Tuesday, September 4, 2012

SHAHIDI AELEZA TAKUKURU ILIVYOMKAMATA MBUNGE
Tausi Ally


SHAHADI wa kwanza katika kesi ya kupokea rushwa inayomkabili Mbunge wa Bahi mkoani Dodoma (CCM), Omary Badwel ameieleza mahakama jinsi mtuhumiwa huyo alivyokamatwa.

Shahidi huyo ambaye ni Ofisa Upelelezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoa wa Pwani, Janeth Machurya jana aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na nia ovu ya kuchukua rushwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Spora Liana.

Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo, Machurya alidai kuwa baada ya kupewa taarifa na mlalamikaji, walichunguza namba za simu ili kujua kama kulikuwa na mawasiliano baina ya watu hao wawili kabla ya siku hiyo ya tukio.

Shahidi huyo alidai kuwa uchunguzi huo ulionyesha kwamba ni kweli namba ya mbunge huyo 0789 089189 iliwasiliana na malalamikaji Spora Liana ambaye ana namba 0784 858855 kuanzia Mei 30 hadi siku ya tukio. “Turijiridhisha namba hiyo ni ya mtuhumiwa na tulithibitisha kuwa ni kweli Juni 4, 2012 Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilikuwa na kikao chake jijini Dar es Salaam na halmashauri ya Mkuranga ilikuwa ni mshiriki, na tayari wakurugenzi walikwishaarifiwa,” alidai Machurya.

Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali, Lizzy Kiwia kutoa ushahidi wake, Machurya alidai kuwa Juni Mosi, 2012 akiwa ofisini kwake Kibaha alipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea akimtaarifu juu ya mbunge huyo kumshawishi Liana na kutaka waonane kwa kile alichodai kuwa kwenye kamati yao imeonekana kuna tatizo na mambo si shwari. Machurya alidai kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo alitafuta namba ya mbunge huyo ili aweze kuthibitisha kama malalamiko yaliyotolewa ni ya kweli.

Ili kuthibitisha hilo, alisema alimtaka Liana kuwasiliana na mbunge huyo lakini kabla ya kufanya hivyo, mbunge huyo alipiga simu yeye kwa mlalamikaji kwa kutumia namba ile ile ambayo alipewa awali na mlalamikaji. Baada ya mbunge huyo kupiga simu, Liana aliweka Loud Speaker (kwa sauti ya juu) na mbunge huyo alisikika akimwambia mlalamikaji kuwa anachelewa hivyo afanye haraka kwani anataka kuondoka.

Kwa mujibu wa shshidi huyo, mbunge alimwambia Liana kuwa amefika, yupo maeneo ya Hoteli ya Peackock na kumtaka wakutane huko. Shahidi huyo aliongeza kuwa baada ya taarifa hiyo, yeye pamoja na mlalamikaji na wapelelelezi wengine walikwenda katika hoteli hiyo na walipofika mlalamikaji na mtuhumiwa waliingia ndani.

"Baada ya mlalamikiwa na mlalamikaji kuingia ndani, mimi nilibaki nje nikiwa na fedha ambazo zilitoka kwenye taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)... nilibaki nje kwa sababu za kiusalama." Alidai kuwa baada ya muda, Liana alitoka nje na kunieleza kuwa waliongea kwa kirefu na kwamba kuna mahitaji ya fedha, Sh8 milioni, ili mbunge huyo aweze kuwakatia wajumbe wa kamati kiasi cha Sh1 milioni kwa kila mmoja,” alidai Machurya.

Aliendelea kudai kuwa, mbunge huyo alimwambia Liana kuwa wajumbe wapo 15 kwenye kamati hiyo lakini wajumbe waliopo ndani ya mtandao huo wa kuwasaidia watu ambao hesabu zao zimekaa vibaya wapo wanane.

Hata hivyo, shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka alidai katika mazungumzo hayo alimwambia mbunge huyo kuwa yeye hana fedha hizo lakini atamtangulizia kiasi kidogo ambacho ni Sh1 milioni na kukubaliana. “Liana alimwambia Badwel kuwa anakwenda kuchukua fedha hizo kwenye mashine ya kuchukulia pesa (ATM), alitoka nje ya hoteli na kuchukua fedha hizo kwangu na kurudi ndani ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa akimalizia kinywaji, na kumpatia fedha hizo na baada ya muda alitoka nje na kunitaarifu kuwa tayari amekwishampatia,” alidai Machurya.

Baada ya mbunge huyo kupatiwa Sh1 milioni, alidai fedha zilizobaki, Sh7 milioni, awekewe kwenye akaunti yake namba 5051602671 ya NMB iliyofunguliwa kwenye tawi la Dodoma, ambayo alimwandikia Spora kwenye kikaratasi. Aliongeza kudai kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, aliingia ndani na kukuta tayari mtuhumiwa huyo ameshawekwa chini ya ulinzi na wachunguzi wenzake na kwamba waliendelea na uchunguzi kwa ajili ya kuthibitisha kama mshtakiwa alikuwa na nia ovu.

Hakimu Mkazi, Faisal Kahamba ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa. Katika kesi hiyo namba 146 ya mwaka 2012, Mbunge huyo anatetewa na Wakili Mpale Mpoki.

Badwel aliyepandishwa kizimbani Juni 4, 2012 alikana kutenda makosa hayo.

Katika shitaka la kwanza, mshtakiwa huyo anadaiwa kuomba rushwa ya Sh8 miloni kutoka kwa Mkurugenzi wa Halimashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Jonathan Liana kwa nyakati tofauti kati ya Mei 30 na Juni 2, 2012 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo alikamatwa Juni 2, 2012 katika hoteli ya Peacock ya jijini Dar es Salaam akipokea rushwa ya Sh1 milioni, kutoka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, kinyume na kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, namba 11 ya mwaka 2007.

Pia, akiwa mtumishi wa umma na kitendo hicho ni kinyume cha kanuni zake za kazi.

Mshtakiwa huyo yuko nje kwa dhamana baada ya kutekeleza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao walisaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh4 milioni kila mmoja na wote kuwasilisha mahakamani hati zao za kusafiria.MWANANCHI

No comments: