Thursday, October 25, 2012

RAI YA JENERALI
Kiongozi tofauti na kundi la majambazi wanaojiita wakuu wa nchi


MWALIMU Julius Kambarage Nyerere amefariki. Baba kaondoka. Jua limekuchwa. Mbuyu mkuu uliotanda katikati ya kijiji umenyauka. Zama zimefikia tamati. Watanzania ni yatima.

Ilani ilitolewa kwa muda wa kutosha. Wiki kadhaa za mateso ya maradhi ya Mwalimu katika Hospitali ya Mtakatifu Tomaso, mjini London, ingetakiwa iwe ni taarifa ya mapema ili watu wake wajiandae kwa lolote ambalo lingetokea. Kwa hakika taarifa za siku za mwisho zilionyesha wazi kwamba hakuwa mgonjwa wa kupona.

Hata hivyo, tangazo rasmi la kifo chake limeweza kuwashitua Watanzania, kama vile lilikuwa jambo lisilotarajiwa. Hali hii inaelezeka kwa utambuzi wa uhusiano maalumu kati ya Mwalimu na Watanzania, ambao walikataa kulizoea wazo la kifo chake.

Hadi jana asubuhi (Oktoba 14, 1999) wengi waliamini kwamba hata pale sayansi ya juu ilipokomea bado muujiza ungetokea na baba yao akainuka kitandani na kupanda ndege kurejea nchini.

Haiwezekani kuwalaumu hata wale walioshawishika kuegemea hisia za ushirikina. Watanzania walitaka mzee wao apone, na hawakukata tamaa hadi dakika ya mwisho. Ukweli ni kwamba hawakujua ni vipi wangeweza kuishi kama taifa bila Nyerere.

Haishangazi. Kwa muda wa nusu karne, nchi hii imetambulika na kujitambulisha kwa jina la Julius Kambarage Nyerere. Tangu alipojiunga na harakati za kudai uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1950, Nyerere hajawahi kuondoka katika hisia za Watanzania.

Aliongoza kampeni ya uhuru kwa ujasiri mkubwa na kwa kufanya kazi bila kuchoka. Alitembelea kila kona ya nchi hii, akiwahamasisha wananchi kukataa ukoloni na kujiunga naye kudai uhuru. Kwa jinsi hii alijipatia fursa muhimu ya kuielewa nchi na watu wake, ujuzi ambao ulimfanya kuwa kiongozi aliyekuwa karibu na wananchi wake kuliko viongozi wengi wa Afrika na dunia.

Hata baada ya uhuru, alipokuwa kiongozi wa dola, hakuacha mtindo wake wa kwenda hadi vijijini, si katika sherehe na ngoma, bali kupiga kambi na kufanya kazi za sulubu bega kwa bega na wanavijiji, huku akiwafundisha alichokijua juu ya kilimo, au afya au ujenzi wa nyumba bora na huku akijifunza kutokana na uzoefu wa wananchi.

Baadhi yetu bado wanakumbuka kambi za Mwalimu katika mikoa ya Dodoma na Kigoma. Alikuwa mwalimu wa kweli, na alipenda kulifundisha taifa lake. Alijua kueleza dhana ngumu na tata kwa lugha nyepesi. Aidha alikuwa na kipaji cha ucheshi kilichomrahisishia mawasiliano.

Pia alikuwa ni msikilizaji makini aliyeweza kuhifadhi taarifa za maelezo marefu na misururu ya takwimu. Watanzania walimjua Nyerere kama kiongozi shupavu aliyeweza kukemea uovu, hasa dhidi ya wanyonge.

Alikuwa mtetezi asiyechoka wa watu wasiokuwa na uwezo na alipingana na kila aina ya unyanyasaji uliofanywa na watu wenye utajiri au vyeo. Alichukia rushwa na alipigana nayo hadi mwisho wa maisha yake.

Alikuwa safu ya mbele katika kupambana na ukoloni, ubeberu na ubaguzi na hakusita kuwakemea wakubwa wa dunia hii kila walipoonyesha dalili za kuwaonea au kuwapuuza wanyonge.

Mwalimu alikuwa miongoni mwa miamba wachache waliotetea haki za nchi ndogo na masikini katika mahafali yote ya kimataifa.

Alikuwa kiongozi asiyetetereka katika misimamo yake na uthabiti huo ulimwezesha kuwaongoza vyema Watanzania katika raha na katika taabu, katika amani na katika vita, Idi Amin alipovamia nchi yetu mwaka 1978 Nyerere alionyesha maana halisi ya cheo cha Amiri-Jeshi Mkuu kwa kusimamia mwenyewe maandalizi ya kivita ya kumwadhibu Amin na kujenga mawasiliano ya mara kwa mara na wananchi ili kuwaeleza kuhusu maendeleo ya vita. Kwa kumwondoa Amin madarakani, Nyerere alikuwa amesaidia dunia kuondokana na mwendawazimu hatari.

Mwalimu aliishi maisha ya kawaida, akakataa mbwembwe na ukwasi unaowatambulisha viongozi wengi wa nchi masikini. Alikwepa anasa na akajijengea mazingira yaliyowasuta wapenda makuu hapa nchini na nje ya nchi. Watu wa nchi nyingine walimstaajabu kwa mwenendo wake wa kujinyima katika mavazi na itifaki, tofauti kabisa na wenzake.

Katika mambo ambayo tungeweza kujifunza kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere ni ari yake ya kutaka kujua na kujiendeleza kila wakati. Wasomi wengi wameziacha bongo zao zikaota magugu kwa sababu ya kutojisomea. Mwalimu alisoma wakati wote, hata wakati akionekana kachoka. Jinsi hii aliweza kujipatia ujuzi na taarifa ambavyo vilimfanya awe na uwezo wa hali ya juu wa kuelewa masuala mbalimbali ya dunia.

Fursa ya kukaa na Mwalimu kwa muda wa saa moja wakati wowote ilikuwa ni fursa ya kunywa maji kutoka kisima cha elimu. Si bure kwamba Mwalimu Nyerere aliendelea kuenziwa na wananchi wa Tanzania, hata miaka mingi baada ya kuwa ameondoka madarakani. Kila wakati Mwalimu alipoitisha mkutano na waandishi wa habari, waandishi na wahariri waliingiwa na shauku kubwa ya kujua anataka kusema nini. Na kila alilosema lilichukuliwa kwa uzito mkubwa.

Si rahisi kufikiria mtu yeyote mwingine ambaye angeweza, kama Mwalimu, kufuta azimio la Bunge la kutaka iwepo serikali ya Tanganyika, mwaka 1993. Wala si rahisi kumfikiria mtu ambaye angeweza, kama Nyerere, kusema fulani hafai kugombea urais, na huyo fulani asigombee. Watu waliokuwa na bahati mbaya ya kukemewa na Nyerere hadharani walijikuta wanatembea na aibu muda mrefu.

Nguvu zake hazikuishia nchini. Kila alikokwenda Mwalimu Nyerere aliwavuta waandishi wa habari, wasomi na viongozi wakuu. Walimsikiliza kwa sababu walitambua kwamba ni mtu makini, mwenye akili na anayetetea maslahi ya watu wake na watu wa dunia ya tatu walio wanyonge na kwamba hakutafuta kujitajirisha binafsi.

Kwamba Rais wa Marekani, Bill Clinton na Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair walitaka wamlipie gharama za matibabu ni ishara ya jinsi alivyokuwa akithaminiwa na viongozi wa nchi za nje.

Heshima yote hii alipewa kwa sababu alitambulika kama mmoja wa Waafrika wachache walioweza kuongoza nchi zao kwa misingi ya ubinadamu na bila kuwaibia watu wao katika Bara lililojaa majambazi wanaojiita wakuu wa nchi, hii si sifa ndogo.

Hakuwa mtu wa kawaida. Sikuwahi kufanya kazi naye kwa muda mrefu, lakini mara chache nilipopata nafasi ya kuwa naye niligundua kwamba watu walioishi naye kwa muda mrefu halafu wakashindwa kujifunza kufikiri walikuwa na matatizo makubwa.

Ukali wa ubongo wake ulikuwa wa kusisimua na wenye uwezo wa kutekenya ubongo wako nao ufanye kazi. Mwalimu Nyerere ameliongoza taifa hili tangu mwaka 1954 na kwa muda wote huo, Watanzania wamemjua kwamba ndiye kiongozi namba moja.

Wako watu waliojaribu kubeza jina la “Baba wa Taifa” katika miaka ya karibuni, lakini sasa wametulia. Kwa karibu kila mtu, hilo ndilo jina lake na hiyo ndiyo hadhi yake.

Haishangazi, basi, kwamba wapo watu wenye wasiwasi kutokana na kifo chake. Wako wanaodhani kwamba baada ya kuondoka kwake, nchi itaingia kipindi cha mashaka makubwa, hata kuvurugika kwa amani.

Wako wanaodhani kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavunjika kwa sababu mwasisi wake ametoweka. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwalimu hakusita kumkemea mtu yeyote, wa Bara au Visiwani, aliyemwona kama anataka kuuvunja Muungano.

Sasa ni dhahiri kwamba hakuna mtu atakayekuwa na uzito wa kuweza kuwakemea wachafuzi, na hawa ni wengi. Aidha yako makundi ya watu nchini yanayodhani kwamba kifo cha Mwalimu kinawaacha katika hali inayoweza kuwaletea matatizo, wakaonewa, kunyanyaswa au kudhuriwa kwa namna nyingine.

Watanzania wenye asili ya nje wanao wasiwasi wa aina hiyo. Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani kadhalika wanaamini kwamba katika uhai wake, Mwalimu alikuwa ni kinga dhidi ya matumizi ya mabavu dhidi ya wapinzani.

Inawezekana hisia zote hizi hazina msingi na kwamba watu wanahofu zinazotokana na kukojua mustakabali wa taifa hili utakuwaje. Kila taifa hupata mashaka kama haya linapoondokewa na kiongozi wake mwasisi. Waasisi ni watu adimu. Hutokea mara moja katika maisha ya taifa. Mwalimu ni miongoni mwa hao. Anachangia nafasi na George Washington, Simon Bolivar, Jose Marti, Mahtma Gandhi/Jawaharlal Nehru na wengine kama hao.

Kwa sababu kufa ni lazima, waasisi nao hufa. Wanapokufa huacha majonzi na hofu, lakini wanaobaki baada yao wanatakiwa kuwa na moyo mkuu, kuelewa kwamba kifo cha mwasisi, kiwe na majonzi kiasi gani, si mwisho wa dunia.

Maisha lazima yaendelee. Njia moja muhimu ya kumuenzi Nyerere kama Baba wa Taifa na mwalimu wetu ni kudhihirisha kwa vitendo kwamba ni kweli alikuwa baba mwema aliyelea vizuri, na mwalimu mahiri aliyetufundisha tukaelimika na tukawa na busara. Tujitahidi kuepuka chokochoko na ukorofi unaoweza kuleta mfarakano katika jamii.

Tukifanya hivyo tutakuwa tumeheshimu wasia wake. Vinginevyo, tutaruhusu migawanyiko isiyo na maana. Au tukianza kuwaonea wanyonge na kuruhusu mambo ya hovyo katika jamii yetu tutakuwa tunamtukana baba yetu na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajitukana wenyewe.

Taifa hili sasa linahitaji moyo mkuu na mshikamano wa hali ya juu, pamoja na ukomavu unaotakiwa kwa kila mwana ampotezaye mzazi wakati amekwishakukomaa.

Mola ailaze roho ya Mwalimu mahali pema peponi. Amina.

Makala hii ya tanzia iliyoandikwa na Jenerali Ulimwengu ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa gazeti la Raia Mwema, ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mtanzania, Oktoba 15, mwaka 1999, siku moja baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.


RAIA MWEMANo comments: