Thursday, August 23, 2012

POLISI ,WANANCHI WASHAMBULIANA DARIbrahim Yamola


MAPIGANO makali yameibuka kati ya wananchi wanaodaiwa kuvamia ardhi eneo la Madale Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Jeshi la Polisi ambalo lilikuwa likifanya operesheni maalumu ya kuwaondoa katika maeneo hayo.
Wakati wananchi hao wakitumia silaha za jadi kama mapanga, mishale na mawe, polisi walikuwa wakitumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.

Operesheni hiyo ilianza jana saa 10:02 alfajiri ambayo ilikuwa ikiratibiwa na Halmashauri ya Kinondoni na kusimamiwa na askari mgambo na Jeshi la Polisi.Katika mapigano hayo askari polisi mmoja alinusurika kifo baada ya Mshale kumchoma kifuani lakini hakuweza kuumia kwa kuwa alikuwa amevaa vifaa maalumu vya kujikinga na risasi, mawe, ambapo aliuchukua mshale huo na kudai kuwa anauhifadhi kama kumbukumbu.

Mara baada ya kuzibomoa nyumba na vibanda hivyo takribani 3,000 askari hao walikuwa wakichoma nguo na vitu mbalimbali walivyovikuta.Baadhi ya wananchi waliokuwapo kushuhudia operesheni hiyo walineemeka kwa kuchukua vitu mbalimbali vilivyokuwa rahisi kubebeka kwao.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Kinondoni, Charles Kenyera alisema, katika operesheni hiyo wamewakamata zaidi ya watu 12 waliokuwa wakiishi kinyume cha sheria katika maeneo hayo.

Kenyera alisema, baadhi ya wavamizi hao wamekuwa wakifanya vitendo vya kikatili kwa wamiliki halali wa maeneo hayo kwa kuwapiga na kuwajeruhi.
“Tangu mwaka 2008 maeneo haya yamevamiwa na watu ambao wengine inaonekana siyo watanzania kwani vitendo wanavyofanya ni vya kinyama sana” alisema Kenyera na kuongeza:
“Tumewakamata zaidi ya watu 12 na silaha kama mishale, mapanga, pinde pamoja na vitu mbalimbali mfano pikipiki,baiskeli na bidhaa walizokuwa wanauza katika maduka yao.”

Kwa upande wake Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Jacob Ngowi alisema, nyumba ambazo zinatarajiwa kubomolewa ni zaidi ya 3000 kimakosa.
“Kuanzia leo (jana) na kuendelea tutazibomoa nyumba zaidi ya 3000 ambapo zaidi ya hekta 5000 zilikuwa zimevamiwa na wananchi hao,” alisema Ngowi na kuongeza:
“Wananchi wanatakiwa kutambua kuwa hakuna maeneo ambayo yako wazi hivi sasa hivyo tunawashauri kufuata taratibu za ununuzi wa viwanjwa ili kuepuka usumbufu watakaoupata”.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema watahakikisha wanaziondoa nyumba ambazo zimejengwa katika maeneo ya uvamizi.
Rugimbana alisema vitendo hivyo vya uvamizi vinatokana na wananchi kununua maeneo hayo kinyemera bila ya kufuata taratibu za kisheria.
“Unakuta mtu anauziwa kinyemela na yeye anakubali na kuanza kujenga lakini kwa hawa wa hapa wanaonekana wengine sio wazawa kwa vitendo na mienendo yao ya kimaisha” alisema Rugimbana na kuongeza:

“Wananchi waliojenga katika maeneo yasiyo halali wanatakiwa kubomoa nyumba zao mapema ili kuepuka usumbufu watakaoupata kutokana na operesheni hii ambayo ni endelevu”.
Mkazi wa eneo hilo, Dastan Okololo alisema wavamizi hao walikuwa wakiwafanyia vitendo vya udhalilishaji hususan kwa wanawake katika maeneo hayo.“Yani hawa walikuwa wanyama kwani ukionekana mgeni machoni pao wanakupiga hadi wanakujeruhi na ukienda kuwashitaki Polisi basi unakuwa unahatarisha maisha yako,” alisema Okololo.

Hivi karibuni wakazi wa Bunju, Boko, Madale, Kinondo na Mboto Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, waliitaka Serikali kuvichukulia hatua vikundi vilivyovamia viwanja vyao ili kuepusha vurugu kwa kuwa hawako tayari kuyapoteza maeneo yao.Walisema viwanja vyao vimevamiwa na makundi yanayojiita Mungiki na Talebani ambayo pamoja na mambo mengine huvunja nyumba zao, kuiba mifugo, kukata miti na kujitwalia viwanja.
Aprili mwaka jana kulitokea vurugu kubwa baina ya wenye viwanja hivyo na wavamizi na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na watu kadhaa kuuawa.


MWANANCHI

No comments: