Thursday, November 8, 2012

AJALI MBAYA YATOKEA MAENEO YA NANGURUKURU- KILWA WANNE WAPOTEZA MAISHA

Picha na Habari na Abdulaziz video,Lindi


ABIRIA wapatao wanne wamekufa papo hapo na wengine 48 wamekimbizwa katika hospitali ya Kinyonga,wilaya ya Kilwa mkoani Lindi,kufuatia basi walilokuwa wakisafiria kutoka jiji Dar es salaam kwenda wilaya ya Liwale,kuacha njia na kupinduka.

Habari kutoka wilayani humo na kuthibitishwa na kaimu kamanda wa Polisi mkoani hapa,Joseph Mfungara, zinaeleza ajali hiyo imetokea katika mteremko mkali wa Nangurukuru wilayani Kilwa

Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walieleza kuwa basi hilo aina ya Mitsubishi lenye namba za usajili T981 AFL lililokuwa likiendeshwa na Shabani Kiparapara wa Jijini Dar es salaam lilipata ajali hiyo eneo la mlima uitwao Kipokonyo.

“Hili basi lilipofika eneo hilo la mlima,lilionekana likienda mwendo kasi na hatimaye kuacha barabara na kuelekea Porini na kupinduka”Walisema mashuhuda hao waliojitambulisha Issa Abdallah na Juma Selemani.

Walisema wananchi waliojitokeza kutoa msaada kwa abiria hao, waliweza kushuhudia watu wanne wakipoteza maisha papo hapo,huku wengine hali zao zikiwa katika hali mbaya.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Lindi, Joseph Mfungamara amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza basi hilo lilikuwa likitokea Jijini Dar es salaam kwenda wilaya ya Liwale.

Mfungamara amewataja marehemu hao kuwa ni,Flora Francis Lamumba (32) mwalimu wa Shule ya msingi,Dorah Francis (35) muhudumu wa Bar,Halima Manicha (60) wote ni wakazi wilaya ya Liwale na Christina Samweli Kika,muhudumu wa Idara ya Afya mkoani Arusha.

Amesema katika ajali hiyo abiria wapatao 48 wamelazwa Hospitali ya wilaya ya Kilwa, Kinyonga,kutokana na kuumia maeneo mbalimbali ya miili yao.

Kaimu kamanda huyo wa Polisi mkoani Lindi, amesema bado chanzo cha ajali hiyo,haijaweza kufahamika mara moja,na kuongeza dereva wa basi hilo Shabani Kiparapara ametoroka mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo,na kwamba anatafutwa ili afikishwe mahakamani kwa hatua zingine za kisheria.

No comments: