Thursday, October 11, 2012

ARV BANDIA ZANG'OA MABOSI MSD

Nora Damian


SERIKALI imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya kutokana na kubainika kuwapo na kusambaa kwa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s).

Mbali na mkurugenzi huyo, pia imemsimamisha Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud Maselo na Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa, Sadick Materu.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki kadhaa sasa tangu gazeti hili liliporipoti taarifa za kuwapo kwa dawa bandia za kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi katika mikoa mbalimbali nchini.

Dawa hizo bandia zilibainika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kufanya ukaguzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema dawa hiyo yenye jina la biashara TT-VR 30 toleo namba OC.01.85, imegundulika kuwa ni bandia baada ya kuifanyia uchunguzi wa kimaabara.

Alisema baada ya kubaini tatizo hilo walifanya ukaguzi kati ya Agosti 6 hadi 31 mwaka huu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na mikoa mingine nchini.

Waziri Mwinyi alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini nyaraka zinaonyesha kuwa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) cha jijini Dar es Salaam kiliiuzia MSD dawa hiyo.

“Wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi kwa sababu wanatakiwa kufanya uchunguzi wa kile wanachokipokea…Tunachoona hapa ni kwamba uchunguzi haukufanyika sawasawa ndiyo maana tumechukua hatua za kuwasimamisha,” alisema Dk Mwinyi na kuongeza kuwa:

“Matumizi ya dawa hiyo inayotengenezwa na TPI yamesimamishwa na imeondolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kurudishwa MSD,” alisema.

Alisema tayari makopo 9,570 ya dawa hiyo yamerejeshwa MSD na kwamba bado wanaendelea na utaratibu wa kuyakusanya makopo mengine 2,600.

Waziri huyo alisema kuwa dawa hiyo ilitengenezwa Machi mwaka huu na muda wa matumizi yake unatarajiwa kuwa Februari mwakani huku zikiwa rangi mbili tofauti, njano na nyeupe.

Alisema dawa zilizokuwa na rangi ya njano zilikuwa na kiambata cha Efaverenz badala ya viambata aina ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine vilivyopaswa kuwepo.

Alisema vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikuwa tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.
Pia alisema wamesitisha usambazaji wa dawa zote zilizokwishatengenezwa na Kiwanda cha TPI ambazo ziko kwenye bohari za kiwanda hicho hadi hapo uchunguzi wa suala hilo utakapokamilika.


Awatoa wasiwasi watumiaji

Aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa waendelee kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi kwa kuwa dawa hiyo yenye mashaka imekwishaondolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Alisema bado wanaendelea na uchunguzi na kwamba hautachukua muda mrefu ili suala hilo liweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Dk Mwinyi alisema wamehakikisha kuwa dawa za ARV’s zenye ubora unaotakiwa zinaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.

Aliwakumbusha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuimarisha Kamati za Dawa za Tiba katika vituo vya huduma za afya ambavyo vina majukumu ya kusimamia upokeaji, uhakiki wa ubora na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.

“Ninatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa dawa zisizo na ubora,”

Baada ya gazeti la Mwananchi  kuchapisha habari za kuwapo kwa dawa hizo bandia sokoni, wataalamu mbalimbali wa dawa walitoa maoni yao akiwamo mtaalamu wa dawa kutoka Hospitali ya Amana, Dk Charles Lymo ambaye aliliambia Mwananchi kuwa kazi ya ARVs ni kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, hivyo endapo mgonjwa atameza dawa bandia, vijidudu vya ugonjwa huo vitaendelea kuushambulia mwili na kuudhoofisha.     MWANANCHI

No comments: