Thursday, August 9, 2012

MGOGORO WA WAFANYAKAZI NA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII NI UKOSEFU WA UBUNIFU
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

TUNACHOSHUHUDIA sasa hivi kuhusu mgogoro unaowiva wa wafanyakazi na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni dalili ya kukosekana kwa ubunifu kwa watawala wetu.
Tumezoea kufanya vitu vya kuiga kiasi kwamba tunashindwa kufikiria vya kwetu au kutafuta suluhisho la kufanya kitu kingine kwa namna bora zaidi.

Uamuzi wa NSSF kuondoa utaratibu wa wafanyakazi kuweza kujitolea fedha zao walizochangia kabla ya kufika wakati wa kustaafu umewaudhi wengi na kusababisha maneno makali ambapo baadhi ya wafanyakazi wanahisi kuwa fedha “zao” zinakuwa kama fedha za serikali, ambazo hawawezi kuzipata pindi wanapotaka.

Naamini yote haya ni matokeo ya watu walioishiwa uwezo wa kubuni vitu na ambao wamezoea kufuata vilivyoandikwa kitabuni au walivyosoma kuwa vinafanyika nchi nyingine. Ninaamini NSSF wanaweza kabisa kuwa walikuwa na sababu walivyoamua kufanya wakiamini ni mfumo mzuri. Naomba nitoe mawazo yangu machache kwanza na sitayapanga sana.

Hifadhi ya jamii kama shirika moja
Kosa kubwa kabisa la mfumo wetu wa “hifadhi ya jamii” ni kuwa na shirika (mfuko) wa hifadhi ya jamii ambao unaendeshwa kama shirika la umma. Na pamoja na hayo, yapo mashirika mengine mengi ya masuala ya pensheni ambayo nayo yanajaribu kufanya kile kile cha “hifadhi ya jamii”.

Naamini kosa kubwa ambalo tumelifanya wakati wa kuunda NSSF kutoka NPF (chini ya sheria namba 28 ya 1997) ni kutengeneza chombo ambacho hakikuwa na tofauti sana na NPF (National Provident Fund).

Ninaamini tulichotakiwa kufanya ni kuunda Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii (National Social Security Authority) na kufanya kuwa chombo ambacho jukumu lake kubwa na la kipekee ni kutoa hifadhi ya jamii (social security).

Chombo hicho kisingekuwa na majukumu ya bima ya afya au mambo mengine bali kingekuwa kinajumuisha kila mfanyakazi wa Tanzania. Yaani, kila mtu anayefanya kazi Tanzania (iwe ya muda mrefu au mfupi) anajikuta anafunguliwa akaunti yake ya Hifadhi ya Jamii. Na muda wote anaoishi atakuwa anachangia (hata akibadilisha muajiri) kiasi cha fedha kwenye mamlaka hii.

Tungekuwa na mamlaka moja tu ya hifadhi ya jamii halisi – yaani inayohusiana na ajali kazini, kifo wakati wa utumishi na uhakika wa kipato wakati wa kustaafu. Mambo mengine yangeachwa kufanywa na vyombo vingine binafsi au vya fani mbalimbali.

 Mifuko mingi ya hifadhi haijaonesha njia
Sasa hivi, wafanyakazi wanaweza kuchagua mfuko ambao wanataka kuutumia kwani pamoja na NSSF kuna Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF)chini ya sheria ya 1999; Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF). Mifuko yote hii kimsingi inafanana sana kwa malengo yake – yaani hifadhi ya jamii.

Na ukitembelea tovuti zao utaona kuwa hata mafao ambayo wanatoa yanafanana – angalau kwa majina!
Sasa kwa nini mifuko hii mingi ambayo yote inataka kumpa hifadhi ya jamii mfanyakazi? Nimesema mifuko inafanana, angalia baadhi ya mafao kwenye mashirika haya (kwa kadiri nilivyoweza kukusanya taarifa kutoka tovuti zao (yawezekana yapo mabadiliko):

NSSF:
Mafao ya uzeeni
Mafao ya kifo
Mafao kwa wanaobaki
Msaada wa mazishi
Mafao ya ajali kazini
Mafao ya uzazi
Mafao ya bima ya afya


PSPF:
Mafao ya uzeeni
Pensheni kwa wanaobaki
Mafao ya ugonjwa
Mafao ya kifo
Msaada wa mazishi
Mafao ya kujitoa


LAPF
Yote kama ilivyo kwa PSPF


PPF
Yote kama ilivyo kwenye PSPF pamoja na mafao ya elimu na mkono wa asante.

Sasa kama mifuko hii inafanana sana kwa aina ya mafao wanayotoa ni kwa nini basi kusiwe na entity moja ambayo angalau ingekuwa inasimamia mambo matano tu makubwa (mafao ya uzeeni, mafao ya kifo, mafao kwa wanaobaki, kupoteza kazi na ajali kazini)?

Mambo hayo matano naamini ni ya msingi na ni haki kwa kila Mtanzania kujua yuko salama – ndio maana ya hifadhi ya jamii. Mambo mengine ambayo yanatolewa naamini yangeweza kabisa kutolewa na kampuni binafsi za bima (iwe ya afya, ajali, nyumba au magari). Mfanyakazi angeamua mwenyewe kununua bima anayoitaka kwa kulipia anavyotaka kama ambavyo tayari wafanyakazi wengi wanafanya. Mashirika ya Hifadhi ya Jamii yasiwe mashirika ya bima ambazo zinaweza kupatikana kwa mashirika binafsi.

Mafao ya kustaafu (pensheni) au hifadhi ya jamii?
Nadhani mojawapo ya mambo ambayo tunahitaji kufikiria namna ya kufanya vizuri ni suala hili la mafao ya kustaafu (pensheni) na kuangalia jinsi inavyohusiana na “hifadhi ya jamii” kwa mtu ambaye hajafikia muda wa kustaafu.

Mtu yeyote anayefuatilia masuala ya hifadhi ya jamii anajua changamoto kubwa ya mifumo ya hifadhi ya jamii. Kati ya maswali muhimu ya kutafakari ni je, wapo wafanyakazi wa kutosha kuweza kuchangia wastaafu waliopo?

Nchi za Ulaya na baadhi ya nchi ambazo watu wake huishi maisha marefu zimejikuta zikipata kazi sana ya kuweza kuhudumia wastaafu wake kwa sababu kizazi cha wanaofanya kazi kinakuwa kimepungua.

Kwa mfano, mahali ambapo watu wanastaafu wakiwa na miaka 55 au 60 lakini bado wanaishi na kufikia miaka 80 au 90 na hilo kuwa jambo la kawaida ni wazi kuwa pensheni ya watu hao inahitaji watu wengi sana kuweza kuimudu.

Kwa mtu ambaye anafuatilia Tanzania – japo kwa juu juu – tunaweza kuona kuwa sasa kizazi cha wastaafu kinazidi kuongezeka (kutoka kwenye utumishi wa umma) na wastaafu hawa wanaanza kuishi muda mrefu zaidi. Swali kubwa ni je wanaochangia mifuko hii sasa (ikumbukwe siyo Watanzania wote wanachangia mifuko ya hifadhi ya jamii) wanaweza kweli kumudu mafao ya wastaafu (pensheni) miaka 10 ijayo?

Naamini swali kubwa litakuwa kwenye kujibu hili hasa kama mifuko hii nayo imeachwa iingie kwenye uwekezaji mkubwa.

Uwekezaji hifadhi ya jamii utaleta matatizo
Tayari wengine tumeshaona dalili za matatizo haya na pole pole watu wengine wameanza kuyaona. Mifuko hii ya hifadhi ya jamii inapoachwa kuwekeza kwenye miradi ya kisiasa inahatarisha kabisa usalama wa mifuko hiyo lakini zaidi inahatarisha hifadhi ya jamii.

Binafsi naamini kungekuwa na mamlaka ya hifadhi ya jamii ambayo kama inafanya jambo lolote la uwekezaji basi lingekuwa likifanywa na chombo kingine huru kutoka kile cha utendaji wa mamlaka hiyo.

Tatizo langu kubwa la msingi la uwekezaji wa mifuko hii – na limeoneshwa na wengine vile vile ni kuwa uwekezaji wa baadhi ya mashirika haya umekuwa ukifanywa kwa kubebana, kulindana, kupendeleana na hata kisiasa.

Hatari yake ni kuwa baadhi ya mifuko japo ina fedha nyingi inaonekana kuwa na haraka ya kuitikia wito wa wanasiasa kuliko kupima kwa kiasi kikubwa kama miradi hiyo inaweza kurudisha fedha au ndio inakuwa ni kuanza kukopana tena.

Ndiyo maana pamoja na hayo yote ninaamini wakati umefika kuanza kufikiria namna ya kufanya vitu hivi kwa njia bora zaidi na siyo ya mambo yale yale.

Je, tunao watu wenye uwezo wa kutaka mfumo huu ubadilike? Je, itatokea kwamba hifadhi ya jamii iunganishwe ili wafanyakazi wote nchini wawe chini ya mfumo mmoja (mafao mbalimbali) na kuhakikisha kuwa wanapata hifadhi hiyo? Je, inawezekana?


RAIA MWEMA

No comments: