Friday, September 21, 2012

TAIFA LA MAFUKARA MILIONI 30 NA MABILIONEA 30
Na Zitto Kabwe,

Mwalimu wangu wa nje ya Darasa Issa Shivji hugawa Watanzania katika madaraja matatu;WalalaHoi, WalalaHeri na WalalaHai akimaanisha watu wenye kuishi kwenye dimbwila Umasikini, watu wenye ahueni na Matajiri. Katika mtandao wa kijamii(twitter) wakati naandika makala hii, mdogo wangu Michael Dalali akaniongezea daraja jipya ‘wakeshahoi’. Hawa wa mwisho nadhani ndio tunasema ‘masikini wakutupwa’ kwa lugha ya mtaani. Sijapata fursa ya kumwuliza Michael ilianifafanulie hili daraja jipya. Leo ninatafakari na wasomaji kuhusu madarajamawili tu, Walalahoi (Mafukara) na Walalahai (Matajiri).

Mwezi Juni, 2012 niliandika andiko katika lugha ya Kiingereza (The Bottom 30M, www.zittokabwe.com)kujibu swali la kwa nini Watanzania ni masikini licha ya utajiri mkubwa uliopo nchini. Katika makala hiyo ‘Mafukara 30M’ nilihitimisha kwamba Watanzania ni masikini kwa sababu watawala wetu wameamua hivyo kwa kutunga na kutekeleza serana mikakati ambayo inanufaisha watu wachache katika tabaka la juu la maishaambao wengi wanaishi mijini na kuacha watu wengi wanaoishi vijijini wakiwamasikini zaidi. Katika tafakuri ya leo nafafanua zaidi huu mtazamo. Watawala wetu ninaamini wakiulizwa tena na wanahabari kwanini Tanzania ni masikini hawatajibu hawajui (Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda wamenukuliwa zaidi yamara moja wakisema hawajui kwa nini nchi wanayoongoza ni masikini). Nimesema nakuandika mara kadhaa sababu za umasikini kuongezeka nchini licha ya kwamba uchumi unaonekana kukua kwa kasi.

Waziri wa Fedha ndugu William Mgimwa wiki iliyopita amerudia tunayoyasema kila siku kwamba Ukuaji wa Uchumi Tanzania haujapunguza umasikini. Tumekuwa tukisema kwamba mikakati ya kiuchumi tunayotekeleza haimsaidii Mtanzania wa kawaida maana hatuoni tofauti ya maisha yake. Serikali ikaendelea na inaendelea kutekeleza mikakati ile ile ikitegemea kupata matokeo tofauti.

Ndugu Mgimwa, Waziri wa Fedha, anasema, “takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi chamiaka 10 iliyopita uchumi umekua kwa wastani wa asilimia saba lakini umasikini umepungua kwa asilimia 2.1 tu ambayo ni ndogo ikilinganishwa na asilimia yaukuaji wa uchumi”. Akanukuliwa “Umasikini umepungua kwa asilimia 2.1 kutokaasilimia 35.6 mwaka 2001 hadi kufikia asilimia 33.4 mwishoni mwa mwaka janakatika kundi la masikini,”. Hakuna kauli mpya hata moja. Kinachosikitisha nikwamba Serikali imeendelea kuona MKUKUTA ndio mkakati pekee wa kuondoaumasikini nchini. Sera na mikakati ya Serikali ya kuondoa Umasikini imeshindwa.Taarifa ya Shirika la SID ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa kati ya mwaka 2001 na2011 watanzania takribani milioni 5 zaidi wameingia katika dimbwi la umasikini.Kwa nini Uchumi unakua kwa kasi kubwa lakini ukuaji huu haupunguzi umasikini,unazalisha masikini zaidi?

Taarifa za Serikali pia zinaonyesha kuwa ukuaji wauchumi hautengenezi ajira kwa watu. Kwa nini hali hii? Kama kawaida hatukosimajibu ya maswali haya. Tunayarudia majibu haya kila wakati tunapopata nafasiya kueleza. Kwamba Sekta za Uchumi zinazokua hazina mahusiano yenye nguvu nawananchi wa kawaida – Madini, Utalii na Mawasiliano. Sekta yenye mahusiano makubwa na wananchi – sekta ya Kilimo - haikui kwa kiwango kinachoweza kupunguza umasikini. Ili kupunguza umasikini Tanzania kwa kiwango kikubwa, sekta ya Kilimo inapaswa kukua kwaasilimia zaidi ya nane (8%) angalau kwa miaka mitatu mfululizo na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia sita (6%) kwa miaka kumi.

Jibu lipo na limeshasemwa sana lakini jawabu halisemwi. Labda tuulize tena. Kwanini sasa sekta ya Kilimo haikui kwa kiwango kinachotakiwa ili kuondoa umasikiniTanzania? Jawabu langu ni kwamba Watawala hawataki. Watawala wetu wamechaguaWatanzania wengi wabakie mafukara.

Umasikini wa Watanzania ni chaguo mahususi la watawala kwa kuamua kutekeleza sera ambazo zinakuza kipato cha mwenye nachona kufukarisha wananchi wengi wa vijijini. Vile vile uamuzi wa watawala kushindwa kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za umma niufukarishwaji wa mwananchi wa vijijini ambaye anakoseshwa huduma za jamii namiundombinu ya kumpa fursa ya kufaidika na shughuli zake za kiuchumi. Ufukarawa mamilioni ya Watanzania ni matokeo ya chaguo la watawala kisera, kimkakati na kimatendo.

Ufukarani tofauti na Umasikini ingawa tunatumia maneno haya tukiamini kuwa yana maanainayofanana. Wakati Umasikini (poverty) ni hali ya kukosa huduma za msingi kama Elimu, Afya, Chakula na Maji safi nasalama kunakotokana na kukosa kipato au kuwa na kipato kidogo, Ufukara(impoverishment) ni hali ya kukoseshwahuduma za msingi za kibinaadamu hatakama kuna juhudi za dhati za kufanya kazi kwa bidii ili kupata uwezo wa kufikia huduma hizo.

Umasikini unaweza kusababishwa na masuala mbalimbali ikiwemo hali ya kuwa masikini tu (‘we are poor because we are poor’) au jiografia nk.Ufukara unatokana na kufukarishwa. Unatokana na maamuzi ya kisera ya Taifa husika (au mataifa ya nje) ambayo yananyonya juhudi za watu kupata maisha yenye kuwapa huduma zote za msingi kama Elimu, Afya Maji na muhimu zaidi chakula cha uhakika. Mafukara wote ni masikini, ila Masikini wote sio mafukara. Nitafafanua.

Mwaka1991 Watanzania masikini wanaoishi Dar es Salaam walikuwa ni takribani asilimia28.1 ya wakazi wote wa Jiji. Miaka 16 baadaye, asilimia 16 ya wakazi wa Jiji laDar es Salaam walikuwa wanaishi kwenye umasikini. Kwa upande wa Watanzania wanaoishi Vijijini, mwaka 1991 kulikuwa na masikini asilimia 40 ya wakazi wote wa Tanzania vijijini. Mwaka 2007, miaka 16 baadaye, asilimia 37 ya Watanzania wa vijijini walikuwa wanaishi kwenye dimbwi la umasikini. Takwimu hizi unazipata kutoka Ofisi ya Takwimu na Shirika la Twaweza limerahisisha taarifa hizi kupitia chapisho lao ‘Growth in Tanzania: Is it reducing poverty?’

Masikini wanaoishi Dar es Salaam na miji mingine nchini wanaweza kujikwamua kutoka umasikini kutokana na fursa zinazojitokeza mijini. Miundombinu ya usafiri na usafirishaji, viwanda vipya na fursa za ajira zinajengwa zaidi mijini kuliko vijijini. Huduma za Elimu na Afya zinaboreka zaidi mijini na hata Walimu na Manesi wanakimbilia kufanya kazi mijini ambako wamerundikana kuliko vijijini ambapo kuna ukosefu wa kutisha wa wafanyakazi wa sekta hizo. Masikini wa mijini sio mafukara.

Masikini wanaoishi vijijini licha ya kufanya kazi kwa bidii na hasa kazi za Kilimohawana fursa za kuondokana na umasikini. Mfumo wa Uchumi wa nchi umejengwa kwamisingi kwamba watu wa vijijini hupokea Bei za kuuza mazao yao kutoka mijini navilevile hupokea bei za kununua bidhaa zinazotengenezwa mijini kutoka hukohuko. Barabara za vijijini zina hali mbaya au hazipo kabisa. Huduma za jamiikama Elimu, Maji na Afya ni mbaya. Huduma za nishati ya Umeme hazipo kabisa katika vijiji 96 kati ya vijiji 100 nchini. Masikini wa vijijini ni Mafukara.Wamefukarishwa kutokana na sera zinazonyonya jasho la kazi yao kwa upande mmojana sera zinazowanyima maendeleo ya miundombinu kwa upande mwingine. Asilimia 75ya Watanzania wanaishi vijijini hivi sasa na kwenye ufukara mkubwa sana. Kwa makadirio ya idadi ya watu Tanzania, Watanzania milioni thelathini waishio vijijini ni mafukara.

Kufunguliwa kwa miundombinu ya Vijijini kama Barabara, Maji na Nishati ya Umeme kunawezakuwaondoa watu wa Vijijini kwenye minyororo ya ufukara kwenda kwenye umasikinina hatimaye kutokomeza kabisa umasikini. Lakini Watawala wanaogawa rasilimaliya nchi hawataki.

Wanasema hakuna rasilimali fedha za kutosha kusambaza umemevijijini ili kukuza viwanda vidogo vidogo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo,kusambaza maji safi na salama ili kuboresha afya na kumpunguzia mwanamke wakijijini muda wa kutafuta maji na kujenga barabara za vijijini ili wakulimawafikishe mazao yao sokoni. Ikifika kujenga shule na zahanati na vituo vya afyawananchi wa vijijini wanaambiwa wajenge wenyewe, wajitolee. Ni kweli hakuna fedha za kuwekeza vijijini?


Ufisadi unatengenezaMabilionea

Itakumbukwa kwamba mwaka 2007 Bunge la Tisa liliibua kashfa mbalimbali zinazoonyesha namna ambavyo fedha za nchi zinavyoibwa na wenzetu wachache. Haina maana kwambaMabunge ya nyuma hayakuwa na Wabunge wenye uwezo au ujasiri wa kuibua masualaya msingi kuhusu fedha za nchi, lakini nadhani wakati au mazingira hayakuwa yanaruhusu.

Tulishuhudia Ufisadi uliofanywa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuibwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 133 za malipo ya Nje (EPA), Utoroshaji mkubwa wa fedha zilizofikia dola za kimarekani milioni 136 kupitia mradi wa Meremeta uliokuwa chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), Uingiaji wa Mkataba wa Madini ya Dhahabu wa Buzwagi uliokuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 400 bila kuzingatia uhitaji wa kuboresha mazingira ya nchi kufaidika na utajiri wa Madini na Wizi mkubwa wa Fedha za msaada wa kuagiza bidhaa kutoka Serikaliya Japani (Commodity Import Support) ambapo zaidi za shilingi bilioni 40ziligawiwa kwa viongozi kadhaa wa Serikali na wafanyabiashara.

Kashfa chache zilijadiliwa sana ikiwemo ile ya Mkataba wa kununua Umeme wa Richmond ambao sasa unelekea kuliingiza hasara Taifa ya zaidi ya shilingi bilioni 90kutokana na hukumu ya Kampuni iliyorithi mkataba wa Richmond dhidi ya Shirika la Umeme TANESCO, ile ya Buzwagi ambayo ilipelekea kuundwa kwa Kamati ya Bomani iliyopelekea kuandikwa kwa Sera mpya ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria mpya yaMadini ya mwaka 2010 na ile ya EPA iliyopelekea baadhi ya watuhumiwa kufikishwamahakamani lakini kuacha kitendawili kikubwa kuhusu Kampuni ya KAGODA ambayoilikwapua zaidi ya shilingi bilioni 40 katika shilingi bilioni 133 zilizoibwa.Masuala ya MEREMETA na Import Support yamezimika na mshawasha wa wafuatiliaji wa mambo kufuatilia masuala haya umepungua sana.

Masuala hayo machache yaliyoibuliwa katika Bunge la Tisa yanaonyesha kwamba kuna rasilimali fedha nyingi katika Taifa ambayo ingeweza kutumika kuwekeza kwenye maendeleo ya watu wa vijijini. Hata hivyo rasilimali fedha hii inatumika kufanya Watanzania wachache kuwa mabilionea kwa njia haramu za kifisadi. Bungela Kumi, ninaamini, litaibua masuala mengine zaidi yanayoonyesha namna ambavyo tumeamua kuwafukarisha Watanzania wengi na kuwabilionesha wachache.

Matrilioni ya shilingi yatoroshwa kila mwaka

Katika Kitabu cha ‘Africa’s Odious debts: Howforeign loans and capital flight bled a continent’ waandishi LeonceNdikumana na James Boyce wameonyesha kwamba katika kipindi cha miaka 40 jumlaya dola za kimarekani 11.4 bilioni zimetoroshwa kutoka Tanzania kwa njia mbalimbali. Hizi ni sawa na wastani wa dola za kimarekani 285 milioni kutoroshwa kila mwaka kuanzia mwaka 1970 mpaka 2010. Sehemu kubwa ya fedha hizi zinatoroshwa na Makampuni makubwa ya Kigeni yanayofanya biashara na kuwekezahapa nchini (utoroshaji mkubwa umefanyika mara baada ya Tanzania kuanza kuzalisha dhahabu kwa wingi na makampuni makubwa ya nje kuanza kutafuta mafuta na gesi asilia kwenye bahari ya Tanzania) na sehemu nyingine ni bakshishi wanayopewa maafisa wa Serikali wanaofanikisha utoroshaji huu. Watanzania hawa(Wanasiasa, Watendaji, Maafisa wa Jeshi na Usalama wa Taifa na Wafanyabiashara)huficha fedha hizi chafu kwenye Mabenki ughaibuni na hasa Uswisi, Dubai,Mauritius, Afrika ya Kusini na maeneo mengine (Tax Havens/Offshore/TreasureIslands). Wengine wamewekeza kwenye mali zisizo ondosheka kama majumba na zinazoondosheka kama hisa kwenye makampuni mbalimbali duniani.

Taarifa rasmi ya Benki ya Taifa ya Uswisi inaonyesha kuwa Watanzania wameficha huko zaidi ya dola za Kimarekani 196 milioni. Uchunguzi unaoendelea unaonyesha kuwa takribani Watanzania 30 wameficha Fedha zao katika Mabenki ya Uswisi. Hii ni bila kuhusisha wale ambao wameficha fedha zao kupitia majumba na hisa kwenye makampuni mbalimbali duniani na hasa katika nchi za Mauritius, Afrika Kusini na Dubai.

Uchunguzi pia unaonyesha kuwa Mtanzania mmoja ambaye hana rekodi yeyote ya Biashara zaidi ya utumishi wa Umma ameficha takribani dola milioni 56 katika Benki mojawapo nchini Uswisi. Serikali ya Tanzania mpaka sasa imekataa kuchukua hatua za kuwajua Watanzania hawa na kuhakikisha kuwa mabilioni haya yanarejeshwa nchini na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo vijijini. Serikali ya Senegal hivi karibuni imetuma maombi rasmi kwa Benki ya Dunia kuisaidia kufanya uchunguzi na kurejesha nchini mwao mabalioni ya fedha yaliyofichwa kwenye mabenki ya nchi za Ulaya na hasa Uswisi.

Ufisadi unafukarisha

Tanzania ina mtandao wa barabara wa zaidi ya kilometa 85,000 zikiwemo za vijijini na wilaya (zinazosimamiwa na Halmashauri za Wilaya) na za Mikoa na Barabara Kuu(zinazosimamiwa na TANROADS). Fedha zinazotoroshwa kila mwaka ni sawa sawa na kutorosha takribani kilometa 800 za babara za lami kila mwaka kwa kutumia gharama za sasa za ujenzi wa barabara. Fedha hizi pia zinaweza kuunganisha umeme kwenye vijiji 1300 (asilimia 10 ya vijiji vyote nchini) kila mwaka kwagharama za sasa za kuunganisha umeme tena kwenye mikoa ambayo haipo kwenyegridi ya Taifa (REA wanatumia takribani shilingi bilioni saba kusambaza umemekatika vijiji 16 vya Jimbo la Kigoma Kaskazini). Fedha hizi pia zingeweza kuajiri walimu wengi zaidi wa vijijini na kwa kuwa miundombinu ya umeme,barabara na maji ingekuwa imeboreshwa walimu hawa wangekaa vijijini nakufundisha watoto wetu. Ufisadi kama huu umekosesha nchi rasilimali zakuendeleza watu wake.

Rushwa na Ufisadi inatengeneza Watanzania wachache kuwa mabilionea. Mabilionea hawa ambao wana ushawishi mkubwa katika kuunda sera za nchi na utekelezaji wakewanapelekea kuundwa kwa sera na sharia zinazolinda utajiri wa walionacho na kuendelea kuhakikisha masikini wanaendelea kuwa mafukara. Rasilimali za nchi zinaboresha maeneo ambayo mabilionea na wasaidizi wao wanaishi na kusahau kabisa kwamba Watanzania wengi wanaishi vijijini na huko ndipo kuna umasikinimkubwa. Umasikini wa vijijini kwa kiasi kikubwa unatokana na sera na matendoyanayofukarisha wananchi wengi.

Ukuaji wa uchumi unaoambatana na ufisadi wa kiwango kinachotokea Tanzania unawafanyawenye nacho kupata zaidi na masikini kuwa mafukara zaidi. Tofauti ya kipato katika jamii imezidi kuongezeka na inaweza kuleta machafuko katika nchi. Takwimu zaPato la Taifa, kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2011,zinaonyesha kwamba asilimia 30 ya Watanzania (the richest 30%) wanamilikiasilimia 75 ya Pato la Taifa.

Tumeona kwamba Watanzania mafukara wanaishi vijijini, asilimia 75 ya Watanzania, na hivyo takribani Watanzania milionithelathini wanaoishi vijijini wanaishi katika dimbwi la umasikini. Vile viletumeona kwamba asilimia 30 ya watanzania wanamiliki asilimia 75 ya Pato lote laTaifa. Pato la Taifa mwaka 2011 lilikuwa shilingi 40 trilioni na hivyo asilimia30 ya Watanzania wanamiliki shilingi 30 trilioni katika jumla ya shilinig 40trilioni.

Kutokana na muundo wa uchumi wetu ambapo sekta ya Huduma (Servicesector) na ile ya Viwanda (Industrial sector) zinachangia zaidi ya asilimia 70ya Pato la Taifa na ukweli kwamba sekta zinazokua kwa kasi ni pamoja naMawasiliano, Madini, Ujenzi na Utalii, ni dhahiri Watanzania na Kampuni zaKitanzania zinamiliki zaidi ya shilingi trilioni moja hawazidi thelathini nakuna watu wanaweza kuwataja mmoja mmoja kwa majina yao au majina ya Kampunizao.

Kwahiyo Watanzania milioni thelathini wamefukarishwa kwa kunyimwa fursa zakiuchumi na hivyo kumiliki sehemu ndogo sana ya Pato la Taifa. Wanafanya kazikwa bidii lakini mfumo wa kinyonyaji unawaweka katika umasikini daima dumu.Tumeona kuwa uchumi wa nchi unazalisha kundi dogo la watu wenye utajiri mkubwa ambaosehemu kubwa umepatikana kwa njia haramu. Watu hawa pia wanamiliki sekta zauchumi zinazokua kwa kasi na hivyo utajiri wao unazidi kuongezeka.

Hawa wanashirikiana na Watanzania walio katikati (walalaheri) kuhakikisha wanaendelea kumilikiuchumi wa nchi. Hawa watu wa kati ndio wanasiasa, warasimu serikalini,wafanyakazi wa kada ya kati ya makampuni ya matajiri hawa au yanayofanya biashara na matajiri hawa. Badala ya watu wa kati kuweka sera madhubuti zakumkomboa Mtanzania wa chini aondokane na ufukara, wanaweka mazingira mazuri kwa matajiri kutajirika zaidi.

Hatimaye tunajenga Taifa la Watanzania Mafukara milioni Thelathini na Mabilionea Thelathini.

Tukatae. Tunaweza kujenga Taifa la watu wenye fursa sawa kwa kufanya maamuzi ya kubomoa mfumo wakiuchumi wa kinyonyaji tunaoujenga tangu kupata uhuru kwa kuacha kubomoa mfumowa uchumi wa kikoloni licha ya Azimio la Arusha. Juhudi za kujenga Taifa lenyewatu sawa ziliyeyuka mara baada ya kuamua kufuata sera za ubinafsishaji ambapozilitafsiriwa kwa kukabidhi mali za Taifa kwa kundi dogo la watu na hivyo kutengeneza mfumo wa kifisadi ambao sasa umeota mizizi. Kazi iliyofanywa kwa miaka ishirini ya kujenga uchumi wa viwanda ziliyeyushwa katika kipindi chamiaka mitano tu ambapo viwanda vyote viligawanywa kwa watu binafsi na vingi leoni maghala tu ya kuhifadhia bidhaa nyingine.

Ufisadi mkubwa ulishamiri kupitia sera ya ubinafsishaji ambapo watawala waliokuzwa kwa‘kanuni’ ya ‘kutosheka’ walijawa na tamaa kubwa na uroho wa mali na kuanzakukusanya chochote kilichokuwa mbele yao. Hivi sasa nafasi yeyote ya uongoziimekuwa ni nafasi ya ulaji na sehemu kubwa ya tabaka la watawala kuanzia kwawenyeviti wa vijijiji, madiwani, Wabunge, Mawaziri na hata Marais wamekuwa‘rent seekers’ yaani watu ambao ni lazima kulimbikiza mali kutokana na nafasiza utawala walizo nazo. Mfano wa Wabunge kulilia nyongeza ya posho za kukaa kitako wakati walimu na madaktari wanaishi katika mazingira magumu ya kazi nimoja ya tabia za kutotosheka na tamaa zinazopamba viongozi wa kisiasa wa zamahizi.

Kutochukua maamuzi madhubuti ya kutokomeza ufisadi na mfumo wake ni kufukarisha Watanzaniakwa sababu rasilimali ambayo inapotea kupitia vitendo vya kifisadi ingewezakuwekezwa katika maendeleo ya watu wa vijijini, kwa kukuza shughuli za kiuchumina kupanua mapato ya wananchi. Hivi sasa vita dhidi ya ufisadi imekuwa niturufu ya kisiasa tu na sio mchakato maalumu wa kuondoa kabisa mfumo wakifisadi. Ni lazima kuondoka kwenye hali ya kwamba wa ushujaa ni kutaja tu Fulani na Fulani ni fisadi, hali ambayo imefikia hata watu wasio na chembe ya uadilifu kuchafua wengine, na kwenda mbele zaidi kwenye hatua za kubomoa mfumo wa kifisadi.

Hata uchumi ukue kwa kasi ya namna gani iwapo ukuaji huo unanufaisha kikundi kidogo cha watu hauna maana na ni hatari kwa uwepo wa Taifa lenyewe. Ni lazima kuchukua maamuzi ya kujenga taasisi zenye nguvu ambazo zitaondoa hali hii ya uchumi kutajirisha wachache na kufukarisha wengi. 

 Taasisi na mfumo utakaohakikisha kuwa watawala wanawajibika kwa umma kwa wanayoyatenda na wasiyoyatenda. Mfumo utakaohakikisha kuwa rasilimali za nchi zinarudi kwawananchi ili kujenga miundombinu vijijini ya barabara, maji, nishati ya umemena huduma za kijamii hasa elimu na afya. Vinginevyo tutaendelea kuwa Taifavipande vipande kutokana na tofauti kubwa ya kipato na fursa ndani ya jamii.

Tanzania yenye Mafukara milioni Thelathinina Mabilionea Thelathini haikubaliki.No comments: