Thursday, November 29, 2012

KASHFA JUU YA KASHFA... UOZO JUU YA UOZO


 Na M. M. Mwanakijiji,TANZANIA haiwezi kukosa kashfa za watawala.

Na kwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo ambavyo tunaona jinsi mlundikano wa kashfa unavyozidi kuongezeka huku dalili za watawala kushidwa kuzishughulikia zikiwa dhahiri mbele yetu.

Kabla hatujatulia na kashfa ya mabilioni Uswisi, imeibuliwa kashfa ya upotevu wa mabilioni huko TANESCO na kabla hiyo nayo haijatulia, imeibuliwa kashfa ndani ya jeshi la polisi.

Kashfa hii ya jeshi la polisi ina kila aina ya kukera, kuudhi, kuchefusha, kuaibisha na kwa kila kipimo kukatisha tamaa.

Kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari ni kuwa kuna kundi la wahalifu ambao wamefanikiwa kuwaingiza mjini vijana wa Kitanzania wapatao 200 kwa kuwafanya waamini kuwa wamechaguliwa kujiunga na jeshi la polisi.

Haikuwa tu kwa imani, lakini inaonekana matapeli hao walifanikiwa kutengeneza utapeli wao hadi vijana wakafika Chuo cha Polisi Moshi (CCP) ambapo walipokelewa na uongozi wa chuo, wakafuata taratibu za kupokelewa makuruta (ikiwemo kunyolewa nywele ziwe za kinjagu) na kuanza na mchakamchaka.

Ni siku tatu baadaye ambapo polisi pale CCP waligundua kuwa vijana hao hawakupaswa kuwepo hapo kwani hawakukubaliwa kujiunga na jeshi la polisi!

Kimsingi hakuna ushahidi kuwa waliwahi kuomba na kukubaliwa kujiunga na jeshi la polisi.

Ukiangalia kwa haraka haraka unaweza kufikiria hii ni kashfa moja tu ya vijana kutapeliwa. Kiukweli hata hivyo ndani ya kashfa hii kuna kashfa nyingine kadhaa ambazo zinanifanya nizidi kuamini kama nilivyowahi kuandika huko nyuma uongozi wa jeshi la polisi ulivyo sasa umedumaa kimaono, unahitaji kupanguliwa na kama tungekuwa na viongozi wazuri basi baadhi ya makamanda wa jeshi hili walitakiwa wa kwanza kuvaa nguo za kuhudumia jamii kupitia magereza!

Lakini tuziangalie hizi kashfa ambazo zimefichika ndani ya kashfa hii – uozo ndani ya uozo ili kuweza kuona ni kwanini serikali ya CCM imeshindwa kulijenga upya jeshi la polisi na kuendelea kutafuta jibu la kwanini kina IGP Mwema na Makamishna Paul Chagonja na Mpelelezi Mkuu Robert Manumba wanalindwa na viongozi wa kisiasa.

Kashfa ya Utapeli

Kashfa ya kwanza humu ndani hailihusu jeshi la polisi hasa, lakini inahusu kutumiwa kwa jina la polisi kuweza kufanyika utapeli ambao kama usingekuwa utapeli, labda tungesema ni mkakati kamambe wa kuandikisha vijana kujiunga na jeshi. Kwamba, kuna mtu/watu ambao wameweza kujipanga, wakaenda mikoani, wakaandikisha watu, wakapokea fedha, wakaweza kukodi mabasi na kuwasafirisha watu hadi chuoni na muda wote huo hakuna mtu hata mmoja wa usalama wa taifa au wa polisi aliyeshtuka ni kashfa ambayo inahitaji Said Mwema na Paul Gonja wajiuzulu juzi!

Kwamba vijana wetu ambao maskini wa Mungu wamesoma, lakini hawana ajira na katika umaskini wao wakaona na wenyewe watafute mahali pa kupata kipato halali badala ya kubangaiza mijini.

Kwamba wakapewa nafasi na watu ambao waliamini wanahusiana na jeshi la polisi na wakaenda na kufuata taratibu mbalimbali (hata kama walitoa rushwa – wangapi wanatoa rushwa kurahisisha mambo yao?) ili mradi watoke katika hali ngumu iliyosababishwa na sera zilizoshindwa za chama tawala. Matokeo yake karibu kila mmoja ameingizwa mjini si pungufu ya shilingi milioni moja! Hii ni kashfa ya uonevu na ya aibu kubwa!

Kashfa ya kushindwa kwa inteligensia

Sasa ndani ya kashfa hii kuna kashfa ya kushindwa kwa mfumo wa inteligensia wa kipolisi (police intelligence failure). Jeshi letu la polisi limewahi kujisifia sana kuwa linapata habari za kiinteligensia ambazo zimesababisha mara kadhaa kusitishwa kwa mikutano ya CHADEMA. Mara nyingi polisi wamekuwa wakituaminisha kuwa wana mfumo mzuri wa kiinteligensia ambao umewawezesha kupata taarifa mbalimbali za uhalifu.

Hata hivyo, ushahidi upo wa kutosha kuwa mfumo wao wa inteligensia ni miongoni mwa mifumo mibovu kabisa ambayo inatumika nchini. Ushahidi wa ubovu wa mfumo huu ni kashfa hii.

Kama inawezekana mtu kupanga, kufadhili, na kufanikisha kutapeli vijana zaidi ya 200 kwa kuwatoa mikoani, kuwakodia mabasi, kuwasafirisha hadi Moshi na kuhakikisha wanalala kwenye chuo kikubwa kabisa cha kipolisi nchini kwa karibu siku tatu na wakanyolewa nywele na ndevu basi mfumo wa kijasusi wa polisi umelegea kama mlenda uliooza. Kuelewa uzito wa hili niseme ni sawasawa na atokee mtu, aende nje ya nchi, awasiliane na Ikulu, apange, na kumsarisha mgeni ambaye ni Rais wa Visiwa vya Solomon akapokelewa pale Kipawa na saluti na ngoma juu, halafu mtu huyo akasindikizwa na ving’ora na vimulimuli huku watu wamejipanga mitaani halafu akafika Ikulu, akachekewa chekewa na kukaribishwa ndani kwa dhifa ya kitaifa ambayo inarushwa na TBC1 halafu akalala pale Ikulu – siku ya pili akatembelezwa kuoneshwa jiji – halafu kesho yake wakaambiwa kuwa mtu huyo hakuwa Rais na kuwa kumbe huko Visiwa vya Solomon hata Rais hawana wana Waziri Mkuu!

Hii peke yake ni kashfa ambayo ingemfanya Manumba kwenda ofisini kwake na kuandika bara ya kujiuzulu! Kama huwezi kugundua utapeli wa polisi unaweza kugundua utapeli wa nani?

Kashfa ya Bunge kushindwa kulisimamia Jeshi la Polisi.

Kama mpendwa msomaji umeweza kufuatilia siasa zetu tangu watawala wa wa sasa walipoingia madarakani mara ya kwanza jambo moja limekuwa wazi – taasisi nyingine zote zimekuwa sikiangaliwa kwa ukaribu na kukaliwa shingoni na Bunge isipokuwa vyombo vya usalama.

Havichunguzwi, haviulizwi, havibishiwi. Tumeliona hili kwenye mlipuko wa mabomu Mbagala na ule wa Gongo la Mboto; tumeona kwenye mauaji ya Mwangosi na mauaji ya Watanzania wengi mikononi mwa Polisi.

Wakati naandika makala hii na ndani ya wiki hii tu bila ya shaka Watanzania tumeshasikia kashfa kadhaa za polisi. Ukiondoa hii ya CCP tumesikia kuna polisi amedaiwa kuua raia huko Bukombe na tumesikia kuna polisi ametuhumiwa kubaka binti aliyekuwa rumande huko Mbozi.

Ukijumlisha na mengine hakuna shaka hata kidogo kuwa chombo cha kusimamia hili jeshi hakifanyi kazi vizuri na sasa jeshi linafanya kazi bila kujali matokeo yake (with impunity). Kila likitokea jambo watamtuma Chagonja, watamtuma Manumba, wataitana wenyewe kwa wenyewe, watachekeana, watapigiana saluti na mwisho tunarudi tena katika hali ile ile iliyokuwepo (status quo).

Binafsi naweza kusema pasi ya shaka kuwa Bunge limeshindwa kufanya kazi yake ya kusimamia jeshi la polisi.

Na hili halimuangukii mtu mwingine yeyote isipokuwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mahusiano ya Kimataifa – Bw. Edward Lowassa.

Siweki uzito wa lawama hizi kwa Lowassa peke yake bali kwa Kamati yake nzima ambayo imetaliwa na wabunge wa CCM watupu – CDM yupo mmoja na CUF mmoja.

Wajumbe wa kamati hii pamoja na Lowassa mwenyewe ni Mussa Azzan Zungu, Capt. John Chiligati, Khalifa Suleiman Khalifa, Rachael Mashishanga, Anastazia Wambura, na Cynthia Ngoye. Timu hii kimsingi ndio wanatakiwa kusimamia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama lakini hadi hivi sasa ushahidi uliopo ni kuwa ama hawajafanya ya kutosha au hawajui la kufanya na wamekuwa kimya. Inawezekana vipi mambo yote yanayotokea kwenye jeshi la polisi hakuna hata mmoja wao aliyeleta hoja Bungeni ya kutaka uchunguzi fulani ufanyike? Wakati wenzao wa kamati zingine wanaonekana kukaa na kuwauliza watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali kamati hii sikumbuki kama imewahi kumuita Mkuu wa Jeshi la POlisi, au Chagonja kumuuliza kuhusu Polisi!

Lakini kwangu kinachonitibua zaidi ni kuwa ninapomuona Lowassa akijaribu kujijenga zaidi kama mgombea mtarajiwa chama tawala kuelekea 2015 ninajiuliza hivi polisi itakuwaje chini yake?

Kama leo hii yuko kimya, na haoneshi uongozi wowote kwa kamati yake kuonesha anajali maisha (siyo ajira) ya vijana kadhaa wanauawa mikononi mwa polisi kweli atawajali wakati polisi wakifanya hivyo hivyo yeye akiwa Rais?

Hata mara moja hajaonekana kwenda kwenye matukio haya ya Polisi na raia lakini hakosi kwenda kwenye mialiko ya kuchangia mamilioni! Labda sasa wakati umefika aanze kupewa mwaliko yeye na Kamati yake kufuatilia matukio ya aina hii?

Wamepigwa wabunge na Polisi, wamepigwa wabunge mbele ya polisi, wamejeruhiwa wananchi na wengine kuuawa lakini kweli kamati ya Ulinzi iko kimya? Fikiria kundi la wanyama wetu limetoroshwa kwenda Qatar na ndege ya kijeshi iliyotua usiku nchini na Qatar wamekataa watendaji wetu wasiende kufuatilia wanyama hao (kwa mujibu wa Balozi Kagesheki) na Lowassa na Kamati yake wako Kimya?

Halafu kuna watu wanataka tuamini kuna mtu analengo la kuwa Rais wa nchii kwa vile anajali sana wananchi na raslimali zetu? Give me a break!

Labda akianza kuonesha uongozi kwenye hili wengine wetu tunaweza kubadili mtazamo na kuanza kuona nia yake inatokana na kuwapenda Watanzania na kuwajali na siyo kutaka madaraka ilia pate madaraka kama fulani.

Ni kashfa ya kushindwa kwa jeshi la Polisi kujipanga kisasa

Sasa niweze kusema ndani ya kashfa hii kuna kashfa iliyo wazi pia ambao imeonekana na watu wamekuwa wakizungumzia. Kwa kuangalia kwa haraka haraka bila kufanya uchunguzi mzito ni rahisi kuona kuwa Jeshi la polisi liko nyuma kiteknolojia. Kwamba, halina mfumo mzuri wa kiteknolojia wa kusimamia ukuruta (recruitment) ya maafisa wake. Inawezekana kabisa matatizo ambayo tunayaona kwa mapolisi wetu yanatokana na mfumo mbaya wa ukuruta.

Kama watu wanaweza kutoa maelfu ya fedha na wakaweza kuamini wamepata namna ya kuingia ndani ya jeshi la polisi nabaki kujiulizza hivi hawa wote walioingia sasa waliingiaje?

Kama Polisi hawana mfumo wa kuweza kutambua mara moja kuwa huyu aliyekuja chuoni hayupo katika orodha ya watu wanaotakiwa kuwa chuoni na inachukua siku tatu kwa mtu kula, kujisaidia, kunyolewa na kukimbizwa mchakamchaka ni aibu ya mfumo vile vile.

Lakini kwa wale ambao tunalifuatilia jeshi la polisi kwa karibu tunafahamu jinsi ambavyo fedha nyingi zimekuwa zikitengwa hasa kuanzia 2007 kwa ajili ya kuboresha jeshi la polisi. Sasa kama fedha zote hizo hazijaweza kulipatia jeshi mfumo wa kisasa wa kuangalia na kuwasiliana basi kuna mtu anakula hizo hela mahali!

Labda watu wako busy kutafuta wawekezaji wa kutoka nje ili wakodishe kambi za polisi pale Mabatini Mwanza, Mabawa Songea, Chang’ombe Dar n.k!!

Sasa, jeshi la polisi haliwezi kufanyiwa mabadiliko chini ya serikali ya CCM. Kama Rais Kikwete alivyosema kwenye mkutano mkuu wa CCM kuwa CCM isitegemee sana jeshi la polisi kutetewa labda kwa muda mrefu jeshi hili limekuwa likijitafutia ujiko zaidi kwa kuipendezesha CCM zaidi kuliko kitu kingine chochote. Na pamoja na kauli ya Rais Kikwete jeshi la polisi bado limekaa ki CCM ndio maana baadh ya watu wanaliita ni “POLICCM”.

Njia pekee ya kuleta mabadiliko ni kuvunjwa kwa jeshi hili na kama nilivyowahi kuandika huko nyuma naamini ni CHADEMA tu ambao wamewahi kuwa waathirika wakubwa wa jeshi hili ambao wanaweza kulivunja na kulipanga upya ili kulileta kwenye karne ya ishirini na moja.

Mabadiliko hayo yatahakikisha kuwa jeshi letu linakuwa ni rafiki wa raia, linalozingatia haki na usawa, na ambalo ni dogo, la kisasa na ambalo madaraka yae yanapunguzwa ili kuunda vikosi vya polisi vya mikoa au mahali (local and regional police authorities) ambavyo havifungamani na makao makuu ya Taifa bali na mahali walipo.

Ni kwa sababu hiyo basi ni jukumu la kila Mtanzania kuona kuwa CCM inaondolewa ili hatimaye tuingize madarakani chama ambacho kitaunda jeshi la polisi la kisasa siyo hili la kisiasa.

No comments: