Friday, August 31, 2012

RAI YA JENERALI


KWA NINI TUNATAKA KUI'ZAIRESHA' NCHI


Katika upuuzi tutakuwa wapuuzi dhaifu

Na Jenerali Ulimwengu,
NIMESEMA mara nyingi kwamba tunahitaji kupunguza upuuzi katika maisha yetu na shughuli zetu kama jamii na kama taifa. Hii ina maana kwamba tunaenenda kipuuzi mno na ndiyo sababu kubwa ya kukosa maendeleo ambayo tunaweza kujivunia, tukiacha hayo maendeleo tunayolazimishwa tuyaangalie na wale wanaojisifu kwa kazi nzuri ambayo haionekani.

Upuuzi kwa kiasi fulani ni jambo jema. Kila mtu anayo haki ya kufanya upuuzi kidogo kama njia ya kujipumzisha, kujiliwaza na kujiburudisha baada ya kazi ngumu, ama ya mwili ama ya akili. Ndiyo maana hata katika jamii zilizoendelea sana katika ujenzi wa uchumi wapo watu ambao wanalipwa kwa mabilioni ya dola ili wapangilie upuuzi utakaowaburudisha wenzao waliotoka kwenye migodi na kazi nyingine za ngwamba. Kwa Marekani wengi wa watu wa aina hii wako Hollywood. Bara Hindi wako Bollywood.

Hata sisi hapa nchini tunao watu wa aina hiyo, hata kama sanaa yao haijakua kiasi cha kuzikaribia Hollywood na Bollywood. Na ni kweli kwamba wanatuburudisha na kutufurahisha kwa kiwango chao. Ni watu muhimu katika jamii kama ambavyo tulikumbushwa si muda mrefu uliopita alipofariki Kanumba.

Hata hivyo, hatutakiwi sote kuwa waburudishaji na watumbuizaji. Wengine hawana budi kufanya kazi nyingine ili taifa lisonge mbele, liweze kujilisha na kujilimbikizia amali kwa siku zijazo, kwa ajili ya vizazi vijavyo. Tukiwa sote ni watumbuizaji ni nani atatulisha, atatuvisha, atatujengea nyumba? Nasema, tunahitaji upuuzi kidogo, na tena huu ni upuuzi uliopangiliwa vyema, lakini upuuzi hautakiwi uwe ndiyo shughuli kuu ya jamii nzima.

Tukitaka kuangalia jamii iliyofanya upuuzi ukawa ndiyo shughuli kuu katika maisha yake, hatuhitaji kwenda mbali sana; tuiangalie Kongo, ambayo Joseph Mobutu aliita Zaire kwa kipindi kirefu akiwa mtawala wake. Kongo imejipambanua kwamba nchi ya upuuzi kabla ya uhuru wake mwaka 1960. Ilipoingiliwa na wazungu ilifanywa kuwa shamba binafsi la Mfalme Leopold II wa Ubelgiji, ambaye alichimba na kuchuma kila alichokitaka na alifanya kila aina ya unyama bila kuulizwa siyo tu na Wakongo bali pia hata Bunge la nchi yake. Kongo haikuwa koloni la Ubelgiji; lilikuwa ni kihamba cha Leopold.

Baada ya uhuru wanasiasa wapuuzi wakalumbana, wakazodoana, wakafukuzana, wakauana, hadi alipoibuka mshindi wa kinyanga’anyiro hicho kwa sura ya Jospeh Mobutu, ambaye aliboresha mbinu za wizi, uporaji, unyang’anyi, udhalimu na uuaji kiasi kwamba ikawa inajulikana kwamba hayo ndiyo maisha ya nchi ya Zaire na huo ndio utamaduni wake. Hiki ndicho kilikuja kujulikana kama Mobutism, u-Mobutu.

Kwa wananchi wa kawaida, hii ndiyo ilikuwa hali ya maisha, nao wakaichukulia hivyo ilivyokuwa na wakajichimbia katika wizi wao na unyang’anyi wao mdogo mdogo (small scakle thievery) ambao ulikuwa ni kiungo muhimu katika kufanikisha wizi mkubwa (large scale thievery) ya Mobutu na genge lake.

Isitoshe, katika kujiliwaza na kujisahaulisha madhila waliyoyapata muda wote, wakiwa ni shamba la Leopold na wakiwa ni shamba la Mobutu, wananchi wa nchi hiyo yenye utajiri kama El Dorado wakaingia katika shughuli ya kujitumbuiza kwa muziki na ngoma. Na hii ikawa ndiyo shughuli yao kubwa. Kongo ikajulikana kwa mambo manne makubwa: moja, utajiri mkubwa uliomnufaisha Mobutu na mafisi waliomzunguka, lakini hasa uliowanufaisha wazungu; pili, vita, fujo na vurumai zisizoisha; tatu, udhaifu wa serikali ambayo haikuonekana majimboni isipokuwa kwa uwapo wa askari wanaopora ili kupata ujira wao; nne, muziki, ngoma na burudani kama soka na ngono.

Taswira hii ya Kongo haijabadilika sana. Mwaka 1997 nilikuwa katika msafara wa Mwalimu Julius Nyerere aliyekwenda Kinshasa kwa mazungumzo na Rais Laurent Kabila. Katika wiki moja tuliyokaa Kinshasa jambo moja kubwa alilobaini ni kwamba Kabila na genge lake walikuwa wamefanikiwa kumfurusha madarakani Mobutu lakini wakabakiza u-Mobutu katika utawala wao. Kabila alikuwa ni Mobutu baada ya Mobutu, mrithi halali wa Leopold. Hadi leo hali haijabadilika sana, baada ya Kabila mdogo kumrithi baba yake aliyeuawa katika mazingira ya kunyang’anyana mali.

Pamoja na yote, K0ngo/Zaire ilipata mafanikio makubwa sana katika upuuzi uliopangiliwa. Haiwezekani kuzungumzia muziki barani Afrika bila kuitaja Kongo/Zaire; hata barani Uropa, wapenzi wa muziki ambao hawana asili ya Afrika wanatafuta muziki wa Kongo/Zaire. Aidha Wakongo ni wasanii katika mambo mengine pia, kama ushonaji wa nguo, ushonaji wa viatu, uchoraji na uchongaji. Pia ni wanasoka wazuri wanaosifika Ulaya ambako wanacheza katika ligi kubwa.

Mobutu, pamoja na kwamba alikuwa mshenzi, alifanya kazi kubwa ya kuhifadhi urithi wa kimuziki wa Kongo. Katika miaka ya 1970 nilikwenda mara kadhaa mjini Kinshasa na nikaweza kujikusanyia albamu kadhaa ya wanamuziki wa zamani wa Kongo, akina, Kabasele, Wendo na Boukaka, yote kwa sababu Mobutu alikuwa amefadhili kazi ya kukusanya nyimbo za zamani na kuziweka katika sahani za santuri.

Uhamasishaji wa vikundi vya ngoma na mapambio ya kumsifu Mobutu ulifikia viwango vya juu kabisa, kiasi kwamba watawala wa nchi nyingine, kama Gnassinbe Eyadema wa Togo, walianza kuiga walichokuwa wakifanya Wazaire katika kumsifu Mobutu. Hata sisi hapa nchini tulivutika na upuuzi huo kiasi kwamba wimbo wa “chama chetu cha Mapinduzi chajenga nchi” ulichukua mahadhi ya wimbo wa kumsifu Mobutu, “Tokobongisa Mobutu Sesse Seko.”

Mobutu alifanikisha upuuzi kwa kiwango cha juu sana, na akaifanya nchi yake kuwa ya kipuuzi ambamo rasilimali za nchi zinaporwa na wageni wakisaidiwa na watawala wa nchi, huku wananchi wakiimba na kukata viuno wakimsifu Bwana Mkubwa. Nchi tajiri kwa rasilimali kuliko nchi nyingi duniani (ardhi nzuri yenye rutuba, misitu, maji, madini ya kila aina) lakini yenye wananchi siyo tu masikini lakini wasiokuwa na amani kutokana na vita za kila mara; lakini wanacheza ngoma, wanafurahi.

Wakichoka kuishi katika vurumai za nchini mwao wanaondoka, wanahamia katika nchi nyingine Afrika na ng’ambo ambako wanakwenda kuimba na kupiga muziki wa dansi, kushona nguo, na kusuka nywele. Kwa jinsi hii wamejipatia umaarufu mkubwa katika upuuzi wao. Laiti wangekuwa ni wapiga muziki mahiri, wanasanaa wakubwa na wasusi wa nywele wa kimataifa na papo hapo wakaiendeleza nchi yao katika kilimo na viwanda, tungelazimika kuwaheshimu kwa yote hayo na mimi nisingethubutu kuwaita wapuuzi ; kwa walivyo, ni wapuuzi waliofanikisha upuuzi wao kwa kiwango cha juu.

Hatari ninayoiona ni hii inayotunyemelea: Kwamba tunaelekea kuifanya nchi yetu kuwa Zaire bila kuwa na wanasanaa wa viwango vya Zaire. Tunataka kuwa wapuuzi bila kuwa na uwezo wa kufanya upuuzi ukafikia kiwango cha kutupatia sifa kama wapuuzi. Hii haitakuwa rahisi, na hii ina maana kwamba hata katika upuuzi tutakuwa wapuuzi dhaifu; hatutawafikia Wazaire kwa upuuzi.

Hii ni kwa sababu nchi yetu inayo misingi ya kitaifa iliyowekwa na waasisi wa taifa hili. Misingi hiyo inakataa nchi yetu kugeuzwa kihamba cha mtu au watu wachache; ni kihamba chetu sote, na wala si chetu kiasi hicho, kwani tumepewa dhamana tu ya kukihifadhi na kukiendeleza kwa ajili ya vizazi vijavyo, kwa niaba ya Watanzania tusiowajua, kwa sababu hawajazaliwa.

Tunao watoto tayari ambao kila wakituchunguza tunavyoenenda ki-Zaire hawaoni mustakabali wao na wa watoto wao; wanatuuliza maswali, tunashindwa kuwajibu; wanaasi, hatuelewi.
Tungekuwa na busara ya kusikiliza vyema wanachosema, tungezisikia sauti za watoto watakaozaliwa mwaka 2099, wakisaili: Mbona mnaigeuza nchi yetu Zaire? Tungesikiliza sauti hizo tungekomesha huu Uzaireshaji (Zairesation) wa nchi yetu, tungekuwa watu makini wenye viwango vidogo tu (vile vya lazima) vya upuuzi.

RAIA MWEMA

No comments: