Friday, July 27, 2012

MGOMO WA WALIMU WAIVA
Ibrahim YamolaCHAMA cha Walimu nchini (CWT) kiko katika hatua za mwisho kutangaza rasmi kuanza kwa mgomo wa walimu nchini, unaotarajiwa kutangazwa rasmi wakati wowote baada ya saa 48 kuanzia asubuhi ya leo.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema mgomo huo sasa umeiva, baada ya mgogoro baina yao na Serikali uliodumu kwa siku 30 kumalizika bila kufikia suluhisho.
Msimamo huo wa CWT unatolewa wakati madai ya Madaktari yakiwa bado hayajapatiwa ufumbuziwa kudumu na kusababisha kuzorota kwa huduma za afya katika hospitali za umma.


“Baada ya kushindwa kutatuliwa, zoezi la kupiga kura limeanza tangu jana (juzi) na litaendelea hadi kesho (leo) saa 3 asubuhi, baada ya muda huo kupita, Chama kitakuwa na kazi ya kupokea matokeo ya upigaji kura kutoka kila Wilaya,” alisema Mukoba na kuongeza:


“Ikiwa walimu watakaounga mkono mgomo watakuwa wengi kuliko wale watakaoupinga, Baraza la Taifa la CWT litakutana kwa dharura kutangaza mgomo ambao utakuwa umeamuliwa na muda wa mgomo huo.

Rais huyo alifafanua kuwa baada ya uamuzi huo kufikiwa CWT itatoa notisi ya saa 48 kwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni Mkuu wa Utumishi wa Umma kumwarifu tarehe ya kuanza kwa mgomo ili alinde mali zake kama Sheria inavyoeleza.


Mukoba alisema, mgogoro na Serikali ulisajiliwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Juni 8 mwaka huu na kupewa namba CMA/DSM/ILA/369/12 na msuluhisi aliyeteuliwa na Tume hiyo Cosmas Msigwa kushindwa kuwasuluhisha.


“Siku 30 zilianza kuhesabiwa Juni 26 na kumalizika Julai 25 mwaka huu, kwa msuluhishi Msigwa kutoa Cheti cha kuthibitisha kuwa mgogoro umeshindikana kusuluhishwa kwa mjibu wa Sheria,” alisema Mukoba na kuongeza:
Ndani ya siku hizo 30 tumekutana kujadiliana kwa vikao vitatu lakini hakukuwa na dalili zozote za Serikali kuhakikisha inatatua matatizo yetu.

Rais huyo alisema, madai ya Serikali kushindwa kuyatatua ilisema ni kutokuwa na takwimu za walimu wangapi wanastahili kulipwa na huenda wengine wameshakufa.
“Hoja hii ilikuwa na nia ya kupotosha ukweli wa madai ya walimu kwa kuwa kikao cha Julai 10 mwaka huu, Serikali iliwasilisha taarifa kuwa ingetumia zaidi ya Sh4 trilioni kulipa mishahara ya walimu tu kama ikilipa mishahara kwa viwango vilivyowasilishwa na CWT iweje itake tena takwimu,” alihoji Mukoba.


Mukoba alisema Serikali ilikuwa haijui walimu wangapi wanafundisha masomo ya Sayansi na wangapi wanafundisha katika mazingira maguku kitendo ambacho walikipinga.
“Tulipinga hoja hizo kwa maelezo kwamba Serikali ndio yenye Shule za mchepuo wa Sayansi na inafahamu fika walimu wa Sayansi ni wangapi kwa kuwa takwimu hizo zilitolewa bungeni katika kipindi cha maswali na majibu” alisema Mukoba na kuongeza:

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mlugo aliliambia Bunge kuwa Serikali imetumia Sh22 bilioni kuwalipa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu Sh500,000 mara moja tu wanapokwenda kuanza kazi, na kama imetambua hilo iweje isifahamu maeneo yenye kuhitaji posho ya mazingira magumu?”.


Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekia Oluoch alitoa wito kwa wazazi na wanafunzi akiwataka kutowafikiria walimu vibaya wakati wakiwa katika mgomo huo na kitakachofanyika ni kudai maslahi yao.
“Tunawapenda sana wanafunzi, lakini watambue kiwango ambacho Serikali inatulipa ni kidogo ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji yetu ndio maana tunaamua kugoma hivyo watuunge mkono,” alisema Oluoch.


MWANANCHI

No comments: