Wednesday, October 24, 2012

MANISPAA YA MTWARA INALICHUKULIAJE SUALA LA OMBA OMBA?

Makala hii niliiandika tarehe 29 Julai mwaka 2009. Nimeona leo niirudie leo niwakumbushie wasomaji wapendwa wa blogu hii juu ya mkoa wa Mtwara. Changamoto kubwa inayokwamisha maendeleo katika mkoa huu ni majungu yanayopandikizwa na watu kwa viongozi wanaojiita wazawa wa mkoa huu na wao kuyabeba kwa kutumia mamlaka yao bila kuchunguza. Masuala mengi yamekuwa kama porojo za kisiasa zenye kuwanufaisha wachache. Hivi sasa limejitokeza wimbi la wanasiasa uchwara wa facebook wenye nia na malengo na kufadhiliwa na hao hao wanasiasa na kuwaneemesha wao. Tabia hii  ya kupandikiza chuki yenye mbegu za ukabila na Udini  za wazi wazi ikiachwa ikamea ...........Itakuja leta madhara makubwa.Na Baraka Mfunguo,


Katika pita pita yangu mtaani jumamosi moja nilikutana na mama mmoja wa makamo kidogo na wanawe wawili. Mama yule alianza kwa kunisalimia na kisha kunitaka msaada nilipomuangalia mama yule na hali yake haonyeshi kama ana ulemavu wa aina yoyote isipokuwa tu yeye anaomba. Nilipomueleza kuwa sina kitu akang'aka akasema "Baaa! hata wewe huna kitu...." akafyonza halafu akatokomea zake.

Kwa miaka yangu niliyoishi mkoani humu, nimeweza kushuhudia mazuri mengi ya mkoa huu ikiwamo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji, vivutio vya utalii,bandari kubwa na yenye ubora wa kimataifa, barabara kwa ajili ya kuunganidha mkoa wa Mtwara na mikoa mingine, Zao la Korosho, Uchimbaji wa gesi  na mafuta pale Msimbati. Kimsingi mkoa wa Mtwara ni mkoa tajiri ambao una rasilimali za kutosha.

Suala lililonifanya niandike makala hii ni hii kero ya omba omba ambao wanazunguka mijini na kuomba misaada huku mamlaka zenye dhamana zikilifumbia macho suala hili. Ninatambua hali za maisha ya watanzania wale ambao wako kwenye ajira na wale wasiokuwa kwenye ajira hali zao za maisha ni tofauti. Lakini hali hii kimsingi imekuwa ni fedheha kwa watu wengi na omba omba atakapoomba msaada ukimpa kesho yake atakufuata tena akikuomba msaada na kikubwa zaidi utamaduni wa huku ni kwamba yeye omba omba anaona kwamba yeye kuomba ni haki yake na wewe kumsaidia ni haki yako pasipo kujali kwamba na wewe pesa hiyo umeitolea jasho.

Kama nilivyosema kwamba Mkoa wa Mtwara una rasilimali lukuki. Lakini rasilimali nyingine iliyosahaulika ni kuwapo kwa viongozi waandamizi katika serikali ya awamu ya nne ya mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Viongozi hawa ndio nadhani wangekuwa chachu ya maendeleo mkoani hapa lakini matokeo yake wao wamekuwa wakijali zaidi shughuli zao. Mfano rahisi jamaa wa AMREF wamezindua na bado wanaendelea na ujenzi wa visima vya maji vya kudumu maeneo ya Mtwara vijijini ambapo wananchi kwa kuona tu kile kitendo wakashukuru Mungu wakisema hawajawahi kuona maji miaka na miaka labda wakiwa matembezini mjini kazi hiyo inafanywa kama msaada na AMREF. Cha kushangaza hata huyo Mbunge haonekani. Mkoani Dodoma inaelezwa pia mradi huo umefanywa na inaelezwa kwamba Mbunge mmoja aitwaye Chibulunje japokuwa alikuwa anakabiliwa na majukumu mengi ya kiserikali, hakuacha jamaa wafanye kazi kimya kimya alikuwa anakuja kuwapa tafu na kuwatia hamasa. (simpigii mtu kampeni na siko chama chochote cha kisiasa nazungumzia maendeleo ya Mkoa wa Mtwara)

Katika mkoa wa Mtwara kuna suala la uzawa ambalo linatawala katika utendaji wa halmashauri nyingi na hata katika uteuzi wa watendaji waandamizi katika nafasi mbalimbali za serikali ukiacha nafasi zile ambazo zinapita moja kwa moja kwa Rais. Na hali hii imekuwa kama kero kwa watu ambao sio wazawa wa mkoa huu kwani endapo itathibitika kama unafanya jambo lolote la maendeleo liwe la kwako binafsi au la wananchi kwa kutumia nguvu zako utafanyiwa fitina mpaka utahamishwa. Na fitina hizi hupelekwa kwa kiongozi mmoja mwandamizi serikalini ambaye ni mzawa wa mkoa huu . Yeye huhakikisha kwamba hakuna mtu anayeitwa mgeni anatakiwa kuleta changamoto za maendeleo ikiwa unafanya kazi ofisi za serikali au taasisi ya serikali. Wapo Mamwinyi ambao nao ukikorofishana nao, tu umekwenda na maji. Waswahili wanasema "ukenda Roma nawe uwe kama wao" msemo huu si kweli katika maendeleo ya sasa

Tabia hizi za kizamani ndizo zimekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo mkoani hapa. Tukubali tusikubali lazima tukabiliane na changamoto za wageni tuachane na ubaguzi. Kama ubaguzi huu utaendelea, basi safari ya maendeleo itachukua miaka mingi sana. Na mimi sioni sababu ya msingi ikizingatiwa mkoa wa Mtwara ni mkoa uliojaaliwa. Kuna Mbunge mmoja ambaye amepata nafasi yake kupitia viti maalum yeye sio mzawa. Pamoja na kupigwa vita kwenye chama na kwenye jamii ya wanawake wanaojiona na vigogo wa juu serikalini na UWT, lakini ameweza kufanya kila jitihada kufanikisha baadhi ya mambo ikiwa miradi mbalimbali kwa ajili ya kuwakwamua wakina mama na umaskini, kusaidia vituo vya afya na mambo mengine ambayo mimi siwezi kuyaelezea. Sipo hapa kwa ajili ya kumkampenia, hiyo sio kazi yangu isipokuwa nataka kuhalalisha kauli yangu.

Leo hii tembelea mkoa wa Mbeya, Arusha, Mwanza halafu uliza kama mikoa hiyo iliegemea dhana ya ubaguzi wa kikabila dhidi ya wageni. Wageni walikaribishwa na wenyeji na kufanya kazi bega kwa bega. Leo hii unaweza kuona maendeleo makubwa katika mikoa hiyo na kutokana na hilo viongozi wakiwamo wabunge wakahamasika wakaona kweli hili linawezekana. Nasema hivyo kwa sababu inawezekana hata katika mkoa wa Mtwara pamoja na ufisadi unaofanywa na hao viongozi wa serikali, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na fedha lakini kama wananchi wakishirikiana vizuri na wageni maendeleo yanawezekana.

Hivi karibuni nilisoma makala moja katika gazeti(silikumbuki) gazeti hilo lilikuwa linaelezea maendeleo na mabadiliko makubwa katika mkoa wa Morogoro. Katika Mkoa huo, kichocheo kinaelezwa ni kuwa na ushirikiano wa bega kwa bega baina ya wananchi wa huko pamoja na wageni ambao wameshalowea. (By the way Nyerere aliikataza hii hali sijui kwanini watu wanaiendekeza). Meya wa pale hana mchezo yeye anahimiza watu wachape kazi katika halmashauri/manispaa/mji kwa kusimamia matumizi sahihi ya pesa mgawanyo halali wa mapato na pia miradi mbalimbali. Kazi hii hufanywa kwa umakini mkubwa na usomi. Imefikia hatua watu wamemshauri agombee Ubunge lakini huyu bwana amekataa binafsi nampongeza huyu mheshimiwa.

Mtwara wanaendekeza uzawa/ukabila/ubaguzi hata wao kwa wao katika mambo mengi ambayo hata hayana kichwa wala miguu nilikwisha wahi kuhadithiwa hadithi kati ya "Mmawiya na mmakonde-malaba" watu wa kabila moja maeneo tofauti lakini wanabaguana ikapelekea mgogoro mkubwa miaka ya 60. Mtwara ukizungumzia hata masuala ya msingi utaambiwa "unaongea nini wewe kwanza sio mtu wa hapa subiri mkataba wako uishe uondoke" Sisi sote ni watanzania Mwalimu Nyerere aliweza kutulea vyema na tunaishi pamoja kwa kushirikiana mpaka leo lakini kuna baadhi ya masuala ambayo tunayaendekeza na yatatuletea matatizo kuanzia chini mpaka ngazi za juu. Mfano unapomwita mtu ambaye ana asili ya Asia ni fisadi papa wakati wapo watu serikalini wenye nafasi za juu za uongozi waliowawezesha wakafikia hapo walipo. kwa nini hao nao wasiwe mafisadi papa? Tena ikiwezekana jamii iwatambue hao watanzania wenzetu wanaojifanya na machungu na nchi wakati ndio madalali wanaoiuza na kuifilisi. Huo naweza kuuita pia ni ubaguzi kama wa huku Mtwara na kamwe tusitegemee maendeleo hapo.

Kutokana na dhana hiyo tusitegemee maendeleo bali ni chukua chako mapema uondoke waache na uzawa wao. Chukulia mfano, mfanyakazi wa kawaida mwenye kipato cha kawaida kapata pesa yake akaamua kufanya jambo la maendeleo litakalowafaidisha wazawa kwa kuwaajiri na kuwapa kipato akigundulika tu . Watu wanaanza kumfitini mpaka zikifika juu unasikia fulani kahamishwa bila sababu ya msingi. Kwa falsafa ya mtoto mdogo tu utagundua kuwa mtu yule kahamishwa kwa sababu anataka kufanya suala fulani la maendeleo nalo si kwa ajili yake ni kwa ajili ya hata watu wa hapa. Mtu ukijenga nyumba Mtwara unahama nayo? Kwa nini mtu ukianza tu unaanza kuona TAKUKURU wanakufuatilia mpaka matakoni hususan Mtwara? Kwani umeiba nini? Mbona hao mafisadi hawakamatwi? Mbona hao wanaochimba gesi na kuleta umeme hatujaona jipya zaidi ya kuishia mtama na huku wilaya nyingine zikitumia majenereta? Hayo ni maendeleo?

Hawa omba omba hawataisha kama nyinyi mnaojiita wazawa hamtaachana na dhana ya ubaguzi na unyanyasaji wa wazi kwa baadhi ya watu. Watu wanaokuja wageni wanaleta utaalam, changamoto ya mabadiliko na maendeleo yenye tija. Leo hii mgeni akija nyumbani kwako ukamkaribisha na kumkirimu utarajie mengi mazuri kutoka kwake lakini ukimnyanyasa tarajia mabaya toka kwake na haitaishia hapo.

Kwa kuhitimisha ningependa niipongeze kazi nzuri anayoifanya mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Mstaafu Anatoli Tarimo (Sasa Joseph Simbakalia) ambaye amekuwa akiifanya kazi yake kwa mapenzi makubwa na kujitoa mhanga wakati mwingine. Ni lazima tumuunge mkono pamoja na watendaji wengine ambao wanautakia maendeleo mkoa huu. Ili tuondokane na suala la omba omba kwanza tuachane na dhana ya ubaguzi , tukubaliane na changamoto za wageni, tufanye kazi, tutilie mkazo katika elimu kwa watoto wetu(badala ya kuwapa ming'oko,korosho ama pweza kwa ajili ya kuuza ama kuzurura mitaani), tuachane na mambo ya kizamani tuende na wakati, tuuheshimu utamaduni wetu kama vile Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyotaka tuwe.

No comments: