Friday, September 21, 2012

NYERERE ANGEMKEMEA DK. SLAA AU CCM?


Na Arcado Ntagazwa,

KATIKA toleo la Raia Mwema Septemba 12 - 18, 2012 ukurasa wa 17 kuna makala yenye kichwa cha habari; Dk. Slaa ni binadamu hukosea, hujikwaa. Mwandishi wa makala ile aliyejitambulisha kwa jina la Mkweli Ukweli, ametekeleza ibara ya 18 (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inayoruhusu uhuru wa mt kuwa na maoni na kueleza fikra zake. Nami natumia haki yangu hiyo ya kikatiba.

Nakubaliana na ukweli kwamba Dk. Wilbroad Slaa (Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA) ni binadamu na hakuna binadamu mkamilifu. Hata Dk. Slaa hajawahi, kwa maneno au kwa vitendo, kudai kuwa yeye si binadamu.

Katika makala ya Mkweli Ukweli, kuna baadhi ya nukuu ambazo kwa makusudi au kwa kutekeleza ajenda anayoijua, ni potofu. Kwa mfano; “... Slaa ni mchafuzi wa amani yetu na haitakii mema Tanzania.” Kutokana na nukuu yake hiyo, mwandishi huyo anapaswa kujua kwamba katika nchi nyingi Afrika, matokeo au mchakato usioridhisha wa Uchaguzi Mkuu ni chanzo cha amani kupotea.

Nakubaliana na maneno aliyonukuu kutoka katika makala iliyowahi kuandikwa na mwandishi Mwanakijiji, maneno ambayo licha ya kuyanukuu Mkweli Ukweli ameyapinga. Maneno hayo kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 yanasema; “.....kama isingekuwa busara alizonazo Slaa kama zile za Mfalme Solomoni, Tanzania ingeingia kwenye machafuko ya kisiasa kutokana na uchaguzi huo ulivyoendeshwa.”

Mwandishi Mkweli Ukweli katika makala yake, hakuonyesha juhudi za kutujuza kuhusu kilichofanywa na vyombo vya dola mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita. Hakutuambia kwa siku tatu mfululizo baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola walijifungia Hoteli ya Kilimanjaro Kempiski walifanya nini kabla ya kuiagiza Tume ya Uchaguzi itoe na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais hadharani.

Nina hakika anajua fika ibara ya 41 (7) ya Katiba ya nchi inasema kwamba tume ikishatangaza mshindi wa urais ndiyo mwisho, ni kama wakatoliki wanavyojua “Roma locuta causa finita”.

Kwa matokeo ya uchaguzi wa urais nchi nzima ambayo mawakala wa vyama vyote walikuwa nayo, nani aliwasihi na kuwazuia watu wasiingie barabarani kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais kama si Slaa?

Penye ukweli uongo hujitenga, mwandishi anajaribu kuweka pamoja mauaji ya watu watatu wanaodaiwa kuuawa na polisi, Januari 5, 2011, mjini Arusha na siku ya mkesha katika viwanja vya National Milling Arusha. Matukio haya kila moja linajitegemea ila mwandishi anataka kuwaaminisha wasomaji wake kuwa tukio moja lilianzisha jingine kwa kufuatana.

Suala la madai ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga kudhalilishwa (wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo) nalo limetajwa katika mlolongo wa mifano. Katika sheria ya madhara (torts) kuna msemo; “volenti non fit injuria” kwamba anayejitolea, yatakayomfika ajilaumu yeye mwenyewe.

Tukio la kuuawa Yohana Mpinga (Mungu amlaze mahali pema peponi) ni la kusikitisha. Kuna watu watano tunajulishwa kuwa wamefunguliwa mashitaka ya mauaji, sheria ifuate mkondo wake lakini, viongozi wa CHADEMA waliofunguliwa mashitaka ya kutoa matusi, shitaka hilo ni tofauti na lile la kutoa uhai wa mtu.

Nukuu ya makala ya Mkweli Ukweli kuhusu waliofunguliwa mashitaka wakihusishwa na kifo cha Yohana Mpinga inasema; “.....aliuawa kwa kupigwa na wanaodaiwa kuwa ni mashabiki wa CHADEMA”. Ni vema nikamjulisha mwandishi kuwa, kutokana na CHADEMA kuwa kipenzi cha wanyonge wengi wa nchi yetu siku hizi, sitaona ajabu watu au hata kuagizwa wajifanye mashabiki wa CHADEMA kwa lengo la kukichafua CHADEMA.

Lugha ya matusi si jambo la kulinda heshima katika jamii lakini wakati mwingine matendo ya anayetukanwa ndiyo chanzo cha kupotea hali ya kutunza heshima. Tukubaliane kuwa si ustaarabu kumtolea matusi mtu mwenye dhamana ya kuitwa mheshimiwa.

Lakini, kwa mfano, mheshimiwa fulani anajua kuwa kuendelea kutumia majina ya kudandia kwa kughushi badala ya majina yake halisi ya Lameck Madelu Mkumbo, siku si nyingi yatamfikisha kwenye makosa ya kijinai. Wanasema ukitaka kuheshimiwa uanze kujiheshimu.

Makala ya Mkweli Ukweli inaendelea kutoa mifano ya kuonyesha kuwa mtendaji mkuu wa CHADEMA (katibu mkuu) anatoa madai mengi. Mwandishi anawaaminisha wasomaji wake kuwa madai hayo yanaweza kupewa sifa ya madai hewa. Lakini nimkumbushe tu mfano wa madai hayo kuwa ya uhakika (si hewa) kuwa ni pamoja na yaliyodhihiri katika kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Kuna swali limeulizwa katika makala yake hiyo ya toleo lililopita la gazeti hili kwamba; “....hivi kweli CCM tunayoijua sisi (Mkweli Ukweli na watu wenye fikra kama yeye) imefika mahali pa kuwa chanzo cha vurugu nchini? Mwenye macho haambiwi tazama.”

Ukiukwaji wazi wazi wa ahadi zinazotolewa kwa kiapo ni sehemu ya ushahidi kuwa CCM inaweza kuwa chanzo cha vurugu. Kwa mfano maagizo ya CCM yanasema; “ - rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, - nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko”. Hizi ni ahadi za mwanachama wa CCM zinazovunjwa na kukifanya chama hicho kuwa chanzo na chimbuko la vurugu.

Ushahidi mwingine kuwa CCM ni chanzo cha vurugu ni makada wake kutoleana bastola hadharani katika mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho. Kwa hiyo, mwandishi ajue CCM ya sasa ni chanzo cha vurugu na hata amani kuanza kutoweka nchini.

Wananchi wanyonge kufukuzwa kutoka ardhi na mashamba yao ili kupisha miungu watu wanaoitwa wawekezaji ni nini kama si chanzo cha vurugu? Yapo mengi, wananchi ndiyo mashahidi wa uovu wanaotendewa.

Baada ya miaka 50 ya uhuru, kweli inaingia akilini mwanakijiji kupigwa marufuku kuoga maji ya mto aliyotujadilia Mwenyezi Mungu? Kutozwa faini ya Sh. 5,000 ni kitu gani kama si chanzo cha vurugu inayoweza kulipuka wakati wowote?

Makala ya mwandishi hiyo anatukumbusha hekima ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokemea mwelekeo wa kupora amani ya nchi yetu. Nakubaliana na hilo.

Lakini sikubaliani na wazo kuwa Baba wa Taifa angekemea kule anakotaka kutupeleka Dk. Slaa. Nina hakika kabla ya hapo CCM na serikali yake wangewekwa kitimoto na Nyerere.

Hebu fikiria wazo la kutumia kodi ya wananchi kuwaongezea mama wajawazito uchungu wa kujifungua kwa kuwabeba katika pikipiki za gurudumu tatu (bajaj), huku kodi hiyo hiyo ya wananchi ikitumiwa kununua magari ya kifahari ya milioni 200.

Nirudie kusema, penye ukweli uongo hujitenga, hivi tukio la Septemba 2, mwaka 2012 kijijini Nyololo mkoani Iringa hatujifunzi chochote? Polisi wanatuhumiwa kumuua mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi na ni polisi hao hao ambao awali walitaka kuficha ukweli, wakisema eti Mwangosi alitupiwa kitu kigumu kutoka upande wa waandamanaji. Yote hayo ni uongo mtupu.

Picha zimewaumbua waliobobea kutunga uongo, kujikosha na kuwasingizia CHADEMA. Wameumbuka. Tatizo la baadhi ya watawala wetu wanatafuta pa kujificha sababu ya ufisadi na rushwa iliyokithiri ndani ya CCM na serikali yake. Kondoo wa kafara CHADEMA.

RAIA MWEMA

No comments: