Saturday, October 13, 2012

CNN INAPOIONYESHA DUNIA USHIRIKINA WA WATANZANIA
Nchi nyingine ni utalii, kwetu ni uchawi


Na Johnson Mbwambo,
WIKI mbili zilizopita, katika Raia Mwema Na. 261, niliandika kuhusu namna nchi yetu ilivyobobea katika ushirikina na uchawi; huku viongozi wetu (au tuseme watawala wetu) wakiwa mstari wa mbele.

Msingi wa hoja zangu katika makala hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na asasi ya Washington DC inayoitwa PEW Research Centre yanayoonyesha kuwa asilimia 93 ya Watanzania wanaamini katika masuala ya ushirikina wakati ambapo kwa Uganda ni asilimia 29 na Kenya ni asilimia 27.

Niliandika kwamba Watanzania wengi wanaamini katika ushirikina kwa sababu ya uvivu wa kufikiri. Nilisisitiza kwamba, mara nyingi Watanzania hawataki kusumbua bongo zao kufikiri, kudadisi na kuchunguza; hata kwa yale mambo madogo kabisa ya kilaghai yanayofanywa na ma-sangoma au hata wale manabii wa uongo ambao hivi sasa wametapakaa kila kona ya Tanzania.

Andiko langu hilo lilivuta hisia za kila aina kutoka kwa wasomaji. Wako walioniunga mkono katika nilichoandika; huku wakitoa ushuhuda wao wenyewe wa namna walivyowahi kutapeliwa na watu hao, lakini wako pia walionishangaa kwa kutoamini katika ushirikina; huku wakinipa vifungu vya Biblia vinavyothibitisha kuwapo kwa wachawi tangu kale na nguvu zao.

Wako hata waliokwenda mbali zaidi na kunialika nihudhurie ibada za ‘manabii’ wao nijionee mwenyewe ‘miujiza’ inayotendeka ndani ya makanisa yao.

Kwa wote hao walionitumia sms au e-mails, ujumbe wangu kwao ni kwamba: Wangejihangaisha japo kidogo tu kutafiti, kudadisi na kuchunguza, wangeligundua kwamba hao wanaowaita sangoma (wachawi) au ‘manabii’ hawana miujiza yoyote wanayoifanya bali ni usanii na u-adakadabra tu ambao unafanikiwa kwa sababu ya uvivu wao wa kufikiri.

Nilikuwa nimefikia uamuzi kwamba sitaandika tena, mwaka huu, kuhusu masuala hayo ya kubobea kwetu katika ushirikina, kwa sababu sina cha ziada cha kuwashawishi Watanzania wenzangu kuiangalia dunia ya sasa katika mtazamo zaidi wa kisayansi na kiteknolojia badala ya mtazamo wa kishirikina.

Lakini nilichokiona kikitangazwa kuhusu Tanzania na televisheni kubwa duniani ya CNN, usiku wa Ijumaa iliyopita, kilinifanya niamue kuandika tena kwa mara ya mwisho kuhusu suala hili la kubobea kwetu kwenye ushirikina.

Waliobahatika kuangalia kipindi cha CNN kinachoitwa Inside Africa, usiku wa Ijumaa iliyopita (Oktoba 5), watakubaliana nami kwamba televisheni hiyo imezidi kuibomoa sifa yetu duniani kwa kushindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza kwamba sisi Watanzania ni washirikina kweli kweli.

Kwa wale ambao hawakubahatika kukiona kipindi hicho, nawashawishi waingie katika mtandao wa cnn.com/insideafrica waone kile ambacho dunia imeonyeshwa kuhusu Tanzania yetu kubobea kwenye uchawi na ushirikina.

Mara nyingi mwandishi wa CNN wa kipindi hicho, Herrol Barnet, anapoingia katika nchi yoyote ya Afrika, wenyeji hufurahia kwa sababu nchi yao hupata fursa ya kutangaziwa mambo yake mema kama vile fursa za utalii, kukua kwa uchumi, biashara nk. ili dunia iyafahamu.

Kwa hakika, ndivyo ambavyo Barnet na wenzake katika CNN wamekuwa wakifanya katika nchi za Afrika walizozitembelea mpaka sasa kwa ajili ya kipindi hicho cha Inside Africa ikiwemo Madagascar waliyoitembelea karibuni.

Lakini Barnet alipoingia Tanzania, wiki mbili zilizopita, kitu cha kwanza alichorusha CNN kuhusu nchi yetu, usiku wa Ijumaa iliyopita, ni kubobea kwetu katika masuala ya ushirikina.

Barnet alikwenda ndani zaidi katika coverage yake hadi kuzungumzia suala la kuuawa kwa albino kwa imani za kishirikina, na hata kumhoji mmojawao aliyeeleza namna anavyoishi kwa shaka kubwa ya kuuawa na wanaosaka viungo vyao.

Kwake yeye Barnet, habari kubwa ya kuanza nayo kuhusu Tanzania si fursa za utalii zilizopo katika nchi yetu hii nzuri, bali ni jinsi Watanzania tulivyozama katika imani za kishirikina!

Maana yake ni kwamba, hata kama Barnet atarusha baadaye katika CNN mambo mengine mazuri kuhusu Tanzania, picha itakayobaki katika vichwa vya walimwengu wanaoingalia televisheni hiyo, ni picha ya nchi iliyozama katika imani za uchawi na ushirikina. Waingereza wanasema first impression is lasting impression!

Ndiyo maana, ndugu zangu, nasisitiza tena kwamba tusipozinduka na kuacha uvivu wa kufikiri, tutaendelea kuzama katika imani hizi; huku wenzetu wengine duniani wakichapa mwendo kimaendeleo katika dunia ya sayansi na teknolojia.

Hakuna asiyejua kwamba mikoa inayoongoza katika ushirikina katika Tanzania, kama vile Rukwa na Shinyanga, ndiyo pia mikoa inayoongoza kwa elimu duni ya wakazi wake na viwango vya chini vya maendeleo. Hata matokeo ya mitihani ya Taifa inathibitisha hilo kwa mikoa hiyo. Nayahusisha mambo hayo kwa sababu ushirikina hustawi pale penye uvivu wa kufikiri.

Katika hili la Barnet, tunaweza kuilaumu televisheni ya CNN kwa kuionyesha dunia kwamba Tanzania ni nchi ambayo ushirikina umetamalaki, lakini natujiulize; je, si ndivyo tulivyo?

Je, si kweli kwamba albino na vikongwe katika Tanzania wanauawa kwa sababu za kishirikina? Je, si kweli kwamba kuna uchunaji ngozi za binadamu katika mikoa ya Kusini kwa sababu za kishirikina? Je, si kweli kwamba ukiwa na upara utaogopa kutembea usiku katika vijiji fulani fulani vya Tanzania?

Lakini kwa upande mwingine, tutailaumi vipi CNN kwa kuitangazia dunia kuwa Tanzania tumebobea katika ushirikina; ilhali vyombo vyetu wenyewe vya habari vinaripoti masuala ya ushirikina katika mtazamo chanya unaoonyesha kuwa navyo vinauamini? Ni nani wa kuwaondolea ujinga huu wananchi kama vyombo vyetu vya habari vinaushabikia ushirikina?

Mfano mzuri ni gazeti moja kubwa la kila siku hapa nchini lilivyoripoti suala lile la Kikombe cha Babu wa Loliondo. Gazeti hilo lilimtuma mwandishi wake kuweka maskani Loliondo na kuandika kila siku habari za Babu wa Loliondo na kikombe chake.

Ripoti za mwandishi huyo hazikuwa za udadisi, utafiti au uchunguzi, bali zilishabikia tu kikombe hicho cha Babu katika namna ambayo ililifanya gazeti hilo lionekane kama vile limeithibitisha dawa hiyo ya Babu kuwa kweli inatibu ukimwi, kisukari na kansa.

Nina hakika gazeti hilo lilichangia katika kuwafanya Watanzania wengi waamini katika kikombe cha Babu, na hata wagonjwa kuacha insulin au ARVs zao, na hivyo hatimaye kufariki.

Sina haja ya kusisitiza hapa kwamba, kote duniani wananchi huzichukulia habari zinazoripotiwa na vyombo vya habari kuwa ndio ukweli, na hivyo waandishi wa habari na vyombo vya habari vina dhamana kubwa kuwaelemisha wananchi kuhusu ujinga wa imani za kishirikina unaoenezwa kwao.

Inasikitisha kwamba gazeti hilo hilo, hivi karibuni, lilimpeleka mwandishi wake mkoani Rukwa kuandika kuhusu kukithiri kwa uchawi katika mkoa huo.

Uamuzi huo ungekuwa ni mzuri kama gazeti lingelenga katika kuandika juu ya ushirikina katika mtazamo hasi, na kwa maana hiyo kuwaelemisha wananchi kwamba baadhi ya mambo wanayoamini kuwa ni uchawi ni abracadabra tu na usanii , na hivyo wasiuamini sana; lakini sivyo lilivyofanya.

Gazeti hilo liliripoti masuala ya uchawi katika makala zake kwa namna ambayo inautukuza, na inayowafanya wasomaji wauamini. Unapoandika (kwa mfano) kichwa cha habari kinachosomeka: “Radi huuzwa Sumbawanga kwa shilingi 40,000 tu”, unatarajia nini?

Maana yake ni kwamba, kwa kichwa hicho cha habari au makala, unatuma ujumbe kwa Mtanzania anayesoma habari hiyo aliye mvivu wa kufikiri, kuamini kwamba mvua na radi vinanunulika na vinatengenezeka huko Sumbawanga! Je, ni kweli?

Sasa wengi wetu tunajua kwamba unaweza kuyasambaza na kuyahamisha mawingu ya mvua kwa kuyanyunyizia kemikali fulani huko angani kwa ndege (kama wafanyavyo Thailand), lakini kwamba sangoma akiwa katika kibanda chake Sumbawanga anaweza si tu kutengeneza mvua, bali pia radi, ni jambo ambalo lingemwingiza sangoma huyo katika kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness, na nina hakika wanasayansi maarufu duniani wangemiminika huko Sumbawanga kujionea maajabu hayo ya dunia!

Ungetaraji mwandishi huyo katika makala yake hiyo angesimulia alivyoshuhudia mwenyewe mvua na radi vikitengenezwa na sangoma aliowahoji na kweli vikatokea, lakini sivyo; kwani badala yake aliishia na tambo za sangoma hao kuwa wana uwezo huo.

Ushahidi wa kile alichokiandika u-wapi hadi mhariri wake aipe makala hiyo kichwa aminishi kwamba radi huuzwa kwa Sh. 40,000 tu Sumbawanga?

Je, mhariri asingeweza kuandika kichwa cha habari chenye shaka kuhusu madai kuwa radi inatengenezeka na inanunulika? Je, mwandishi naye asingeandika makala yake katika mtazamo hasi, au basi wa kuonyesha shaka kuhusu tambo za sangoma hao za kutengeneza mvua na radi?

Kidogo ninachojua ni kwamba ukiingia kwenye google unaweza kujielemisha zaidi kuhusu jinsi radi zinavyotokea, zinapenda kupiga wapi na namna gani ya kujiepusha nazo wakati wa mvua nk. Hakika, ukijielemisha kwa undani kuhusu radi utasita kuamini kwamba binadamu anaweza kutengeneza radi au ujinga mwingine kama ule wa kwamba binadamu anaweza kuruka hewani kwa ungo!

Hayo pembeni, uvivu wetu wa kufikiri linapokuja suala la ushirikina unanikumbusha tukio moja lililotokea wakati nikiwa Mzumbe Sekondari, kule Morogoro, mwaka 1977, ambalo simulizi yake ndiyo hitimisho langu katika safu yangu ya leo.

Mzumbe Sekondari ipo karibu na kijiji kinachoitwa Changarawe. Ukiwa shuleni na ukitaka kwenda mjini, ni lazima upite Changarawe; kwani ndiko mabasi yanakosimama.

Asubuhi moja nilifika Changarawe ili nipakie basi kwenda Morogoro mjini. Nilikuta wanavijiji wa Changarawe wameizunguka nyumba moja huku wakifoka, na baadhi wakiwa wameshika mapanga.

Ingawa bado nilikuwa kijana mdogo na si kuwa mwandishi wa habari, nilijisogeza karibu na nyumba ile kujua kulikoni. Nikaambiwa kuwa ndani amejifungia mchawi ambaye alikutwa alfajiri akiwa amelala juu ya paa la nyumba hiyo uchi wa mnyama.

Kama si polisi kufika mapema eneo la tukio, wananchi wale walikuwa wamepanga kuichoma ile nyumba ili ‘mchawi’ afe au akitoka wamuue kwa kumkata mapanga. Bahati nzuri polisi walifanikiwa kuuvunja mlango na kuondoka na huyo aliyeitwa mchawi.

Kwa kuwa nilikuwa nakwenda mjini, nililifuatilia suala hilo polisi; hasa kwa sababu kulikuwa na polisi mmoja niliyemfahamu ambaye anatoka milima ya Upare kama mimi.

Polisi yule aliniambia kwamba mtuhumiwa huyo wa uchawi alifikishwa kituoni hapo akionekana kama vile alinyeshwa dawa ya usingizi, na kwamba katika maelezo yake aliyoyaandika polisi, alisema ya kuwa jirani yake alimgongea mlango usiku wa manane na alipomfungulia alimkamata na kushindilia tambara lililokuwa na unyevunyevu kwenye pua yake.

Aliandikisha maelezo polisi kwamba alianguka na kupoteza fahamu, na kwamba alipozinduka akajikuta yuko uchi juu ya paa la nyumba yake; huku wananchi wakiwa wamezunguka nyumba yake wakitaka kumuua kwa kumtuhumu kuwa ni mchawi.

Alisema ya kuwa aliruka chini na kufanikiwa kukimbilia ndani na kujifungia hadi polisi walipofika na kumwokoa.

Maelezo yake hayo yalithibitishwa na vipimo vya hospitali alikopelekwa na polisi ambavyo vilionyesha kuwa mtuhumiwa huyo wa uchawi aliwekewa chloroform puani ambayo ndiyo iliyosababisha alale fofofo na kupoteza fahamu.

Na kweli polisi waliporudi Changarawe na kuipekua nyumba ya yule jirani, walikuta chupa iliyokuwa na maji ya chloroform na uani pia walikuta pia ngazi.

Baadaye ukweli ukafahamika. Kilichotokea ni kwamba yule mtuhumiwa na yule jirani walikuwa wanagombea mwanamke, na kwamba kama mbinu ya kumpiku, jirani alikuwa akisambaza habari kijijini hapo kwamba yule jamaa ni mchawi na huwanga usiku!

Kwa hiyo, ili kumvunjia heshima akataliwe na yule mwanamke, na pengine auawe na wanakijiji wenye hasira, jirani yule alisuka mpango huo wa kumvutisha kwa nguvu chloroform usiku wa manane, kumvua nguo zote na kuubeba mwili wake hadi kwenye paa la nyumba yake kwa kutumia ngazi.

Lengo lake lilikuwa kwamba wanavijiji watakapopita asubuhi karibu na nyumba yake wamkute amelala uchi wa mnyama kwenye paa, na hilo lingethibitisha madai yake ya siku nyingi kuwa jamaa yule ni mchawi.

Kinachosikitisha katika simulizi hii ni kwamba ingawa polisi waliwasimulia wanavijiji kuhusu matumizi ya chloroform katika tukio hilo, na ingawa jirani yule aliyemsingizia mwenzake uchawi alitoroka na kuhama kijiji kuwakwepa polisi, bado jamii yote katika kijiji cha Changarawe iliamini kuwa yule bwana ni mchawi na alikuwa akiwanga uchi juu ya paa!

Kwa nini walishikilia kuamini hivyo licha ya ushahidi wa hospitali wa kutumika kwa chloroform? Ni kwa sababu imani za kishirikina zilikita katika mioyo yao kutokana na kuwa kwao wavivu wa kufikiri.

Na kwa hakika, kama si polisi wale kufika mapema mahali pale, yule jamaa angekuwa marehemu; kwani wangemuua kwa mapanga kwa imani potofu kuwa ni mchawi, na kwamba alikuwa anawanga juu ya paa; kumbe masikini mtu wa watu alikuwa ni mwathirika tu wa uovu wa jirani aliyekuwa anagombea naye mwanamke!

Ndugu zangu, tuachane na ushirikina, na tuanze kuitazama dunia yetu hii katika mazingira yake ya sasa. Tuitazame nchi yetu Tanzania katika mwanga wa kisayansi na kiteknolojia; vinginevyo kina Herrol Barnet wa CNN, BBC, Al Jazeera nk. wataendelea kuitangazia dunia kwamba Tanzania hakuna tujuacho zaidi ya kubobea kwenye ushirikina.

Mwanafalsafa wa kale wa Ugiriki, Socrates, alipata kusema kuwa pamoja na mwanga mkubwa (elimu) uliopo duniani, bado kuna watu wanaoishi gizani (ujingani). Watanzania tusikubali kuwa miongoni mwa watu hao wanaoishi bado gizani wakati kuna mwanga tele duniani!

Tafakari.


RAIA MWEMANo comments: