Friday, November 2, 2012

CCM HAITANG'OKA KWA KUPIGIWA VIGELEGELE

Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,
Historia imeonesha kuwa hakuna utawala uliodumu muda mrefu madarakani ambao uliweza kuondolewa na wapinzani wake bila ya kutokea mgongano fulani.

Mgongano huo unaweza kuwa ni wa kifikra na wakati mwingine unaweza kuwa ni wa mapigano. Kati ya hizo mbili kunaweza kuwapo migongano ya watu na watu, makundi na makundi na hata sehemu kubwa ya jamii.

Watawala hupenda kutawala

Ikumbukwe kuwa watawala wanapenda kutawala na hawawezi kuachia madaraka kwa sababu wengine nao wanataka kutawala.

Watawala wanapenda kwa sababu pamoja na mengi ambayo wanaweza kusema wanafanya kwa ajili ya jamii wanayoitawala nyuma yake ni kuwa, kutawala kuna manufaa. CCM na watendaji wake serikalini wananufaika na kutawala na kwa muda wa miaka hamsini sasa ni wao ndio wamekuwa wanufaika wakuu wa kutawala kwao.

Kupitia kutawala kwao wameweza kuwa na maisha yao. Wameoa na kujenga familia, wameanzisha biashara, wamesomesha watoto, wamesaidia ndugu, jamaa na marafiki na kwa hakika kutawala kumekuwa ni sababu ya wao kuendelea kuwa na furaha.

Kuwaondoa madarakani ni chanzo cha wao kukosa furaha hiyo. Kukaa nje ya madaraka ni sawasawa na kumkataza fisi asiendelee kunyofoa mfupa ambao fisi wengine wanataka kuula.

Kuachishwa kula mfupa huo haliwezi kuwa jambo jema kwa kundi la fisi hata kama kwa kufanya hivyo kunaweza kukaleta mbweha na ndege nao kuja kujinoma.

Hivyo kudhania kuwa ati CCM itaamua kuondoka kwa kheri na kwa furaha ni kutokuelewa asili ya madaraka. Hili ni jambo la muhimu kuliangalia hasa baada ya kampeni na hatimaye uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Jumapili iliyopita.

Baada ya uchaguzi huu sababu nyingi zinatolewa za kuelezea kwa nini CHADEMA haikufanya vizuri sana kama ilivyotarajiwa na kuwa CCM imeendelea kushangaza umma kwa kufanya vizuri.

Bila ya shaka kuna watu ambao watapenda kuzugumzia takwimu tu kuwa CHADEMA kuongeza viti vitatu kati ya 29 vilivyopiganiwa ni jambo jema na kuwa ni CCM ndio imepoteza zaidi.

Kitakwimu hili linaweza kuwa kweli na likawa sababu ya watu kupongezana. Lakini ukiangalia kwa karibu inakatisha tama kwa CHADEMA. Kama CHADEMA pamoja na mikutano yake, M4C, na kupambwa sana kwenye TV na radio bado haijaweza kuiadhiri CCM ina maana moja CCM bado iko hai.

Simba anayenguruma hajafa

Ukimwona simba amelala usidhani kafa. Kuna imani ambayo imejengwa kwa muda mrefu kuwa CCM iko kwenye kamba kama bondia ambaye yu karibu kusalimu amri.

Imani hii tumeiona kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 na kwenye chaguzi za diwani (zote mbili zilizopita). Ukiangalia jinsi ambavyo CCM imekuwa ikisemwa na kubezwa unaweza kuamini kabisa kuwa hakuna mtu hata mmoja ambaye bado ni mwanachama wa CCM au ambaye hataki CCM iwe madarakani.

Hata hivyo matokeo ya uchaguzi mara hizi zote yametuonesha kuwa CCM bado ipo, siyo tu kuwa inapumua kwa kweli bado haiitaji mashine kupumua.

Bado inaweza kuunguruma na hatari ambayo ni rahisi kuiona naweza kuielezea kwa namna ya swali: Kama CCM katika udhaifu wake bado inaweza kushinda itakuwaje pale itakapokuwa na nguvu zaidi? Kama samba anayechechemea anaua swala itakuwaje akipona si pundamilia watakiona?

Kuidharau CCM au kupuuzia nia yake ya kutaka kuendelea kukaa madarakani ni hatari zaidi kwa CHADEMA. Kwa sababu mwisho wa siku CHADEMA itakuwa kama fisi anayefuatilia mkono wa mtu. Atahurubi “mkono uko karibu kudondoka” au “tuendelee kuwaeleza wenzetu kuwa kwa kadiri anavyotingisha mikono ndivyo anavyokaribia kuiangusha” na watu ambao wanaamini hilo watajikuta wamejipanga kusubiri mikono ianguke; siku zinapita, miezi inapita, mikono inaendelea kutingishika na vidole kuyumbishwa; havianguki.

Mithili ya fisi, CHADEMA itazidi kusubiri?

Hatari ya hili la kuiangalia CCM kuwa itaanguka au kuwa iko karibu kuanguka inasahau jambo moja kubwa kuna wakati ambapo inabidi uisaidie ianguke. Kwa wale ambao wamewahi kukata miti mikubwa wanajua kuwa kuna wakati ukisha kata mti huukati ukaumaliza bali unaukata halafu unatafuta mahali ili kuvuta kamba na kuuangusha; yaani unausaidia uanguke. CCM iko katika hali ya kuanguka na kila sababu ya kuanguka ipo; hata hivyo CHADEMA bado inaonekana haiku tayari kuiangusha CCM na matokeo yake ni haya ya kucheza ‘hiki na hoko’.

CHADEMA inapozidi kujiandaa na chaguzi nyingine zijazo inapaswa kuanza kujiuliza maswali ya akili badala ya kuendelea na kampeni isiyolipa. Maswali haya ni mengi lakini naomba nipendekeze machache tu.

Je, ni maslahi ya CHADEMA kushiriki uchaguzi wowote ule bila ya sheria inayosimamia tume ya uchaguzi kubadilishwa?

Je, ni maslahi ya CHADEMA kuendelea kushiriki chaguzi hizi mbalimbali bila kufanya mabadiliko katika mfumo wa kuandikisha wapiga kura ili kuhakikisha wenye haki ya kupiga kura wanaandikishwa katika kila uchaguzi?

Je, ni maslahi ya CHADEMA kuendelea kushiriki uchaguzi chini ya mfumo ambao umetengenezwa ili kuzuia upinzani usije kushika madaraka?

Je, CHADEMA inahitaji kufanya nini ili kuimaliza kabisa CCM badala ya kuiacha iwe kama mzimu usio kubali kufa?

Je, CHADEMA itaendelea kushiriki chaguzi ambazo wanachama wake na mashabiki wake wanauawa na kujeruhiwa mpaka nani auawe ndio wajue kuwa CCM haitoachia madaraka kwa vigelegele?

Bila kujaribu kujibu maswali haya na mengine CHADEMA itaendelea kutuhubia kitu ambacho tayari tunakijua waanze kufanya tusivyovijua ili tuone wakishinda uchaguzi tena siyo kidogo bali uwe wa kishindo. Vinginevyo watakapoanguka 2015 watatupa maelezo ya kwa nini mkono utaanguka 2020!RAIA MWEMA

No comments: