Thursday, August 16, 2012

WAMEFUNGUA MILANGO YOTE YA NCHI NA MADIRISHA PIA

Na Johnson Mbwambo,
Katika hili, heri ‘Komredi’ Mugabe

WIKI iliyopita gazeti la Guardian lilichapisha matokeo ya utafiti kuhusu sekta ya utalii uliofanywa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Dk. Charles Kitima. Kwa hakika, matokeo ya utafiti wake yanafikirisha na kuhuzunisha kwa yeyote anayeipenda nchi hii.

Kwa mujibu wa utafiti huo, karibu Shilingi trilioni 1.2 zinazopatikana kila mwaka kutoka katika sekta ya utalii nchini, huishia nje ya nchi (capital flight) yanakotoka mashirika makubwa ya kimataifa – Multinational Companies (MNCs) yanayomiliki hisa nyingi katika biashara za sekta hiyo nchini.
Kwa ufupi, utafiti wa Dk. Kitima unaonyesha kuwa wageni ndio wamiliki wakubwa wa biashara katika sekta hiyo. Anatoa mfano wa vitalu vya uwindaji ambavyo asilimia 95 vinamilikiwa na wageni; huku wazawa wakiambulia asilimia 5 tu.

Na ni kwa sababu hiyo ya asilimia kubwa ya biashara ya sekta ya utalii kumilikiwa na wageni, mapato karibu yote katika sekta hiyo huishia nje ya nchi; kwa maana hiyo ya capital flight.
Ingawa utafiti wa Dk. Kitima uligusa sekta ya utalii tu, ni imani yangu kwamba hali ni hiyo hiyo katika sekta nyingine kuanzia ya madini, fedha (mabenki) hadi ya mawasiliano ya simu za mikononi.

Hali hii inatufanya baadhi yetu tuanze kujiuliza kama kweli hii ndo stahiki yetu katika kiwewe chetu hiki kipya cha kukaribisha uwekezaji wa kigeni kwa staili ya kuwafungulia si tu milango yote; bali pia na madirisha yote!

Nasema hivyo kwa sababu, licha ya kuwa mimi si mchumi, naelewa ya kuwa hata makandokando mengine madogo ambayo wazawa tulistahili kuyapata kutoka kwa wawekezaji hao wa kigeni, hatuyapati katika viwango vya kuridhisha kama tulivyoahidiwa wakati milango hiyo ya uwekezaji ikifunguliwa yote na madirisha pia!

Chukulia mfano huo huo wa sekta ya utalii. Tuliambiwa kuwa kuanzishwa kwa mahoteli ya wawekezaji wa kigeni katika maeneo ya utalii kungeliwawezesha wazawa kupata masoko ya bidhaa zao, lakini uzoefu umeonyesha picha tofauti kabisa.
Tuna mahoteli ya namna hiyo hapa nchini ambayo hata juisi tu za machungwa zinatoka Afrika Kusini; achilia mbali ndizi mbivu.

Katika hali hiyo, wakulima wa Tanzania na watengeneza bidhaa zetu wengine hawawezi kunufaika na kufunguliwa kwa mahoteli hayo nchini.
Hivi karibuni niliwahi kukaa, kwa siku moja, katika hoteli moja ya aina hiyo mkoani Arusha na kujaribu kuhesabu vitu vya Kitanzania (made in Tanzania) katika hoteli hiyo. Matokeo yalinisikitisha mno kwa sababu karibu kila kitu katika hoteli hiyo kilikuwa ni cha kigeni – kuanzia maji ya kunywa hadi sosi za nyanya!

Lakini pia chukulia mfano mwingine wa suala la ajira. Tuliambiwa kuwa kufunguliwa kwa milango hiyo kungeongeza ajira nchini, lakini tumeshuhudia baadhi ya mahoteli hayo yakiajiri hadi wakaribishaji wageni kutoka nje; achilia mbali kwenye nafasi za uongozi wa idara zao mbalimbali ambako wamejaa maofisa kutoka nchi zao.

Hiyo inathibitisha kwamba si tu tuliongopewa kuhusu ongezeko la ajira, lakini pia hata zile tambo nyingine kwamba wazawa tungechota ujuzi na uzoefu kutoka kwa wawekezaji hao wa kigeni nazo zimebakia ndoto tu. Huo ujuzi na uzoefu utachotwaje wakati nafasi zote nyeti wanashika wenyewe wageni?

Na kama nilivyosema mwanzo, hali ni hiyo hiyo karibu katika sekta zote nyeti nchini za biashara; yaani madini, utalii, viwanda, mabenki, mawasiliano nk.

Faraja pekee katika kipigo hiki tunachokipata kutoka kwa uwekezaji wa kigeni tulioukaribisha kwa kufungua milango yote na madirisha yote ingekuwa katika mapato. Lakini kama utafiti wa Dk. Kitima unavyoonyesha, mapato yote huishia nje ya nchi yanakotoka makampuni hayo – Sh. trilioni 1.2 kwa mwaka, na hiyo ni sekta ya utalii tu! Nina hakika hata katika ulipaji kodi tunapigika vibaya vilevile.

Sasa, kama tunapigika kwenye mapato na kodi, kama tunapigika kwenye ajira, kama tunapigika kwenye matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini, kama tunapigika kwenye suala la kuchota ujuzi na uzoefu nk, kwa nini tusihoji tunanufaikaje na wawekezaji hawa wa kigeni tuliowafungulia milango yote na madirisha yote ya nyumba pia?

Ni kwa kuzingatia yote hayo angalau katika hili mimi binafsi nakubaliana na msimamo wa Rais wa Zimbabwe, ‘Komredi’ Robert Mugabe ambaye ameshinikiza uwepo wa sheria inayowalazimisha wawekezaji wageni kuwa na ubia na wazawa.

Kila biashara kubwa nchini Zimbabwe, kupitia Tangazo la Serikali Na. 280 la mwaka 2012, sasa humilikiwa na wageni kwa asilimia 49 tu na wazawa asilimia 51. Na hiyo ni kwa sekta zote za madini, utalii, nishati, usafiri, mawasiliano, elimu na fedha.

Ingawa ‘Komredi’ Mugabe ameshutumiwa sana kwa uamuzi wake huo uliotafsiriwa kuwa ni wa kidikteta, lakini naamini alilenga katika kuifanya nchi yake inufaike ipaswavyo na uwekezaji huo wa kigeni.

Kuwafanya wazawa wamiliki asilimia 51 ya hisa katika kila biashara kubwa kunahakikisha kuwa angalau mapato ya asilimia hiyo hiyo 51 yatabaki nchini Zimbabwe kila mwaka kuiendeleza nchi hiyo, na si kuishia yote nje ya nchi (kupitia capital flight) anakotoka mwekezaji kama ilivyokuwa zamani.

Ikumbukwe kwamba wawekezaji wote wa kigeni wanapoingia katika nchi yoyote hawana lengo lolote la dhati la kuiendeleza nchi husika. Lengo lao kubwa pekee ni kujitengenezea mapesa na kuyapeleka kwao kila mwaka. Na ndiyo maana hujiondokea haraka kwa kufunga au kuuza biashara zao wanapoona hawapati tena faida au kipindi cha unafuu wa kodi (tax holiday) walichopewa kinapomalizika.

Lakini hali ni tofauti kwa mwekezaji mzawa. Yeye mapato yake (mabilioni yake) anayoyapata kila mwaka atayazungusha hapa hapa nchini – mathalan atajenga majumba, ataanzisha shule, atajenga kiwanda na mambo mengine mengi tu ambayo, hatimaye, yataiendeleza nchi kwa namna moja au nyingine.

Naamini hata zile nchi za Mashariki ya Mbali – Malaysia, Singapore, Indonesia nk ambazo zilipiga hatua haraka kimaendeleo zina sheria hizi za kuhakikisha wazawa wanakuwa na hisa za kutosha katika kila biashara kubwa inayoanzishwa na mwekezaji wa kigeni.

Wazawa wa Malaysia, kwa mfano, walinufaika sana na utaratibu huo chini ya utawala wa Dk. Mahathir Mohamed hadi Juni 2009 wakati mtawala mwingine wa nchi hiyo, Najib Razak, alipobadilisha mambo, na sasa nchi hiyo imeanza kuyumba kiuchumi kwa sababu mapesa mengi yanayotengenezwa kila mwaka nchini humo huishia nje yanakotoka mashirika yaliyowekeza huko.

Ndugu zangu, nisisitize tena kuwa matokeo ya utafiti wa Dk. Kitima yanafikirisha. Kwangu mimi nayachukulia kama ni kengele ya uamsho kwa watawala wetu ambao wameifanya nchi yetu kuwa shamba la bibi kweli kweli.

Wameigeuza nchi kuwa shamba la bibi kweli kweli kwa kufungua milango yote ya nchi na madirisha yake yote pia ili tu wasifiwe na asasi za Bretton Woods za World Bank na IMF kwamba wameboresha mazingira ya uwekezaji wa kigeni katika nchi zao!
Natujiulize: Je, wanaisikia kengele hiyo ya uamsho ya kina Dk. Kitima? Na kama hawaisikii, tufanyeje waamke?

Tafakari.


RAIA MWEMA
No comments: