Thursday, September 27, 2012

RAI YA JENERALI

UTETEZI WA HAKI,UTAMBULISHO WA MSINGI WA MTANZANIA

Na Jenerali Ulimwengu,
TUKITAKA tunaweza kuwa Taifa kubwa, na tukitaka tunaweza kuwa Taifa dogo, kwani yote yamo ndani ya uwezo wetu. Tunazo kila aina ya rasilimali zinazotuwezesha kuwa Taifa kubwa, na pia rasilimali hizo zinaweza kutufanya tukawa kituo cha wageni kuja kuchuma na kutuachia mashimo na majangwa yanayoonyesha ni wapi wageni walichimba na visiki vinavyodhihirisha ni wapi walikata na kuchukua bila alama ya kuonyesha ni nini tulichopata na wapi tuliwekeza hicho tulichokipata.

Naamini kwamba nimekwisha kueleza kwa urefu mambo ambayo tunayafanya ambayo hayatusaidii kuweza kusema kwamba tunafanya vyema kiasi kwamba baadhi ya wasomaji wangu wanadhani kwamba nawakatisha tamaa. Kusudio langu ni kueleza udhaifu tulio nao katika hali ya uwezo mkubwa ili tuone fursa tulizo nazo na ambazo hatuzitumii, fursa ambazo tungezitumia ( hata kwa kiwango kidogo tu) zingeweza kutupeleka mbele na mbali mno.

Jambo la msingi hapa ni imani. Ili kuweza kuzitumia fursa hizi hatuna budi, kama Waafrika, kwanza tuamini kwamba hili ni bara letu, na kama Watanzania tuamini kwamba hii ni nchi yetu. Hili linaweza kuonekana kama jambo lisilo na mjadala, lakini kwangu mimi mjadala bado ni muhimu.

Mjadala huu bado ni muhimu kwa sababu tunafanya mambo yetu na kuandaa mipango yetu kama vile ni watu wa kupita hapa tulipo kwa muda lakini lengo letu likiwa ni kwenda kwingine au kurudi tulikotoka. Hatuonyeshi hali ya watu tunaojua kwamba hapa ndipo kwetu na, kama Taifa, hatuna kwingineko tunakoenda.Nimekuwa nikieleza kwa urefu kwamba tumekuwa watu wa mpito.

Watu wa mpito hufanya mambo yao kimpito-mpito. Makazi yao yatakuwa ya mpito mpito : vijumba vya fito, matope na nyasi, wakati mwingine bila hata tope. Kesho wakiamua kuhama, kila mwanafamiliia anashika upande wake na nyumba inabebwa na kwenda kupandikizwa katika maskani mpya. Hakuna haja ya kujenga njia pana kwa sababu njia ziliopo zinatosha kupitisha binadamu, mifugo na nyoka.

Elimu ya vijana katika jamii kama hiyo ni elimu inayowafundisha kuchuma matunda, kuchimbua mizizi na kukamata swala kwa ajili ya mlo wa siku moja au mbili. Hata wakifundishwa kulima, kilimo wanachofundishwa ni kilimo cha mchicha, unaochumwa baada ya wiki tatu, na wala si cha mnazi unaokuja kuvunwa baada ya miaka 15 au 20.

Mipango yote na shughuli zote zinakuwa zinalenga wakati uliopo, na labda kidogo tu baadaye. Jamii ya aina hiyo inakuwa jamii ya mpito, hata kama haina mahali kunakojulikana inakoenda (destination).

Jamii inayojua (au inayodhamiria) kwamba itabaki na itadumu hufanya mambo yake si kwa kuhesabu miaka wala miongo bali kwa kuangalia milele, muda usiohesabika wala kufikirika, karne na milenia. Mipango yake daima huwa ya mambo makubwa na yenye sura ya kudumu milele. Hii ndiyo jamii inayoweza kuwa na matarajio ya kujenga taifa kubwa. Taifa kubwa haliwezi kupatikana ndani ya jamii inayopanga mambo yake kwa kuangalia vipindi vya uchaguzi vya miaka mitano mitano.

Sasa, nitajaribu kueleza ni sifa gani zinaifanya jamii iweze kujenga huo u-milele ambao ndio unaifanya jamii iwe ni taifa kubwa. Kwanza ni kujitambua, kujenga utambulisho ambao ndicho kielelezo cha utaifa. Mkuasanyiko wa watu wengi haujengi taifa iwapo watu hao wengi hawana utambulisho unaowadhihirisha wao ni nani, kwao wao wenyewe na kwa wanaowaangalia.

Imesemwa mara nyingi, nami nimekuwa nikiirejea dhana hii, kwa sababu nimekulia katika jamii iliyokuwa imeanza kujenga taifa lililojitambulisha kwa hulka yake, Taifa la Watanzania. Bila kusita, nasema tena kwamba katika mafundisho na maelekezo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, nchi hii ilianza kujenga taifa la watu waliokuwa na utambulisho mahsusi kwao wao wenyewe na kwa wageni waliokuja nchini au waliotupokea tulipokwenda ughaibuni.

Hulka hii ilikuwa na sifa gani ? Sifa zilikuwa nyingi lakini zote zilihusiana na uongofu na kupenda na kutetea haki. Watanzania walijulikana kama watetezi wa haki kila mahali duniani. Utetezi wa haki hautegemei iwapo haki unayoitetea ni yako wewe mwenyewe, ya ndugu yako au ya mtu unayemjua na unayempenda, hapana. Utetezi wa haki ni ule utetezi wa misingi ya haki hata kama humjui unayemtetea, na hata kama unayemsuta kwa kutomtendea haki huyo unayemtetea (ambaye humjui) ni ndugu au rafiki yako.

Tulifundishwa kurudia : « Binadamu wote ni ndugu zangu, na Afrika ni moja ». Kwa jinsi hii kila tulipopata habari za binadamu kuonewa na mijitu yenye nguvu kubwa za kivita na kiuchumi, hatukusita kukemea kwa kuhofu kwamba tutanyimwa misaada. Kwa jinsi hii wananchi wa Vietnam wakawa ni ndugu zetu kweli kweli, na kwa jinsi hii Wachina wakawa ni ndugu zetu wa dhati.

Wakati Mwalimu anakwenda Umoja wa Mataifa na kusema ni jambo la dhuluma, uonevu na lisiloingia akilini kwamba Umoja huo unaweza kuwa na mwanachama kama Afrika Kusini ya kibaguzi na kuisusia serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China iinayowakilisha robo ya binadamu wa dunia, hakufanya hivyo kwa sababu alikuwa na damu ya Kichina bali ilikuwa ni kutokana na msimamo wa kimsingi.

Tulifundishwa pia (na inabidi tuwafundishe wana wetu) kwamba haki haigawanyiki ; ama iko kila mahali ama haiko po pote. Haiwezekani kutetea haki kwa ajili ya sehemu ya watu na kuikataa kwa ajili ya sehemu nyingine ya watu, wawe ni watu wa jamii au nchi moja au jamii mbalimbali au nchi mbalimbali.

Ndiyo maana mambo yaliyokuwa yakifanyika Guatemala, au Chile, au El Salvador, au Timor Leste, au Afrika Kusini au Msumbiji… ko kote kulikotokea hali ya kusigina haki za watu, Watanzania tulipaza sauti kuwaunga mkono wanyonge na kuwakemea waonezi, hata pale walipokuwa ni wakubwa.

Hii ilijenga taswira ya Tanzania kama nchi ndogo yenye Taifa kubwa. Hadi leo wapo watu wengi katika Afrika na duniani wanaoitazama Tanzania kwa macho hayo ya miaka mingi iliyopita, wasijue kwamba tulikwisha kuiacha misingi hiyo.

Ndiyo maana wanashitushwa na matukio ya siku hizi wanapoambiwa kwamba Tanzania nayo inaweza kuvumilia polisi wake kuwafanyia unyama raia wake.

Kila siku linapotangazwa tukio jingine la aina hii tunapokea maswali mengi ambayo tunashindwa kuyajibu. Tunashindwa kujibu juu ya upuuzi wa « Kikombe cha Loliondo » kilichopigiwa mbiu na wakuu wa serikali waliotaka tuamini kwamba tunaweza tukazifunga Muhimbili, Bugando, KCMC na Bombo, halafu tukawa na siha njema tu kwa « kunywa kikombe .»

Tunaulizwa kuhusu mauaji ya albino, tunashindwa kutoa majibu ya kuridhisha. Tunaulizwa kuhusu nchi yetu kuwa na viwango vya juu vya imani za kishirikina ; tunashindwa kujibu. Maswali haya tunayoulizwa yanatokana na watu wengi wasiojua kiasi cha mabadiliko yaliyotokea nchini mwetu kwa sababu wanaamini kwamba nchi yetu bado ni « nchi ya Nyerere ». Masikini, hawajui tulikwisha kuachana na mzee huyo kitambo !

Kwa kumalizia sehemu hii ya mjadala huu nasisitiza kwamba hatuna budi kujitafuta, kujitambua na kujithamini kama Watanzania, kama Waafrika na kama binadamu. Utambulisho mmoja wa awali kabisa ni ule unaotufanya tutambulike kama watetezi wa haki wasioogopa kupaza sauti pale haki inapovunjwa, hata kama anayeathirika kwa kunyimwa haki hatumjui.


RAIA MWEMA

No comments: