavoainishwa kwenye uzalishaji wa zao la mkonge ina mkanganyiko mkubwa hususan katika kuelekea katika sera ya Ujamaa na kujitegemea.” Hii ilitokana na sekta hiyo haikuwa na uwezo ya kuratibu kusimamia kwa ufanisi na weledi njia za uzalishaji na jamii. Masuala kama ya urasimu na usimamizi kutoka serikali kuu iliongeza mwanya mkubwa wa rushwa pamoja na upotevu wa rasilimali ( Bolton,1985:156).

Mpaka mwaka 1975 ilikuwa wazi kwa watunga sera kwamba maendeleo yote ya ndani na nje ya nchi ambayo msingi wake ulijikita katika utaifishwaji wa njia kuu za uchumi hayatoi suluhisho bora juu ya mustkabali wa maendeleo ya nchi wala njia sahihi za kujenga uchumi imara , ulio bora na unaojitegemea. Baadhi ya wachambuzi na watafiti wanatanabaisha kwamba suala la utaifishwaji wa njia kuu za uchumi umezaa kundi Fulani la watu ambao wanatumia mtaji wa serikali na wananchi wake kwa namna na uelekeo ambao ni wa kibepari. (Shivji 1974, 85-90).

Ni miaka kadhaa sasa baada ya mwalimu kututoka na hali inajidhihirisha wazi kwamba tabaka lile ambalo lilitokana ama na matunda ya sera ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi mara baada ya kubinafsishwa kwa njia kuu hizo wamegeuka na kuwa mabepari na matajiri wa kutisha. Wale ambao walikuwa wakituimbia nyimbo za ujamaa na wale ambao walikuwa wanajifanya wakisema “zidumu fikra za mwenyekiti wa CCM”.Ndio wamegeuka kuwa matajiri wa kutisha pamoja na familia zao huku wakiendelea kujilundikia mali zinazotokana na hujuma katika nchi hii kupitia mikataba mbalimbali feki, wakiwa kama watunga sheria(Wabunge), wakiwa kama wawakilishi, wakiwa kama madiwani, wakiwa kama watumishi wa serikali/Umma. Najua ipo siku umma wa watanzania utawaambia basi Na huo  ndio  utakuwa mwisho wao.

Ni ndani ya CCM ambako kuna uozo mwingi na asilimia kubwa ya walio ndani yake walimsaliti mwalimu kwa kutofanya na kusimamia misingi iliyowekwa. Tujiulize ikiwa CCM imeshindwa kusimamia mashirika yake tu kwa mfano SUKITA na mengineyo itaweza kuisimamia serikali ipi katika  miaka 50 ya uhuru wa nchi? Matokeo yake baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho wamemgeuza mwalimu kama mtaji wao wa kisiasa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.No comments: