Monday, October 22, 2012

MAADUI WA UISLAM NA WAISLAM TANZANIA


Na Mohamed Mtoi na Asha Dii (Kupitia Jamii Forums),
Ndugu zangu.

Tunapo kuwa tunajiuliza mhemko wa udini unatoka wapi au nani wameusababisha na kuuasisi si vibaya tukajua maadui wakuu kwa upande wetu waislamu. Ukimjua adui ni rahisi kupambana naye na ni nusu ya ushindi kwenye vita ya kutafuta haki au usawa au kuondoa tunao uita unyanyasaji kwa waislamu au mfumo kristo kama wengine wanavyo penda kuita (Mimi sio muumini wa dhana ya mfumo kristo) maana nimeona wakati wote waislamu wenzangu wakishika nafasi kubwa serikalini, kwenye mashirika ya umma na hata mashirika binafsi.

Siuoni mfumo kristo kama unavyoitwa au kama baadhi ya waislamu wenzangu wengine wanavyotaka kuaminisha umma wa kiislamu juu ya hii dhana. Nasema sioni kwa kuwa bado naamini katika uwezo na si mfumo kristo, si uoni kwa kuwa hii nchi niya wakristo, wapagani, waislamu, wahindu na dini nyingine. Si uoni mfumo kristo kwa kuwa nimeshuhudia watu kama kina omari mahita, na said mwema wakiwa viongozi wa vyombo ambavyo mara kadhaa vimesababisha mauwaji ya waislamu wenzetu na ndugu zetu wakristo pia. Mtanisamehe bure wenye mtazamo tofauti na wangu lakini siuoni mfumo Kristo nikimuangalia JK na makamu wake, si uoni mfumo Kristo nikimuangalia wajina wangu Mohamedi Sheini na Sharif Hamad, siuoni mfumo Kristo nikimuangalia Chande Othman (yule jaji mkuu) na Othaman Rashid (mkurugenzi wa Usalama wa Taifa), siuoni hata nikiungalia kwenye wizara na taasisi nyingine za serikali.

Wanaoongela mfumo Kristo hawana uthibitisho wa kutosha kuhalalisha madai yao ambayo kwa sasa nayaita hayana mashiko bali yametawaliwa na ukame wa maono na kiangazi cha fikra kinacho piga macho pazia mchana wa jua kali.

Kwa waislamu na wasio kuwa waislamu, Lazima tutambue kuwa adui wa waislamu sio wakristo, wapagani, wahindu,au dini nyingine zinazopatikana kwenye huu ulimwengu.

Lazima tujue kuwa sisi ni ndugu tunaohitaji kuishi kwa upendo na kuvumiliana bila kuathiri imani zetu, na ikitokea lazima tutafute njia za amani kupata suluhu.

Kwa mtazamo wangu hawa ndio maadui wakubwa wa uislamu kwa Tanzania.

 Adui namba moja kwa waislamu ni kutokuwa na mashule na vyuo vingi vyenye kutoa elimu bora kwa vijana wa kiislamu na hata wale wa upande wa pili wanaokuja kuitafuta elimu. Najua kuna watu watapinga sana lakini ukweli mchungu lazima tuuseme ili tupate pa kuanzia, mtakuwa mashahidi hata shule tulizo nazo hazifanyi vizuri sana kwenye mitihani ya kitaifa lakini pia hata mashule yetu hayana mfumo wa kuandaa masheikh walio iva kwenye elimu dunia na akhera. Mimi napendekeza harakati zetu ziwe kwenye kujenga mashule ya viwango pamoja na kuajiri walimu bora bila kujali dini zao ili kuwaandaa vijana bora wanaoendana na kasi ya sayansi na teknolojia kuelekea soko la ajira ya ushindani na pia viongozi bora wa dini.

 Kukubali kufanywa nyezo ya CCM kupata uhalali wa kutawala kwa kura za waislamu. Lazima tujue kuwa CCM wametutumia vya kutosha na kutudanganya vya kutosha, sasa tuseme basi! Mfano:~ Wametudanganya swala la mahakama ya kadhi wakati wa kampeni 2010 waislamu waliotaka tuwe na kadhi kwa kauli hadaa ya CCM wakapiga kura za kuhadaiwa lakini baada ya matokeo wakatugeuka! Huku ni kuonekana kuwa tu-malofa wa kudanganywa, tuunge mkono chama ambacho hakita tugawa lakini pia ambacho hakita tugawa na kuharibu umoja wetu wa kitaifa.

 BAKWATA imekuwa ni kama taasisi ya CCM, wanamuweka wanayetaka wao. Lazima tupiganie BAKWATA kiwe chombo huru cha waislamu na tuweke viongozi wenye maono mapana tunao taka sisi sio CCM hii itasaidia kurejesha imani kwa BAKWATA. Napendekeza Qualification ya kuongoza BAKWATA iwe ni PhD kwa kuangalia uwezo wa elimu akhera na elimu dunia lakini pia pamoja na uwezo wa kuongoza na kusimamia mambo. Chuo kikuu cha MUM kinaweza kusaidia kuratibu kupatikana wataalamu na watendaji wengine wa BAKWATA ambao nao kiwango cha chini cha kuanzia kiwe shahada moja na kuendelea.

 Kutokufuata mafundisho ya mtume. Mtume wetu Muhammad S. A. W alikuwa mwema, mwingi wa hekima na busara. Lazima tuyafuate mafundisho yake na kukumbushana mema na kukatazana mabaya, uislamu haujajengwa kwenye misingi ya uhasama, vurugu, fujo, chuki na mambo mengine mabaya. Uislamu umejengwa kwenye misingi ya usafi wa matendo mema, kumcha Mungu, ukarimu, na kuhurumia na kuwajali wengine. Tukiyafanya haya tutawaepuka wale wanao utumia uislamu wetu kama daraja ambalo baadae hutuchafua wote. Mfano wale walio ingia kuchoma na kuvunja kanisa na kuiba sadaka, baadhi ya vifaa vya kanisa na mikate.

"Uislamu ni unadhifu" hii ni moja ya tafsiri ya hadithi za mtume wetu kipenzi Muhammad S. W. A. Tuyafuate mafundisho yake kwa matendo ili tumuenzi kipenzi chetu.
    Lugha ya Kiarabu katika Mafundisho

Lugha ya kiarabu inayotumika kufikisha ujumbe uliopo kakika kitabu kitukufu cha Kiislam. Ni wazi kuwa njia kubwa ya kupata mafundisho ya Mwenyezi Mungu ni kwa kupitia Msahafu ambao una mafunzo mbali mbali ya njia na namna mbali mbali ya kuishi… Na bahati mbaya ama nzuri msahafu ni kitu takatifu kwetu, hauguswi ovyo bali uwe na udhu na kujipanga kwa kutaka kusoma na kuelewa sio kwa mzaha...

Dini ya Kiislam ni dini ya kistaarabu, iliyojaa mafunzo yaliyojaa wema na upendo ikiwa na hadithi lukuki ya namna ya kuishi katika jamii bila kumkwaza Mwenyezi Mungu na wale waliokuzunguka. Katika dini yetu ya Ki Islam kuna hadi hadithi ya dhambi ambayo inaweza pata kwa kutema mate ovyo na mbele ya hadhara… LAKINI bahati mbaya sana mengi ya yaliyo mafundisho ni mengi ambayo viongozi wetu wengi wa Ki-Islam hufundisha yale ambayo wanaona yanatakiwa..

kuna baadhi ya misikiti mwaka mzima mawaidha yale yale, umuhimu wa sadaka, usizini, usiibe, n.k Mawaidha ambayo baadhi ya Viongozi wetu hawazingatii wala kufuatilia… Hilo sio tatizo sana kama ilivyo tatizo la waumini wengi ambavyo tunaingia mkumbo na kukubali mengi ya tushawishiwayo/ambiwa hata kama havihusiani na dini vitahusishwa kwa njia moja ama nyingine… Kama ilivyokuwa swala la sensa.


Kujivua Uislam kwa Waumini wa Waislam

Wale ambao kwa kiasi kikubwa wangekuwa wakombozi katika kuendeleza na kukuza Uislam na kurudishia heshima yake stahili katika jamii yetu hujivua Uislamu, wapo waislamu wengi wasomi, sikubaliana na hoja kuwa Waislamu wasomi hawapo… Ama kuwa waliosoma ni wachache… Hiyo sio kweli, mana tupo katika wakati ambao nchi ina viongozi wa Ki-Islam ngazi za juu, kati na chini kuliko wakati wowote ule katika historia ya Uongozi wa nchi.

Hata ni ajabu kuwa kuna lawama kubwa sana za ukandamizaji na hali viongozi wa juu wengi ni Waislam katika taifa ambalo sio la kiislamu bali la wanachi wenye imani mbali mbali. Ninaposema kujivua Uislam nina maana wale ambao ni Waislam katika jamii hasa ambao wamejichanganya katika jamii badala ya kuji acknowledge kuwa wao ni Waislam hujifanya kana kwamba wapo huko bahati mbaya… Hao ndio walikuwa njia ya kuelewesha umma, iwe waislam ama sio waislam kuwa sio yote yale ambayo huwakilishwa huwa ni sawa na sahihi… Swala ambalo linazidi udidimiza Uislamu.


Mafunzo ya Vitisho katika Dini

Katika dini yetu ya Kiislam mafunzo ya dini huambatanishwa sana na vitisho… Na mara nyingi elimu akhera hupewa wakati tukiwa watoto… Unafundishwa kwa njia ya vitisho kwa namna moja ama nyingine. Ukifundishwa kuwa kitu Fulani ni kosa adhabu yake unapewa ‘imagination’ ya kuogofya na kutisha. Kwa mtoto hadi pale unapokuwa kama hujabahatika kuisha maisha ya kueleweshwa kwa njia zaidi ya elimu unapowa unaweza kuwa rigid sana katika imani hata kwa yale ambayo sio msingi kuwa rigid. Naamini kuwa ni DHAMBI kubwa sana kushika msahafu huna udhu, sembuse kuukojolea?

Mimi kama muumini nikiwa karibu nastahili kumuelwesha yeyote asielewa (hasa ambaye ni dini tofauti) kuwa haruhusiwi hata kuugusa let alone kuukojolea. Haya mafunzo ndio sasa kwa namna moja ama nyingi umepelekea tatizo kubwa lililo zaa matatizo katika jamii nzima. Haya mafunzo ya vitisho ndio yalifanya Yule kijana Muislam katika lile alilomwambia mwenzie na kupelekea mwenzie kutaka kufanya majaribio kama ni kweli… Ndio maana kwa kiasi kikubwa namlaumu sana aliye tulia tuliiii akisubiri mwenzie akojolee kuona kama atageuka nyani... Kwa mtazamo wangu katenda dhambi kubwa! Karuhusu na kushawishi kwa nguvu zote kitabu kitakatifu kichezewe.. Kwa kweli inasikitisha...Kukosekana kwa ustaarabu

Ustaarabu, sijajua kuwa tulikwamia wapi hasa… Katika jamii ya watu waliochanganyikana hatuwezi wote kuwa sawa, hatuwezi wote tukaamini kitu kimoja. Na kawaida kila kundi lina namna yake ya kutamka na kuita kundi ambalo hawawakubali… Kuna maneno kama “Kafiri” na “wagalatia”. Kutumia maneno kama hayo kwa kumuita mtu hivyo moja kwa moja hujenga chuki kubwa sana… Sasa hapa nashindwa kuelewa kuwa dhambi inapimwa pale ambapo muumini anatataka? Mradi anawakilisha dini yake ana ruhusa ya kutenda dhambi zingine? Huwezi hata siku moja kumbadilisha mtu Imani, msimamo ama mawazo yake kwa kukashifu, kumkejeli ama kumdharau!

Ni lazima umuingilie kwa kumuelewesha… Ni lazima umweleze kwa nini hapo alipo sio sahihi na kwa nini huko unakotaka aende kuna manufaa juu yake! Kuna mambo mengi wanadamu hufikiria ama kujisemea moyoni kuhusu watu mbali mbali, lakini tunajua fika kuwa kutamka haitakiwi… Sio sababu huwezi, sio sababu wamuogopa, wala sio sababu labda atakuadhibu… Ila tu kwa sababu kubwa kuwa inakuwa SIO ustaarabu kutamka lile ufikirialo juu yake! Tulichotofautiana na Wakristo katika “name calling” katika waliomini katika dini ni kwamba Waislam tuliowengi tunakutamkia kuwa wewe ni “Kafiri” na Mkristo anakufikiria ila atatamka akiwa na waumini wenzie (huo mfano hauingii kwa majority ya JF members walio na ushabiki wa matusi yasio na tija wala kujenga).Umimi wetu Waislamu

Inawezekana kweli serkali kwa njia moja ama nyingine imeweka mazingira ya kuupendelea ukristo, labda sio kwa nia hiyo ila ilitokea tu ama kwa makusudi. Hata hivyo kulitazama hilo swala linatokana na vile sisi twajitazama vipi... Kama tungejitazama kuwa tuna haki na hii nchi kama mtu yeyete yule iwe Mkristo ama sio mkristo ina mana tungeweza piganaia kuweka na kutengeneza mazingira ya kuhakikisha kuwa na sisi tunakuwa na kupata hilo ambalo tunaona tunapunjwa badala ya kulalamika..

Umimi umekuwa mkubwa saana kwa waislamu walio wengi... In the sense kuwa mimi ni muislamu basi kila kitu hadi nchi iendeshwe Kiislamu... HAPO nauliza kwa misingi ipi? kwa nini? na wa imani nyingine iwe vipi? Ama haihusu sababu sio Waislamu? Na kama haihusu - ni vigezo vipi vya fikra vinatumika kufikiri hili kwa kina?

Inakuwa mimi, mimi mimi... Mimi kama Muislam nina haki hii…. Mimi Muislamu matatizo yangu yanasababishwa na huyu… Mimi nakandamizwa… Mimi ndio nastahili sio Yule (hata kama muislamu mwenzio). Dini inafundisha tumheshimu kiongozi wetu, sasa hiyo ruhusa ya kumdarau kiongozi wako kwa ushabiki sio hoja unatoka wapi? Haya basi wewe ni Muislamu unakandamizwa; umejiuliza Waislamu wengine walifika hapo unapopataka wamefikaje? (Kiongozi anakuja na hoja aliyefiika hapa ni msaliti sio muislamu kamili – Huyo kiongozi ni Mungu??) Unapolalamika unakandamizwa ni haki kulalamika LAKINI Je upo tayari kwa mabadiliko? Upo tayari a wewe kucheza nafasi yako ama unasaburi uletewe hayo mabadiliko katika sahani? Kama yote hayo ni kweli hatutakomboka kwa kulalamika ama kwa vitendo vya hasira bali kwa vitendo vya kujenga na kuweka misingi bora ya UISLAMU mbeleni ndani ya taifa letu!

Waislam… Bado tupo nyuma.. Bado tuna safari ndeeefu, nab ado tunahitaji kujikomboa kabla ya kukombolewa. Dunia ya leo kila mmoja ana maslahi yake binafsi... Inatakiwa kutulia, kutafakari, kujuwa hasa ni nini UNATAKA, nini haki na sawa na kipi ambacho hata Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtume Mohammad (S.A.W) atakubali kuwa ni haki ufanye. Maisha yamebadilika…. Dunia imebadilika.. Nyakati zimebadilika. Inatakiwa tusibadilike Uislamu wetu ila tubadilike yale ambayo sio lazima yafafanuliwe kwa Uislam kwa maslahi ya wachache wenye niya na malengo ya kutumia Uislam na Waumini wa Waislam vibaya! Tufanye mambo kwa kujipanga, kutafakari na ustaarabu huku tukimhusisha Allah kumuomba kutupa hekima katika matendo yetu.

BTW, Nakubaliana na swala la BAKWATA, Hicho chombo inabidi kivunjwe kwa manufaa ya wengi sababu ni asilimia kubwa ya Waislam tunapingana nacho na kuona kuwa hakifai.

Huo ni mtazamo wangu, kama kuna mahala nimeonesha kutoelewa swala kwa ukina kwa namna ya maelezo, nakaribisha kuelezwa/eleweshwa.

Wabillah Tawfiq.JAMII FORUMS

No comments: