Friday, October 5, 2012

KUSHINDA BILA KUSHINDANISHWA WAZIMU WA DEMOKRASIA
CHADEMA kataeni upuuzi huo uliobuniwa na CCM


Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela
,

MOJAWAPO ya nukuu ambazo zinakumbukwa sana kutoka katika kauli za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere ni ile ambayo ilikuwa inasema kuwa “mtu mwenye akili, akijua kuwa na wewe una akili akakushauri jambo la kipumbavu na wewe ukakubali atakudharau”.

Kimsingi kauli hii ilikuwa inamaanisha kuwa kama mtu ana akili timamu ni lazima awe na uwezo wa kupima mambo ambayo anaambiwa au anashauriwa na watu wengine wenye akili. Mtu ambaye ana akili halafu anashauriwa na watu wengine wenye akili mambo ya kipumbavu naye anakubali mtu huyo anadharaulika.

Ninaamini kauli hii ya Nyerere inaweza kupelekwa mbele kidogo. Viongozi wenye akili wakijua wananchi wao wana akili na wakawashauri jambo la kipumbavu na wananchi wakakubali basi viongozi hao wanawadharau wananchi. Viongozi wa aina hiyo huweza kujiaminisha kuwa wanaweza kutenda jambo lolote bila kuulizwa.

Na mojawapo ya mambo ambayo binafsi nimeshayakataa huko nyuma na kuendelea kuyakataa kwa sababu ni ya kijinga ni hili la watu ambao wanataka nafasi za umma kwa njia ya demokrasia lakini inapofika kutumia demokrasia ati wanapita bila kupingwa. Halafu wanaenda na kujitambulisha kuwa wao ni ‘wawakilishi’ wa kundi lile ambalo hawakupigiwa kura.

Kura ni uchaguzi

Kama jamii yetu inataka kuwa na viongozi wazuri tu na wenye uwezo na wenye kukubali haiitaji kuweka utaratibu wa kura. Kwa sababu kama tayari watu wapo wenye uwezo, wenye kupendwa, wenye ushawishi na wanaotoka katika familia mashuhuri kwa nini basi tusiamue tu kuwafuata watu hawa na kuwapa nafasi za kutuongoza?

Fikiria mfano mzuri wa jinsi mke wa Rais Kikwete pamoja na mtoto wa Rais Kikwete walivyoweza kupita kuwa wajumbe wa NEC kupitia wilaya zao. Salma Kikwete yeye amepita ‘bila kupingwa’ huko Mkoa wa Lindi wakati mwanae Ridhiwani amepita ‘bila kupingwa’ kuwakilisha Wilaya ya Bagamoyo. Si wao tu wapo na wengine ambao wamepita bila kupingwa vile vile.

Sasa kura ingeamua hawa wawili wanakubalika kiasi gani. Ikumbukwe kuwa sisemi hata kidogo kuwa hawakustahili bali nasema ni demokrasia ya kipuuzi kupitisha watu bila kuwashindanisha halafu wakapewa nafasi ya kuwa wawakilishi wa watu sehemu yoyote ile. Edward Lowassa amepita huko Monduli baada ya kupigiwa kura wakati Frederick Sumaye ameanguka kule Hanang kwenye sanduku la kura vile vile. Bila kuwapa wananchi nafasi ya kuchagua na kutumia haki yao hiyo tunajuaje kama mtu anakubalika kweli?


Kuondoa wapinzani ili kupita bila kupingwa

Mojawapo ya matokeo ya mfumo huu hatari ni kuwa tunakaribisha umafia wa kisiasa. Kama mtu akitaka kugombea nafasi fulani sema ya ubunge na akajua kuwa hasimu wake naye anaweza kumpiku si anaweza kufanya kila mbinu ili hasimu wake asiendelee kugombea?

Je, kama kuna uwezekano wa kutumia ushawishi wa fedha kumfanya mgombea mwingine au wagombea wengine wajitoe au wasitimize vigezo vya kuweza kuwa wagombea kwa nini mtu asichukue hatua kufanya hivyo kama baada ya siku atatangazwa kuwa ni “mbunge mteule”?

Mfano mzuri wa hili ni kile kilichotokea Jimbo la Nyamagana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010. Aliyekuwa mgombea wa CCM kwenye jimbo hilo na wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alikuwa amejihakikishia kwa kiasi kikubwa kwamba angeweza kushinda.

Lakini kwa namna ya ajabu zilifanyika jitihada kubwa sana ili mgombea wa CHADEMA Ezekiah Wenje asiweze kushiriki na hivyo yeye Masha kuwa mgombea pekee na kuwa mbunge aliyepita bila kupingwa. Katika kutengeneza mizengwe ya hali ya juu, Ezekiah Wenje akatangazwa kuwa hana sifa ya kuwa mgombea kwa vile ni raia wa Kenya. Ikumbukwe kuwa Idara ya Uhamiaji ilikuwa chini ya Lawrence Masha.

Ingekuwa nchi nyingine Masha angefungwa kwa kutumia madaraka yake vibaya! Kweli kwa muda kidogo Masha akawa ‘mgombea pekee’. Bahati nzuri wapo watu waliofanya jitihada kubwa kuhakikisha Wenje anarudishiwa haki yake.

Matokeo yake ni nini? Uchaguzi Mkuu ulipofika walipopambanishwa hao wawili Wenje alimbwaga Masha kwa kura nyingi. Lakini kama wasingepambanishwa Masha angerudi kama mbunge!Mfumo huu unalea woga

Sasa jambo jingine ambalo limekuja na mfumo huu mbovu ni kuwa unalea woga. Kama mtu anajua hawezi kushinda kwenye sanduku la kura yuko tayari kufanya lolote lile asijikute anapambanishwa. Fikiria kwa mfano mtoto wa Kikwete anagombea Bagamoyo na mtu ambaye si maarufu halafu anaangushwa au anapita kwa kura chache sana si ataonekana vibaya? Fikiria Salma Kikwete anagombea kule Lindi (ambako haishi!) si ingekuwa aibu ya karne! Sasa huu woga ndiyo umefanya huu mfumo uendelee.

Wanasiasa waoga na ambao hawawezi kusimama mbele ya wapiga kura na kuhukumiwa nao hutegemea mtindo huu. Ndiyo maana leo hii Bunge letu lina watu ambao kwa kweli si wabunge halali (japo ni wa kisheria) kwani hawakuchaguliwa na wananchi. Ikumbukwe Katiba yetu iko wazi sana kuwa zipo aina zifuatazo za wabunge; anayeingia kwa ofisi yake (ex-officio) yaani Mwanasheria Mkuu , wabunge wa kuchaguliwa kutoka majimbo ya uchaguzi (ndiyo wengi zaidi), wabunge wa viti maalumu, wabunge wenye kuwakilisha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na wale wa viti 10 vya kuteuliwa na Rais.

Katiba iko wazi katika hili. Ibara ya 66:1a inasema kuwa aina ya kwanza ya wabunge watakuwa ni wale “waliochaguliwa kuwakilisha majimbo yauchaguzi”. Si “waliokosa wapinzani”; si “waliopitishwa na NEC”; si walioachwa wagombee wenyewe! Bali wale waliochaguliwa kuwakilisha katika majimbo ya uchaguzi.

Kwamba ati mtu amejikuta peke yake kwenye jimbo na hakuna aliyerudisha fomu ya kugombea basi “kunamfanya awe amechaguliwa” ni ujinga wa hali ya juu na sisi kama taifa kukubali jambo hili kunathibitisha tu kuwa tunastahili dharau kutoka kwa watawala.

Kama hawajachaguliwa wanaweza vipi kuwa wabunge wa “kuchaguliwa”? Na unaweza vipi kuchagua kama hata nafasi ya kuulizwa “unakubali au unakataa” haipo?

Hata kuuliza “ndio” au “hapana” au hata kuwaweka na “jembe na kuku hatuwezi? Wakati wa Nyerere inaweza kujengwa hoja kuwa demokrasia ilikuwa kamili. Kwani hata pale ambapo mgombea alikuwa ni mmoja tu wananchi bado walipewa nafasi ya kupiga kura kati ya mgombea huyo na nyumba au jembe! Leo hii watu wanadharau na kusema “hakukuwa na demokrasia” kwa sababu ati watu walipewa “mtu na jembe” wanasahau kuwa kwa kufanya hivyo watu walitumia haki yao ya kuchagua.

Leo hii haki hii ya kuchagua imefutwa kabisa kuanzia kwenye vyama na hadi kwenye taifa na watu wanafikiria kuna demokrasia zaidi sasa? Demokrasia gani ambayo hairuhusu watu kuchagua kwa uhuru hata kama wanachagua jiwe?

Fikiria kwa mfano, jimbo mojawapo ambalo mbunge wake amevuliwa ubunge halafu uchaguzi unarudiwa na kabla ya kurudiwa yule mgombea mwingine anajitoa si ina maana yule mwingine aliyebakia atakuwa mgombea na atapita bila kupingwa? Kweli hiyo ni demokrasia?

Huu ni wazimu wa demokrasia. Ni matumaini yangu CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani nchini na kinachobeba jina la “cha demokrasia” kitakuwa cha kwanza kufuta upuuzi huu katika mfumo wake wa uongozi (wasiwepo kabisa watu ambao watashika nafasi bila kuchaguliwa) na vile vile kuwa kinara wa kupinga mfumo huu dhaifu uliobuniwa na CCM kitaifa. Na sisi wananchi tusikubali hata kama mtu hawezi kushinda ni bora ajitokeze ili kuwapa watu nafasi ya kuchagua.

Kama watu wenye akili timamu tukikubali mambo ya kipuuzi na tukijua ni ya kipuuzi basi tunastahili kudharauliwa.

RAIA MWEMA

No comments: