Friday, July 13, 2012

WANANCHI WA MTWARA WAWAKILISHA KERO YAO KWA DC
Abdallah Bakari, MtwaraWAKAZI wa Kijiji cha Mayaya, Wilaya ya Mtwara mkoani hapa, wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 15 kufuata huduma za maji na matibabu vijiji jirani


Wakazi wa kijiji hicho walimweleza mkuu wa wilaya(DC) hiyo, Wilman Ndile kupitia risala yao iliyosomwa na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Mohamed Ussi, kuwa wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 15 kufuata maji Kijiji cha Tangazo au Lingwayamba hali inayowafanya kushindwa kushiriki vema katika shughuli za uzalishaji kipato kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo muhimu.


Mbali na maji lakini pia wakazi hao walisema kijiji chao chenye wakazi 1,458 kilichoanza 1986 hakina huduma ya zahanati hali inayowalazimu kutembea umbali wa kilometa 15 hadi Kijiji cha Mdimba kufuata huduma hiyo au kilometa 20 kwenda Mahurunga kuliko na kituo cha afya.


“Maji ndiyo kero yetu kubwa kwa sababu kila siku tunalazimika kutembea umbali wa kilomita 30 kufuata huduma hiyo, hivi sasa tunanunua dumu moja la lita 20 kwa Sh500, hali zetu kiuchumi ni mbaya hivyo tunakuomba utusaidie katika hili”, alisema Hassan Masoud mkazi wa Mayaya.


Mwananchi mwingine aliyepata nafasi ya kutoa kero baada ya mkuu huyo wa wilaya kuwataka kumweleza nini kero zao mbali na zile zilizoelezwa katika risala yao, yeye alisema kuwa kutokuwapo kwa huduma ya zahanati kunawafanya wajawazito kuwa hatarini kwani wengi wao wanajifungulia majumbani.


Wakazi hao walidai kuwa tangu kuanzishwa kijiji hicho huduma hizo muhimu hazijapatikana kwa uhakika kwani wanatumia visima vifupi viwili ambavyo hata hivyo havina maji ya kutosha hali inayowafanya watembee umbali huo kufuata maji, huku huduma nyingine kama zahanati na ofisi ya kijiji zikiwa ni misamiati migumu kwao.


Akijibu hoja hizo mkuu wa wilaya alisema kuwa ofisi yake inayachukua matatizo hayo na kwenda kuyafanyia kazi kwa haraka ili kuwaondolea kero hizo wanakijiji hao, kwani nao wanastahili kuhudumiwa na Serikali yao waliyoiweka madarakani kwa ridhaa yao.

“Nimewaelewa, sasa sisi ni watu wazima haina maana kudanganyana hapa kwamba eti kesho mtapata maji hapana,nitakachofanya kwa haraka sanani kukutana na wenzangu wote wanahusika na masuala haya na baada ya wiki moja mtajulishwa ni hatua zipi zitafuata ili kuondoa kero hizo”, alisema DC Ndile.


Mkuu huyo wa wilaya ambaye yupo katika ziara ya kujitambulisha kwa wananchi na viongozi vijijini akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali kutoka halmashauri ya wilaya hiyo, alisema kuwa ili kuondokana na matatizo hayo ni vema pia wananchi wakaanzisha mfuko wa maji ili Serikali ipate pa kuanzia kama inavyosema sera ya maji.


MWANANCHI

No comments: