Monday, July 23, 2012

WAZIRI ANUSURU VISIMA VYA GESI KUWEKWA REHANI

Neville Meena, Mtwara


WAKATI Serikali imezindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, imebainika kuwapo kwa mpango ya kuviweka rehani baadhi ya visima vya gesi inayotoka katika kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi.


Mpango huo ulifichuliwa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akikabidhi eneo kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa kampuni tatu za China, katika kitongoji cha Mchepa, kijiji cha Madimba.


Profesa Muhongo alisema kumekuwapo na mpango wa mwekezaji katika mradi wa umeme wa Songosongo kuviweka rehani visima vya gesi kwa madai ya kutafuta fedha katika taasisi za kimataifa nje ya nchi.


“Leo hii wakati tunazindua ujenzi wa mradi hapa tayari zimeanza kuwapo dalili za watu kutaka kuchezea gesi yetu, wameanza kuinyemelea kule Songosongo wanasema kuwa eti tuwaruhusu waweke visima vyetu rehani ili wapate mikopo katika taasisi za fedha,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:


“Hili haliwezekani na nasema hivi wasikie, kama tumepoteza kwenye madini inatosha, hatutarajii tena kupoteza kwenye gesi na hatutarajii kuwa na mikataba mibovu, kama tuliwahi kufanya makosa imetosha”.


Kampuni ambayo inaendesha wa gesi mradi wa Songosongo ni Pan African Energy Ltd, ambayo mwaka jana alidaiwa Bungeni kwamba iliibia Serikali ya Tanzania Sh20 bilioni.


Profesa Muhongo alisema Pan African Energy wanajenga hoja ya kuruhusiwa kufanya hivyo kama hatua ya kufidia madeni wanayolidai Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambayo hata hivyo baadaye alipofuatwa hakuwa na takwimu sahihi za madeni hayo.
Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo aliwaagiza Tanesco kuweka mpango wa kuanza kulipa madeni hayo ili kutotoa mwanya wa mipango yenye mwelekeo kuhujumu sekta ya gesi.
“Tanesco wamenithibitishia kwamba wanakusanya mapato kati ya Sh60 na 70 bilioni na malipo ya mishahara kwa watumishi ni Sh11 bilioni kwa mwezi sasa hizo fedha nyingine zinakwenda wapi? Mwaagiza kwamba waanze kulipa madeni,” alisema Waziri huyo.
Bomba la Gesi


Ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa Kilometa 512 unatarajiwa kugharimu Sh1.86 trilioni ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China na unasimamiwa na Serikali ya nchi hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Petroli nchini, Yona Killagane alieleza kwenye uzinduzi huo kuwa muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi 18 na kwamba Serikali ya Tanzania inachangia asilimia 10 ya gharama husika.
“Ujenzi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha Sentimita 36 lenye urefu wa kilometa 487 katika eneo la nchi kavu na bomba jingine la kipenyo cha sentimita 24 urefu wa kilometa 24 baharini katika eneo la Somanga Fungu ambalo litaungana na bomba kuu kutoka Mtwara,” alisema Killagane na kuongeza:


“Bomba la Songosongo – Somanga Fungu litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo milioni 140 kwa siku na hili la Madimba litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi milioni 210 kwa siku”.


Alieleza kuwa mradi mzima ukikamilika utakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo 784 milioni kwa siku ambazo zitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 3,920.
Alisema umeme utakaozalishwa utakuwa na unafuu mkubwa wa gharama na kwamba Serikali itaokoa zaidi ya Sh1.6 bilioni kwa mwaka ambazo hutumika kugharamia umeme unaotokana na mashine za mafuta.


Kampuni za ujenzi


Ujenzi huo utaongozwa na Kampuni ya China Petroleum Technology Development Corporation (CPTDC), ikisaidiana na kampuni za China Petroleum Pipeline Bureau (CPP) na China Petroleum Pipeline Engineering Corporation (CPEC).


Makamu wa Rais wa China, Yan Wei ambaye alikabidhiwa eneo ambako uchimbaji huo utafanyika alisema mradi huo unahuisha historia ya miaka 42 ya uhusiano baina ya China na Tanzania iliyojengwa katika mradi wa Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).


“Tunafutahia kuona historia ikiendelea kuuhishwa, miaka 42 tangu ilipojengwa reli ya Tazara. Tunaahidi kwamba mradi huu pia utakuwa wa aina yake katika historia ya uhusiano baina ya nchi zetu mbili, Tanzania na China,” alisema Wei.
Historia ya mradi


Ahadi ya kupatikana kwa kiasi cha megawati 3000 za umeme ilitolewa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa ya kuukaribisha mwaka 2012 pale aliposema kwamba ujenzi wa bomba hilo utaligeuza tatizo la umeme kuwa historia.


“Maombi yetu kwa Serikali ya China ya kupata mkopo wa kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na mtambo wa kuchakata gesi inayotoka Songosongo yamekubaliwa,” alisema Kikwete katika hotuba yake ya Desemba 31, mwaka jana.


Makubaliano ya awali ya ujenzi wa bomba hilo yalisainiwa China Septemba 26, 2011 na Tanzania ikiwakilishwa na ujumbe ulioongozwa na alioyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na kufuatiwa ujumbe mwingine ambao uliongozwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo.


Mmoja wa wahandisi ndani ya Tanesco aliwahi kusema kwamba kila megawati 100 za umeme zinahitaji kujengewa kituo kidogo cha usambazaji, hivyo kwa megawati 3920 vitahitajika vituo vya namna hiyo visivyopungua 38.


Alisema ujenzi wa kituo kimoja gharama zake si chini ya Dola za Marekani milioni 15 ambazo ni karibu Sh24 bilioni na kwa hesabu hizo kiasi kinachohitajika kwa ajili ya ujenzi wa vituo 38 si chini ya Sh900 bilioni.
Profesa Muhongo jana alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Tumejipanga na kwenye bajeti yetu tutaweka wazi mipango yote ya ujenzi wa miundombinu tunavyojiandaa kupokea umeme huu ambao utakuwa mwingi.”
Alisema katika mipango inayondaliwa ni kuanza ujenzi wa njia mpya za umeme zenye uwezo wa kusafirisha nishati hiyo ya msongo wa kilovolt 400, tofauti na njia za sasa ambazo uwezo wake ni msongo wa kilovolt 220.
MWANANCHI

No comments: