Tuesday, August 14, 2012

IANZISHWE MAMLAKA YA KUSIMAMIA NA KURATIBU VIWANJA VYA MICHEZO NCHINI.

Na Baraka Mfunguo,


Ni siku kadhaa sasa tangu kuhitimishwa kwa mashindano makubwa ulimwenguni ya Olimpiki yaliyofanyika katika jiji la London nchini Uingereza. Tanzania kama zilivyo nchi nyingine nayo ilishiriki mashindano hayo adhimu. Kama ilivyo ada Tanzania ilikwenda kule kwa ajili ya kushindana lakini matokeo yake ikabaki kuwa mshiriki kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri katika mashindano hayo.
Pengine ni kutokana na kutokuwa na maandalizi ya muda mrefu, Serikali kutoweka program maalum kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo kutokana na vipaumbele vyake ama wanamichezo wenyewe kutokuwa na ari ya kushiriki katika mashindano hayo kwa kukatizwa tamaa na urasimu na ubinafsi uliopo katika vyama vya michezo nchini ama ni ukosefu wa mbinu muhimu za kiushindani pamoja na mambo mengine ambayo wataalam wa michezo watakuja kuyaelezea.

Kikubwa katika nchi nyingi za kiafrika wanamichezo wanaokuwa katika ushindani na ubora katika mashindano ya michezo mbalimbali, haitokani na maandalizi kutoka katika nchi zao bali ni jitihada zao binafsi ndizo zinazowafikisha hapo walipo. Serikali/nchi huja kuzinduka pale inapoona nyota ya mtu inapong’aa na ndio huanza kujipendekeza ili ionekane .

Moja ya sababu ya wanamichezo wetu kutokuwa na ushindani mkali kimichezo ni kutokuwa na vifaa pamoja na miundombinu rafiki kwa ajili ya michezo yao. Ninasema hivyo kwa sababu mwanamichezo anatakiwa aandaliwe kuanzia ngazi ya chini ili kuweza kuyafikia mafanikio yake.
Serikali ya enzi za Mwalimu Nyerere ilikuwa na nia ya dhati na ndio maana iliweza kutenga maeneo ya wazi kwa ajili ya shughuli ya michezo kwa ajili ya watoto lakini kwa kadiri siku zilivyozidi kwenda watu wakajibadilishia matumizi ya ardhi hizo kupitia mianya ya rushwa na kwa sasa hakuna viwanja vya michezo, kingine ni masuala ya siasa kuingizwa katika michezo mathalan unaweza kusikia kwamba viwanja vya michezo katika baadhi ya mikoa kumilikiwa na chama cha siasa. Lakini hata viwanja vyenyewe ambavyo vinakuwa vinasimamiwa na chama hicho cha siasa , mara nyingi vimegeuka kuwa mapagala na sehemu ya kujifichia majangili. Matumizi yake huja tu wakati wa kampeni za kisiasa.

Lakini udhaifu mwingine ni ule wa serikali kutoipa vipaumbele michezo mingine kama ilivyo michezo ya soka na ngumi na kupelekea michezo mingine kudorora, Wizara ya Elimu kutokuwa na mtaala unaohusiana na michezo ambapo miaka ya enzi za mwalimu haya yote tuliyashuhudia kwa serikali kuwa na mtaala wa michezo, wakawepo waalimu wa michezo. Na wanafunzi wakashiriki michezo. Pengine sehemu ambayo angalau unaweza ukasema pana viwanja vya michezo angalau inaweza kutosheleza baadhi ya michezo shiriki ya Olimpiki, ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kampasi ya Mlimani.

Hoja yangu ni Serikali sasa kuweka nia ya kuanzisha Mamlaka itakayokuwa inasimamia viwanja hivi vya michezo pamoja kuratibu na kusimamia taasisi zinazolenga kukuza michezo kwa kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha ushirikishi wa michezo ya aina zote. Katika nchi zilizoendelea, kwa kiasi kikubwa viwanja vya michezo husimamiwa na kuratibiwa na mamlaka ya viwanja vya michezo.
Ndio Mamlaka ya viwanja vya michezo. Mamlaka hiyo inasimamia viwanja vya aina zote za michezo mathalan Viwanja vya mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, kriketi, raga, wavu, tenisi, mpira wa mikono , mpira wa gofu na viwanja vinavyotumika kwa ajili ya mbio za magari yaani “Grand Prix” na hata kuratibu maeneo kwa ajili ya mashindano ya magari, baiskeli na pikipiki kwa nyika na masafa kama mashindano yale ya Paris-Dakar.

Pia Mamlaka inatakiwa kusimamia viwanja vya ndani vya michezo yaani “indoor stadiums” kwa ajili ya michezo na matamasha mbali mbali ya muziki na dansi. Vile vile viwanja vya mazoezi ambavyo vitaweza kuwashirikisha wanamichezo wenye taaluma na kazi ya michezo, Wanamichezo wa ridhaa, na wanamichezo ambao hushiriki michezo kama njia ya kujifurahisha na kuboresha afya zao.

Mamlaka yaweza kupanua wigo na kuweza kusimamia, kuratibu na kumiliki aina mbalimbali za majengo kwa ajili ya kuzalisha fedha aina za majengo hayo ni ofisi, hosteli za michezo,sehemu za kuegeshea magari, maeneo ya wazi yaliyowekwa kwa ajili ya michezo na starehe kama kupiga kambi “camping”, vijiji vya michezo, migahawa , mahoteli pamoja na idara tengwa kwa ajili ya masuala ya dharura kama vile moto ama ajali wakati wa mchezo husika ambapo kutaweza kuwapo na huduma ya kwanza mwisho huduma za kiusalama .

Ni faida zipi zinazoweza kujitokeza endapo mamlaka hii inaweza kuanzishwa.

1. Kwanza mamlaka hii ikianzishwa itakuwa na uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wengi Tanzania ukiacha wanamichezo . Tanzania hivi sasa inakabiliwa na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana. Mamlaka hii ikianzishwa itawasaidia watanzania wengi ambao wanataaluma za michezo pamoja na wasiokuwa na taaluma za michezo il hali wanasifa za kupata ajira wakawezeshwa na kusaidia kuendesha gurudumu la taifa letu.

2. Kuongezeka kwa vipato vinavyotokana na mauzo ya tiketi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimichezo pamoja na shughuli ambazo hazitahusiana na michezo. Kwa kuweka tozo za aina mbalimbali ambazo zitawezesha kuweka ubora wa viwanja vyetu vya michezo na kuwa wa kimataifa.

3. Kuondoa urasimu uliopo katika umiliki wa viwanja vya michezo kumilikiwa na serikali ambayo hutumia mwanya huo kumilikisha chama chake cha siasa na hivyo kutowapatia watanzania wengine wasiofungamana na upande wowote wa kisiasa kushiriki katika michezo.

4. Kuinua ari ya vijana kupenda michezo pamoja na jamii kwa ujumla kwa kuweza kuyarudisha maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya michezo yaani maeneo ya wazi kumilikiwa na kusimamiwa moja kwa moja na kuwa na hati miliki. Ambapo awali mmiliki hajulikani ni nani isipokuwa inajulikana kama ni eneo la wazi na kuleta mianya ya rushwa na ufisadi. Viwanja vya wazi vikirudishwa vitasaidia kukuza michezo hususan kwa watoto na watu wazima katika ngazi za chini .

5. Kuwa na mamlaka ya kisheria inayoiwezesha kufanya kazi zake kwa kuweka taratibu, sheria ndogo na sheria itakayowezesha kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Kuingia mikataba mbalimbali itakayowezesha wazabuni mbalimbali kujenga vitegauchumi ambavyo vitatumika kama viwanja vya michezo ama vinginevyo kama Mamlaka itakavyoridhia. Kuchukua mikopo yenye lengo la kukuza na kuongeza mitaji yenye tija ili iweze kujiendesha kibiashara pasipo kutegemea ruzuku ya serikali.

6. Viwanja vya michezo kama chanzo cha kipato ambacho kinaweza kuiletea faida kubwa serikali kwa njia ya kodi. Hivi sasa, njia kubwa ambayo viwanja vya michezo vinaweza kuiletea kipato serikali ni kupitia mchezo wa mpira wa miguu wa Simba na Yanga. Kwa kuwa na Mamlaka ya viwanja vya michezo kwanza , kutaondoa utegemezi wa aina moja ya michezo lakini vile vile kutaamsha ari ya wadau kutoka maeneo mbali mbali kuweza kuchangia na kuboresha viwanja vyao vya michezo katika maeneo wanayotoka. Pili kutaondoa urasimu pamoja na mianya ya wizi na rushwa katika mauzo ya tikiti kutokana na kuwa na chombo maalum kinachotumika kwa ajili ya kudhibiti mapato ya viwanja vya michezo. Lakini la mwisho ambalo ni la muhimu zaidi kuweza kuingia ubia na wamiliki wa viwanja binafsi kwa kuweka viwango na taratibu ambao nao kama ilivyo ada watachangia kiasi cha mapato ya viingilio vya kila mchezo ama shughuli ya kijamii kwa mamlaka.

7. Itasaidia kufufua michezo ambayo imekwisha sahaulika kama mpira wa wavu, mpira wa mikono, Kriketi n.k Kuanzia ngazi za chini. Ikumbukwe kwamba pamoja na Mamlaka kusimamia viwanja vya michezo, lakini mamlaka kupitia baadhi ya watendaji wake ambao wenye taaluma ya kila mchezo watashiriki katika kuhamasisha kuibua vipaji vya kila mtoto kuanzia ngazi za chini kabisa na kuweza kuhamasisha jamii kushiriki katika michezo.

8. Kuwa na Bima maalum ya viwanja vya michezo vitakavyowawezesha watumiaji pamoja na mamlaka husika kugharamiwa pindi janga linapojitokeza wakati wa mchezo wa aina yoyote.

9. Kuweza kupokea michango ya aina zote kutoka katika asasi binafsi, serikali pamoja na za kimataifa yenye lengo la kuwezesha kuendeleza malengo ya mamlaka.

10. Mwisho kuwa na mamlaka na uwezo wa kutathmini maeneo ambayo ni mazuri kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya michezo, Kuboresha viwanja vya zamani ili viendane na wakati.

Kwa kuhitimisha naweza kusema kwaba ili mamlaka hii iweze kufanya kazi kwa ufanisi inatakiwa siasa isiingie katika utendaji wake ili mamlaka isitumike kama kichaka cha wachache kwa ajili ya kujinufaisha. Na weza kusema kwamba nchi hizi ambazo zimefanya vizuri katika mashindano haya ya olimpiki ni matokeo ya wao kuwekeza kwa muda mrefu katika michezo kwa kuwawezesha wanamichezo wake kupata nyenzo muhimu pale wanapohitaji na mahali popote. Na nyenzo mojawapo ni viwanja bora vya michezo. Kamwe na izingatiwe mbali ya kuwa mchezo na uanamichezo unatokana na kipaji cha mtu, lakini mchezo ama uanamichezo ni taaluma kitu ambacho wanamichezo wetu bado hawajakitilia maanani.

No comments: