Thursday, July 12, 2012

PARADOX: MGOMO WA MDs UNAWADHURU WAGONJWA, KUWAFUTIA USAJILI MDs KUNASAIDIA WAGONJWANa M. M Mwanakijiji,


Hoja kubwa ambayo imekuwa ikitolewa na wale wanaopinga mgomo wa madaktari ni kuwa mgomo una madhara ya moja kwa moja kwa wagonjwa na hasa upatikanaji wa huduma ya afya. Wanaopinga mgomo wa madaktari wanasema "madaktari hawana uzalendo" na wanafanya hivyo kwa kuendekeza "pesa" na siyo "wito wao". Wanatuambia - ndugu zetu hawa - kuwa mgomo wa madaktari una madhara ya moja kwa moja kwa wagonjwa na kuwa "madaktari wanawatoa kafara wagonjwa" kwa kuamua kugoma. Hoja zao tunazielewa hata kama hatuzikubali baadhi yetu sisi.

Hoja yao hiyo ingekuwa na nguvu na kuonesha ukweli kama ndugu zetu hawa hawa wangekuwa wa kwanza kulaani kitendo cha serikali kuanza kuwafutia usajiri madaktari na hata kuwaondoa kazini. Mtu mwenye hekima anajiuliza kuna tofauti gani basi kati ya mgomo wa hiari wa madaktari na amri ya nguvu ya kuwaondoa madaktari kazini? Kuna tofauti gati ya kimatokeo (consequential difference) kati ya daktari kugoma kutokwenda kazini na daktari kufutwa usajili wake na asiende kazini? Mgonjwa anaona tofauti gani?


Utaona hoja inayotolewa ni ya kuwakomoa madaktari. Kwamba "kwa vile serikali ilitaka mrudi kazini katika mazingira yale yale na kwa masharti yale yale nanyi mkakataa basi tunawakomoa ili tuone mtatumia elimu yenu wapi!". Sasa hili ni zuri kwenye kulipiza kisasi lakini kiakili halina mantiki, ni woga, na matumizi ya ubabe wa serikali (the tyranny of the government). Lengo ni kutaka kupigiwa magoti, kubembelezwa na hatimaye kuwafanya madaktari hawa - wengi vijana - wawe katika hali ya kukata tamaa (desperation) ili hatimaye mmoja mmoja waje kuomba msamaha na wakubali kurudishiwa usajili kwa masharti makubwa zaidi! Ni mbinu hii hii kwa wale waliosoma Boarding school wanaikumbuka hutumiwa na shule kuwarudisha wanafunzi walioleta vurugu; pale ambapo shule inawafukuza halafu ili warudi basi wanatakiwa kuweka sahihi makaratasi ya kutojihusisha na vurugu au masharti mengine magumu. Wanafunzi wanaokubali masharti hayo kimsingi wanajifunga utumwa; hawawezi kulalamika - bila kujikuta wanakumbushiwa walichotia saini!


Hivyo basi tunaweza kuona pia tofauti nyingine kubwa; madhara ya kuwafutia madaktari usajili au kuwatimua kazini ni makubwa zaidi kuliko madhara ya mgomo wa madaktari. Nitarudia sentensi hiyo na ninatumaini watu itawafikirisha kidogo: madhara ya kuwafutia madaktari usajili au kuwatimua kazini ni makubwa zaidi kuliko madhara ya mgomo wa madaktari. Madhara haya kwanza ni kwa wagonjwa na pili yanaingiza mchakato mwingine kabisa. Lakini zaidi ni madhara ya hatari kwa sababu kama madaktari wakiwa majasiri na kuamua kujiuzulu na kutojali usajili waliokataliwa na wakaamua bora warudi kulima kuliko kulazimishwa kufanya kazi kwenye mazingira magumu serikali haitokuwa na jinsi isipokuwa kurudi nyuma na kuwa itakuwa imepoteza hazina kubwa na kwa hakika itaingia gharama kubwa zaidi kuwa-replace hawa kuliko kama ingekaa na kukubali madai yao ya msingi!


Hoja ya kwamba madaktari wangeendelea kurudi kazini wakati "serikali inashughulikia matatizo yao" ni hoja yenye kuvutia dhaifu wa fikara. Matatizo ya madaktari siyo sawa na kero za muungano ambazo kwa miaka hamsini zimekuwa zikishughulikiwa kwa uvivu. Matatizo ya madaktari na hasa changamoto ya sekta ya afya ni wazi sana - maslahi, vitendea kasi na mazingira ya kazi. Kimsingi hayo matatu tu yanahitaji sera inayoeleweka na ambayo inazingatia unyeti wa sekta hii. Kufikiria sekta ya afya na fani ya udaktari kama fani nyingine ni kukosa kabisa kuelewa vitu vinavyoitwa "vipaumbele".


Binafsi ninaamini mgogoro mkubwa wa sekta yetu ya afya unasababishwa kwa sababu serikali imeng'ang'ania kujihusisha na utoaji wa huduma ya afya na hasa uajiri wa madaktari. Sielewi kwanini bado serikali inataka kuendessha hospitali nyingi hata za chini. Binafsi naamini mojawapo ya vitu ambavyo serikali ingeweza kuvifanya vizuri ni kuendesha hospitali za rufaa tu na vituo vya afya ya msingi na kuachilia huduma zote za katikati na mahsusi kufanywa na sekta binafsi. Serikali ingeweza kabisa kutengeneza mazingira mazuri kwenye afya ya msingi na mazingira mazuri kabisa kwenye rufaa. Madaktari na taasisi bbinafsi zingeweza kutoa huduma ya afya nyingine - isiyohusisha rufaa (na hata rufaa) lakini ikipunguza mzigo mkubwa wa serikali.


Leo serikali inapata mzigo mkubwa kwa sababu inajaribu kuendesha mambo mengi kutoka serikali kuu; halmashauri, polisi, magereza, maji, elimu, ulinzi, tawala za mikoa vyote vinaendeshwa toka serikali kuu. Matokeo yake serikali kwa kweli haiwezi kuhudumia sekta nyeti kama ya afya kwa uzuri zaidi. Na kuamua kuwafuta usajili madaktari hakusaidii kabisa kuondoa tatizo lilipo bali kunalichochea kwani kunajengwa katika hoja kuwa - madaktari watasalimu amri na kuja kuomba radhi. Sasa kama madaktari hawaombi radhi na baada ya kuona serikali inaamua kuwafutia wenzao usajili wakaamua kujiuzulu ili kulinda haki zao serikali itafanya nini?


Ikumbukwe kuwa punda hubeba mizigo kwa muda mrefu na huweza kwenda umbali mrefu na mizigo mingi tu. Lakini punda naye ambaye husifiwa kuwa ni "mnyama wa kazi" naye huchoka. Na kuna wakati - kwa wale waliowahi kufuga punda wanajua hili - punda hugoma. Haendi kwa fimbo, upinde au ulimbo! Sasa punda akigoma hata umtukane vipi au umshawishi kwa fimbo haendi! na akitaka kukuudhi zaidi - na sijui wanawajuaje - punda hukaa chini kukuonesha tu kuwa haendi unakoktaka aende hadi umpunguzi mizigo.


Madaktari wetu wamekuwa kama punda; wameenda na kwenda na kubebana na kubeba na sasa nina wasiwasi kuwa wanaweza kukaa chini na kusema "screw this!". Na wakifanya hivyo, siyo usajili wala udahili utakaoweza kubadilisha na kimsingi kulazimisha serikali kuanza upya.


Vyovyote vile ilivyo, uamuzi wa kuwafutia madaktari usajili ili kuwalazimisha kurudi kazini ni uamuzi wa kiwoga, wa kibabe na ambao umejaa kushindwa ndani yake. NI uamuzi unaoonesha upeo wa uwezo wa watawala wetu kutatua matatizo yetu. NI uamuzi ambao unahitaji kupingwa na kulaaniwa kwani unakwepesha matatizo. Kwani, hata madaktari wakiamua kurudi na kufanya kazi kwa kuhofia usajili wao kufutwa bado matatizo ya msingi yatakuwepo pale pale na bado yataendelea kuchemka chini kwa chini (simmer).


Na kwa kadiri matatizo bado yanafurukuta basi bado migogoro itatukuta.


Na. MMM

No comments: