Friday, November 9, 2012

JK AKUMBANA NA MABANGO UZINDUZI WA BOMBA LA GESI KINYEREZI

RAIS Jakaya Kikwete amejikuta akipokewa na mabango wakati akizindua mradi mkubwa wa bomba la gesi asilia linalotoka Mtwara hadi eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam.


Mradi huo unatarajiwa kumaliza kabisa tatizo la umeme wa mgawo ifikapo mwaka 2015 kwa kuzalisha megawati 3,000 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya umeme kwa sasa.

Wanaume wawili waliokuwa na mabango kwenye kundi la watu zaidi ya 20, waliyanyanyua juu mabango yanayomtaka Rais Kikwete aingilie kati malipo ya fidia za viwanja na mali zitakazoathirika kwenye moja ya mradi wa gesi eneo hilo baada ya kuzungushwa kwa muda mrefu.

Tukio hilo lilitokea wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik akitoa hotuba ya kuwakaribisha wageni na kuelezea umuhimu wa mradi huo kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Watu hao walinyoosha juu mabango hayo kuelekea jukwaa kuu, alikokuwa amekaa Rais Kikwete jambo lililosababisha maofisa usalama kuwaamuru washushe chini, lakini kundi hilo lilianza kuzomea hivyo kusababisha usikivu hafifu kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi.

Kuona hivyo, Mkuu wa Mkoa alisitisha hotuba yake na kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo akisema taarifa za madai yao tayari wanazo na zinashughulikiwa kuanzia leo.

Sadick aliwasisitizia kuwa kitendo walichokifanya wakazi hao siyo sahihi kwa sababu madai yao hayahusu mradi ambao unazinduliwa na Rais Kikwete bali kampuni binafsi ya Kilwa Energy ambayo ipo kwenye mchakato wa kuwekeza katika mradi wa kuzalisha umeme.

“Madai yenu tunayajua na tayari tumeanza kuyashughulikia, lakini mnapaswa kufahamu kuwa madai yenu hayahusu mradi huu ambao Mheshimiwa Rais anauzindua leo,” alisema Sadick na kuongeza:

“Madai yenu yanahusu mradi wa kampuni binafsi ya Kilwa Energy ambao bado haujasainiwa. Tumekwisha kukubaliana kesho (leo) tutakutana na viongozi wenu kujadili.”

Moja ya bango lilisomeka: “Mtukufu Rais tunaomba utusaidie malipo ya fidia ya viwanja vyetu maana tumezunguswa muda mrefu.”

JK atoboa siri za vigogo

Akitoa historia ya matumizi ya gesi asilia hapa nchini, Rais Kikwete alitoboa siri ya mapingamizi kutoka kwa baadhi ya vigogo serikalini kwenye harakati za kusaini mkataba wa kufua umeme.

Alisema kipindi hicho alikabiliwa na wakati mgumu baada ya vigogo hao kumkaba waziwazi na wengine kumwandikia barua ya kumtaka asianzishe mchakato wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.

Alisema wakati huo alikuwa Waziri wa Maji na Nishati kipindi cha mwaka 1988 hadi 1994, kwenye Serikali ya Awamu ya Pili.

Rais Kikwete alisema aliandikiwa barua nyingi za kupinga matumizi ya gesi asilia ili kuzalisha umeme na badala yake wakamshauri itumike katika mradi wa kuzalisha mbolea mkoani Mtwara.

“Vigogo hao walitaka gesi hiyo itumike kuzalisha mbolea badala ya umeme. Wakaandika barua nyingi za kuupinga huo mradi (wa kuzalisha umeme) na mpaka sasa zipo wizarani... Mmeziona?” alihoji Rais Kikwete.

Aliongeza: “Vigogo hao waliamini kuwa maji peke yake yanatosha kuzalisha umeme, wakati si kweli. Mimi nilikataa na faida zake zinaonekana leo.”

Alisema kwa sasa gesi imesaidia Taifa kupunguza mgawo wa umeme kuliko vyanzo vingine vinavyotumika nchini.

Akitoa takwimu hizo, Rais Kikwete alisema katika Gridi ya Taifa, gesi inachangia asilimia 54.8 wakati maji ni asilimia 15.4 na mafuta asilimia 29.8.

Pamoja na kutoa madai hayo, Rais Kikwete hakuwataja wazi vigogo hao, lakini watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wanaweza kuziona kwenye kumbukumbu za mafaili wizarani kwao.Mgawo wa umeme kwisha

Rais Kikwete alisema mradi huo unaotarajiwa kumalizika mwaka 2014 utamaliza kabisa kero ya mgawo wa umeme ambayo imekuwa ikilisumbua Taifa kwa muda mrefu sasa.

Alisema mradi huo utaanza kwa kuzalisha megawati 900 na ifikapo 2015 utakuwa unazalisha megawati 3,000 na kufanya mgawo wa umeme kuwa historia.

Alisema tafiti za kitaalamu zinaonyesha kuwa kiwango cha gesi kilichopo eneo la nchi kavu kinaweza kutumika kwa miaka 90 kwa matumizi ya hapa nchini na kuuza nje ya nchi.

Tanzania tajiri vyanzo vya nishati

Rais Kikwete alijigamba kuwa Tanzania ni tajiri kwa kuwa na vyanzo vingi vya nishati ila tatizo ni fedha za kuendeleza miradi hiyo.

Alitaja vyanzo hivyo kuwa ni makaa ya mawe, urani, upepo na jua.

“Tanzania ni ya saba duniani kwa utajiri wa madini ya urani… Tuna makaa ya mawe… Kule Singida kuna eneo lenye upepo mkali kuliko eneo lolote duniani.”

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema pamoja na kuwa na urani nyingi duniani, Serikali yake haina mpango wa kuzalisha silaha hatari duniani za nyuklia.

Alisema madini hayo ya urani yatatumika kwa ajili ya kuzalisha umeme labda ije itokee kwenye Serikali zitakazofuata ingawa anaamini haitatokea hivyo.

Gesi kuinua uchumi nchini

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Yona Kilagane alisema kwamba baada ya mradi huo kukamilika mbali na kuzalisha umeme, gesi hiyo itasambazwa kwa mabomba hadi viwandani, jumbani na kwenye magari badala ya mafuta.

Kutokana na matumizi hayo, Kilagane alisema gesi hiyo itasaidia viwanda kuzalisha bidhaa kwa bei nafuu, kutoa ajira na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Alisema Dar es Salaam pekee inatumia magunia ya mkaa 40,000 kila siku, hivyo matumizi ya gesi yatapunguza kasi ya ukataji wa miti ovyo.


Kampuni mahiri kusimamia mradi

Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Lu Younqing alisema kampuni inayosimamia mradi huo ni ya pili kwa ukubwa kati ya zile zilizosajiliwa nchini kwao.

Alisema kampuni hiyo ya China National Petroleum Corporation (CNPC) ndiyo iliyojenga bomba la gesi lenye urefu kuliko yote duniani, ambalo lina urefu wa kilomita 7,000.

Alisema ujenzi wa bomba kwenye mradi wa hapa nchini litakuwa na urefu wa kilomita 532 na anaamini utakamilika kabla ya muda uliopangwa 2014.


MWANANCHI

No comments: