Tuesday, November 20, 2012

DOZI HII YA WAHISANI KWA UGANDA YAIFAA TANZANIA

Na Johnson Mbwambo,
RAIS Yoweri Museveni wa Uganda anaishi hivi sasa na wasiwasi mkubwa. Ana wasiwasi kwamba orodha
ya nchi za Ulaya zinazoungana na Ireland kuisimamishia nchi yake misaada inaweza kuongezeka zaidi, na hivyo kuisababishia serikali yake matatizo makubwa ya kibajeti.

Mpaka wiki iliyopita orodha hiyo ilishafikia nchi nne ambazo ni Ireland, Norway, Denmark na Uingereza. Kuna kila dalili kuwa Sweden na nchi nyingine kadhaa za EU nazo zitajiunga katika orodha hiyo.

Kilichoiponza Uganda kusitishiwa misaada na nchi hizo ni fedha zinazokaribia dola milioni 13 zilizofisadiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Uganda – fedha ambazo zilitolewa na nchi hiyo kusaidia kuboresha miundo mbinu katika mikoa miwili ya Kaskazini mwa Uganda iliyoathiriwa vibaya na vita dhidi ya wapiganaji wa Lord’s Resistance Army.

Nchi hizo zinataka fedha hizo zilizokwibwa na watawala zirejeshwe zote na wahusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria; vinginevyo Uganda isahau kupata misaada kutoka katika nchi hizo.

Hicho ndicho kinachomkosesha raha Rais Museveni, na hilo linaeleweka; maana, kama zilivyo nchi nyingi za Afrika, asilimia 25 ya bajeti ya Serikali ya Uganda hutegemea fedha za wahisani; hususan wa nchi za Ulaya Magharibi.

Katika tapatapa yake, Rais Museveni ameagiza kusimamishwa kazi maofisa 12, na wawili kati yao tayari wameshafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuhusika na wizi wa fedha hizo za wahisani.

Rais Museveni aliamini kwamba hatua hiyo ingewatuliza wahisani na kurejesha misaada, lakini badala yake, wiki iliyopita, nchi nyingine zaidi (Norway) iliongezeka katika orodha ya nchi zilizotangaza kuisimamishia misaada.

Ni dhahiri nchi hizo nne za wahisani zimeamua kuendelea na msimamo wao huo kwavile haziridhishwi na maofisa waliokamatwa mpaka sasa. Nchi hizo zinaamini kwamba waliokamatwa ni ‘vijidagaa’ tu, lakini mapapa hasa waliohusika na ufisadi huo ni vigogo wa serikali wanaolindwa na Rais Museveni mwenyewe.

Sina hakika mvutano huu kati ya wahisani hao wa Ulaya na Serikali ya Rais Museveni kuhusu suala hilo la kusitishwa misaada utaishaje, lakini ni maoni yangu kwamba, angalau kwa sasa, Serikali ya Rais Museveni ‘imeshikishwa adabu’ na wahisani hao.

Kama wahisani hao hatimaye watairejeshea Uganda misaada, nina hakika mambo hayawezi kuwa tena kama yalivyokuwa katika Uganda. Yaani Rais Museveni hawezi tena kuendelea na mapambano dhidi ya ufisadi ‘kisanii’. Ni lazima atakuwa mkali zaidi dhidi ya ufisadi kuliko alivyokuwa mwanzo; maana alishang’atwa na nyoka!

Na ndiyo maana nadiriki kusema kwamba ‘dozi’ hiyo ambayo wahisani hao waliitumia Uganda ‘kuishikisha adabu’ inafaa pia kutumiwa na wahisani hao nchini mwetu Tanzania; maana hali ya ufisadi katika nchi yetu haitofautiani sana na ya Uganda.

Katika Uganda alikuwa ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyebainisha katika ripoti yake wizi wa fedha hizo katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Hapa Tanzania, kila mwaka ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) huanika wizi wa sampuli mbalimbali wa fedha za umma zikiwemo tulizozipata kutoka kwa wahisani, lakini wanaokamatwa na kufikishwa mahakamani kwa wizi huo ni wachache mno.

Katika hali hiyo, kwa nini wahisani wetu nao wasitumie ‘dozi’ ile ile waliyoitumia wenzao Uganda ili kumbana Rais wetu, Jakaya Kikwete, aache naye kuendesha vita dhidi ya ufisadi kisanii? Maana, kama ilivyo Uganda, nasi Tanzania bajeti yetu inategemea mno fedha za wahisani hao.

Wiki iliyopita (kwa mfano) nilifuatilia mjadala wa Bunge kuhusu hoja binafsi ya Mbunge Zitto Kabwe (CHADEMA) ya kutaka zirejeshwe nchini dola zaidi ya milioni 196 zilizofichwa na vigogo wetu katika benki za Uswisi.

Nilisikiliza kwa makini mjadala wa hoja hiyo binafsi ya Zitto na majibu ya Serikali; hususan ahadi yake kwamba itafanya uchunguzi, na kwamba kikao kijacho cha Bunge kitaelezwa hatua iliyofikiwa juu ya uchunguzi huo.

Hata hivyo, kwa mtazamo wangu, hoja na ahadi za serikali zilikuwa ni za ‘kisanii’. Kwa maneno mengine, sikuiona dhamira ya kweli ya Serikali ya kutaka fedha hizo zirejeshwe nchini; achilia mbali dhamira ya kutaja hadharani majina ya mafisadi waliohusika na ufichaji huo wa pesa Ughaibuni.

Ni mtazamo wangu pia kwamba, kama ilivyokuwa katika kashfa nyingine za EPA, Richmond nk, hii nayo ya pesa za Uswisi inachezwa ‘kisanii’ na Serikali kwa kuipiga ‘danadana’, na inafanya hivyo ikitaraji kwamba baada ya muda kashfa hii nayo itakufa kifo cha asili kama zilivyokufa hizo nyingine.

Unaweza kusema kwamba, inachokifanya Serikali katika suala hili la fedha za Uswisi ni ku-buy time tu ili hatimaye kashfa hii iishe yenyewe. Na itaisha haraka hasa kama itaibuka kashfa nyingine mpya kuififisha hii ya fedha za Uswisi. Hilo ndilo ambalo Serikali inaomba litokee, na ndio asili ya ku-buy time katika kashfa hii ya fedha zilizofichwa Uswisi.

Hebu fikiria; tangu Benki Kuu ya Uswisi iitangazie dunia kwamba vigogo wa Tanzania wameweka mamilioni ya dola katika benki zake inakaribia miezi mitano sasa; lakini bado watawala wetu na Bunge letu bado liko kwenye ‘mijadala’ ya hatua zipi zichukuliwe!

Yaani miezi takriban mitano tangu kashfa hiyo ya fedha za Uswisi iibuliwe, bado nchi ipo katika malumbano ya wenyewe kwa wenyewe ya kuulizana iachiwe TAKUKURU na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au iundwe Kamati Maalumu ya Bunge kufuatilia!

Hivi kweli hizo fedha za Uswisi zitakuwa bado zinasubiri malumbano haya yaishe ili zichukuliwe? Kwa nini mafisadi waliozificha wasitumie kipindi hiki cha malumbano ya wenyewe kwa wenyewe kuzihamisha fedha hizo na kuzifunga akaunti hizo za Uswisi?

Kwa hakika, sitashangaa kama siku moja Watanzania tutaambiwa kuwa akaunti hizo za Uswisi zimeshafungwa na waliozifungua, na kwamba wachunguzi wetu wamefika huko na kukuta hakuna hata senti moja ya kuirudisha Tanzania!

Waliopata kusoma kitabu cha riwaya cha Sidney Sheldon (Tilly Bagshawe) kinachoitwa After the Darkness watakuwa wanafahamu jinsi unavyoweza kuzizungusha fedha chafu (wenyewe wanaita kuzi-wire) katika benki za miji mbalimbali duniani; kiasi kwamba kuzifuatilia na kujua sasa zilipo yaweza kuchukua miaka 10!

Katika riwaya hiyo ambayo msingi wake ni tukio la kweli, fedha chafu za kampuni ya kimataifa inayoitwa Quorum zilitolewa New York zikawa wired Ulaya, na zikatoka Ulaya na kuwa wired Marekani ya Kusini, na zikatolewa Marekani ya Kusini na kuwa wired Afrika (Madagascar)! Kwa staili hiyo, iliwachukua FBI na CIA muda mrefu mno kuwakamata wahusika.

Naamini hivyo ndivyo pia itakavyotokea kwa pesa hizo za mafisadi wa Tanzania zilizofichwa Uswisi. Fedha hizo zitakuwa wired na mafisadi hao kwenye mabenki mbalimbali duniani; kiasi kwamba si TAKUKURU yetu wala Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inayoweza kuzifuatilia kote huko na kuzirejesha nyumbani!

Ndiyo maana mimi binafsi naamini kwamba Serikali inacheza mchezo wa kisiasa tu, lakini haina dhamira ya kweli ya kuona fedha hizo zinarejeshwa nchini na wahusika wanakamatwa.

Kama kweli Serikali yetu ingekuwa na dhamira hiyo, ingeshaliiomba mapema kabisa Benki Kuu ya Uswisi kuzizuia kwa muda akaunti hizo hadi hapo uchunguze utakapokamilika na kufahamika uhalali wake.

Kwa kadri ninavyofahamu, hilo halijafanyika, na hiyo maana yake ni kwamba maofisadi waliozificha huko walipata fursa ya kutosha kuzifunga akaunti hizo mara moja au kuzi-wire fedha hizo katika mabenki mbalimbali ya kifisadi duniani.

Mafisadi hao wanaweza hata kuwapa marafiki zao wa Ughaibuni fedha hizo ili wawanunulie mali huko kwa majina yao, na hivyo ‘kuwatunzia’ fedha hizo kwa njia hiyo hadi mambo yatakapopoa kabisa kuhusu ufisadi huo hapa Tanzania.

Nirudie kusisitiza tena kwamba kwa danadana hii ya Serikali ya ku-buy time katika suala la fedha hizo zilizofichwa Uswisi, sitashangaa kama mwisho wa yote hakutakuwa hata na senti tano itakayokutwa kwenye akaunti hizo!

Danadana hizi za ku-buy time za serikali yetu katika masuala ya ufisadi ili hatimaye kashfa zinazoibuliwa zife kifo cha asili kwa kupitwa na wakati, zinaweza tu kukomeshwa na ‘dozi’ ile ambayo wahisani wameipa Uganda baada ya fedha zao za msaada walizotoa kuibwa na vigogo wa nchi hiyo.

Tunajua serikali yetu inategemea mno misaada ya wahisani wa nje, na ndiyo maana Rais Kikwete haishi kusafiri nje (Magufuli alimwambia mkoani Arusha hivi karibuni asafiri sana nje ili alete mapesa ya kujenga barabara zaidi…!).

Katika hali hiyo, sioni namna yoyote ambayo Rais Kikwete anaweza kuendelea kupambana na ufisadi ‘kisanii’ kwa kupiga danadana kashfa mbalimbali za ufisadi iwapo wahisani wa nje watasimamisha misaada kwa Tanzania hadi wawaone ‘mateka wakubwa’ wa vita hiyo dhidi ya ufisadi tunayodai tunaiendesha Tanzania wakifikishwa mahakamani na kufungwa!

Najua wapo wenye fikra fupi wanaoweza kunihukumu kwamba sina uzalendo kwa kuwataka wahisani watusimamishie misaada inapotokea fedha wanazotupa zinakwibwa, lakini tusisahau kuwa hizo pesa ni za walipakodi wao ambao wengi wao wala si watu matajiri.

Wanapotoa fedha zao za kodi kutusaidia si kwamba wao ni matajiri. Wengi ni wafanyakazi viwandani na maofisini wenye maisha ya kawaida kabisa, lakini wanakubali sehemu ya kodi zao wanazolipa tuletewe kwa sababu wanaamini kuwa sitatusaidia, kama taifa, kujijengea uwezo wa kujiendeleza.

Sasa, vigogo wetu wanapoamua kuzikwiba fedha hizo au kuzi-fisadi maana yake ni kwamba hatuwatendei haki wananchi hao wa Ulaya waliokubali kodi zao wanazolipa ziletwe nchini kutusaidia.

Na ndiyo maana nasisitiza kusema tena kwamba; ile ‘dozi’ ambayo wahisani hao waliitumia Uganda, hivi karibuni, baada ya fedha zao ku-fisadiwa inaweza pia ‘kututibu’ kama wataitumia pia hapa Tanzania ambako pia vigogo hufisadi fedha za umma zikiwemo zilizotoka kwa wahisani!

Tafakari.


RAIA MWEMA

No comments: